Spishi Zilizo Hatarini mwa Kutoweka—Mweneo wa Hilo Tatizo
DODO wamekuwa ishara ya kutoweka. Wa mwisho wa ndege hao wasioweza kupuruka alikufa karibu mwaka wa 1680 katika kisiwa cha Mauritius. Nyingi za spishi ambazo kwa sasa zimo hatarini vilevile zinaishi katika visiwa. Katika miaka 400 ambayo imepita, spishi 85 kati ya 94 za ndege wajulikanao kuwa wametoweka zimekuwa ndege wa visiwa.
Wanyama walio katika kontinenti zilizo kubwa wamo hatarini mwa kutoweka pia. Fikiria simbamarara ambao zamani walitangatanga kotekote Urusi. Sasa ni jamii tu ya Amur inayobaki Siberia, nayo idadi yayo imepungua sana kufikia kati ya 180 na 200. Simbamarara wa kusini mwa China waripotiwa kufikia idadi ya kati ya 30 na 80 tu. Katika India na China wanyama hao wanakabiliwa na kutoweka “katika miaka kumi ijayo,” laripoti The Times la London. Vilevile, katika India, ambayo ni makao ya karibu thuluthi mbili ya simbamarara wanaopatikana ulimwenguni pote, wenye mamlaka wakadiria kwamba viumbe hao wenye fahari waweza kutoweka kwa mwongo mmoja.
Vifaru na duma wanapungua pia. Katika China panda wakubwa hutanga-tanga kwa makundi madogo ya kumi-kumi tu. Wanyama waitwao pine marten wanakaribia kutoweka katika Wales, na kuchakulo-wekundu “waweza kutoweka Uingereza barani na Wales katika miaka kumi hadi 20 ijayo,” ladai The Times. Ng’ambo ya Atlantiki katika Marekani, popo ndiye mnyama wa nchi kavu aliye hatarini zaidi mwa kutoweka.
Hali za bahari-kuu za ulimwengu ni mbaya vilevile. Kitabu The Atlas of Endangered Species chaeleza kasa wa bahari kuwa “labda kikundi kilicho hatarini zaidi mwa kutoweka” kati ya viumbe wa bahari. Amfibia waonekana kuwa afadhali; lakini, kulingana na gazeti New Scientist, spishi 89 za amfibia zimekuwa “hatarini mwa kutoweka” katika miaka 25 ambayo imepita. Asilimia zipatazo 11 za spishi za ndege zinakabiliwa na kutoweka vilevile.a
Lakini vipi juu ya viumbe wadogo, kama vile vipepeo? Hali ni ileile. Zaidi ya robo ya spishi 400 za vipepeo wa Ulaya zimo hatarini—19 zikikaribia kutoweka. Mnamo 1993, kipepeo mkubwa wa Uingereza aitwaye tortoiseshell alijiunga na dodo katika orodha ya spishi zilizotoweka.
Hangaiko Lenye Kuongezeka
Ni spishi ngapi za viumbe ambazo hutoweka kila mwaka? Jibu lategemea ni mtaalamu yupi unayemuuliza. Ingawa wanasayansi hawakubaliani, wote wanatambua kwamba spishi nyingi zimo hatarini mwa kutoweka. Mtaalamu wa ikolojia Stuart Pimm aonelea hivi: “Ubishi juu ya jinsi tunavyopoteza upesi [spishi] hasa ni mjadala juu ya wakati wetu ujao.” Yeye aongezea hivi: “Katika karne ambazo zimepita, sisi wanadamu tumeharakisha mwendo wa kutoweka kwa spishi kushinda mwendo wa kiasili kwa mbali. Matokeo ni kwamba hatuna wakati ujao mzuri.”
Sayari yetu, Dunia, ni kama nyumba. Watu wengine ambao huhangaikia spishi zilizo hatarini mwa kutoweka husoma ikolojia, neno lililofanyizwa mwishoni-mwishoni mwa karne ya 19 kutokana na neno la Kigiriki oiʹkos, limaanishalo “nyumba.” Ikolojia hukazia uhusiano kati ya viumbe wenye uhai na mazingira yao. Katika karne ya 19 kulikuwa na upendezi wenye kuongezeka katika hifadhi, labda ukichochewa na ripoti za kutoweka kwa viumbe. Katika Marekani, jambo hilo lilifanya mbuga za kitaifa na maeneo ya hifadhi yafanyizwe ili kulinda viumbe. Kwa wakati huu, kuna hifadhi za wanyama wa pori zikadiriwazo kuwa 8,000 ulimwenguni pote ambazo zinatambuliwa kimataifa. Pamoja na maeneo mengine 40,000 ambayo husaidia kudumisha makao, hayo hufanyiza karibu asilimia 10 ya eneo la nchi kavu la ulimwengu.
Watu wengi wenye kuhangaika sasa wanapendekeza yale yaitwayo mashirika ya mazingira, ama kupitia mashirika ambayo hutangaza viumbe walio hatarini mwa kutoweka au yale ambayo hufundisha tu watu juu ya utegemeano wa uhai. Na tangu Mkutano wa Dunia wa Rio wa 1992, uelewevu mkubwa zaidi juu ya masuala ya kimazingira hufuatwa katika sera ya serikali.
Tatizo la spishi zilizo hatarini mwa kutoweka ni la duniani pote nalo lazidi kuongezeka. Lakini kwa nini? Je, majaribio yoyote ya kuzuia kutoweka kwa spishi wakati huu yanafanikiwa? Na vipi juu ya wakati ujao? Wewe Unahusikaje? Makala zetu zifuatazo zitatoa majibu.
[Maelezo ya Chini]
a Spishi ambayo imetoweka ni ile ambayo haijaonekana porini kwa miaka 50, na spishi iliyo hatarini mwa kutoweka yarejezea zile ambazo zimo katika hatari ya kutoweka hali zao za sasa zisipobadilika.