Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Maradhi ya Moyo Nashukuru kuwa sehemu ya tengenezo ambalo, mbali na kutuongoza kiroho, linajali hali-njema yetu ya kimwili. Ule mfululizo “Maradhi ya Moyo—Ni Nini Kinachoweza Kufanywa?” (Desemba 8, 1996) ulituonyesha jinsi ya kutambua dalili za maradhi ya moyo. Wakati baba-mkwe wangu alipoonyesha dalili hizi, tulitambua kwamba hali yake yaweza kuwa mbaya na tukampeleka katika hospitali moja. Alikuwa akipatwa na maradhi ya moyo; lakini baada ya siku 24 hospitalini, akawa hayuko hatarini tena.
E. S., Brazili
Baba yangu alikufa kutokana na kutanuka kwa mshipa mkuu wa moyo katika 1995, hivyo nilipoliona toleo hilo kwa mara ya kwanza, sikuwa na moyo mkuu wa kulisoma. Hata hivyo, nililisoma mwezi mmoja baadaye, na makala hizo ziliniandalia faraja, nikijua kwamba wengine wameshiriki huzuni ambayo maradhi ya moyo yaweza kuiletea familia.
S. J., Kanada
Mwezi wa Julai uliopita mume wangu alipoteza fahamu akiwa katika kazi ya kuhubiri mlango hadi mlango na ikabidi akimbizwe hospitalini. Kwa furaha, aliokoka pindi hiyo. Makala zenu zilikuja kwa wakati unaofaa kwetu. Ilitufanya tulie machozi tulipoiona ile sehemu “Familia Zahitaji Utegemezo,” kwa sababu hivyo ndivyo tumekuwa tukihisi hasa.
M. A., Japani
Jumapili iliyopita nilikuwa nikisikia maumivu yenye kuendelea kwenye mkono wangu wa kushoto na ncha za vidole vyangu kufa ganzi. Nikawazia ilikuwa tu michonyoto na maumivu ya kawaida. Niliposoma makala zenu juu ya maradhi ya moyo, nikatambua wazi kwamba ninaugua dalili hizo! Nikaenda kwenye chumba cha matibabu ya dharura katika hospitali, na madaktari wakakuta kwamba moja ya ateri kuu katika moyo wangu ilikuwa imeziba. Walinifanyia upasuaji siku iliyofuata. Kuna uwezekano mkubwa kwamba ikiwa makala zenu hazikuandikwa, nisingekuwa hapa kuandika taarifa hii ya asante!
N. S., Marekani
Mimi nilithamini hasa lile sanduku “Dalili za Mshiko wa Moyo.” Lilinifanya ning’amue kwamba mwapendezwa kibinafsi na matatizo yetu na kwamba mwatupatia tunachohitaji ili kukabiliana nayo.
M. B., Senegal
Tangu baba yangu apatwe na maradhi ya moyo, maisha katika familia yetu yamebadilika sana. Katika pindi hizi zenye magumu, makala zenu zimethibitika kuwa faraja kubwa kwetu.
P. G., Italia
Ujitiisho wa Mke Mimi kwa kweli nilithamini ile makala “Ujitiisho wa Mke—Wamaanisha Nini?” (Desemba 8, 1996) Mume wangu si mwamini, na ni vigumu nyakati nyingine kuwa katika ujitiisho kwake. Ninataka kuweka kielelezo bora zaidi ili niweze kumvuta. (1 Petro 3:1) Hata hivyo, nataka kubaki imara katika utumishi wangu kwa Yehova. Makala yenu ilinitia moyo, na ilinifanya niwe mwenye furaha kujua kwamba Mungu wangu ananilinda.
M. S., Marekani
Niliipata makala hiyo kuwa yenye kuelimisha. Kwa kuwa misongo kutoka kwa Shetani inazidi, twahitaji habari kama hii ili tubaki katika imani. Nilifurahia hasa kile kielelezo cha Biblia cha Abigaili na hoja iliyotokezwa kwamba mke apaswa kuonyesha ufahamu na asifanywe ahisi hatia kwa kuchukua hatua ya kwanza katika hali fulani.
D. M., Marekani
Louis Pasteur Nina umri wa miaka 12 na nilitaka kuwajulisha kwamba nilithamini ile makala “Louis Pasteur—Kilichofunuliwa na Kazi Yake.” (Desemba 8, 1996) Tunajifunza kumhusu katika somo langu la sayansi. Nilitumia makala hii kutayarisha ripoti na nikapata alama kumi zaidi katika maksi zangu!
A. P., Marekani