Kuutazama Ulimwengu
Wanawake Washauriwa Kukinza Mnajisi
Utafiti mpya umeonyesha kwamba wanawake wana uwezekano mkubwa wa kuepa kunajisiwa na kujeruhiwa ikiwa watapigana badala ya kusihi au kulia. Wakichunguza rekodi ya wanawake ambao wameshambuliwa kingono, watafiti katika Chuo Kikuu cha Brandeis katika Waltham, Massachusetts, waligundua kwamba wanawake waliopigana au kupiga mayowe na wakakimbia walifanikiwa zaidi ya wale ambao hawakufanya hivyo. “Kwa kweli, wanawake walionajisiwa kwa wepesi zaidi au kuumizwa ni wale ambao hawakupigana, wakitegemea badala ya hivyo kusihi au kusababu na washambulizi wao,” lasema gazeti American Health. Dakt. Sarah Ullman, aliyeongoza uchunguzi huo, atoa shauri hili: “Mwanamke hapaswi kusita kupiga mayowe, kupigana na kukinza kwa nguvu zake zote. Kusihi na kuombaomba labda hakutasaidia.”
Kanisa Katika Polandi
Yapata miaka minne hivi baada ya kuanguka kwa Ukomunisti katika Polandi, Kanisa Katoliki lakabiliwa na magumu mazito sana. Kulingana na Guardian Weekly la London, uchunguzi wa maoni ya watu ulifunua kwamba “ukasisi umepoteza sehemu kubwa ya sifa yao ya uadhama.” Laongezea kwamba “idadi ya watu wanaotoa maombi ya kwenda seminari inapungua na hudhurio la mafundisho ya kidini lafifia.” Wengi walioulizwa waamini kwamba uvutano wa Katoliki ni mwingi sana katika maisha ya umma. Guardian laandika kwamba “wasomi [Wapolandi] waamini kwamba ijapokuwa wakati uliopita Polandi ilipata sifa kwa bidii ya kidini, ya Ukatoliki wayo ulikuwa wa kijuujuu tu na kidesturi.” Wengine wanasadiki kwamba kanisa lilikuwa hasa chombo cha kumaliza Ukomunisti na kwamba halikukomesha Wakatoliki Wapolandi “kutotalikiana au kutoa mimba maadamu sheria iliwaruhusu kufanya hivyo.”
“Uutumie Ama Uupoteze”
Uchunguzi mwingi uliofanywa ulimwenguni pote umeonyesha kwamba kadiri mtu atumiavyo ubongo wake, ndivyo aelekea zaidi kutopata matatizo ya ubongo. “Kuwa na elimu zaidi hakumaanishi tu kwamba utakuza ubongo wako zaidi unapokuwa ungali mchanga, bali kwamba wautumia zaidi katika maisha yako, na hilo hutokeza aina fulani ya kinga” dhidi ya ugonjwa wa akili. “Kusoma, kuandika na kufanya hesabu kwaweza kuwa njia bora ya kulinda ubongo wako dhidi” ya hali ya kudhoofika kiakili, laripoti The Toronto Star la Kanada. Msaikolojia wa nuroni Marilyn Albert alisema: “Utafiti huu umethibitishwa kabisa hivi kwamba twajua ni kweli.” Akaongezea hivi: “Kwa habari ya ubongo, yamaanisha ‘uutumie, ama uupoteze.’”
Kansa Zinazoletwa na Mnururisho
Miaka saba baada ya aksidenti ya nyukilia ya Chernobyl katika Ukrainia, madaktari katika Belarus (zamani Belorussia) waripoti ongezeko kubwa katika idadi ya kansa ya kikoromeo katika watoto. Kulingana na jarida la Kifaransa la kitiba Le Concours médical, visa vilivyoripotiwa katika Belarus vya kansa ya kikoromeo katika watoto viliongezeka kutoka wastani wa visa 4 kwa mwaka kati ya 1986 na 1989 hadi visa 114 kwa mwaka kutoka 1990 hadi Juni 1992. Kwa sababu nururishi-isotopu inayosababisha kansa ya kikoromeo, iodini 131, ilitolewa katika aksidenti hiyo kwa kiasi kingi kuliko elementi nyingine za nururishi, wanasayansi wanatumaini kwamba aina nyingine za kansa zinazoletwa na mnururisho zitakuwa chache.
Kuku Walio na “UKIMWI”
Inaonekana kwamba UKIMWI si wa wanadamu na aina fulani za nyani tu. Gazeti Indian Express la Bombay, India, liliripoti kwamba maradhi yafananayo na UKIMWI yameambukia kuku wa nchi hiyo. Kulingana na Express, maradhi hayo ya virusi iitwayo gumbaro, yanayosababisha ukosefu wa kinga mwilini, “yamefikia viwango vya juu sana nchini, yakiathiri [mamia ya maelfu] ya ndege.” Zaidi ya ndege milioni 1.5 wenye kutaga mayai wamekufa. Ripoti hiyo ilidai kwamba kuna uwezekano wa kuwa na upungufu mkubwa sana wa mayai katika India.
Matatizo ya Matineja
“Vijana wa leo [katika United States] wanakabili hofu na hatari halisi kuliko miaka ya utineja inayokumbukwa na wazazi wao na mababu zao,” laripoti International Herald Tribune. Likinukuu tarakimu za U.S., Tribune lilisema kwamba idadi ya matineja wanaokunywa kileo imeongezeka kwa asilimia 30 zaidi ya miaka ya 1950. Ujiuaji wa tineja umepanda kutoka visa vichache sana hadi kuwa kisababishi kikubwa cha tatu cha kifo baada ya aksidenti na uuaji. Miongoni mwa vijana kuanzia umri wa miaka 10 hadi 14, mimba zisizotakwa ziliongezeka kwa asilimia 23 kutoka 1983 hadi 1987, na kiwango cha kisonono kiliongezeka mara nne kati ya 1960 na 1988. Wanasaikolojia wanatafuta kwa kupapasa-papasa njia mpya za kuelewa na kusaidia vijana.
Kuwatazama Bila Kuwala
Kushika na kula nyangumi kumekuwa suala kuu katika miaka ya karibuni. Katika nchi chache, kama vile Japani, watu fulani wadai kwamba nyama ya nyangumi ni sehemu ya ulaji wao wa kitamaduni na wanakasirishwa na upigaji marufuku wa biashara ya nyangumi iliyowekwa na Tume ya Kimataifa ya Kuhifadhi Nyangumi. Hata hivyo, Wajapani fulani, wamevumbua kwamba nyangumi waweza kuleta faida bila kushikwa na kuliwa. Wakazi wa Visiwa vya Bonin, kusini mwa Tokyo, wana shughuli ya kupanua uvutio wao wa karibuni kwa watalii, kutazama nyangumi. Kwa kuona nyangumi katika makao yao ya asili badala ya kwenye sahani zao, watazamaji wa nyangumi hushangilia, hasa nyangumi wanapopuliza maji juu na kuruka huku na kule.
“Kichaa cha Bunduki”
Chini ya kichwa hicho, tahariri ya The New York Times la Mei 25 ilitoa maelezo juu ya kesi ya mtu mmoja wa Louisiana aliyeachiliwa huru kwa mashtaka ya kuua bila kukusudia mwanafunzi wa kigeni Mjapani mnamo Oktoba 1992. Mwanafunzi huyo wa umri wa miaka 16 alikuwa amefinya kengele ya mlango wa mtu huyo kimakosa. Amri ya mtu huyo ya kusimama wima ilipokosa kutiiwa na mwanafunzi huyo, ambaye hakuelewa maana yake, alimpiga risasi kifua mwanafunzi huyo Mjapani. “Una haki ya kumkabili kwa bunduki kila mtu anayekuja mlangoni pako,” akasema wakili wa mtu huyo kwa kumtetea. Tahariri hiyo ilisema kwamba, hilo, lamaanisha kwamba yeyote anayekuja mlangoni pako, kutia na “mhubiri . . . , aweza kutazamia risasi akijaribu kufinya kengele ya mlango wako.” “Sisi Wajapani hatuelewi ni kwa nini jamii ya Amerika inapenda sana kutumia bunduki,” akasema ripota Mjapani. “Kwa kweli, ni jambo rahisi,” tahariri hiyo ikajibu. “Hebu wazia ujinga, kutovumilia, maoni yaliyopotoka juu ya ‘haki ya kubeba silaha’ na kukataa kujifunza” kutokana na vifo vya watu wasiohesabika wanaouawa kwa bunduki.
Madereva Wanawake
Wanawake wanaoendesha magari husemwa kuwa wa hali ya chini kwa wanaume wenye ustadi wa kuendesha. Je! mambo ya hakika yathibitisha maneno hayo ya kijuujuu? Si kulingana na The Motorist, jarida linalochapishwa na Shirika la Magari la Afrika Kusini. Kati ya aksidenti zote za barabarani katika nchi hiyo katika mwaka mmoja wa karibuni, zaidi ya asilimia 83 zilihusisha madereva wanaume. Hivyo, makampuni mengi ya bima huwatolea madereva wanawake viwango vizuri kuliko wanaume. “Uhakika huu katika ustadi wa kuendesha wa wanawake,” laeleza gazeti lililotajwa juu, upo kwa sababu kampuni hiyo “yaamini kwamba wanawake si wagomvi sana wanapoendesha, si wenye kutokeza hatari mara nyingi, na wasioelekea kuvunja sheria za barabarani.” Gazeti hilo lamalizia kwamba mwelekeo unaofaa, bila kujali jinsia ya dereva, ndio huhakikisha tabia nzuri za kuendesha.
Hali ya Afya ya Ulimwenguni
Afya ya tufeni pote yaendeleaje? Ripoti iliyotia ndani mambo mengi iliyochapishwa karibuni na WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni) yatoa habari njema na mbaya. Habari njema ni kwamba ukambi, polio, kifaduro, na pepopunda ya watoto wachanga yamepungua kwa sababu ya jitihada za tufeni za kuchanja watoto. Maradhi ya moyo katika karibu nchi nyingi zilizositawi vilevile yamepungua. Viwango vya vifo vya vitoto vichanga na watoto vinapungua ulimwenguni pote, na matazamio ya maisha yanaongezeka. Habari mbaya, laripoti WHO, ni kwamba maradhi ya kitropiki, kama vile kipindupindu, homa ya manjano, kidingapopo, na malaria, “yaonekana kuwa yanaenea kwa njia isiyoweza kudhibitiwa.” UKIMWI, kifuakikuu, na kisukari pia yaongezeka.
Kamari ya Vidio
Mashine za kucheza kamari ya vidio ni “zenye kuzoewa kama dawa ya kulevya ya kokeni” na hazipaswi kuwa mahali pa hadhara, asema Garry Smith, profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Alberta. Akihojiwa katika The Edmonton Journal la Kanada, Smith, aliyeongoza uchunguzi wa kamari ya uzoevu, aandika kwamba uzoevu wa kamari ya vidio waweza kutokea katika “muda mfupi kama miezi sita.” Yeye aeleza kwamba mweneo wa kamari huleta ongezeko la uhalifu na matatizo mengine makubwa. Theluthi mbili ya wazoevu wa kamari hupunja na kulaghai, hudanganya, na kuiba ili kuendeleza tabia yao. Uzoevu huo huleta mshuko wa moyo na mawazo ya kujiua yanayosababisha uendeshaji magari wa kutojali na aksidenti, pamoja na kukosa kulipa madeni “na gharama za mifumo ya utunzaji wa afya.” Kulingana na Smith, “kila mcheza kamari mzoevu agharimu jumuiya dola za [Kanada] 56,000.”
Wabalehe wa Miaka ya 1990
Vittorino Andreoli, mchunguzi wa akili katika Chuo Kikuu cha Verona, Italia, aripoti kwamba tofauti na vizazi vilivyopita, vijana wa leo “wanakosa au wana uelewevu uliopungua wa wakati ujao.” Yeye aongezea kwamba jambo hili hufanya iwe vigumu kwa vijana “kujidhabihu kwa ajili ya furaha ya wakati ujao.” Wengi pia hukosa “uelewevu wa mema na mabaya,” ikimaanisha kwamba “mwenendo wote waamuliwa kwa hali ya wakati huo tu” badala ya kanuni fulani ya adili iliyowekwa. Vijana wengi leo hawaelewi kifo ni nini. Andreoli asema kwamba “wao wanajua kifo cha televisheni tu, cha madanganyo . . . Vijana wanajua jinsi ya kuleta kifo, lakini hawajui hicho ni nini. Hivyo, wanaweza kukisababisha au hata kukipasisha juu yao wenyewe, wakiwazia matokeo tofauti kabisa.”