Je, Watoto Wako Salama Wakiwa na Mbwa Wako?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AFRIKA KUSINI
SYDNEY mwenye umri wa miaka miwili alitembea-tembea karibu sana na mbwa mkali aina ya Rottweiler aliyekuwa amefungwa. Mbwa huyo alishambulia, akaharibu ngozi ya kichwa cha Sydney, na karibu ang’oe sikio lake la kushoto. Atahitaji kupandikizwa vipande vingi vya ngozi kwa miaka kadhaa.
Kwa sababu watu wengi zaidi wanatumia mbwa kwa ajili ya ulinzi, kunakuwa na ripoti zenye kuongezeka za mbwa kushambulia watoto. Mbwa fulani ambao wamejulikana kuwa huuma watoto ni Rottweiler, Doberman pinscher, bullmastiff, Alsatian (German shepherd), na bullterrier. Uchunguzi uliofanywa Afrika Kusini ulifunua kwamba katika visa vilivyochunguzwa, watoto wengi walioumwa walishambuliwa na mbwa waliowajua. Karibu nusu yao waliumwa na mbwa wa majirani, na robo waliumwa na mbwa wao wenyewe. Asilimia 10 tu ya mashambulizi hayo ilitoka kwa mbwa koko. Mara nyingi wahasiriwa, labda bila kujua, walikuwa wamemchokoza mbwa kwa njia fulani. Kwa wazi, mashambulizi mengi ya mbwa yaweza kuepukwa ikiwa wenye mbwa na wazazi wanachukua tahadhari za msingi.
Mzoeze Mtoto
Wazoezaji wengi wa mbwa hukazia kwamba watoto wadogo na mbwa hawapasi kuachwa peke yao bila usimamizi wa mtu mzima. Watoto wadogo hawajui jinsi ya kutendea wanyama. Ni lazima wafundishwe. Hivyo, watu wengi hutumia kanuni ya kwamba ikiwa mtu mzima hawezi kuwapo, mbwa na watoto wadogo watenganishwe. Mzoezaji Brian Kilcommons aonelea hivi katika kitabu Childproofing Your Dog: “Kutokana na masimulizi tusikiayo, matatizo mengi hutokea wakati mtu mzima hawi mwangalifu.”
Mara nyingi, wanyama huhitaji kukingwa dhidi ya mashambulizi ya watoto! Kilcommons aliitwa asaidie wakati mbwa wa familia moja alipotaka kumwuma mtoto. Baba aliyechanganyikiwa alieleza kwamba mwana wake mwenye umri wa miaka miwili na nusu alimkimbilia mbwa aliyekuwa amelala na kumpiga teke barabara. Mbwa huyo, bila shaka akiwa na maumivu, aliitikia kwa kutaka kumwuma mtoto huyo. Katika hali hii mbwa huyo alidhihirisha kujizuia kunakostahili pongezi kwa kutomwuma mtoto huyo. Mzoezaji huyo ashauri wazazi hivi: “Usiruhusu mtoto wako amfanyie mbwa jambo ambalo huwezi kumruhusu amfanyie mtoto mwingine.”
Mfunze mtoto wako jinsi ya kutendea wanyama kwa fadhili. Mfunze kutomchezea mbwa kamwe. Wazazi wahitaji kuwa chonjo kwa hatari yoyote iwezayo kutokea wakati watoto na mbwa wako pamoja. Ukiona kwamba mbwa anajaribu kwenda zake au kujificha kutoka kwa mtoto, mkomeshe mtoto huyo asimfuate mbwa. Mtoto huyo akimfuata na kumzingira mbwa, kinga yake pekee ni kubweka, kunguruma, au hata kuuma. Wazazi wapaswa kuadhibu kwa upatanifu, ili kwamba wote mbwa na mtoto wajue kwamba mzazi amaanisha asemacho.
Usimtende mbwa kama mtengwa. Wenzi wa ndoa wenye mbwa wanapopata mtoto wao wa kwanza, mwelekeo waweza kuwa kumpuuza mbwa na kumwondosha na kumweka nje kwenye ua. Ingawa ni jambo la busara kutahadhari, mzoezaji Richard Stubbs ashauri: “Mbwa hapasi kutendwa kama mtengwa. Badala ya hivyo, dumisha kawaida ya mbwa kadiri iwezekanavyo, na umpe kiasi kifaacho cha uangalifu.”
Fikiria jinsi mtoto wako atakavyoitikia mbwa asiowajua. Ikiwa amwona mtu asiyejulikana akimtembeza mbwa barabarani, atafanya nini? Atakimbia bila kujidhibiti na kumgusagusa mbwa huyo? Mfunze kutofanya hivyo. Ni lazima kwanza aombe ruhusa ya mwenye mbwa. Kisha, mwenye mbwa akikubali, aweza kumsogelea mbwa polepole, ili asimhofishe. Apaswa kujijulisha kwa kusimama mbali kidogo na kuzungumza na mbwa kwa utulivu. Mbwa mwenye urafiki atamkaribia mtoto wako. Ni vyema zaidi kutowakaribia mbwa wanaotembea barabarani wakiwa peke yao.—Ona sanduku “Ishara za Mwili za Mbwa,” ukurasa wa 22.
Mzoeze Mbwa
Msifu mbwa wako sikuzote na uwe na mwelekeo chanya. Adhabu au maneno makali hayaharakishi kujifunza bali hufanya kinyume cha hilo. Ni vizuri mbwa ajue wakati wa kuja anapoitwa na pia kutii amri za msingi kama vile “keti!” Mbwa ajifunza kujitiisha kwa bwana wake, na hilo humpa mwenye mbwa udhibiti mzuri zaidi katika hali iwezayo kuwa ngumu. Maneno sahili huwa na matokeo zaidi. Endelea kuyatumia yayo hayo. Mbwa wako afanyapo jambo lililotakiwa, mpe thawabu mara hiyo kwa kumsifu, kumpigapiga kwa kumwonyesha upendo, au kipande cha chakula kitamu. Ili kupata matokeo unayotaka kukazia, ni lazima umpe thawabu hiyo mara hiyo baada ya kitendo hicho. Jambo lifuatalo lililo la maana ni kurudia hadi mwenendo huo uimarike kabisa.
Ukipata mbwa, ama mdogo, ama mkubwa zaidi, huenda akahitaji msaada wa kuwazoea watoto. Watoto huitikia kwa njia tofauti na watu wazima. Wana kelele zaidi na ni wenye kutenda bila kujidhibiti nao huelekea kumkimbilia mbwa, jambo ambalo laweza kumwogopesha. Ni vema kumzoeza mnyama rafiki wako kuzoea mwenendo huo usiotabirika. Watoto wasipokuwapo, mzoeze mbwa kelele za ghafula. Fanya mazoezi hayo kama mchezo. Mtolee mbwa amri kwa sauti kuu, na umkimbilie. Kisha, mthawabishe mbwa wako mara hiyo. Ongeza kiwango cha mipaazo yako ya sauti hatua kwa hatua. Sikuzote malizia kwa kumpongeza na kumgusagusa mnyama rafiki wako. Muda si muda atafurahia mchezo huu.
Watoto wadogo hupenda kuwakumbatia mbwa, lakini wanapasa kufunzwa kutofanya hilo, kwa kuwa mbwa fulani huhisi wanatishwa kwa mguso wa karibu hivyo. Ikiwa watoto hukumbatia mbwa wako, waweza kumzoeza kukubali hilo. Mkumbatie mbwa wako kwa kipindi kifupi, kisha mpe kipande cha chakula kitamu na sifa. Hatua kwa hatua mkumbatie kwa muda mrefu zaidi. Mbwa wako akinguruma au akibweka, pata msaada kutoka kwa mzoezaji mwenye sifa za kustahili.
Mbwa Mkali
Mbwa wengine huelekea kuwa wakali kiasili na wanaweza kuwa hatari kwa washiriki wa nyumba yako. Mbwa wa kiume waelekea sana kudhihirisha tabia hizi za ukali.
Mbwa mwenye mwelekeo wa kutawala hapendi kushikwa, hasa kwenye sehemu nyetivu kama vile uso na shingoni. Ingawa hivyo, nyakati nyingine mbwa huyo aweza kukukaribia, kukudukua, au hata kuweka wayo wake pajani mwako, “akiomba” uangalifu wako. Huenda akalinda mahali anapoona kwamba ni pake nyumbani, na kutoruhusu hata washiriki wa familia kupaenda. Mara nyingi yeye hulinda vitu kama vile vichezeo na huenda akanguruma au kuacha kuvitafuna akikaribiwa anaposhughulika navyo.
Ili kuimarisha utawala wao, mbwa kama hao hupuuza kimakusudi amri wanazozijua. Wanaweza kuwapiga kumbo watoto au kutarajia kutoka mlangoni wakiwa wa kwanza. Wanaweza pia kuwa na mwelekeo wa kupanda watu. Hilo, asema Brian Kilcommons, ni “tendo la kutawala” na “halihusiani na ngono.” Yeye aonya kwamba hilo “sikuzote ni ishara ya kwamba mbwa huyo hufikiri ndiye mwenye mamlaka. Bila shaka wapaswa kutarajia matatizo.” Mbwa huyo pia aweza kusitawisha tabia ya kuchukua mkono wa bwana wake mdomoni ili kudai uangalifu.
Ishara hizi za ukali hazipasi kupuuzwa. Ukali huo hautakwisha tu; utaelekea kuongezeka, na watoto nyumbani huenda wakawa hatarini. Wazoezaji wengi hupendekeza kuhasi mbwa kama huyo, haidhuru jinsia yake, kwa kuwa hilo kwa kawaida husaidia kupunguza ukali.
Si jambo la hekima kumtolea mbwa mkali wito wa ushindani ili kuonyesha ni nani bwana-mkubwa. Kwa hakika, kumkabili kwa ukali na kumpa nidhamu kali, kwaweza kuwa hatari. Kwa njia za ujanja zaidi, mbwa huyo aweza kuonyeshwa ni nani aliye bwana-mkubwa.
Kila wakati mbwa mkali akukaribiapo akitaka uangalifu na umpe, unaimarisha itikadi yake kwamba yeye ndiye bwana-mkubwa. Kwa hiyo mbwa kama huyo adaipo uangalifu, mpuuze. Familia nzima yapaswa kushirikiana katika kufanya hivyo. Mbwa huyo atatatanishwa mwanzoni na aweza hata kubweka na kukutazama kwa njia ya kuvutia, lakini kinza kishawishi hicho. Anapoenda zake na labda kwenda kulala pembeni mwake, basi ndio wakati wa kumpa uangalifu mchache. Kwa njia hiyo mbwa wako ajifunza kwamba wewe ndiye kiongozi na ndiwe unayeamua wakati uangalifu utakapotolewa.
Michezo ya ukali kama vile vuta nikuvute na mieleka yaweza kutia moyo mielekeo ya kutawala ya mbwa na yapasa kuepukwa. Badala ya hivyo, cheza michezo isiyo ya ukali.
Ni vyema zaidi mbwa kutolala katika chumba cha kulala. Chumba cha kulala ni mahali pa pendeleo, na kulala hapo kwaweza kukuza hadhi anayofikiria kuwa nayo mbwa kushinda watoto nyumbani. Badala ya hivyo, weka kitanda cha mbwa jikoni au katika kibanda cha mbwa cha nje. Mara nyingi wenye mbwa huumwa kwanza na mbwa mkali katika vyumba vyao vya kulala.
Ikiwa mbwa wako haitikii jitihada zako, au ikiwa unapomzoeza, au wakati wowote, wahisi ukiwa hatarini, pata msaada kutoka kwa mzoezaji-mbwa stadi. Daktari wako wa mifugo aweza kukupendekezea mmoja. Zungumza naye kwanza kuhusu njia zake za kuzoeza, na uhakikishe kwamba unaridhika na uwezo wake kabla ya kumwajiri. Mzoezaji Richard Stubbs atahadharisha hivi: “Ingawa mbwa mkali aweza kuitikia vizuri mzoezaji mtaalamu, hilo si hakikisho kwamba atafanya hivyo na bwana-mkubwa wake.” Ni lazima mwenye mbwa ahakikishe kwamba anaweza kudumisha udhibiti juu ya mbwa wake katika hali za hatari.
Mbwa wachache wataendelea kuwa wakali hata baada ya mazoezi bora zaidi, na kubaki nao kwaweka familia hatarini. Baada ya kuwa umejaribu kadiri uwezavyo, huenda ukahisi ni vizuri kumwondosha mbwa huyo badala ya kujiingiza katika hatari ya kujeruhiwa. Ni jambo la busara kutafuta shauri kutoka kwa daktari wa mifugo au mzoezaji. Huenda ukaweza kupata makao mengine kwa mbwa wako, lakini bila shaka una wajibu wa kumweleza bwana-mkubwa mpya juu ya matatizo uliyopata na mbwa huyo.
Mzoezaji Peter Neville ashauri hivi: “Mbwa wenye mwelekeo wa kutawala wapasa kutendewa chini ya miongozo yenye uangalifu sana na kwa kuchunguza vizuri sana ni nani atakayeendelea kuwa hatarini na kwa kiasi gani. Ikiwa usalama hauwezi kuhakikishwa kwa mtu aliye hatarini zaidi katika familia, basi ni afadhali mbwa huyo apewe makao mapya kwa mtu mpya aliyeteuliwa kwa uangalifu, au auawe.”
Watoto waweza kujifunza na kunufaika kihisia-moyo kutokana na kuwa na mbwa wakiwa wanyama rafiki. Kwa kuandaa usimamizi ufaao, wazazi husaidia kuhakikisha kwamba kumbukumbu zote za watoto wao kuhusu wanyama rafiki wao ni nzuri.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Ishara za Mwili za Mbwa
Tabia ya kawaida ya mbwa mkali hufunua makusudio mabaya. Kwa kumfunza mtoto wako kutambua ishara hizi za mwili za mbwa, waweza kumsaidia kuepuka hali hatari.
● Mbwa mkali atajaribu kuonekana mkubwa zaidi. Huenda manyoya juu ya shingo yake yakasimama. Huenda mbwa huyo akanguruma au kubweka huku mkia wake ukinyooka kuelekea juu. Mkia ukitikiswa kwa mtikiso thabiti, wa haraka na wenye msisimko, hiyo si ishara ya urafiki. Mbwa huyo apaswa kuachwa.
● Huenda mbwa mwenye hofu akajikunyata akiinamisha kichwa chake na masikio na mkia wake ukiwa chini au katikati ya miguu yake. Mbwa huyu akikaribiwa, aweza kuwa mkali kwa sababu ya hofu. Mwache.
● Mbwa aliyetulia husimama kichwa chake kikiwa si juu sana wala si chini sana, mdomo ukiwa wazi, na mkia chini kidogo ya usawa wa mgongo, lakini usioning’inia chini. Kutikisa mkia ni ishara ya urafiki. Kwa kawaida ni sawa kufanya urafiki na mbwa huyu.
(Kutoka katika kitabu Childproofing Your Dog, kilichoandikwa na Brian Kilcommons na Sarah Wilson.)
[Sanduku katika ukurasa wa 23]
Usalama wa Mbwa
1. Wasimamie watoto wadogo na mbwa.
2. Mfunze mtoto wako kutomchezea mbwa.
3. Omba ruhusa ya mwenye mbwa kabla ya kumgusagusa mbwa aiyejulikana.
4. Mzoeze mbwa wako kutii amri za msingi.
5. Mzoeshe mbwa wako kukumbatiwa.
6. Epuka michezo ya ukali.