Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 7/22 kur. 10-13
  • Internet—Kwa Nini Utahadhari?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Internet—Kwa Nini Utahadhari?
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Jihadhari na Wale Wawindao Watoto!
  • Uhitaji wa Mwongozo wa Mzazi
  • Kudumisha Maoni Yaliyosawazika
  • Je, Kweli Ni Hatari Kuchumbiana Kwenye Intaneti?
    Amkeni!—2005
  • Intaneti Kutumia kwa Hekima Kifaa cha Ulimwenguni Pote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2011
  • Jinsi ya Kuepuka Hatari za Intaneti
    Amkeni!—2004
  • Je, kwa Kweli Wahitaji Internet?
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 7/22 kur. 10-13

Internet—Kwa Nini Utahadhari?

KWA hakika Internet ina uwezo wa kutumiwa kielimu na katika uwasiliano wa siku kwa siku. Hata hivyo, kando na tekinolojia yake ya hali ya juu ionekanayo kuwa yenye kuvutia, Internet inakumbwa na baadhi ya matatizo yaleyale ambayo yamekumba kwa muda mrefu televisheni, simu, magazeti ya habari, na maktaba. Hivyo, swali lifaalo laweza kuwa, Je, yaliyomo katika Internet yafaa familia yangu na mimi?

Ripoti nyingi zimeeleza juu ya kupatikana kwa habari za kiponografia kwenye Internet. Ingawa hivyo, je, hiyo yadokeza kwamba Internet ni hifadhi iliyojaa tu waachamaadili waliopotoka kingono? Wengine hupinga kwamba kusema hivyo ni kutia chumvi kupita kiasi. Wanasababu kwamba ni lazima mtu afanye jitihada halisi na ya makusudi ili kupata habari mbaya.

Ni kweli kwamba ni lazima mtu afanye jitihada ya kunuia ili kupata habari isiyofaa, lakini wengine wanabisha kwamba yaweza kupatikana kwa urahisi sana kwenye Internet kuliko penginepo. Kwa kubofya vibonyezo vichache, mtumizi aweza kupata habari yenye kuamsha ashiki, kama vile picha dhahiri za kingono kutia ndani kisehemu cha habari iliyo na sauti na visehemu vya vidio.

Suala la wingi wa ponografia ipatikanayo kwenye Internet ni habari inayojadiliwa sana kwa wakati huu. Watu fulani wahisi kwamba ripoti zinazodokeza tatizo lililoenea sana huenda zimetiwa chumvi. Hata hivyo, ikiwa ulipata kujua kwamba hakukuwa na nyoka 100 wenye sumu katika bustani yako, bali wachache tu, je, ungekosa kuhangaikia sana usalama wa familia yako? Wale wawezao kufikia Internet watakuwa wenye hekima kutahadhari.

Jihadhari na Wale Wawindao Watoto!

Habari za hivi majuzi zimeonyesha kwamba watu fulani wavutiwao na watoto kingono wamejiunga na mazungumzo ya mahali pa kupigia gumzo kwenye mfumo wa kompyuta pamoja na vijana. Wakijifanya kuwa watoto wachanga, watu wazima hawa kwa werevu wamefaulu kupata majina na anwani kutoka kwa vijana wasioshuku kitu.

Shirika The National Center for Missing and Exploited Children (NCMEC) limethibitisha baadhi ya utendaji huu. Kwa kielelezo, katika 1996, polisi walipata wasichana wawili wa South Carolina, Marekani, wenye umri wa miaka 13 na 15 ambao walikuwa wamepotea kwa juma moja. Walikuwa wamekwenda kwenye jimbo jingine na mwanamume mwenye umri wa miaka 18 waliyekutana naye kwenye Internet. Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 35 alishtakiwa kumshawishi mvulana mwenye umri wa miaka 14 wafanye ngono isiyo halali wakati wazazi wake hawakuwapo nyumbani. Visa vyote viwili vilianza kwa mazungumzo kwenye mahali pa kupigia gumzo kwenye Internet. Mtu mzima mwingine, katika 1995, alikutana na mvulana mwenye umri wa miaka 15 kwenye mfumo wa kompyuta na kwenda kwa ujasiri hadi kwenye shule yake ili kukutana naye. Na zaidi mtu mzima mwingine alikiri kuwa alifanya ngono na msichana mwenye umri wa miaka 14. Msichana huyo alikuwa ametumia kompyuta ya baba yake ili kuwasiliana na matineja kupitia mahali pa kupata habari katika mfumo wa kompyuta. Yeye pia alikutana na mtu mzima huyo kupitia mfumo wa kompyuta. Vijana wote hawa walikuwa wameshawishiwa hatimaye kufunua utambulisho wao halisi.

Uhitaji wa Mwongozo wa Mzazi

Ingawa visa kama vilivyotajwa hapo juu havitokei mara nyingi kwa kulinganishwa, hata hivyo ni lazima wazazi wachunguze jambo hili kwa uangalifu. Ni vifaa gani vipatikanavyo kwa wazazi ili kuwakinga watoto wao dhidi ya kuwa shabaha za uhalifu na kutumiwa vibaya?

Makampuni yanaanza kuandaa vifaa kuanzia mifumo ya uainishaji kama vile ya sinema, hadi programu za utambuaji-neno ambazo huchuja yaliyomo yasiyofaa, hadi mifumo ya kuthibitisha umri. Mifikio fulani huzuia habari hata kabla ifikie kompyuta ya familia. Hata hivyo, mingi ya mifikio hii si yenye kutegemeka kabisa, na yaweza kushindwa kwa njia kadhaa. Kumbuka kwamba muundo wa awali wa Internet ulikuwa kuufanyiza ukinze vizuizi, kwa hiyo ni vigumu kufanya uchujaji.

Katika mahojiano na Amkeni!, sajini wa polisi ambaye husimamia kikundi cha uchunguzi wa utumiaji vibaya wa watoto katika California alitoa shauri hili: “Hakuna kibadala cha mwongozo wa mzazi. Mimi mwenyewe nina mtoto mwenye umri wa miaka 12. Mke wangu nami tumemruhusu atumie Internet, lakini twafanya hivyo tukiwa familia na twaweka miongozo yenye uangalifu kwa muda wa wakati utumiwao.” Baba huyu anatahadhari hasa kuhusu mahali pa kupigia gumzo, naye huwekea vizuizi imara utumizi wa mahali hapo. Yeye aongeza hivi: “Kompyuta ya kibinafsi haiko katika chumba cha mwana wangu bali ipo mahali palipo wazi nyumbani.”

Wazazi wahitaji kuwa na upendezi halisi katika kuamua watawaruhusu watoto wao watumieje Internet, ikiwa wataitumia. Ni tahadhari gani zenye kutumika na zifaazo zipasazo kufikiriwa?

Mwandishi David Plotnikoff wa gazeti San Jose Mercury News atoa vidokezi vyenye msaada kwa wazazi wanaoamua kuwa na Internet nyumbani.

• Wanayojionea vijana wako kwenye Internet yatakuwa yenye kufaa zaidi unapoitumia pamoja nao, wakijifunza ubora wa uamuzi na mwongozo wako. Bila mwelekezo wako, yeye aonya, “habari yote iliyo katika Internet itakuwa kama maji bila gilasi.” Kanuni unazosisitiza ni “mpanuo wa mambo ya akili ya kawaida ambayo ulifundisha watoto wako muda mrefu uliopita.” Kielelezo ni kanuni zako kuhusu kutozungumza na watu wasiojulikana.

• Internet ni mahali pa umma na hapapasi kutumiwa kama huduma ya kulea mtoto. “Kwa vyovyote, hungemwacha peke yake mtoto mwenye umri wa miaka 10 katika jiji kubwa na kumwambia aende afurahie kwa saa chache, sivyo?”

• Jifunze kutambua tofauti kati ya mahali pa Internet pa michezo au pa kupigia gumzo na mahali pa kupata msaada wa mgawo wa masomo ya nyumbani.

Kijitabu cha NCMEC kiitwacho Child Safety on the Information Highway hutoa miongozo kwa vijana:

• Usifunue habari yako ya kibinafsi kama vile anwani yako, nambari ya simu ya nyumbani kwenu, au jina na mahali ilipo shule yenu. Usipeleke picha bila ruhusa ya wazazi wako.

• Wajulishe wazazi wako mara moja ukipata habari inayokufanya uhisi kutostarehe. Usijibu kamwe ujumbe wowote usio na fadhili au wenye ukali. Waeleze wazazi wako mara moja ili wawasiliane na huduma za mifumo ya kompyuta.

• Shirikiana na wazazi wako katika kuweka kanuni za kutumia Internet, kutia ndani wakati wa siku na urefu wa kipindi cha wakati utumiwao kwenye Internet na mahali pafaapo kufikia; shikamana na maamuzi yao.

Kumbuka kwamba tahadhari zina manufaa kwa watu wazima pia. Watu wazima fulani tayari wamenaswa katika mahusiano yasiyotakiwa na matatizo mabaya kwa sababu ya kutokuwa waangalifu. Ile hali ya kutofahamika ya mahali pa kupigia gumzo—ule ukosefu wa kutazamana jicho kwa jicho na usiri wa majina bandia, umefanya watu fulani wakose kujali na kufanyiza hisi isiyo ya kweli ya usalama. Watu wazima, jihadharini!

Kudumisha Maoni Yaliyosawazika

Baadhi ya habari na huduma nyingi zipatikanazo kwenye Internet zina thamani ya kielimu na zaweza kuwa na kusudi lenye manufaa. Idadi zinazoongezeka za mashirika zinahifadhi hati zake za ndani kwenye mifumo yake ya ndani. Uwasilianaji wa Internet ambapo washiriki wanaweza kuonana na kusikiana ambao unazuka unatokeza uwezekano wa kubadili kabisa namna za usafiri na mikutano ya shughuli fulani. Makampuni hutumia Internet ili kusambaza programu zake za kompyuta, hivyo yakipunguza gharama. Huduma nyingi ambazo wakati huu hutumia wafanyakazi kushughulikia mambo ya kibiashara, kama vile kusafiri na makampuni ya kunadi hisa, yaelekea yataathiriwa kwa kuwa watumizi wa Internet wana uwezo wa kushughulikia baadhi ya au mipango yao yote. Ndiyo, athari ya Internet imekuwa kubwa, na yamkini itaendelea kuwa njia ya maana ya kushiriki habari, kufanya shughuli, na kuwasiliana.

Kama vifaa vingi, Internet ina matumizi yenye manufaa. Lakini, kuna uwezekano itumiwe vibaya. Wengine waweza kuchagua kuvinjari zaidi sehemu zifaazo za Internet, huku wengine wakichagua kutofanya hivyo. Mkristo hana mamlaka ya kuhukumu uamuzi wa mtu mwingine juu ya mambo ya kibinafsi.—Waroma 14:4.

Kutumia Internet kwaweza kuwa kama kusafiri kwenye nchi ya kigeni, kukiwa na mambo mengi ya kuona na kusikia. Usafiri wakuhitaji uonyeshe adabu na utahadhari kwa busara. Hali hiyohiyo yahitajiwa ukiamua kuingia kwenye Internet—njia kuu bora ya habari.

[Blabu katika ukurasa wa 12]

“Kompyuta ya kibinafsi haiko katika chumba cha mwana wangu bali ipo mahali palipo wazi nyumbani”

[Blabu katika ukurasa wa 13]

Internet ni mahali pa umma na hapapasi kutumiwa kama huduma ya kulea mtoto

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

Uhitaji wa Uungwana na Hadhari

Uungwana

Jifunze kanuni za uungwana na za uhusiano mwema. Makampuni mengi ya kuandaa huduma za Internet huchapisha miongozo yenye ufikirio na inayokubalika ya mwenendo. Watumizi wengine watathamini kutambua kwako miongozo hiyo na kuifuata, na vilevile kuonyesha adabu.

Hadhari

Vikundi fulani vya mazungumzo hujadili mambo ya kidini au ya kubishaniwa. Uwe mwangalifu kuhusu kupeleka maelezo yako kwa mazungumzo kama hayo; yaelekea kwamba anwani yako ya E-mail itatangazwa kwa wote katika kikundi hicho. Hilo mara nyingi hutokeza mawasiliano yenye kuchukua wakati mwingi na yasiyotakiwa. Kwa hakika, kuna vikundi fulani vya habari ambavyo si vizuri kusoma, achilia mbali kuwasiliana navyo.

Namna gani kufanyiza kikundi cha mazungumzo, au kikundi cha habari, kwa Wakristo wenzi? Hilo laweza kutokeza matatizo makubwa zaidi na hatari kuliko ilivyotarajiwa mwanzoni. Kwa kielelezo, watu mmoja-mmoja wasio na nia nzuri wamejulikana kujiwakilisha isivyofaa kwenye Internet. Kwa wakati huu, Internet yenyewe haiwezeshi watu mmoja-mmoja wanaotokezea kwake wathibitishe utambulisho wao halisi. Isitoshe, kikundi kama hicho chaweza kulinganishwa kwa njia fulani na kikusanyiko kikubwa cha kijamii, kikihitaji wakati na uwezo wa mwenyeji wa hicho kikundi kuandaa usimamizi unaohitajiwa na wenye daraka.—Linganisha Mithali 27:12.

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

Wakati Wako Una Thamani Kadiri Gani?

Katika karne hii ya 20, maisha yameendelea kuwa tata hatua kwa hatua. Uvumbuzi ambao umewanufaisha watu fulani mara nyingi umekuja kuwa vipoteza-wakati kwa wengi. Na zaidi, programu za televisheni za ukosefu wa adili na zenye jeuri, vitabu vya ponografia, mirekodio ya muziki uliopotoka, na mambo kama hayo ni vielelezo vya tekinolojia ambazo zimetumiwa vibaya. Hazitumii wakati wenye thamani tu bali pia zinaharibu hali ya kiroho ya watu.

Bila shaka, mambo ya kutangulizwa kwanza na Mkristo ni yale ya kiroho, kama vile kusoma Biblia kila siku na kufahamu vizuri kweli za Kimaandiko zenye thamani sana zinazozungumziwa katika magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! na vichapo vinginevyo vya Watch Tower Society. Manufaa zidumuzo milele huja, si kutokana na kupitia-pitia Internet, bali kutokana na kutumia wakati wako ili kutwaa ujuzi wa Mungu wa pekee wa kweli na wa Mwana wake, Yesu Kristo, na kuutumia kwa bidii.—Yohana 17:3; ona pia Waefeso 5:15-17.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki