Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 8/8 kur. 12-14
  • Chakula cha Wote—Je, ni Ndoto Tu?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Chakula cha Wote—Je, ni Ndoto Tu?
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Usalama wa Chakula”—Kwa Nini Haupatikani?
  • ‘Twahitaji Hatua Ichukuliwe, Si Mikutano Mingi Zaidi’
  • Ni Nani Atakayelisha Wenye Njaa?
  • Biblia Inasema Nini Kuhusu Upungufu wa Chakula Uliopo Duniani Leo?
    Habari Zaidi
  • Utapiamlo Utakoma Karibuni!
    Amkeni!—2003
  • Ugumu wa Kulisha Majiji
    Amkeni!—2005
  • Kujaribu Kulisha Watu Bilioni Moja
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 8/8 kur. 12-14

Chakula cha Wote—Je, ni Ndoto Tu?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA

“KILA mwanamume, mwanamke na mtoto ana haki ya kutokuwa na njaa na utapiamlo” ukatangaza Mkutano wa Chakula Ulimwenguni ambao ulidhaminiwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) huko nyuma katika mwaka wa 1974. Mwito ulitolewa wakati huo wa kumaliza kabisa njaa ulimwenguni “kwa mwongo mmoja tu.”

Lakini, wawakilishi wa mataifa 173 walipokutana katika makao makuu ya FAO jijini Roma mwisho-mwisho wa mwaka uliopita kwenye Mkutano wa Chakula Ulimwenguni wa siku tano, wao walikusudia kuuliza: “Kwa nini hatukufaulu?” Kuandaa chakula kwa wote hakujashindwa tu, bali sasa, zaidi ya miongo miwili baadaye, hali imekuwa mbaya zaidi.

Masuala muhimu ya chakula, idadi ya watu, na umaskini ni dharura. Kama ilivyotambuliwa na hati iliyotolewa katika mkutano huo, matatizo haya yasiposuluhishwa, “uthabiti wa kijamii wa nchi nyingi na maeneo mengi huenda ukaathiriwa vibaya, labda hata ukiathiri amani ya ulimwengu.” Mchunguzi mmoja alikuwa wazi zaidi: “Tutapatwa na uharibifu wa ustaarabu na tamaduni za kitaifa.”

Kulingana na Mkurugenzi-Mkuu wa FAO Jacques Diouf, “zaidi ya watu milioni 800 leo hawana chakula cha kutosha; miongoni mwao mna watoto milioni 200.” Inakadiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2025, idadi ya sasa ya ulimwengu ya bilioni 5.8 itakuwa imeongezeka hadi bilioni 8.3, ongezeko kubwa likitokea katika nchi zinazoendelea. Diouf alalamika: “Idadi yenyewe ya wanaume, wanawake na watoto ambao hawana haki ya msingi ya kuishi na hadhi ni kubwa sana. Vilio vya wenye njaa huandamana na msononeko wenye ukimya wa uharibifu wa udongo, ufyekaji wa misitu na kumalizwa kwa samaki katika sehemu za uvuvi.”

Ni suluhisho jipi linalopendekezwa? Diouf asema kwamba suluhisho ni kuchukua “hatua yenye moyo mkuu,” ya kuandaa “usalama wa chakula” kwa nchi zenye uhaba wa chakula na vilevile stadi, vitega-uchumi, na tekinolojia ambazo zitaziwezesha kujilisha.

“Usalama wa Chakula”—Kwa Nini Haupatikani?

Kulingana na hati iliyotolewa na mkutano huo, “usalama wa chakula huwapo wakati tu watu wote, katika nyakati zote, wawezapo kupata kihalisi na kiuchumi chakula salama chenye lishe na cha kutosha ili kutimiza mahitaji yao ya lishe na kuweza kwao kuchagua vyakula wavipendavyo ili wawe na maisha yenye utendaji na afya nzuri.”

Jinsi usalama wa chakula uwezavyo kuhatarishwa ulionyeshwa na tatizo la wakimbizi nchini Zaire. Ingawa wakimbizi Warwanda milioni moja walikuwa wakifa njaa, mashirika ya UM yalikuwa na chakula cha kutosha cha kuwalisha. Lakini mipango ya usafirishaji na ugawanyaji ilihitaji idhini za mamlaka za kisiasa na ushirikiano wa wenye mamlaka za huko — au wenye kuongoza vita ikiwa kambi za wakimbizi zilikuwa chini yao. Dharura nchini Zaire yaonyesha kwa mara nyingine tena jinsi ilivyo vigumu kwa jumuiya ya kimataifa kuwalisha wenye njaa, hata wakati ambapo kuna chakula. Mchunguzi mmoja alisema: “Ni lazima mashirika mengi yaombwe mashauri na kubembelezwa kabla ya jambo lolote kufanyika.”

Kama ilivyotajwa na hati ya Wizara ya Kilimo ya Marekani, usalama wa chakula waweza kudhoofishwa kabisa na visababishi kadhaa vya msingi. Mbali na misiba ya kiasili, visababishi hivyo vyatia ndani vita na mzozo wa kindani, sera za kitaifa zisizofaa, utafiti na tekinolojia duni, kudhoofika kwa mazingira, umaskini, ongezeko la watu, ukosefu wa usawa wa kijinsia, na afya mbaya.

Kumekuwa na matimizo kadhaa. Tangu miaka ya 1970, wastani wa nishati ya lishe, ambao ni wonyesho wa chakula kinachotumiwa, umepanda kutoka kalori 2,140 hadi 2,520 kwa kila mtu kila siku katika mataifa yanayoendelea. Lakini kulingana na FAO, kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu kwa mabilioni kadhaa kufikia mwaka wa 2030, “kudumisha tu viwango vya sasa vya kupatikana kwa chakula kutahitaji kuongeza haraka sana mazao ili kuongeza ugavi wa chakula kwa zaidi ya asilimia 75 bila kuharibu mali ya asili ambazo sisi sote hutegemea.” Kwa hiyo jukumu la kuandaa chakula kwa watu wenye kufa njaa ni gumu sana.

‘Twahitaji Hatua Ichukuliwe, Si Mikutano Mingi Zaidi’

Uchambuzi mwingi ulitolewa dhidi ya mambo yaliyojadiliwa katika Mkutano wa Chakula Ulimwenguni na wajibu ambao mkutano huo ulijitwisha. Mwakilishi mmoja wa Amerika ya Latini alishutumu “uhafifu” wa azimio la kupunguza idadi ya watu wenye utapiamlo ili kuwa nusu tu kuwa “la kuaibisha.” Mataifa 15 yalionyesha tofauti katika kuelewa mapendekezo yaliyokubaliwa na mkutano huo. Hata kufikia hatua ya kuandika azimio hilo dogo na mpango wa hatua ya kuchukuliwa, likasema gazeti la Italia La Repubblica, “ilichukua miaka miwili ya mabishano na majadiliano. Kila neno, kila koma lilichunguzwa kwa uangalifu ili migawanyiko iliyokuwapo . . . isitokee tena.”

Wengi waliosaidia kutayarisha hati za mkutano hawakufurahia matokeo hayo. “Tunatilia shaka sana ikiwa mapendekezo mazuri yaliyotangazwa yatatimizwa,” akasema mwingine. Suala kuu lilikuwa kama kupata chakula kwapasa kufafanuliwa kuwa “haki inayotambuliwa kimataifa,” kwa kuwa “haki” inaweza kutetewa katika mahakama za kisheria. Mkanada mmoja alieleza: “Mataifa tajiri yaliogopa kwamba yangelazimishwa kutoa msaada. Hiyo ndiyo sababu yalisisitiza kwamba uzito wa azimio hilo upunguzwe.”

Kwa sababu ya mazungumzo yasiyo na mwisho katika mikutano yenye kudhaminiwa na UM, waziri wa serikali moja ya Ulaya alisema: “Baada ya kusuluhisha mambo mengi katika mkutano wa Cairo [juu ya idadi ya watu na maendeleo, uliofanywa mnamo 1994], tumejikuta tukiyarudia mambo yaleyale katika kila mkutano.” Yeye alipendekeza: “Kutekeleza mipango ya hatua za kuchukuliwa kwa manufaa ya wanadamu wenzetu ni lazima kuwe jambo kuu la ajenda zetu, bali si Mikutano mingi zaidi.”

Wachunguzi walisema pia kwamba hata kuhudhuria tu mkutano huo ni gharama kubwa sana kwa mataifa fulani ambayo karibu hayawezi kuigharimia. Taifa moja dogo la Afrika lilipeleka wajumbe 14 kwa kuongezea mawaziri 2, wote hao wakikaa Roma kwa zaidi ya majuma mawili. Gazeti la habari la Italia Corriere della Sera liliripoti kwamba mke wa rais mmoja wa Afrika, ambaye katika nchi yake mapato ya wastani ya kila mtu hayapiti dola 3,300 kila mwaka, alitumia dola 23,000 kwa kununua vitu kwa fujo katika eneo la mitindo ya hali ya juu la Roma.

Je, kuna sababu ya kuamini kwamba Mpango wa Hatua ya Kuchukuliwa uliokubaliwa kwenye mkutano utafanikiwa? Mwandishi mmoja wa habari ajibu: “Twaweza tu kutumaini kwamba serikali zitauchukua kwa uzito na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba mapendekezo hayo yatatekelezwa. Je, zitafanya hivyo? . . . Historia inatilia shaka.” Msemaji huyohuyo alitaja jambo lenye kuvunja moyo kwamba japo mataifa yalikubali katika Mkutano wa Dunia wa 1992 wa Rio de Janeiro kuongeza michango kwa msaada wa maendeleo kufikia asilimia 0.7 ya mapato yote ya serikali, “ni nchi chache tu zimetimiza malengo hayo.”

Ni Nani Atakayelisha Wenye Njaa?

Historia imeonyesha vema kwamba japo makusudio yote mazuri ya wanadamu, “njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” (Yeremia 10:23) Basi haielekei kwamba wakiwa peke yao wanadamu wanaweza kuandaa chakula cha kuwatosha wote. Pupa, usimamizi mbaya, na kujiona kuwa bora kumeongoza wanadamu kwenye hatari. Mkurugenzi-Mkuu wa FAO, Diouf, alisema: “Kinachohitajika katika uchanganuzi wa mwisho ni mabadiliko makubwa ya mioyo, akili, na nia.”

Hilo ni jambo ambalo ni Ufalme wa Mungu pekee uwezalo kutimiza. Kwa hakika, karne nyingi zilizopita Yehova alitabiri hivi kuhusu watu wake: “Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” — Yeremia 31:33.

Yehova Mungu alipotayarisha makao ya bustani ya awali ya mwanadamu, alimwandalia mwanadamu “kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu” kuwa chakula. (Mwanzo 1:29) Huo ulikuwa uandalizi mwingi, wenye lishe, na upatikanao kwa urahisi. Ni hayo tu ambayo mwanadamu alihitaji ili kuridhisha mahitaji yake ya chakula.

Kusudi la Mungu halikubadilika. (Isaya 55:10, 11) Zamani za kale alitoa uhakikisho wa kwamba ni yeye pekee atakayeridhisha kila uhitaji wa mwanadamu kupitia Ufalme wake unaotawalwa na Kristo, akiandaa chakula cha kuwatosha wote, akiondoa umaskini, akidhibiti misiba ya kiasili, na kuondoa mapambano. (Zaburi 46:8, 9; Isaya 11:9; linganisha Marko 4:37-41; 6:37-44.) Wakati huo “hakika dunia yenyewe itatoa mazao yake; Mungu, Mungu wetu, atatubariki.” “Kutakuja kuwapo nafaka nyingi duniani; juu ya milima zitafurika.”—Zaburi 67:6; 72:16, NW.

[Credit Line katika ukurasa wa 12]

Dorothea Lange, FSA Collection, Library of Congress

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki