Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 1/8 kur. 13-18
  • Jinsi Wainka Walivyopoteza Milki Yao Yenye Fahari

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jinsi Wainka Walivyopoteza Milki Yao Yenye Fahari
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Nani Waliokuja Kabla ya Wainka?
  • Ngano na Uhalisi
  • Hekalu Lenye Kung’aa la Jua
  • Milki Hiyo Ilidumishaje Muungano?
  • Kodi ya Mita
  • Washambulizi Kutoka Kaskazini
  • Mwanzo wa Mwisho wa Milki Hiyo
  • Inka wa Mwisho
  • Wazao wa Siku ya Kisasa wa Wainka
  • Elimu Yaleta Mabadiliko
  • Cuzco—Jiji Kuu la Kale la Wainka
    Amkeni!—1997
  • Lazima Ujumbe Uenezwe
    Amkeni!—2006
  • Mambo Tunayoweza Kujifunza Kutokana na Makaburi ya Peru
    Amkeni!—2004
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 1/8 kur. 13-18

Jinsi Wainka Walivyopoteza Milki Yao Yenye Fahari

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA PERU

Macheo. Milima ya Andes yenye theluji kileleni ilikuwa imetiwa rangi nyororo ya nyekundu-nyeupe na miale ya nuru ichomozayo katika anga ya asubuhi. Wenye kuamka mapema miongoni mwa Wahindi hao walifurahia joto lenye kuondoa ubaridi wa usiku kwenye kimo cha meta 4,300. Polepole, miale ya jua ilifika chini na kuangaza hekalu la jua lililo katikati ya jiji kuu la Milki ya Inka, Cuzco (limaanishalo “Kitovu cha Ulimwengu”). Kuta zenye dhahabu ziliangaza miale ya jua. Michongo ya dhahabu tupu ya Ilama, vicuñas, na tai iling’aa katika bustani ya Wainkaa iliyokuwa mbele ya hekalu. Wapita-njia walipiga busu hewani katika kuabudu mungu wao, jua. Walishukuru kama nini kuwa hai na kubarikiwa na jua lililowapa riziki, kama walivyoamini!

KATI ya karne ya 14 na ya 16, milki kubwa yenye fahari ilitawala pwani ya magharibi ya Amerika Kusini. Wakitawalwa na wasanifuujenzi na mafundisanifu wenye akili, Wainka walikuwa watu waliojipanga ili kujiboresha kijamii. Milki ya Inka yenye fahari ilitia ndani eneo la karibu kilometa 5,000, ikitokea sehemu ya kusini ya Kolombia ya sasa hadi chini sana Argentina. Kwa kweli, “Wainka walidhani walitawala karibu ulimwengu wote.” (National Geographic) Wao waliamini kwamba ng’ambo ya milki yao, hakukuwa na chochote cha maana cha kuteka. Lakini, sehemu nyingine za ulimwengu hata hazikujua kwamba milki hii ilikuwapo.

Wainka walikuwa nani? Walitoka wapi?

Ni Nani Waliokuja Kabla ya Wainka?

Ugunduzi wa kiakiolojia waonyesha kwamba Wainka hawakuwa wakazi wa awali wa kontinenti hiyo. Tamaduni nyinginezo zilizositawi vizuri ziliwatangulia kwa mamia kadhaa ya miaka hadi maelfu kadhaa. Hizo zimeainishwa na waakiolojia kuwa tamaduni za Walambayeque, Wachavin, Wamochica, Wachimu, na Watiahuanaco.

Vikundi hivyo vya mapema viliabudu wanyama mbalimbali—jagua, puma, na hata samaki. Staha kwa miungu ya milima ilienea kote miongoni mwao. Vyombo vyao vya ufinyanzi vilionyesha kwamba baadhi ya makabila hayo yalifanya ibada ya ngono. Karibu na Ziwa Titicaca, juu sana kwenye mpaka baina ya Peru na Bolivia, kabila fulani lilijenga hekalu lenye ishara za uume, ambazo ziliabudiwa katika sherehe za uzazi ili kuhakikisha kwamba kuna mazao mazuri kutoka kwa Pacha-Mama, limaanishalo “Mama Dunia.”

Ngano na Uhalisi

Ilikuwa karibu mwaka wa 1200 kwamba Wainka walitokea. Kulingana na mrekodi-matukio Garcilaso de la Vega, mwana wa binti-mfalme wa Inka na kabaila mmoja Mhispania aliye na cheo, ngano yasema kwamba Inka wa awali, Manko Kapak akiwa pamoja na dada yake aliyekuwa mke wake, alitumwa duniani na baba yake, mungu-jua, aende Ziwa Titicaca akalete watu wote chini ya ibada ya jua. Leo, hekaya hii ingali inasimuliwa watoto katika baadhi ya shule.

Hata hivyo, mbali na ngano, huenda ikawa Wainka walitokana na mojawapo ya makabila ya Ziwa Titicaca, lile kabila la Watiahuanaco. Baada ya muda, milki hiyo yenye kuenea ilitwaa utendaji mwingi wenye kupangwa vizuri wa makabila yaliyoshindwa, ikipanua na kuboresha mifereji na matungazi ambayo tayari yalikuwa yamejengwa. Wainka walijua sana kujenga majengo makubwa. Kuna mawazo mengi kuhusu jinsi wasanifuujenzi wao walivyoweza kujenga ngome na hekalu la Sacsahuaman, ambalo laonekana sana katika jiji la Cuzco kutoka uwanda wa juu. Majabali makubwa mno yenye uzito wa tani 100 yaliunganishwa pamoja. Hakuna mota iliyotumiwa kuyashikanisha. Matetemeko ya ardhi hayajaathiri sana mawe hayo yaliyounganishwa vizuri sana katika kuta za jiji la kale la Cuzco.

Hekalu Lenye Kung’aa la Jua

Katika jiji la kifalme la Cuzco, Wainka walipanga ukuhani kwa ajili ya kuabudu jua katika hekalu la mawe lililong’arishwa. Kuta za ndani zilipambwa kwa dhahabu safi na fedha. Pamoja na ukuhani, makao ya kipekee ya watawa yalianzishwa, kama lile lililojengwa upya katika hekalu la jua la Pachácamac, nje tu ya Lima. Mabikira warembo sana walizoezwa kutokea umri mchanga wa miaka minane kuwa ‘mabikira wa jua.’ Uthibitisho wa kiakiolojia waonyesha kwamba Wainka pia walitoa wanadamu kuwa dhabihu. Wao walikuwa wakiwatoa watoto kuwa dhabihu kwa apus, au miungu ya mlima. Miili fulani ya watoto imepatikana ikiwa imeganda kwenye vilele vya Andes.

Ingawa Wainka na makabila ya mapema hawakujua kuandika, wao walisitawisha mfumo wa kuweka rekodi kwa kutumia kile kilichoitwa quipu. Hiki kilikuwa “chombo kilichotengenezwa kwa kamba kubwa yenye kamba ndogondogo zenye rangi mbalimbali zilizoshikanishwa na kupigwa fundo na kutumiwa na Waperu wa kale” kuwa kikumbusha cha watunza-rekodi waliopewa mgawo wa kutunza orodha na rekodi ya mambo.—Webster’s Ninth New Collegiate Dictionary.

Milki Hiyo Ilidumishaje Muungano?

Sheria kali na mbinu zilizopangwa ziliimarisha hiyo serikali moja kuu. Takwa la kwanza lilikuwa kwamba wote wajifunze Kiquechua, lugha ya Wainka. “Kiquechua,” chasema kitabu El Quechua al Alcance de Todos (Kiquechua Kilicho Rahisi kwa Kila Mtu Kujifunza), chaonwa kuwa “chenye mambo mengi zaidi, chenye kutofautiana zaidi, na vilevile chenye uzuri zaidi kati ya lahaja za Amerika Kusini.” Kingali kinazungumzwa na watu wapatao milioni tano waishio katika milima ya Peru na mamilioni wengine katika nchi tano ambazo zamani zilikuwa zimekuwa sehemu ya milki hiyo. Kikundi kimoja kilichopo kusini-mashariki ya Ziwa Titicaca kingali kinazungumza lugha ya Kiaymara, lahaja itokanayo na Kiquechua cha nyakati za kabla ya Wainka.

Kutumia lugha ya Kiquechua kukawa na matokeo ya kuunganisha karibu makabila 100 yaliyoshindwa, na kulisaidia curaca (mkuu) wa kijiji ambaye alisimamia kila kikundi. Kila familia ilipewa ardhi ya kulima. Baada ya utekaji, Wainka waliruhusu dansi na sherehe za kienyeji za makabila ziendelee na waliandaa tamasha na michezo ili kuridhisha watu wote waliotiishwa.

Kodi ya Mita

Pesa hazikuwapo pote katika hiyo milki, jambo lililomaanisha kwamba dhahabu yenyewe haikuwa na thamani kwa watu mmoja-mmoja. Uvutio wake ulikuwa kwamba uliangaza jua. Kodi ya pekee iliyowekwa, ile mita (Kiquechua, “zamu”), ilikuwa takwa kwamba raia wachukue zamu ya kufanya kazi ya lazima katika miradi mingi ya barabara na majengo ya Wainka. Kwa hiyo maelfu ya wafanyakazi Wahindi walisajiliwa na serikali.

Wakitumia wafanyakazi wa mita, wajenzi stadi Wainka walijenga mifumo ya barabara zenye urefu wa zaidi ya kilometa 24,000! Wakianzia Cuzco, Wainka walijenga mfumo wa barabara zenye mawe za kuunganisha sehemu za mbali zaidi za milki hiyo. Wajumbe wenye kukimbia waliozoezwa, walioitwa chasquis, walizitumia. Wao walikuwa katika mabanda yaliyokuwa kila baada ya kilometa moja au tatu. Yule chasqui mwenye ujumbe alipofika, chasqui mwingine alianza kukimbia kando yake, kama mkimbiaji wa kupokezana kijiti. Wakitumia mfumo huo, wao walikimbia umbali wa kilometa 240 kwa siku. Kwa muda mfupi, Inka mwenye kutawala alipata ripoti kutoka sehemu zote za milki yake.

Kando za barabara, Wainka walijenga maghala makubwa sana. Hayo yalijazwa chakula na mavazi kwa matumizi ya majeshi ya Wainka walipokuwa safarini kuteka sehemu nyinginezo. Wainka waliepuka vita ilipowezekana. Wakitumia mbinu, alituma wajumbe kualika makabila kukubali kujitiisha chini yake, kwa sharti ya kwamba wao wakubali kuabudu jua. Wakikubali, wao waliruhusiwa kujiendeleza wenyewe katika kabila lao, wakielekezwa na wafunzi Wainka waliozoezwa. Ikiwa wangekataa, wao walitekwa kwa njia ya kikatili sana. Mafuvu ya kichwa ya maadui waliokufa yalitumiwa kama bilauri za kunywa chicha, pombe kali iliyopikwa kutokana na mahindi.

Ilikuwa chini ya Inka wa tisa, Pachacuti (mwaka wa 1438 na kuendelea), mwana wake Topa Inka Yupanqui, na mnyakua-utawala wa taifa Huayna Kapak, kwamba milki hiyo ilipanuka haraka sana kufikia ukubwa wake kabisa kaskazini hadi kusini. Lakini hiyo haikudumu.

Washambulizi Kutoka Kaskazini

Karibu na mwaka wa 1530, mtekaji wa Kihispania Francisco Pizarro na askari-jeshi wake walitoka Panama, wakishawishiwa na ripoti za kuwapo kwa dhahabu katika bara hili lisilojulikana ambalo wakati huo lilikuwa limekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mwana-Mfalme Huáscar, aliye na haki ya kurithi kiti cha enzi, alikuwa ameshindwa na kufungwa gerezani na ndugu yake wa kambo Atahuallpa, ambaye alikuwa akielekea jiji kuu.

Baada ya safari ngumu kuelekea ndani kwenye jiji la Cajamarca, Pizarro na wanaume wake walikaribishwa vema na mnyakua-utawala Atahuallpa. Hata hivyo, kwa hila Wahispania walifaulu kumwondoa kwenye kiti chake na kumshika mateka, na wakati huohuo, wao wakawachinja-chinja maelfu ya majeshi yake waliopigwa bumbuazi na ambao hawakuwa wamejitayarisha.

Na ingawa alikuwa ameshikwa mateka, Atahuallpa aliendeleza vita ya wenyewe kwa wenyewe. Aliwatuma wajumbe waende Cuzco wakamwue ndugu yake wa kambo Inka Huáscar na vilevile mamia ya washiriki wa familia ya kifalme. Bila kujua, akarahisisha mpango wa Pizarro wa kuwateka.

Akiona pupa ya Wahispania ya kupata dhahabu na fedha, Atahuallpa akaahidi kujaza chumba kikubwa kwa sanamu za dhahabu na fedha kama fidia ili aachiliwe. Lakini wapi. Kwa mara nyingine tena alitendwa kwa hila! Baada ya fidia iliyoahidiwa kurundikwa, Atahuallpa, Inka wa 13, ambaye alionwa kuwa mwabudu-sanamu na watawa hao, kwanza alibatizwa kuwa Mkatoliki kisha akanyongwa.

Mwanzo wa Mwisho wa Milki Hiyo

Kukamatwa na kuuawa kimakusudi kwa Atahuallpa kulikuwa pigo kubwa sana kwa Milki ya Inka. Lakini hao Wahindi wakawakinza washambulizi hao, na kipindi cha mwisho cha milki hiyo kikadumu kwa miaka mingine 40.

Msaada ulipofika, Pizzarro na askari-jeshi wake wote walitamani kwenda Cuzco kunyakua dhahabu zaidi za Wainka. Kwa kufuata dhahabu, Wahispania hawakusita kutumia njia za kikatili za mateso ili wapate kujua siri kutoka kwa Wahindi za mahali zilipo hazina au za kuwaogofya na kunyamazisha wakinzani wowote wale.

Akiandamana na ndugu ya Huáscar, Mwana-Mfalme Manko wa Pili, ambaye angekuwa Inka (Manko Inka Yupanqui) afuataye, Pizzarro alienda mpaka Cuzco na kulipora hazina kubwa sana ya dhahabu. Nyingi za sanamu za dhahabu ziliyeyushwa kuwa vipande vya dhahabu ili kupelekwa Hispania. Si ajabu kwamba maharamia Waingereza walitamani kushika meli za Kihispania zilizobeba hazina nyingi kutoka Peru! Akiwa amejaza kwelikweli shehena ya dhahabu, Pizarro aliondoka kuelekea pwani, ambako katika 1533 alianzisha jiji la Lima likiwa kitovu cha serikali yake.

Sasa akiwa amefahamu vizuri pupa na hila za wanyakuaji hao, Manko Inka Yupanqui akapanga maasi. Wengine pia waliasi dhidi ya Wahispania, lakini hatimaye hao Wahindi walilazimika kurudi nyuma hadi sehemu za mbali na kuwakinza hao Wahispania kwa kadiri ilivyowezekana. Mojawapo ya sehemu hizo salama huenda zilitia ndani jiji takatifu la Machu Picchu lililofichika ndani milimani.

Inka wa Mwisho

Katika tendo la mwisho, Tupac Amarú, mwana wa Manko Inka Yupanqui, akawa Inka (1572). Sasa magavana-wakuu wa Kihispania wakasimamia Peru. Gavana-Mkuu Toledo alikuwa na mradi wa kuangamiza kabisa Wainka. Akiwa na jeshi kubwa, aliingia eneo la Vilcabamba. Tupac Amarú alikamatwa katika msitu. Yeye na mkewe mwenye mimba walipelekwa Cuzco ili kufishwa. Mhindi mmoja wa Kañari aliinua upanga wa kumwua Tupac Amarú. Yale maelfu ya Wahindi waliokusanyika barazani walitoa sauti ya huzuni iliyosikika kwa kuwa kwa pigo moja Inka wao alikatwa kichwa. Makapteni wake waliteswa hadi kifo au walinyongwa. Kwa mauaji hayo ya kikatili, utawala wa Wainka ukaisha.

Magavana-wakuu waliowekwa, pamoja na watawa wa kiume na makasisi wengi Wakatoliki, polepole walieneza uvutano wao, mwema na mbaya, juu ya Wahindi, ambao kwa muda mrefu walionwa kuwa watumwa tu. Wengi walilazimishwa kufanya kazi katika machimbo ya dhahabu au fedha, mojawapo ukiwa mlima uliojaa mawe ya fedha, uliokuwa Potosí, Bolivia. Ili kuweza kumudu hali hizo za kikatili, hao Wahindi waliotendwa vibaya walianza kutumia matawi ya koka kwa sababu ya hali yake ya kulevya. Peru na Bolivia hazikupata uhuru kutoka Hispania mpaka miaka ya mapema ya karne ya 19.

Wazao wa Siku ya Kisasa wa Wainka

Hali ya wazao wa Wainka ikoje katika enzi hii ya kisasa? Jiji kuu la Peru, Lima, kama ilivyo na majiji mengine mengi ya kisasa, lina mamilioni ya wakazi. Lakini katika mikoa ya mashambani, nyakati nyingine huonekana kana kwamba saa ilikoma miaka mia moja iliyopita. Vijiji vingi vilivyo peke yake vingali vinatawalwa na makasisi Wakatoliki. Kwa mkulima Mhindi, kanisa Katoliki lililo katika baraza la kijiji ndilo kivutio kikuu. Zile sanamu-umbo nyingi za watakatifu waliovalia vizuri, taa zenye rangirangi, madhabahu ya dhahabu, mishumaa yenye kuwaka, sherehe za kifumbo zinazoongozwa na kasisi, na hasa dansi na sherehe—zote hizo huwa kikengeushi ahitajicho. Lakini vikengeushi kama hivyo vipendezavyo macho haviondoi kamwe itikadi za kale. Na matumizi ya tawi la koka, ambalo linaonwa kuwa lina uwezo wa kifumbo, bado linaathiri maisha ya wengi.

Wakiwa na roho yao isiyoshindika, wazao hao wa Wainka—wengi sasa wakiwa wa uzao mchanganyiko—wamefaulu kudumisha dansi zao zenye kupendeza na muziki wao wa kiasili uitwao huaino. Hata kama mwanzoni wanawaogopa wageni, ukaribishaji-wageni wao wa kiasili hujitokeza. Kwa wale ambao wanawajua wazao hao wa Milki ya Inka kibinafsi—na waonao jitihada zao za kila siku za kuishi na za kuonyesha hangaiko la kibinafsi—hadithi yao kwa kweli inavunja moyo sana!

Elimu Yaleta Mabadiliko

Katika mahojiano na Amkeni!, Valentin Arizaca, mzao wa Wahindi wenye kuzungumza Kiaymara kutoka kijiji cha Socca kwenye Ziwa Titicaca, alisimulia hivi: “Kabla ya kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, nilikuwa Mkatoliki kwa jina tu. Nikiwa pamoja na baadhi ya marafiki wangu, nilifanya matendo mengi ya kipagani. Pia nilitafuna tawi la koka, lakini sasa nimeyaacha hayo yote.”

Akikumbuka sana ushirikina mwingi ambao ulimtia hofu daima ya kutompendeza apus, Petronila Mamani, mwenye umri wa miaka 89, alisema: “Kwa kawaida nilipeleka matoleo ili kuridhisha miungu ya mlima na kuhakikisha riziki yangu. Sikutaka kamwe kutowapendeza na kujihatarisha kupatwa na tauni ambazo zingetokea. Sasa, nikiwa mzee kwa umri, nimejifunza kuona mambo kwa njia tofauti. Kwa sababu ya Biblia na Mashahidi wa Yehova, nimeacha kufikiri kwa njia hiyo.”

Mashahidi wa Yehova wanafundisha Wahindi wengi wenye kuzungumza Kiquechua na Kiaymara jinsi ya kusoma. Wao, nao huwafundisha wengine Biblia. Kwa njia hii maelfu ya Wainka na Wahindi wa Kihispania wanafundishwa ili waboreshe maisha yao. Wao pia wanajifunza juu ya ahadi ya Mungu iliyo katika Biblia juu ya ulimwengu mpya wa haki, amani, na uadilifu, ambao karibuni utasimamishwa duniani kote.—2 Petro 3:13; Ufunuo 21:1-4.

[Maelezo ya Chini]

a Neno “Inka” laweza kurejezea mtawala mkuu wa Milki ya Inka na laweza pia kurejezea wenyeji.

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Milki ya Kifahari ya Wainka

AMERIKA KUSINI

Cuzco

Potosí

MILKI YA WAINKA

BAHARI YA KARIBEA

BAHARI YA PASIFIKI

KOLOMBIA

EKUADO

ANDES

PERU

Cajamarca

Lima

Pachácamac

Vilcabamba

Machu Picchu

Cuzco

Ziwa Titicaca

BOLIVIA

CHILE

ARGENTINA

[Picha katika ukurasa wa 16]

Juu: Hekalu la awali la jua latumika likiwa msingi wa kanisa hili la Katoliki katika Cuzco

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kushoto: Sanamu ya uume ya wakati wa kabla ya Wainka katika hekalu lililo Chucuito

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kulia: Damu ya dhabihu za Wainka ilitiririka kwenye mawe haya yaliyochongwa

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kulia: Matungazi yaliyonyunyiziwa maji katika Machu Picchu, karibu na Cuzco

[Picha katika ukurasa wa 17]

Chini: Mwono kupitia mlango mmoja wa zamani katika Machu Picchu

[Picha katika ukurasa wa 17]

Chini kulia: Majabali yenye uzito wa tani 100 ya ngome ya hekalu ya Sacsahuaman

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki