Via Egnatia—Barabara Kuu Iliyosaidia Kuleta Mpanuko
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UGIRIKI
KATIKA mwaka wa 50 W.K., kikundi cha wamishonari Wakristo kilikwenda kwa mara ya kwanza Ulaya. Walikuwa wamekuja kwa mwaliko uliopokewa na mtume Paulo katika maono: “Vuka uingie Makedonia utusaidie.” (Matendo 16:9) Ujumbe juu ya Yesu Kristo ambao Paulo na waandamani wake walileta ulikuwa na athari kubwa sana Ulaya.
Msaada mkubwa sana katika kueneza Ukristo katika Makedonia ulikuwa Via Egnatia, barabara kuu ya Roma iliyotengenezwa. Baada ya kutua kwenye bandari ya Neapolisi (sasa Kaválla, Ugiriki) mwisho wa kaskazini mwa Bahari ya Aegean, wamishonari hao kwa wazi walisafiri kwenye barabara kuu hiyo hadi Filipi, jiji kuu la wilaya ya Makedonia. Barabara hiyo iliendelea hadi Amfipolisi, Apolonia, na Thesalonike, zilizokuwa sehemu ambazo Paulo angetua pamoja na waandamani wake.—Matendo 16:11–17:1.
Sehemu za hii barabara kuu ya kale bado zipo hadi wakati huu na bado hutumiwa kila siku. Sasa kuna mipango ya kujenga barabara kuu mpya ambayo itafuata njia ya barabara ya kale na kuwa na jina lilo hilo.
Ni nani aliyejenga barabara kuu ya awali? Ilijengwa lini, na kwa kusudi gani?
Kwa Nini Ilihitajika
Roma ilipozidi kupata ushindi kuelekea mashariki, Makedonia ilikuja kuwa mkoa wa Roma katika mwaka wa 146 K.W.K. Hata hivyo, kupatikana kwa sehemu hiyo kulitokeza uhitaji mpya kwa milki hiyo—uwezo wa kupanga vikosi vya kijeshi haraka katika maeneo mapya. Ile Via Appia, au Barabara ya Appia, kwenye Peninsula ya Italia tayari ilikuwa imeunganisha Roma na Pwani ya Adriatiki ya kusini-mashariki. Lakini sasa milki hiyo ilihitaji barabara kuu kama hiyo kwenye Peninsula ya Balkani, kwa hiyo Via Egnatia ikafikiriwa. Ilipewa jina la mhandisi mkuu wa huo mradi, ambaye alikuwa prokonso wa Roma Gnaius Egnatius.
Kuanzia mji wa bandari wa Dirakiamu katika mkoa wa Ilirikamu (Durres, Albania), Via Egnatia iliendelea hadi jiji la kale la Bizantiamu (Istanbul, Uturuki), ikiwa na urefu wa kilometa 800. Ujenzi ulianza katika mwaka wa 145 K.W.K. na kuchukua miaka 44 kumalizika. Kama ilivyokusudiwa, upesi Via Egnatia ikaja kuwa msaada mkubwa sana kwa sera ya Roma ya upanuzi katika Mashariki.
Sehemu Ngumu Sana za Kujengea Barabara
Hata hivyo, sehemu hiyo ilifanya iwe vigumu kujenga hiyo barabara kuu. Kwa mfano, katika hatua ya awali barabara hiyo yakutana na Ziwa Ohrid, ambalo barabara hiyo hulipitia kaskazini. Kisha, baada ya kuzunguka-zunguka ikipitia vijia vya milimani na kuelekea upande wa mashariki kuvuka sehemu ngumu yenye mabonde-mabonde kama makombe, milima isiyo na misitu, na mabonde yaliyo na maziwa kwa sehemu, barabara hiyo hatimaye yafikia uwanda wa kati wa Makedonia.
Hiyo barabara kuu ikaribiapo jiji la Thesalonike, hufuata eneo la mashambani lililo tambarare na wazi. Lakini sehemu ya upande wa mashariki wa jiji ina milima-milima. Ikijipinda kupitia milima hii, Via Egnatia yateremka kuingia katika bonde lililo na maziwa yenye kingo zenye mabwawa machache. Ikiendelea, hiyo yazunguka-zunguka kupitia mabonde na mabwawa hadi ifikiapo jiji la kale la Neapolisi.
Kutoka hapo njia hiyo yafuata pwani ya Aegean kuelekea mashariki na kuvuka kuingia eneo la Thrasi. Katika sehemu yake ya mwisho, hiyo barabara kuu huendelea kwa mwendo ulionyooka na ulio tambarare hadi mwisho wake, Bizantiamu.
Kutimiza Kusudi Lake
Hiyo Via Egnatia ikawa njia ya moja kwa moja na ifaayo sana kati ya Roma na sehemu zilizotawalwa na Waroma zilizokuwa mashariki ya Bahari Adriatiki. Ilirahisisha kufanyizwa kwa koloni za Waroma katika miji ya Makedonia na ikaathiri sana maendeleo ya kiuchumi, idadi ya watu, na utamaduni wa eneo hilo. Hiyo barabara kuu ilirahisisha kusafirishwa kwa shaba nyekundu, asfalti, fedha, samaki, mafuta, divai, jibini, na vitu vinginevyo.
Ufanisi uliotokezwa na biashara hiyo ulifanya miji fulani iliyokuwa kandokando ya barabara hiyo, kama vile Thesalonike na Amfipolisi, kuwa baadhi ya majiji makubwa zaidi katika Balkani. Thesalonike, hasa, ulisitawi na kuwa kituo kikuu cha biashara, kilichojaa utendaji wa kisanaa na kitamaduni. Ni kweli, gharama ya kudumisha barabara hiyo kwa sehemu ililipiwa na jumuiya zilizokuwa kando yake. Lakini, pia jumuiya hizo zilipata kwa wingi manufaa ya biashara ya kimataifa.
Fungu Katika Kueneza Ukristo
Hata hivyo, Via Egnatia, ililetea watu wengi walioishi katika eneo hilo manufaa kuu zaidi kuliko ufanisi wa kimwili. Kwa mfano, chukua mfanya-biashara mwanamke mwenye ufanisi Lidia. Yeye aliishi Filipi—jiji la kwanza katika Ulaya kusikia Paulo akihubiri habari njema. Baada ya kutua Neapolisi katika mwaka wa 50 W.K., mtume Paulo na waandamani wake walisafiri kilometa 16 kuelekea kaskazini-magharibi kwenye Via Egnatia hadi Filipi.
“Siku ya sabato,” akaandika Luka, “tulitoka nje ya lango kando ya mto, ambako tulikuwa tukifikiri kulikuwako mahali pa sala; nasi tukaketi na kuanza kusema na wanawake waliokuwa wamekusanyika.” Miongoni mwa wanawake waliomsikiliza Paulo alikuwa Lidia. Siku hiyohiyo, yeye na nyumba yake wakawa waamini.—Matendo 16:13, 14.
Kutoka Filipi, Paulo na washiriki wake waliendelea kwenye Via Egnatia kupitia Amfipolisi na Apolonia hadi Thesalonike, jumla ya kilometa 120. (Matendo 17:1) Ili kuhubiri habari njema katika Thesalonike, Paulo alitumia vikusanyiko vya Wayahudi vya siku ya Sabato katika sinagogi la huko. Kwa hiyo, Wayahudi fulani na “umati mkubwa kati ya Wagiriki” wakawa waamini.—Matendo 17:2-4.
Vivyo hivyo leo, Mashahidi wa Yehova katika Albania na Ugiriki wanatumia sehemu za barabara hiihii kuu ili kufikia watu wanaoishi katika maeneo hayo. Lengo lao ni kueneza habari njema ya Ufalme wa Mungu, kama tu vile mtume Paulo na waandamani wake wamishonari walivyofanya. (Mathayo 28:19, 20; Matendo 1:8) Kwa hakika, Via Egnatia ni barabara kuu ya Roma ambayo imesaidia upanuzi wa kiroho, katika karne ya 1 na vilevile kuendelea hadi karne hii ya 20!
[Ramani katika ukurasa wa 16, 17]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
UINGEREZA
ULAYA
AFRIKA
BALKANI PENINSULA
MAKEDONIA
UGIRIKI
Dirakiamu, Ilirikamu (DURRES, Albania)
Thesalonike
Apolonia
Amfipolisi
Filipi
Neapolisi (Kaválla)
Bizantiamu (Istanbul)
BAHARI NYEUSI
BAHARI YA MARMARA
THRASI
BAHARI YA AEGEAN
Troasi
UTURUKI
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Barabarani kuelekea Neapolisi
[Picha katika ukurasa wa 17]
Barabarani kuelekea Filipi