Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 9/8 kur. 18-19
  • Cuzco—Jiji Kuu la Kale la Wainka

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Cuzco—Jiji Kuu la Kale la Wainka
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Jiji la Kale
  • Ujenzi wa Kipekee wa Cuzco
  • Dini Katika Cuzco
  • Jinsi Wainka Walivyopoteza Milki Yao Yenye Fahari
    Amkeni!—1998
  • Lazima Ujumbe Uenezwe
    Amkeni!—2006
  • Kuhubiri Ufalme Katika Uwanda wa Altiplano Huko Peru
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Mambo Tunayoweza Kujifunza Kutokana na Makaburi ya Peru
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 9/8 kur. 18-19

Cuzco—Jiji Kuu la Kale la Wainka

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Peru

TULISISIMKA ndege yetu ilipofanya mzunguko mkubwa na kuteremka katika bonde jembamba. Tulikuwa karibu kutua katika jiji la kihistoria la Cuzco, Peru. Ingawa hilo jiji liko zaidi ya meta 3,400 juu, milima yenye mawemawe ilionekana kama imeinuka sana, ikifanya mfikio wetu kwenye uwanja wa ndege uonekane kuwa hatari sana. Kwa furaha, tulitua salama. Ilitazamiwa kuwa raha kuona jiji hili mashuhuri lenye wakaaji 275,000, ambalo wakati mmoja lilikuwa jiji kuu la Milki kubwa mno ya Inka.

Utamaduni wa kale wa Inka bado ni dhahiri katika Cuzco. Wakazi wengi wa jiji wangali wanazungumza Kiquechua. Kwa hakika, watu wapatao milioni nane katika safu ya mlima ya Andes wangali wanazungumza lugha hii ya kale. Hivi majuzi, jumuiya ya Waquechua waliwashawishi wenye mamlaka kubadili jina la Cuzco liwe Qosqo, kwa kuwa matamshi ya Qosqo yakaribiana na jina la awali katika Kiquechua.

Jiji la Kale

Wanahistoria husema kwamba jiji hili lilianza miaka ipatayo 1,500 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo. Hiyo ilikuwa karibu na wakati ambapo Musa aliwaongoza wana wa Israeli kuondoka Misri. Kisha, miaka 600 hivi iliyopita, Pachacuti, maliki wa tisa wa Inka, alichukua udongo kidogo na kuufanyiza kiolezo cha jiji jipya la Cuzco lililobuniwa upya. Pachacuti alianza kutawala miaka 89 kabla ya kufika kwa washindi wa Kihispania karibu na mwaka wa 1527. Chini ya usimamizi wake jiji hilo lilifanyizwa kuwa jiji kubwa lililopangwa vizuri lenye maelfu ya nyumba, ambalo ni msingi wa Cuzco wa kisasa.

Kulingana na wenyeji fulani, hilo jiji liligawanywa katika sehemu nne, kuanzia kitovu ambako baraza la jiji, lilikuwapo. Katika Kiquechua baraza hili lilijulikana kuwa huacaypata, mahali pa sherehe, starehe, na kunywa. Wataalamu fulani wa Kiquechua hudai kwamba “Cuzco,” au “Qosqo,” lamaanisha “Kitovu cha Ulimwengu.” Hivyo, kitovu cha baraza la Cuzco kikawa chawpi, au “kitovu cha kitovu cha Milki ya Inka.”

Kutoka Cuzco, maliki wa Inka alitawala eneo ambalo sasa ni sehemu za Argentina, Bolivia, Chile, Ekuado, Kolombia, na Peru za wakati huu—sehemu kubwa yake ikiwa ardhi yenye ufanisi na yenye rutuba. Watu walifaulu kwa kilimo kwa kujenga matuta mengi kwenye altitudo tofauti-tofauti. Katika matuta hayo yenye mazao, wao walipanda mimea ambayo hadi sasa inaandaa kiasi kikubwa cha chakula cha ulimwengu, kama vile viazi-ulaya na maharagwe-lima.

Kusafiri kupitia eneo la Inka kungekuwa kugumu sana kama si mfumo bora wa barabara, ambao ulivuka milki hiyo. Katika Cuzco lenye kuvutia mtu aweza kuwazia kwa urahisi Wainka wa kale wakifika wakiwa na misafara yao ya Ilama, hayawani wachukua-mizigo yenye kulemea wa Andes. Shehena yao nzuri ilitia ndani vito, shaba, fedha, na dhahabu.

Dhahabu ilipatikana kwa wingi, lakini Wainka hawakuitumia kama pesa. Kwa sababu ya kumeremeta kwa rangi ya kimanjano yenye kung’aa, dhahabu ilihusianishwa na mungu wa Wainka, jua. Mara nyingi, mahekalu yao na makao ya wafalme yalipambwa kwa mabamba ya dhahabu. Wao hata walifanyiza bustani ya dhahabu, yenye wanyama na mimea waliochongwa kwa dhahabu safi. Ebu wazia ono lenye kuvutia la Cuzco la kale, majengo yake yenye mabamba ya dhahabu yakimeremeta katika jua! Kwa kueleweka, wingi huo wa dhahabu ulivutia washambulizi Wahispania wenye pupa, ambao walilishinda na kulipora katika mwaka wa 1533.

Ujenzi wa Kipekee wa Cuzco

Wainka waliachia Cuzco la kisasa urithi wa mtindo mzuri na ulio wa kipekee wa ujenzi wa mawe. Mengi ya majengo ya leo yamejengwa kwenye kuta za mawe ambazo zimebaki hivyohivyo kwa mamia ya miaka. Mawe fulani yalikatwa ili yatoshee kabisa katika mahali hususa pa kuta. Ukuta mmoja, ambao umekuwa kivutio chenye kupendwa na watalii, una jiwe kama hilo, lenye pembe 12 tofauti-tofauti! Kwa sababu ya kukatwa kwa pembe nyingi, mawe hayo ni kama funguo zinazotoshea tu katika matundu yalinganayo na funguo zake.

Waashi Wainka walikuwa wajenzi stadi. Bila msaada wa tekinolojia ya kisasa, wao waliweza kukata mawe kwa usahihi sana hivi kwamba mara tu yawekwapo, hata kisu hakikuweza kuingizwa kati ya mawe hayo! Baadhi ya mawe hayo yana uzito wa tani kadhaa kila moja. Jinsi watu hao wa kale walivyoweza kupata stadi kama hizo bado ni fumbo.

Dini Katika Cuzco

Baada ya kukubali dini ya Katoliki, wazaliwa wa Quechua kwa ujumla hawaonwi tena kuwa waabudu-jua. Hata hivyo, wao hudumisha itikadi zao za kipagani za kuabudu viumbe ambazo ni za kale hata kuliko ibada ya jua ya Wainka. Wao bado husherehekea msimu wa mavuno kwa kutoa matoleo kwa kile wakiitacho Pacha-Mama, kutokana na neno la Kiquechua limaanishalo “dunia mama.”

Mashahidi wa Yehova wanaendeleza programu yao ya elimu ya Biblia nchini Peru kwa mafanikio sana. Kwa muda fulani sasa, Watch Tower Society imeandaa fasihi ya Biblia katika Kiquechua ili watu wenye kuzungumza Kiquechua waweze kupokea ujumbe wa Ufalme katika lugha ya asili. Kuna sehemu sita ambapo mikutano ya Kikristo inafanywa katika lugha hiyo.

Cuzco halifikiriwi tena kuwa kitovu cha ulimwengu, lakini watalii humiminika kuzuru jiji hili la kipekee. Labda wewe pia siku moja utazuru Peru yenye kuvutia sana!

[Picha katika ukurasa wa 18, 19]

1. Kutazama Cuzco kutoka juu likiwa na baraza lake la jiji

2. Wainka walikata mawe kwa usahihi sana hivi kwamba kisu hakiwezi kutoshea kati ya mawe hayo

3. Mavazi ya kawaida ya Peru

4. Llama ni hayawani wachukua-mizigo yenye kulemea wa Andes

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki