Wazoezwaji Wapya wa Uchezaji Kamari—Vijana!
JE, WEWE hutikisa kichwa kwa kushangazwa na kina ambacho watu wazima, wanaume kwa wanawake, wamenaswa na uraibu wa uchezaji kamari? Je, wewe huona ikiwa vigumu kuwazia unaposoma juu ya wacheza-kamari walio watu wazima wakiacha kazi na matimizo yao ya maisha—kazi, biashara, familia, na, kwa wengine, uhai wao—kwa ajili ya kucheza kamari? Je, waweza kufahamu sababu ya msingi inayofanya mtu mzima aliye na elimu na aliyekomaa, ambaye, baada ya kushinda dola milioni 1.5, aliendelea kucheza hadi akapoteza dola milioni 7 usiku uo huo? Katika visa vingi ni pupa, kufuatia sana dola yenye kukwepa. Hata hivyo, mara nyingi mno, ni ule msisimko wenyewe wa kucheza kamari.
Mkiwa wazazi wenye watoto wachanga, je, nyinyi hujifariji kwa wazo la kwamba uchezaji kamari ni mchezo wa watu wazima waliokomaa? Basi fikirieni tena. Fikirieni wazoezwaji wapya wachanga walio tayari kujiunga na uchezaji kamari—au ambao tayari wanacheza kamari. Huenda mambo ya hakika yawashangaze.
Maelezo yafuatayo ya makala yalionekana katika magazeti ya habari na magazeti hivi majuzi: “Kuna Uwezekano Mkubwa wa Uchezaji Kamari Kuwa Utendaji Mbaya wa Adili wa Matineja Katika Miaka ya 1990.” “Vijana Zaidi Wanakuwa Waraibu wa Uchezaji Kamari.” “Kokeni Aina ya Kraki ya Miaka ya 1990: Uchezaji Kamari Wanasa Watoto.” “Mwana Wangu Hangeweza Kuacha Kucheza Kamari.”
Sasa, soma chini ya vichwa vikuu. “Mamlaka zalaumu huo msiba kwa sehemu kubwa juu ya ongezeko la uchezaji-kamari lililodhaminiwa na serikali na kanisa,” likaandika gazeti moja la habari. “Leo kubahatisha kunapatikana sana kwa vijana zaidi ya wakati mwingineo. Na wastadi wanaonya kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wacheza-kamari wenye ushurutisho zaidi walio watu wazima huingia kwenye hilo zoea kabla ya kufikisha miaka 14,” hilo gazeti likasema. “Zamani ilikuwa kwamba wacheza-kamari wengi wenye ushurutisho zaidi walianza kucheza kamari walipokuwa na umri wa miaka 14 hivi. Sasa twaona umri huo ukishuka hadi miaka 9 au 10,” akasema mtafiti mwingine. “Kwa nini? Kwa sababu fursa iko,” yeye akaongeza. “Watoto . . . hukumbwa na matangazo ya uchezaji kamari kila mahali. Ni raha inayokubalika kijamii.” “Hali hiyo inaendelea kuharibika haraka,” akasema msemaji wa Shirika la Kusaidia Waraibu wa Uchezaji Kamari. “Watoto waanza katika umri mchanga zaidi na zaidi, na wengi wao wananaswa zaidi ya wakati mwingineo wote.”
Kulingana na uchunguzi wa wacheza-kamari matineja katika jimbo moja la Marekani, asilimia 3.5 hivi walikuwa wacheza-kamari wenye ushurutisho wa wakati ujao; asilimia nyingine 9 yamkini wangekuja kuwa wacheza-kamari wenye “kujihatarisha.” “Kwa uhalisi, hizo idadi zimeonyesha kwamba kuna viwango vikubwa vya uchezaji kamari miongoni mwa vijana kuliko vilivyo katika watu wazima,” akasema William C. Phillips, mratibu wa huduma za kutoa shauri kwenye chuo kimoja cha Marekani. “Katika mwongo ufuatao tutakabili matatizo zaidi ya uchezaji kamari wa vijana kuliko tutakavyokabili utumizi wa dawa za kulevya—hasa utumizi usio halali wa dawa za kulevya,” akasema mshauri mwingine wa uraibu. Profesa Henry Lesieur alifanya uchunguzi wa wanafunzi wa vidato vya chini na vya juu vya sekondari. The Los Angeles Times liliripoti kwamba “matokeo yake yanafanana sana na uchunguzi wa wanafunzi wa vyuo: Asilimia za matineja walio wacheza-kamari ‘wa kupita kiasi’ au ‘wenye ushurutisho’—watu ambao wamepoteza udhibiti wa utendaji wao wa kucheza kamari—ni wastani wa asilimia 5 hivi ya idadi ya matineja taifani.”
Wanatiba wa uchezaji kamari wanakubali kwamba si idadi ya wacheza-kamari vijana inayowatia wasiwasi bali ni “mtazamo wa watoto, wazazi, na hata waelimishaji kuhusu uchezaji kamari wa matineja. . . . Watoto wengi na wazazi wao wanaona uchezaji kamari kuwa ‘kipitisha wakati kisichodhuru,’ kikiwa na matokeo yasiyo mabaya sana kama kujiingiza katika madawa ya kulevya na alkoholi au jeuri au ukosefu wa adili.” Lakini mshauri wa tabia Durand Jacobs alionya kwamba uchezaji kamari waweza kuingiza vijana katika uhalifu, uhepaji wa wajibu wao mbalimbali, na tamaa ya kupata pesa kirahisi.
Kwa kielelezo, fikiria mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari ambaye alianza kucheza kamari katika umri mchanga. Alipokuwa shuleni alitumia nyingi za saa zake za darasa kucheza kamari na wanafunzi wengine. Alipopoteza na pesa zake zikaisha, aliiba pesa kutoka katika michango ambayo wanafunzi walichanga kwa ajili ya vikapu vya chakula kwa familia zenye uhitaji. Kwa kucheza kamari akitumia pesa alizoiba, yeye alitumaini kununua tena televisheni ya familia yake na pete ya kito ambavyo alikuwa ameweka rehani ili kulipa madeni ya mapema ya uchezaji kamari. Kufikia wakati alipokuwa kidato cha kwanza, tayari alikuwa ameshafungiwa siku 20 katika jela ya watoto kwa kuiba dola 1,500 na alikuwa amejiingiza kupita kiasi katika uchezaji karata wa pesa na mchezo wa biliadi wa dola tano-tano. “Nilipokuwa nikiendelea kukua, hivyo viwango vilizidi kuwa vya juu,” yeye alisema. Mara akawa akiiba kutoka kwa majirani wake ili kulipia madeni yake ya kucheza kamari. Mama yake alitamauka. Kufikia umri wa miaka 18 alikuwa amekuwa mcheza-kamari mwenye ushurutisho.
Katika Uingereza, wastadi wa jamii wasema kwamba, sheria zisizo kali za uchezaji kamari huruhusu watoto wacheze na mashine za kutumbukizia visarafu. Katika nyanja za ndege na mahali penye maduka mengi, idadi kubwa za watoto hutegemeza uraibu wao kwa kuiba kutoka kwa wazazi wao na kuiba madukani.
“Miongoni mwa vijana, namna ya kamari ipendwayo zaidi na yenye kuongezeka kwa haraka mno katika vidato vya chini na vya juu vya shule ya sekondari na katika vyuo ni kubahatisha matokeo ya michezo miongoni mwa [wanafunzi] wenyewe nyakati fulani wakitegemezwa na wabahatishaji wa mahali hapo,” akasema Jacobs. “Ningekadiria kwamba kuna shule chache za sekondari na vyuo vichache ambavyo havina vikundi vilivyopangwa vizuri vya kutoa pesa nyingi za kubahatisha.” Kuongezea hayo kuna karata, bahati nasibu, na majumba ya kamari ambayo matineja wengi wanaruhusiwa kuingia kwa sababu ya kuonekana kuwa wenye umri mkubwa kuliko miaka yao.
“Moja ya hoja ambayo lazima itaarifiwe,” akasema Jacobs, “ni kwamba wengi wa watu waliendelea kuwa wacheza-kamari wenye ushurutisho kwa sababu walipoanza wakiwa matineja walikuwa washindaji.” “Ile ‘idadi kubwa zaidi’ ya vijana, yeye alisema, walijulishwa uchezaji kamari na wazazi wao au watu wa ukoo ambao waliona tu kuwa raha na mchezo,” likaendelea The Los Angeles Times. Mshauri mwingine wa utumizi mbaya wa vitu vyenye kuraibisha alieleza hivi: “Ni lazima wazazi wafikirie jambo lilelile la kale ambalo wamehitajika kushughulika nalo katika alkoholi na dawa za kulevya. Kulingana na maoni yangu kadiri unavyopanua uchezaji kamari, ndivyo wazoezwaji wapya wa uchezaji kamari watakavyopatikana.” Wastadi wanaotibu wacheza-kamari wenye ushurutisho wanasema kwamba kama ilivyo tu na dawa za kulevya na alkoholi, wanaponaswa katika uchezaji kamari vijana wengi zaidi wanategemeza uraibu wao kwa kuiba, kuuza dawa za kulevya, na kufanya ukahaba. Huenda wazazi wakaona uchezaji kamari kuwa “raha na mchezo,” lakini maofisa wa polisi hawaoni hivyo.
“Vijana waliopatwa na uraibu wa mashine hizi za kutumbukizia visarafu huenda walianza katika umri wa miaka 9 au 10. Walimaliza pesa za matumizi yao ya kibinafsi, pesa za mlo wa shuleni, na kiasi kidogo cha pesa wanazopata nyumbani. Mwaka mmoja au miwili baadaye wavulana hao walianza kuiba vitu. Kila kitu kingeuzwa kutoka chumbani mwao, vibao vya kupigia mpira, vitabu, hata hazina kama vile rekodiplea: watoto wengine wangepata vichezeo vyao vimeenda pia. Hakuna kitu nyumbani kilichokuwa salama. Moody alisikia akina mama waliohuzunika wakirundika vitu vyao katika chumba kimoja ili kuvilinda, au kuficha pochi zao chini ya matandiko ya kitanda walipokuwa wakilala. Wakiwa katika hali ya hangaiko, akina mama hao hawangeweza kufahamu zaidi kile kilichokuwa kikiwapata watoto wao kama vile ndege wenye makinda hawangeweza kufahamu lililotukia wanaponyang’anywa mayai na ndege aina ya mlembe. Hao watoto bado walifaulu kuiba mahali fulani. Kufikia umri wa miaka 16, polisi walikuwa wakibisha mlangoni.”—Easy Money: Inside the Gambler’s Mind, kilichoandikwa na David Spanier.
Kama ilivyotajwa katika makala hizi, watu wazima na vijana wengi wamejulishwa uchezaji kamari kupitia makanisa—karata, bahati nasibu, na kadhalika. Je, mashirika ya kidini na viongozi wavyo ambao wanadai kuwa wafuasi wa Kristo wanapaswa kutia moyo, kuendeleza, na kutegemeza uchezaji kamari katika namna yoyote ile? Kwa hakika sivyo! Uchezaji kamari katika namna zao zote huvutia moja ya sifa mbaya kuliko zote za binadamu, tamaa ya kupata kitu bure, au kwa kuweka wazi zaidi, pupa. Wale wanaouendeleza hutia watu moyo kuamini kwamba ni haki kupata faida kutokana na mapotezo ya wengine. Je, Yesu angeendeleza utendaji kama huo huku ukileta mvunjiko wa familia, aibu, afya mbaya, na uharibifu wa maisha ya mtu? Kamwe! Badala ya hivyo, Neno la Mungu lililopuliziwa husema wazi kwamba watu wenye pupa hawataurithi Ufalme wa Mungu.—1 Wakorintho 6:9, 10.
Lazima wazazi wafundishe watoto wao katika umri wa mapema kwamba uchezaji kamari wa aina yoyote ni kosa. Usiuone kuwa raha na mchezo bali uuone ukiwa mwanzo wa uvivu, udanganyaji, upunjaji, na ukosefu wa ufuatiaji haki. Katika majiji mengi mashirika ya kutoa msaada, kama vile Shirika la Kusaidia Waraibu wa Uchezaji Kamari, yameanzishwa. La maana zaidi ni, ikiwa una tatizo, tafuta shauri lililopuliziwa lipatikanalo katika Neno la Mungu, Biblia. Wengine ambao wamefikiria kujiua wanasema wanawiwa maisha zao na kufuata shauri hilo lililopuliziwa.
Kwa kupendeza, Mashahidi wa Yehova wamesaidia wengi ambao walinaswa katika mtego wa uchezaji kamari wenye ushurutisho wajiweke huru. Mchezaji mmoja wa kamari yenye kushurutisha aliandika kwamba baada ya miaka mingi ya kujiingiza katika upotovu wa adili, kutia ndani uchezaji kamari wa kupindukia, “mabadiliko ya mara hiyo na yenye kutazamisha yalianza kutokea msichana-rafiki wangu nami tulipoanza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Uchezaji kamari ulikuwa wenye kuraibisha sana, na ulithibitika kuwa mgumu kuuweza. Kwa msaada wa Yehova na utegemezo wa msichana-rafiki wangu—pamoja na funzo, sala, na kutafakari, hasa juu ya maoni ya Mungu kuhusu pupa—nilidhibiti uraibu huu wa kucheza kamari, na msichana-rafiki wangu, ambaye sasa amekuwa mke wangu kwa miaka 38, nami tuliweka maisha zetu wakfu kwa Yehova. Ingawa tumetumikia mahali ambapo kuna uhitaji mkubwa na katika utumishi wa wakati wote kwa miaka mingi nami nimetumika nikiwa mwakilishi asafiriye wa Watchtower Society, uraibu wangu uko bado na ninaudhibiti tu kwa msaada na mwongozo wa Yehova.”
Ikiwa uchezaji kamari ni tatizo kwako, je, waweza kuwekwa huru kutokana na huo uraibu? Ndiyo, ikiwa utaendelea kukubali msaada wa Mungu na kuutolea wengine ambao huenda wakawa na uhitaji wa huo.
[Blabu katika ukurasa wa 9]
Karibuni kutakuwa na matatizo zaidi ya uchezaji kamari wa vijana kuliko yatakavyokuwa ya dawa za kulevya
[Blabu katika ukurasa wa 11]
Watu wenye pupa hawataurithi Ufalme wa Mungu
[Sanduku katika ukurasa wa 10]
Visarafu vya Kuchezea Kamari Vyakubaliwa Katika Kanisa laKatoliki la Las Vegas
Watu wanaozuru Kanisa la Most Holy Redeemer mara nyingi huomba kasisi: “Padre, utaniombea nishinde?”
Kila mwaka mamilioni ya watu huzuru Las Vegas, Nevada, Marekani, kutoka ulimwenguni pote, ili kucheza kamari. Ndani ya madhabahu yenye wangavu wa rangi za ujoto, ya hilo Kanisa Katoliki ya Kiroma ambapo sanamu za shaba zenye fahari zilizo na Mandhari ya Kuzaliwa kwa Yesu, Mlo wa Mwisho, na Kusulubishwa huonekana ukutani, taratibu za uchezaji kamari zatumiwa katika viti vya kanisa: Waabudu huweka visarafu vya majumba ya kamari katika kisahani cha kukusanyia sadaka.
“Mara moja-moja sisi hupata kisarafu cha dola 500 katika moja ya hivyo visahani,” akasema Padre Leary katika lahaja ya Kiireland.
Kanisa Katoliki ya Kiroma lililo upande wa juu zaidi wa Ukanda wa Las Vegas lilitumiwa na waabudu hao kwa miongo mingi, lakini wakati manne ya majumba ya kuchezea kamari ya hoteli—MGM Grand, Luxor, Excalibur, na Tropicana—yalipojengwa kwenye ncha ya kusini mwa huo Ukanda, Kanisa jipya la Most Holy Redeemer lilijengwa umbali wa jengo moja kutoka hapo.
Kasisi alipoulizwa kwa nini jambo hilo lilifanywa, yeye alisema hivi: “Kwa nini isiwe hivyo? Hapo ndipo mahali ambapo watu wapo.”
Ndipo pia mahali ambapo pesa ziko. Kwa hiyo kwa nini isiwe hivyo?
[Picha katika ukurasa wa 9]
Uchezaji kamari huongoza kwenye mashirika mabaya