Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 6/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Hudhurio la Kanisa Lapunguka
  • Wafanya-Biashara wa Mifupa
  • Saa za Mikononi Ambazo Hufanya Zaidi ya Kuonyesha Wakati
  • Kutoona Vizuri
  • Sala za Kupitia E-Mail
  • Pengo la Mapato Lapanuka
  • Mavuno Muhimu
  • Matatizo ya Bima ya Makasisi
  • Wanafunzi wa Singapore Washinda
  • Pesa Kutoka Mbinguni?
  • Wagonjwa Wadumishwa Ujoto Wakati wa Upasuaji
  • Hawafaidi Umma
  • Singapore—Kito cha Asia Kilichopoteza Mng’ao
    Amkeni!—1997
  • Je, Wahitaji Bima?
    Amkeni!—2001
  • Nimepata Shangwe Maishani kwa Kufanya Mapenzi ya Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 6/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Hudhurio la Kanisa Lapunguka

Inafikiriwa kwamba nchini Marekani, watu wanaopungua nusu kati ya wale waliolelewa katika makanisa mashuhuri ya Kiprotestanti kwa miaka 30 ambayo imepita hudumu katika dini yao wakiwa watu wazima. Watu wakadiriwao kuwa milioni 78 nchini Marekani ni Waprotestanti “kwa jina tu.” Hilo lamaanisha kwamba wao hujitambulisha kuwa Wabaptisti, Waepiskopali, Wamethodisti, Wapresbiteri, au washiriki wa kanisa jingine lolote la Kiprotestanti, lakini wao si washiriki wa kanisa la kwao wala hawahudhurii huko.

Wafanya-Biashara wa Mifupa

“Wakazi wenye kukata tamaa wa Kabul wanachimbua mifupa ya wanadamu ili kuuza itumike katika kutayarisha vyakula vya kuku,” laripoti shirika la habari la Reuters. Mfupa, ambao una kalsiamu, fosfati, na kabonati nyingi, hutumiwa kutayarisha vyakula vya wanyama, sabuni, na mafuta ya kupika. Kiunzi cha mfupa chenye uzani wa kilo sita chaweza kuwa na bei ya senti 50, ambazo ni pesa nyingi kwa kulinganisha katika jiji hilo lililo fukara kabisa. “Ni biashara nzuri,” asema Faizdeen mwenye umri wa miaka 14. “Ingawa mara nyingi mimi hukusanya mifupa ya wanyama, ni rahisi zaidi kupata mifupa ya wanadamu hapa.” Kwa kusikitisha, miaka mingi ya vita ya wenyewe kwa wenyewe katika Afghanistan imefanya bidhaa hiyo yenye madini mengi kupatikana kwa urahisi.

Saa za Mikononi Ambazo Hufanya Zaidi ya Kuonyesha Wakati

Katika Rio de Janeiro, wanafunzi 77 waliondoshwa baada ya kupatikana na saa za tarakimu zivaliwazo mkononi ambazo zilitumiwa kuiba mtihani wa kujiunga na chuo kikuu, laripoti gazeti O Globo. Saa hizo zilifanya sanasana kama kitafuta-namba za simu; lakini badala ya kupokea namba za simu, hizo ziliandaa majibu sahihi kwa maswali ya mtihani. Gazeti hilo lasema kwamba wanafunzi walilipa kufikia dola 14,000 kila mmoja kwa saa hizo. Kwa kupendeza, huko nyuma katika 1987, kamati ya kufanyiza mitihani katika Uingereza na Wales iliwaonya walimu watahadhari na wenye kuiba mtihani wanaotumia saa za mkono zenye kompyuta.

Kutoona Vizuri

Watu wengi wanaotazama kioo hukubali umbo wanaloona kwenye kioo—kuwa wao wenyewe. Lakini watu wanaougua tatizo fulani liitwalo body dysmorphic hutazama kioo na kuona umbo lililoharibika. “Ni hali ambayo watu hukazia akili sehemu fulani ya mwili, wakijidhania kuwa wana sura mbaya sana, wakati ambapo kwa hakika wao ni kawaida kabisa,” lasema The Province, la British Columbia, Kanada. Eric Hollander, ambaye ni daktari wa magonjwa ya akili wa New York, asema kwamba uchungu wa kasoro hizo zinazowaziwa waweza kuwa mkubwa sana hivi kwamba karibu asilimia 25 ya wale wanaougua tatizo hilo hujaribu kujiua.

Sala za Kupitia E-Mail

Wayahudi wenye kumhofu Mungu wamekusanyika kwa muda mrefu kwenye Ukuta wa Kilio katika Yerusalemu ili kulia na kutoa sala. Mara nyingi, waabudu huandika sala zao katika karatasi ndogo na kuziweka katika mianya ya ukuta huo. Lakini, sasa, Wayahudi kutoka ulimwenguni kote waweza kupeleka sala kwa E-Mail kupitia Internet. Kulingana na gazeti Computerworld, wafanyakazi wa Virtual Jerusalem Web, mahali pa mfumo wa Internet, hukusanya sala zao, huzichapisha, na kuzipeleka kwenye Ukuta wa Kilio, ambako, “kulingana na mapokeo ya Kiyahudi, Mungu aweza kuzitoa.”

Pengo la Mapato Lapanuka

Kulingana na ripoti ya majuzi ya Umoja wa Mataifa juu ya maendeleo ya kijamii, asilimia 83 ya mapato ya ulimwengu huendea asilimia 20 ya watu wote, ambao ndio matajiri zaidi. Yaani, jumla ya mali ya mabilionea 358 wa ulimwengu yatoshana na jumla ya mapato ya watu 2,400,000,000 walio maskini zaidi. Katika 1960 wastani wa mapato ya kila mwaka ya watu wanaoishi katika nchi zilizoendelea kiviwanda ulizidi ule watu wanaoishi katika nchi zinazoendelea kwa dola 5,700. Lakini, katika 1993 tofauti kati ya wastani wa mapato ya kila mtu katika mataifa yaliyoendelea kiviwanda na mataifa yanayoendelea ilikuwa imefikia dola 15,400.

Mavuno Muhimu

“Mashine zimefanya vizuri kuliko wanadamu katika mashamba ya ngano ya China kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo,” shirika la habari la Reuters liliripoti. Lilisema kwamba zaidi ya mashine 800,000 za kuvuna zilitumiwa. Ngano zililetwa kwa mara ya kwanza katika China muda fulani kabla ya mwaka wa 1300 K.W.K. nazo zimekuzwa kwa mafanikio katika mashamba madogo ya familia—hasa kwa kutumia mikono—tangu wakati huo. Lakini kwa sababu China ina asilimia 20 ya idadi ya watu ulimwenguni, lakini asilimia 7 tu ya eneo la kilimo, “maofisa wa kilimo wanajitahidi kuongeza utumiaji wa mashine katika mashamba ya taifa hilo,” yasema ripoti hiyo.

Matatizo ya Bima ya Makasisi

Makanisa mengi yana bima ya dhima ya kuyalinda dhidi ya madai ya madhara ya watu mmoja-mmoja. Lakini, makampuni fulani ya bima katika Marekani yameanza kuacha kuweka bima ya “mwenendo mbaya kingono” wa makasisi, laripoti National Underwriter. John Cleary, mshauri mkuu wa Church Mutual Insurance Company, alisema: “Dhima . . . nyingi hazitatia ndani mwenendo mbaya kingono kwa sababu huo ni tendo la kimakusudi, kwa kweli huo ni uhalifu.” Isitoshe, Donald Clark, Jr., wakili anayewakilisha vikundi kadhaa vya kidini, alisema kwamba mabadiliko hayo ya bima yadokeza kwamba “tisho liwezalo kutukia la hasara kubwa ya kifedha ya misiba ya aina hii ifanyizwayo na wanadamu labda ni baya zaidi kuliko matokeo ya misiba ya kiasili.” Tangu 1984, Church Mutual, mojawapo ya makampuni ya bima yaliyo mashuhuri nchini Marekani, limepata madai ya fidia kati ya 1,500 na 2,000 kutokana na mwenendo mbaya kingono, kulingana na Bwa. Cleary.

Wanafunzi wa Singapore Washinda

Zaidi ya wanafunzi nusu milioni kutoka nchi tofauti-tofauti 41 walifanya mtihani wa dakika 90 wa kujaribu kulinganisha viwango vya elimu ulimwenguni kote. Matokeo yakawa nini? Matokeo ya mtihani yadokeza kwamba Singapore inatokeza wanafunzi bora zaidi katika hisabati na sayansi. Nyuma ya Singapore, nchi nyinginezo kumi bora katika hisabati zilikuwa Korea Kusini, Japani, Hong Kong, Ubelgiji, Jamhuri ya Cheki, Jamhuri ya Slovakia, Uswisi, Uholanzi, na Slovenia. Matokeo bora zaidi ya sayansi yalitokezwa na nchi za Singapore, Jamhuri ya Cheki, Japani, Korea Kusini, Bulgaria, Uholanzi, Slovenia, Austria, Hungaria, na Uingereza. Taifa hilo lenye watu wapatao 3,400,000 tu lilishindaje ulimwengu wote? Labda ni kupitia bidii. Wanafunzi wa Singapore hutumia wastani wa muda wa saa 4.6 kwa siku wakifanya masomo ya nyumbani, huku wastani wa kimataifa ni muda wa saa 2 hadi 3, laripoti Asiaweek.

Pesa Kutoka Mbinguni?

Wakazi wa Overtown, mji maskini ulio katika ujirani wa Miami, Florida, walifurahi sana wakati pesa zilipoonekana kana kwamba zinaanguka kutoka mbinguni. Lakini ikawa kwamba kumbe si mana kutoka mbinguni, bali ni pesa za dola milioni 3.7 zilizoanguka barabarani chini wakati gari lenye ulinzi lilipoanguka kwenye barabara za juu, juu ya makazi hayo. Polisi wakadiria kwamba angalau watu 100 walikimbia kuzoa pesa hizo, lakini yaelekea kwamba kulikuwa na watu wengi zaidi. Kulingana na gazeti The New York Times, “Polisi wa Miami waliwaamuru watu waliozoa pesa hizo wazirudishe kwa muda wa saa 48 bila kushtakiwa wizi.” Lakini kufikia wakati kipindi hicho cha msamaha kilipotimia, ni watu watatu pekee waliokuwa wamerudisha pesa, na bado dola 500,000 zilikuwa zinakosekana. Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 18 aliripotiwa kwamba alisema: “Pesa hizo zilianguka katika nyua za watu. Ungewatarajia wafanye nini?”

Wagonjwa Wadumishwa Ujoto Wakati wa Upasuaji

Vyumba vya kufanyia upasuaji vinavyodumishwa vikiwa baridi ili kupunguza ukuzi wa bakteria zilizo hewani huzidisha mara tatu hatari ya kuambukizwa, wadai uchunguzi mmoja mpya uliofanywa na daktari mmoja wa nusukaputi Daniel Sessler wa Chuo Kikuu cha California. “Maambukizo hayasababishwi na bakteria zinazoelea hewani,” asema Dakt. Sessler, “bali husababishwa na kinga ya mgonjwa ambayo imepunguka dhidi ya bakteria zilizo kwenye ngozi au ndani ya mwili.” Vyumba baridi vya kufanyia upasuaji vyaweza kupunguza halijoto ya mwili wa mgonjwa kufikia digrii 16 Selsiasi chini ya sufuri. Na halijoto iliyo chini hupunguza mtiririko wa damu yenye oksijeni, ambayo ni muhimu katika kupigana na maambukizo. Sessler asema kwamba “chembe na vimeng’enya vinavyosaidia kinga havifanyi kazi vizuri mwili unapokuwa baridi.” Sessler na wenzake walipata kwamba kuongezea upungufu wa maambukizo, wagonjwa ambao halijoto za mwili wao zilidumu kuwa za kawaida walibaki hospitalini kwa muda mfupi zaidi kwa karibu siku tatu kuliko wale ambao hawakuwa na joto.

Hawafaidi Umma

Katika Japani, asilimia 49 ya watu waliohojiwa walisema kwamba maofisa wa serikali yao hufanya kazi kwa kujifaidi tu wenyewe, laripoti Mainichi Daily News. Ni asilimia 7 tu ya watu waliohojiwa walifikiri kwamba maofisa wa serikali hufanya kazi kwa “kufaidi umma,” na ni asilimia 3 pekee waliosema kwamba wanafanya kazi kwa kufaidi nchi. Ni Wajapani wachache sana waliofafanua maofisa wa serikali kuwa wenye bidii na wenye mioyo myeupe. Uchunguzi huo ulifanywa Desemba iliyopita, baada ya mwaka ambao kashfa kadhaa zilizohusisha watumishi wa serikali ya Japani wenye vyeo vya juu zaidi kufunuliwa.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki