Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Watoto Walio na Mkazo wa Akili Asanteni sana kwa mfululizo wa makala “Watoto Walio na Mkazo wa Akili—Wanaweza Kusaidiwaje?” (Julai 22, 1993) Nilipoyasoma, nililia kwa shangwe na kwa huzuni. Nikiwa na karibu umri wa miaka minne hivi, nilipatwa na jeuri ya kingono mikononi mwa baba yangu. Nilikua huku nikiwa na maumivu ya daima na hofu. Sasa nimekuwa Mkristo kwa miaka 20, na kwa msaada wa Yehova—na makala kama hizi—nimeanza kupata nafuu. Habari hiyo yaniwezesha pia kumlinda binti yangu.
S. S., Italia
Nina umri wa miaka 17 na nimo na mkazo mkubwa sana wa kihisiamoyo. Kuna utumizi mwingi wa maneno mabaya nyumbani kwetu. Hata ingawa baba yangu hajayasoma makala haya, sioni vile kila mzazi mwenye kutenda vibaya anavyoweza kuyapuuza. Natumaini makala hizo zitafungua macho ya wazazi wa aina hiyo.
T. B., United States
Binti yangu wa miaka mitatu alitendwa vibaya kingono. Alisumbuka kwelikweli kwa ono hilo; mtoto si mchanga mno asiweze kuumizwa kihisimoyo. Nilikasirika sana na kuhuzunika hivi kwamba nilitaka mwandike makala juu ya kusaidia wazazi waone jinsi mambo yanavyoweza kuwa mabaya kwa watoto wetu. Maneno hayawezi kuonyesha shangwe yangu kwa kusoma makala hizi. Sijapata kamwe kusoma jambo lenye kupendeza hivyo. Yaonyesha wengine kwamba twamtumikia Mungu ambaye huelewa maumivu makali ambayo watu wanapatwa nayo.
M. G., United States
Asanteni hasa kwa makala “Wazazi Wenye Kuwatenda Watoto Vibaya—Wasababishaji Wakubwa wa Mkazo wa Akili.” Nilikulia katika malezi kama hayo, kukiwa na kutendwa vibaya kihisiamoyo na kingono. Makala hiyo ilionyesha jinsi jambo hilo laweza kufanya maisha ya mtu yawe magumu. Inafariji kujua kwamba kuna mtu anayeelewa kwelikweli.
B. S., United States
Nikiwa mwokokaji wa kutendwa vibaya kingono na kihisiamoyo wakati wa utotoni, kwa kweli naweza kutambua madhara yasiyotakwa yanayosababishwa na mkazo wa akili wa utotoni. Isipokuwa umepatwa nao, huwezi kuanza kuelewa uharibifu unaoletea maisha ya mtu. Kule kujichukia mwenyewe, hatia, ogofyo, na hisia zenye kulemea za kutostahili haziwezi kuvumiliwa wakati mwingine. Ni sala yangu kwamba wazazi wanaosoma habari hii watajichanganua wenyewe kiakili na wawatendee watoto wao kwa huruma na hisiamwenzi.
D. I., United States
Mara tu nilipoliona jalada lalo, nilianza kutoa machozi. Mtoto wangu mwenye umri wa miaka saba alitushinda kushughulika naye, na hatukujua la kufanya. Hatimaye tulimpeleka kwa mstadi wa akili na matatizo ya kihisiamoyo. Muda wa siku moja baada ya yeye kurudi nyumbani, tulipokea toleo la watoto walio na mkazo wa akili. Bado tuna maswali mengi yasiyojibiwa, lakini kupitia makala kama hizo, sala, na utegemezo wa marafiki, tunapata angalau maswali yetu mengi yakijibiwa.
D. G., United States
Nina umri wa miaka 13, na miaka miwili iliyopita nilikuwa mgonjwa sana. Nilikuwa pia na mshuko wa moyo wa pindi kwa pindi. Natamani ningalikuwa na makala hizo wakati huo. Mama yangu alinipeleka kwenye hospitali ya pekee ya watoto kwa sababu madaktari wa mji wetu hawakuelewa tatizo langu. Madaktari wa hospitali hiyo waligundua kwamba nilikuwa na kile makala yenu ilikiita “matatizo ya akili.” Wazee wa kutaniko letu, pamoja na wazazi wangu, walinisaidia kushinda mkazo wangu wa akili. Natumaini kwamba makala zenu zitasaidia vijana wengine washinde mkazo wa akili.
J. B., United States
Mimi ni kijana aliye na mkazo wa akili pia. Nina umri wa miaka saba, na mama na baba yangu walitengana. Hilo ndilo jambo ambalo huufanya uwe mkazo mwingi. Nina matatizo ya tumbo kama tu vile mlivyoandika. Asanteni kwa kujali.
J. H., United States