Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 4/22 kur. 12-15
  • Tumaini Thabiti Kati ya Huzuni ya Chernobyl

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tumaini Thabiti Kati ya Huzuni ya Chernobyl
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Siku Hiyo ya Aksidenti
  • Matokeo ya Baadaye
  • Matokeo ya Mnururisho kwa Afya
  • Kufikiria Yaliyotukia
  • Uhakika Kati ya Hofu Ambayo Imeenea
  • Chernobyl Kutembelea
    Amkeni!—2006
  • Tisho la Nyukilia—Je! Limekwisha Hatimaye?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Cheche za Mnururisho Suala Linalohangaisha
    Amkeni!—2001
  • Hakuwa Mzee Mno Asimtumikie Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 4/22 kur. 12-15

Tumaini Thabiti Kati ya Huzuni ya Chernobyl

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Ukrainia

APRILI 26, 1986, aksidenti mbaya zaidi katika historia ya viwanda vya nyukilia ilitokea Chernobyl, Ukrainia. Baadaye mwaka huo Mikhail Gorbachev, aliyekuwa rais wa Sovieti wakati huo, alisema kwamba msiba huo ulikuwa kikumbusha kibaya sana kwamba “mwanadamu bado hadhibiti kani zenye nguvu sana ambazo amevumbua.”

Likikazia umaana wa msiba wa Chernobyl, toleo la Ujerumani la Psychology Today la Februari 1987, liliripoti hivi: “Msiba huo wa kitendanishio katika Chernobyl . . . ulikuwa badiliko kubwa katika historia ya ustaarabu wa kisasa. Nao ulikuwa msiba mkuu utakaotuathiri sana kwa karne nyingi.” Gazeti The New York Times lilisema kwamba “kiasi cha mnururisho ambacho kilikuwa [kimeingia] katika anga, udongo wa juu na maji ya ulimwengu kinatoshana na mnururisho uliotolewa na majaribio yote ya kinyukilia na mabomu yote yaliyopata kulipuliwa.”

Gazeti la Ujerumani Hannoversche Allgemeine lilitabiri kwamba “katika miaka 50 ijayo watu wapatao 60,000 ulimwenguni pote wangekufa kwa kansa kwa sababu ya kuyeyuka kwa kitendanishio cha kinyukilia cha Sovieti . . . Wengine zaidi 5,000 wangepatwa na madhara mabaya sana ya kurithi na kufikia 1,000 wangepatwa na kasoro za afya tangu kuzaliwa.”

Msiba wa Chernobyl ulitokeza hofu, wasiwasi, na ukosefu wa uhakika ambao umekumba mamia ya maelfu ya uhai. Lakini, wengine wamepata tumaini thabiti kati ya huzuni kubwa. Ebu fikiria familia ya akina Rudnik, ambayo ina Victor na Anna na binti zao wawili, Elena na Anja. Katika Aprili 1986 akina Rudnik walikuwa wakiishi Pripet, umbali unaopungua kilometa tatu kutoka kwa kitendanishio cha Chernobyl.

Siku Hiyo ya Aksidenti

Katika asubuhi ya Jumamosi hiyo yenye msiba, matendo ya kishujaa ya zima-moto kwenye kitendanishio hicho kilichokuwa kimeharibika yalizuia matokeo mabaya zaidi. Kwa muda wa saa kadhaa hao zima-moto walipatwa na ugonjwa wa mnururisho, na kadhaa kati yao wakafa baadaye. Grigori Medwedew, naibu wa mhandisi mkuu katika Chernobyl katika miaka ya 1970, aeleza hivi katika kitabu chake Burned Souls: “Wingu lilielea kupita shamba dogo la misunobari ambalo hutenganisha mahali pa kitendanishio na mji, likifunika msitu huo mdogo kwa majivu yenye mnururisho.” Iliripotiwa kwamba tani nyingi sana za hewa ya mnururisho ziliingia katika anga-hewa!

Kwa kutokeza, maisha katika Pripet, jiji lenye wakazi zaidi ya 40,000, yalionekana yakiendelea kama kawaida Jumamosi hiyo. Watoto walikuwa wakicheza barabarani, na watu walikuwa wamejitayarisha kusherehekea sikukuu ya Sovieti ya Mei 1. Hakukuwa na matangazo ya aksidenti hiyo wala onyo la hatari. Anna Rudnik alikuwa nje akitembea-tembea na binti yake mwenye umri wa miaka mitatu, Elena, walipokutana na baba wa kambo wa Anna. Huyo baba alikuwa amesikia juu ya aksidenti hiyo. Kwa sababu alikuwa na wasiwasi juu ya hatari ya mnururisho, kwa haraka aliwapeleka kwa gari kwake umbali wa karibu kilometa 16.

Wingu hilo lenye mnururisho liliinuka na kuingia katika anga-hewa na kupeperushwa mamia ya kilometa kuvuka Ukrainia, Belorusia, (sasa ni Belarusi), Urusi, na Poland, na vilevile juu ya Ujerumani, Austria, na Uswisi. Jumatatu iliyofuata, wanasayansi katika Sweden na Denmark wakawa na wasiwasi waliporekodi viwango vya juu vya mnururisho.

Matokeo ya Baadaye

Majeshi ya Sovieti, zima-moto, wastadi wa ujenzi, na wengine walipelekwa Chernobyl. Kundi hilo—la watu wapatao 600,000—likaja kuitwa “wamalizaji.” Wao walizuia msiba mbaya hata zaidi ambao ungepata Ulaya kwa kuziba kitendanishio kilichoharibika kwa kasha la chuma na simiti ambalo lilikuwa na kimo cha orofa kumi na unene wa meta mbili.

Watu walianza kuhamishwa siku chache zilizofuata. “Tulilazimika kuacha nyumba yetu, tukiacha kila kitu—mavazi, pesa, hati, chakula—kila kitu tulichokuwa nacho,” akaeleza Victor. “Tulikuwa na wasiwasi sana kwa sababu Anna alikuwa na mimba ya mtoto wetu wa pili.”

Watu wapatao 135,000 walilazimika kuhama—makao yote yaliyokuwa katika eneo la karibu kilometa 30 kutoka kwa kitendanishio hicho yaliachwa. Akina Rudnik walihamia kwa watu wa ukoo. Lakini, punde si punde watu hao wa ukoo walianza kuhofu kwamba akina Rudnik wangewaambukiza huo mnururisho. “Wakawa na wasiwasi,” asema Anna, “na hatimaye wakatuambia tuondoke.” Wahamishwa wengine pia walipatwa na mambo hayo yenye kuhuzunisha. Hatimaye, katika Septemba 1986 akina Rudnik walipata makao katika Kaluga, kilometa zipatazo 170 kusini-magharibi ya Moscow, Urusi.

“Hatimaye tukaelewa kwamba hakuna tumaini la kurudi nyumbani,” Anna akasema. “Tulikuwa tumepoteza nyumba yetu nzuri ya familia, ambako tulizaliwa na kulelewa. Lilikuwa eneo maridadi sana lenye kujaa maua na nyasi, na yungiyungi ya maji katika hori. Msitu ulijaa beri na uyoga.”

Ukrainia haikuharibiwa tu umaridadi wayo bali pia fungu layo la kukuza nafaka zaidi katika Muungano wa Sovieti liliathiriwa. Kiasi kikubwa cha mavuno ya nchi hiyo katika vuli hiyo kilikuwa kimechafuliwa. Vivyo hivyo, katika Skandinavia, asilimia 70 ya nyama za reindeer ilitangazwa kuwa haifai kuliwa kwa sababu wanyama hao walikuwa wamekula ukungu wenye mnururisho. Na katika sehemu fulani za Ujerumani, mboga ziliachwa zioze shambani kwa sababu ya hofu ya kuchafuliwa.

Matokeo ya Mnururisho kwa Afya

Tarakimu rasmi zilizotolewa miaka mitano baada ya hiyo aksidenti zasema kwamba watu 576,000 walihatarishwa na mnururisho huo. Inaripotiwa kwamba visa vya maradhi ya kansa na yasiyo ya kansa ni vingi zaidi miongoni mwa watu hawa. Hasa vijana wameathiriwa. Gazeti New Scientist la Desemba 2, 1995, liliripoti kwamba mmoja wa wataalamu mashuhuri wa thiroidi katika Ulaya aamini kwamba “kufikia asilimia 40 kati ya watoto waliohatarishwa na mmwagiko mwingi sana wa Chernobyl walipokuwa chini ya umri wa mwaka mmoja wangeshikwa na kansa ya thiroidi wakiwa watu wazima.”

Kwa sababu Anna alikuwa amehatarishwa na mnururisho wakati wa mimba, madaktari walisisitiza kwamba atoe hiyo mimba. Victor na Anna walipokataa, wao walilazimika kutia sahihi azimio lililosema kwamba wao wangemtunza mtoto wao hata kama angezaliwa kilema. Ingawa Anja si kilema, yeye ana matatizo ya kutoweza kuona mbali, matatizo ya kupumua, na maradhi ya moyo. Kwa kuongezea, afya za wengine katika familia ya akina Rudnik zimedhoofika tangu msiba huo. Wote wawili Victor na Elena walikuwa na matatizo ya moyo, na Anna ni mmoja kati ya watu wengi walioorodheshwa kuwa wagonjwa wa Chernobyl.

Miongoni mwa wale walionururishwa sana ni wale wamalizaji walioziba kitendanishio kile kilichoharibika. Yasemekana kwamba maelfu ya watu waliosaidia kusafisha mahali hapo walikufa vifo vya mapema. Waokokaji wengi wana matatizo ya kineva na akili. Wengi wameshuka moyo, na wengi hujiua.

Angela ni mmojawapo waokokaji walioanza kupatwa na matatizo mabaya sana ya afya. Wakati wa msiba alikuwa akiishi Kiev, jiji kuu la Ukrainia, zaidi ya kilometa 80 kutoka Chernobyl. Lakini baadaye, alikuwa akiwapelekea vitu wale wamalizaji kwenye mahali pa kitendanishio. Svetlana, mwokokaji mwingine, aishiye Irpin’, karibu na Kiev, alishikwa na kansa na kufanyiwa upasuaji.

Kufikiria Yaliyotukia

Katika Aprili 1996, miaka kumi baada ya aksidenti hiyo mbaya, Mikhail Gorbachev alikiri: “Hatukuwa tayari kwa kisa kama hicho.” Kwa wakati uo huo, Rais Yeltsin wa Urusi alisema: “Mwanadamu hajapata msiba mkuu kama huu, wenye matokeo mabaya sana na yaliyo magumu sana kuondoa.”

Kwa kutokeza, toleo la Ujerumani la Scientific American lililinganisha matokeo ya baadaye ya msiba wa Chernobyl na kile ambacho kingetokea kwa vita ya kiasi ya nyukilia. Wengine wanakadiria kwamba idadi ya watu ambao wamekufa kwa sababu ya msiba huo ni karibu 30,000.

Kulingana na ripoti za habari mwaka uliopita, kufikia mwaka wa kumi wa ukumbusho wa aksidenti hiyo, bado kulikuwa na eneo fulani la kilometa 29 ambalo limezingira kiwanda hicho ambalo halifai kwa mwanadamu kuishi. Hata hivyo, ripoti ilionyesha kwamba “wakazi 647 wenye kuazimia wamerudi kisirisiri, wamehonga maofisa au wamerudi tu waziwazi katika eneo hilo.” Ripoti hiyo ikaonelea: “Hakuna mtu yeyote kamwe aishiye katika eneo la kilometa 10 kutoka kwa kiwanda hicho. Ukanda mwingine wa kilometa 20 kuzunguka ule wa kilometa 10 ndio una mamia machache ya watu ambao wamerudi.”

Uhakika Kati ya Hofu Ambayo Imeenea

Kwa maelfu mengi ya watu ambao walipata kuishi karibu na Chernobyl, maisha yamekuwa magumu na yangali ni magumu sana. Uchunguzi mmoja uliofanyiwa wale waliohamishwa ulionyesha kwamba asilimia 80 hawafurahii makao yao mapya. Wao wana huzuni, uchovu, wasiwasi, nao ni wenye kuchokozeka kwa urahisi na wapweke. Chernobyl haikuwa tu aksidenti ya kinyukilia—ilikuwa pigo kubwa sana la kijamii na kiakili. Haishangazi kwamba wengi hurejezea matukio kuwa ama kabla ya Chernobyl ama baada ya Chernobyl.

Kwa kutofautisha na wengine wengi, familia ya Rudnik hukabiliana na hali hiyo vizuri sana. Wao walianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova na tokeo likawa kwamba wao walisitawisha imani thabiti katika ahadi zinazopatikana katika Neno la Mungu kuhusu ulimwengu mpya wa Mungu wenye uadilifu. (Isaya 65:17-25; 2 Petro 3:13; Ufunuo 21:3, 4) Kisha, katika 1995, Victor na Anna walionyesha wakfu wao kwa Mungu kwa kubatizwa kwa maji. Baadaye binti yao Elena alibatizwa pia.

Victor aeleza: “Kujifunza Biblia kulituwezesha kupata kumjua Muumba wetu, Yehova Mungu, na makusudi yake kwa wanadamu duniani. Hatujashuka moyo tena, kwa kuwa twajua kwamba Ufalme wa Mungu ujapo, aksidenti mbaya kama hizo hazitatukia tena. Twatazamia wakati ambapo eneo lililo karibu na nyumba yetu karibu na Chernobyl litaboreka na kuwa paradiso ya ajabu.”

Angela na Svetlana, ambao pia wanaitibari katika ahadi za Mungu za ulimwengu mpya wenye uadilifu, pia wana mtazamo mwangavu japo magonjwa yao yaliyosababishwa na mnururisho. “Bila kumjua Muumba na makusudi yake,” Angela alisema, “maisha yangekuwa magumu. Lakini kuwa na uhusiano wa karibu na Yehova hunisaidia kuwa na mtazamo mzuri. Tamaa yangu ni kuendelea kumtumikia nikiwa mhubiri wa wakati wote wa Biblia.” Svetlana aliongezea: “Ndugu zangu na dada zangu wa Kikristo ni msaada mkubwa kwangu.”

Funzo la Biblia limefunulia watu kama hao kwamba aksidenti zinazosababishwa na “wakati na tukio lisilotazamiwa” huathiri watu mahali popote waishipo na kupata mtu yeyote yule. (Mhubiri 9:11, NW) Lakini wanafunzi wa Biblia pia wamejifunza kwamba hata matatizo yao yawe yenye kudhuru kama nini, hakuna madhara ambayo Yehova Mungu hawezi kusuluhisha, hakuna jeraha ambalo hawezi kuponya, na hakuna upotezo ambao hawezi kurudisha.

Wewe pia wawezaje kukuza uhakika katika ahadi za Mungu na hivyo kuwa na tumaini jangavu? Mwandikaji wa kitabu cha Biblia cha Mithali ajibu: “Ili matumaini yako uyaweke kwa BWANA, leo nimekujulisha wewe haya [“nimekupa ujuzi,” NW], naam, wewe.” (Mithali 22:19) Ndiyo, unahitaji kutwaa ujuzi kupitia funzo la kawaida la Biblia. Mashahidi wa Yehova katika eneo lenu watafurahi kukusaidia kufanya hivyo. Wao huandaa programu ya funzo la Biblia bila malipo kwa wakati unaokufaa na mahali panapokufaa.

[Blabu katika ukurasa wa 14]

“Mwanadamu hajapata msiba mkuu kama huu, wenye matokeo mabaya sana na yaliyo magumu sana kuondoa.”—Rais Yeltsin wa Urusi

[Blabu katika ukurasa wa 15]

Chernobyl haikuwa tu aksidenti ya kinyukilia—ilikuwa pigo kubwa sana la kijamii na kiakili

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Tass/Sipa Press

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki