Bustani ya Wanyama—Je, Ni Tumaini la Mwisho la Wanyama wa Pori?
KATIKA nyakati za majuzi mabadiliko makubwa yametukia polepole katika bustani za wanyama zenye maendeleo zaidi ulimwenguni. Ukiwa wonyesho wa nje, wao wamerekebisha upya bustani hizo kwa kupatana na wazo lenye ufikirio la kuwa na “mandhari ya asili”—kule kufanyizwa kwa mazingira ya asili ya wanyama, yaliyo kamili kwa mimea, mawe, mimea yenye kutambaa, ukungu, kelele, na hata wanyama na ndege ambao huambatana pamoja. Ingawa ni gharama kubwa kufanya hivyo—dola bilioni 1.2 hivi hutumiwa ili kuboresha bustani za wanyama na matangi ya viumbe vya bahari kila mwaka Marekani pekee—mabadiliko hayo huonwa kuwa ya lazima kwa kufikiria daraka jipya la bustani za wanyama.
Utume wa Karne Ijayo
Huku uhaba wa wanyama na mimea ukitisha sayari, bustani za wanyama zilizo mashuhuri ulimwenguni zimeazimia kuhifadhi wanyama, kuelimisha watu, na kufanya utafiti wa kisayansi katika karne ya 21. Zikichochewa na mwito huo na kusukumwa na udharura wa hali, bustani nyingine za wanyama hata zimeacha kabisa kutumia jina bustani ya wanyama na badala ya hivyo zinatumia maneno kama “hifadhi ya wanyama wa pori” au “mbuga ya hifadhi.”
Kichapo The World Zoo Conservation Strategy ndicho kinachoongoza harakati hizo mpya. Kikifafanuliwa na mwandikaji mmoja kuwa “hati muhimu zaidi ambayo jumuiya za bustani za wanyama zimepata kutokeza,” kichapo Strategy hasa ni mkataba wa masuala ya wanyama; hicho “chafafanua wajibu na madaraka ya bustani za wanyama na matangi ya viumbe vya bahari vya ulimwengu ili kuhifadhi aina nyingi za wanyama wa pori wa duniani kote.” Kikiondosha shaka zozote juu ya hayo mambo mapya, Strategy chaongezea: “Haki ya kuwapo kwa bustani ya wanyama au kuwapo kwa matangi ya viumbe vya bahari kwa hakika yategemea mchango wake katika kuhifadhi wanyama wa pori.”
Kuelimisha umma na kufanya utafiti wa kisayansi, hasa kuhusu uzalishaji wa wanyama walio utekwani, ni muhimu sana katika daraka hili jipya. Miongoni mwa vijana wa leo mna wale watakaotunza bustani za wanyama kesho, ambao watakuwa na daraka la kuhifadhi mabaki yaliyookoka kati ya spishi nyingi zinazozidi kutoweka porini. Je, wao watatumia amana hiyo kwa hekima na kwa ujitoleaji? Na je, mwanadamu kwa ujumla atakuwa na ufahamu zaidi kuhusu mambo ya asili? Kwa kusudi hilo, Strategy chatia moyo kila bustani ya wanyama kuelimisha watu, na kujiona kuwa sehemu ya “mfumo wa ulimwenguni pote wa kutahadharisha watu.”
Bustani za Wanyama Zaungana Katika Mfumo wa Duniani Kote
Kwa sababu ya ukubwa sana wa kazi hiyo, bustani nyingi za wanyama zinaungana ili kufanyiza mfumo wa duniani kote, ambao sasa una ushirika wa bustani za wanyama zipatazo 1,000. Mashirika ya kimataifa, kama vile Shirika la Ulimwengu la Bustani za Wanyama na Muungano wa Kimataifa wa Hifadhi ya Asili na Maliasili, huunganisha bustani hizo pamoja na kuandaa mawasiliano na mwelekezo.
Kikitaja sababu kubwa sana ya kuwa na ushirikiano kama huo, kitabu Zoo—The Modern Ark chasema: “Kuzalisha wanyama wa familia moja kusipokomeshwa, bustani hizo za wanyama haziwezi kuridhika kwa kudhibiti tu wanyama wachache zilizo nao kama vile simbamarara wa Siberia. Badala ya hivyo, simbamarara wote wa Siberia walio utekwani katika bustani zote za wanyama za kontinenti fulani—au hata ulimwenguni pote—waonwe kuwa wa familia moja.” Ndiyo, mamia ya kila spishi huhitajika ili kukomesha kuzalisha wanyama wa familia moja—ambako ni utangulizi wa kutoweza kuzaa na kutoweka kabisa kwa wanyama—na kwa wazi bustani moja ya wanyama haiwezi kutimiza jambo hilo. Kichapo Strategy chasema: “Kukusanywa kwa mali zote ziwezazo kutumika kutahitajika ili kuipa Dunia yetu . . . uwezekano mzuri zaidi wa kuokoka. Kuna wengi wanaoamini kwamba tukishindwa kuhifadhi spishi nyinginezo tutashindwa kujiokoa.” Bila shaka, mtazamo huu wa kutotazamia mazuri haufikirii ahadi ya Biblia ya dunia iliyorudishwa kuwa paradiso.—Ufunuo 11:18; 21:1-4.
Vifaa vya Kusaidia Bustani za Wanyama Kufanikiwa
Tatizo la kutoweka kwa wanyama limechochea pia uundaji wa vifaa fulani vya tekinolojia ya hali ya juu viwezavyo kutumika kimataifa katika uzalishaji wa wanyama walio utekwani: rekodi za uzalishaji wa wanyama, International Zoo Yearbook (IZY), na Mfumo wa Habari za Spishi Zipatikanazo Kimataifa (ISIS) unaotegemea kompyuta.
Kila rekodi ya uzalishaji wa wanyama huorodhesha habari nyingi juu ya wanyama wote wa spishi moja wanaoishi katika bustani mbalimbali za wanyama, hata wawe wapi ulimwenguni. Hiyo ikiwa rekodi ya kimataifa, ndiyo ufunguo wa kuhifadhi chembe za urithi na kukomesha kuzalisha wanyama wa familia moja. Bustani ya Wanyama ya Berlin ilifungua rekodi ya kwanza kabisa ya kuzalisha wanyama mnamo 1923 ilipoanza kuzalisha nyatisinga wa Ulaya, ambaye karibu atoweshwe na Vita ya Ulimwengu ya Kwanza.
Ili kuboresha usambazaji wa habari za kisayansi kama vile rekodi za uzalishaji wa wanyama, IZY, na habari za idadi ya wanyama, shirika la ISIS lilijiunga na mfumo mkuu wa kompyuta katika 1974 Marekani. Mfumo wake wa kompyuta wenye kupanuka na ugavi mkubwa unaozidi kuongezeka wa habari unasaidia bustani za wanyama kuweza kufanya kazi pamoja ili ushirikiano wa bustani nyingi za wanyama utimizwe.
Vifaa vya kibiolojia vinavyotumiwa na bustani za wanyama hutia ndani kupiga chapa za DNA, kupachika viinitete, utungishaji wa yai nje ya mwili, na cryogenics (kugandisha shahawa na viinitete). Kupiga chapa za DNA husaidia bustani za wanyama kutambulisha uzazi wa mnyama bila kukosea hata kidogo, jambo lililo muhimu katika kudhibiti kuzalisha wanyama wa familia moja, kama vile miongoni mwa wanyama ambao hutembea kwa makundi makubwa, ambao ni vigumu sana kujua uzazi wao. Kwa wakati uo huo kupachika kiinitete na kutungisha yai nje ya mwili huharakisha uzalishaji. Njia moja ya kutimiza hilo ni kuongeza “wazazi” wengi zaidi kwa spishi iliyo hatarini mwa kutoweka. Viinitete vyao vyaweza kuingizwa katika spishi zilizo na uhusiano wa karibu nao—hata wanyama wa kufugwa—ambao nao huwa mama-walezi. Mbinu hiyo imefanya ng’ombe amzae ng’ombe-mwitu na paka wa nyumbani kumzaa paka wa jangwa wa India ambaye yumo hatarini kabisa mwa kutoweka. Pia imepunguza gharama, hatari, na athari za kusafirisha mnyama aliye hatarini mwa kutoweka. Viinitete au shahawa zilizogandishwa ndizo huhitajika tu kusafirishwa.
Kukiwa na uwezekano wa spishi fulani kutoweka kabisa, bustani fulani ya wanyama imeingilia sayansi ya kugandisha shahawa na viinitete na kuziweka akiba kwa muda mrefu. Vitu hivyo vilivyogandishwa hutoa tazamio la kuzaliwa kwa wazao miongo mingi, na labda hata karne nyingi baadaye, baada ya wanyama hao kutoweka! Ingawa imejaa tashwishi, hiyo imeitwa “jambo la pekee liwezalo kufanywa.”
Uchunguzi Porini Husaidia Bustani za Wanyama Kuzalisha Watoto Zaidi
Uchunguzi wa kisayansi wa wanyama, kutia ndani tabia zao wakiwa katika makao yao ya asili, ni muhimu sana katika kuzalisha wanyama walio utekwani na ndio kichocheo cha kufanyiza “mandhari ya asili” katika bustani za wanyama. Ili wanyama wadumishe afya nzuri na kuweza kuzaana, ni lazima bustani za wanyama zifikirie silika za wanyama hao na “kuwafurahisha.”
Kwa mfano, duma wa kiume na duma wa kike hujitenga wakiwa porini nao huwasiliana kwa harufu tu iliyo katika mkojo wao na kinyesi chao. Harufu humjulisha duma wa kiume wakati ambapo duma wa kike yu tayari kujamiiana, kisha yeye hukaa na duma wa kike kwa siku moja au mbili tu. Bustani za wanyama zilipogundua tabia hiyo, zilirekebisha mahali walipo wanyama hao ili kutenganisha duma wa kiume na duma wa kike wakati wote ila tu katika pindi fupi za kujamiiana, na wakafaulu; watoto wakazaliwa.
Ingawa kutoonana kwa duma hufanya wapendane zaidi, sivyo ilivyo na heroe. Wao hujamiiana tu katika makundi makubwa sana ambayo bustani za wanyama haziwezi kushughulikia. Kwa hiyo bustani fulani za wanyama katika Uingereza zilifanya majaribio—“zilirudufisha” ukubwa wa kundi kwa kioo kikubwa sana. Kwa mara ya kwanza, ndege hao walianza michezo ya kutazamisha ya kujamiiana! Je, mifano hiyo inakupa dokezo la utata wa wanyama wa pori wa dunia? Kwa hakika bustani za wanyama zinakabili ugumu mkubwa sana.
Mradi wa Kuokoa Wanyama Ni Halisi Kadiri Gani?
Ikionyesha uwezekano wa hiyo programu mpya kufaulu, spishi nyingine zilizozalishwa utekwani zimerudishwa katika bustani zao za asili. Miongoni mwa hao ni tai wa California, nyatisinga wa Ulaya, nyatisinga wa Marekani, choroa wa Arabia, golden lion tamarin, na farasi-mwitu. Hata hivyo, kuna shaka juu ya matazamio ya wakati ujao.
“Jamii ya kibinadamu ni tata sana, na matatizo ya ulimwengu ni mengi sana,” chasema Strategy, “hivi kwamba japo ukuzi wa ufahamu na hangaiko kuhusu asili na mazingira, haijawezekana kukomesha hatua nyingi zenye kuleta uharibifu.” Tokeo ni kwamba, “ni lazima wahifadhi wajitayarishe kutafuta njia za kukabili kipindi cha matatizo kinachotazamiwa,” chaongezea. Kwa kawaida, jambo hilo lataka ushirikiano katika kila tabaka la jamii. Ushirikiano wa sasa, kulingana na mwandishi mmoja wa kisayansi, “ni mbali sana na ushirikiano unaohitajika.” Ikiwa misongo inayofanya wanyama watoweke yapungua tu lakini haikomi, hata jitihada bora zaidi huenda bado zisifaulu. Bustani kubwa na zilizo kamili—si maeneo madogo pekee, ambayo hutokeza kuzalisha wanyama wa familia moja—ni lazima zitayarishwe. Ndipo tu bustani za wanyama ziwezapo kuachilia wanyama bila wasiwasi ili warudi porini. Lakini, je, tumaini kama hilo ni halisi, au ni dhana tu ambayo haiwezi kufaulu?
Isitoshe, ni vigumu hata zaidi kuamini kwamba suluhisho ni ushirikiano wa bustani zote za wanyama. “Ukweli mchungu,” asema Profesa Edward Wilson, “ni kwamba bustani zote za wanyama ulimwenguni pote leo zaweza kutoshea spishi 2,000 tu za wanyama, ndege, wanyama-watambaazi na amfibia”—na hizo ni spishi chache sana. Kwa hiyo bustani za wanyama zina jukumu gumu la kuamua ni spishi gani zitakazohifadhiwa na spishi zitakazojiunga na orodha ndefu ya wanyama wanaotoweka.
Kwa wataalamu wa uhifadhi, hilo lazusha swali lenye kutisha, Kwa kufikiria kutegemeana kwa viumbe vyote vilivyo hai, ni lini wanyama na mimea watakapokuwa hatarini kufikia hatua ambapo wataanzisha kutoweka kwingi kwa wanyama ambako kutaharibu uhai ubakio duniani, kutia ndani na wanadamu? Wanasayansi wanaweza kukisia tu. “Kutoweka kwa spishi moja au mbili au hamsini kutakuwa na athari ambazo sisi hatuzijui,” asema Linda Koebner katika Zoo Book. “Kutoweka kwa wanyama kunatokeza badiliko hata kabla ya sisi kuelewa athari zake.” Kwa wakati uo huo, chasema kitabu Zoo—The Modern Ark, “bustani za wanyama zadumu kuwa hifadhi muhimu zaidi ya uhai katika vita vya dunia vya kuangamiza wanyama, vita ambavyo haviwezi kutabirika na ambavyo vizazi vya wakati ujao vitatulaumu kabisa.”
Basi, je, kuna msingi wowote wa kuwa na tumaini? Au je, vizazi vya wakati ujao vitabaki na dunia isiyo na wanyama na mimea, vyenyewe vikingoja kutoweka?
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mwanadamu ndiye adui yao mbaya zaidi
[Hisani]
Simbamarara na Tembo: Zoological Parks Board of NSW
[Picha katika ukurasa wa 8]
Wanyama fulani walio hatarini mwa kutoweka—nyatisinga, duma, na kifaru mweusi
[Hisani]
Nyatisinga na Duma: Zoological Parks Board of NSW
Kifaru: National Parks Board of South Africa