Maoni ya Biblia
Je! Kucheza Kamari Kwafaa Wakristo?
KUCHEZA KAMARI NI ZOEA LENYE GHARAMA. MARA NYINGI HUMALIZA NUSU YA MAPATO YA MTU NA YAWEZA KULETA MADENI MAKUBWA SANA. ZOEA HILI LAWEZA KUHARIBU NDOA NA KAZI-MAISHA NA HUENDA HATA LIKASABABISHA WENGINE WAHUSIKE KATIKA UHALIFU. WALIONASWA WANA URAIBU NA WAWEZA KUSUMBULIWA NA ATHARI ZA KUACHA KAMA ZILE ZIONWAZO KATIKA WARAIBU WENGINE.[1]
KUCHEZA KAMARI hufanyika kotekote hivi kwamba nchi fulani zaona jambo hilo kuwa “starehe ya kitaifa.”[2] Hata hivyo, kucheza kamari ni nini hasa? Kucheza kamari ni “kushindania matokeo ya tukio la wakati ujao,” yataarifu The World Book Encyclopedia. “Kwa kawaida wacheza-kamari hushindania fedha au kitu kingine cha thamani kikiwa ndicho kishindanio cha matokeo watabiriyo. Matokeo yakivumbuka, mshindi huzoa vishindanio vya washinde.”[3]
Kucheza kamari si jambo jipya. Wamaya wa kale wa Amerika ya Kati walikuwa wakicheza mpira uliopendwa sana uitwao poktatok—uliojulikana kwa Waazteki kuwa tlachtli—“ambamo watu fulani walipopoteza utajiri wao [kwa kucheza kamari ya mchezo huo], walishindanisha uhai wao wenyewe,” lasema gazeti Américas.[4] Wakale hawa waliambukizwa na homa hiyo ya kushindania vitu, nyakati nyingine “wakijasiria maisha ya utumwa kwa kushindania matokeo yasiyofaa kitu ya mdundo mmoja wa mpira.”[5]
Kwa nini wengi wameambukizwa na homa hiyo ya kucheza kamari? Kulingana na Duane Burke, msimamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Michezo ya Umma katika Marekani, “watu zaidi na zaidi wanaona kucheza kamari kuwa namna ya starehe inayokubalika.”[6] Hata mashirika fulani ya kidini huidhinisha kucheza kamari kuwa njia ya kuchangisha fedha.
Ingawa kucheza kamari kwapendwa sana na kuna historia ndefu, je, kwaweza kuwa starehe safi tu kwa Wakristo? Au mengi zaidi yahusika?
Kwa Nini Watu Hucheza Kamari?
Kwa ufupi, ili washinde. Kwa wacheza-kamari, kucheza kamari huonekana kuwa njia ya haraka na ya kusisimua ya kuchuma fedha bila jitihada na nidhamu ihusikayo katika kufanya kazi ya kimwili. Wakati mwingi hutumiwa kuwaziawazia “kushinda donge nono” na umaarufu na mali ambazo kibunda hicho chaweza kuwaletea.[7]
Lakini vipingamizi vya mcheza-kamari ni tele. Kwa kielelezo, mwanatakwimu Ralf Lisch asema kwamba katika Ujerumani “wewe waelekea kupigwa na radi mara nne mwakani kuliko ku[shinda] madonge ya bahati-nasibu [ya Ujerumani].”[8] Ikiwa hilo halisadikishi, yeye aongezea ulinganisho unaofuata: “Ikiwa wewe ni mwanamume, uwezekano wako wa kudumu hadi [umri wa] 100 ni mkubwa mara 7,000 kuliko [ule wa kushinda bahati-nasibu].”[9] Ajabu ni kwamba, huenda mcheza-kamari akawa ajua hilo. Basi, ni nini humfanya aendelee kucheza kamari?
Kulingana na Dakt. Robert Custer, katika kitabu chake When Luck Runs Out, kwa watu fulani wachezao kamari, “lile pato la fedha ni upande mmoja tu wa kushinda. . . . Kwao jambo la maana ni kile kijicho, staha, uvutio, kusifiwa-sifiwa ambako kushinda fedha kwaweza kuleta.” Aongezea kwamba kwa watu hao jambo la maana ni ule “msisimko wa kuweza kuonyesha-onyesha kibunda cha manoti au kusema tu, ‘Nilijishindia donge kubwa,’ na kuishi wakionea hilo fahari.”[10]
Kwa upande mwingine, kushinda—na ule msisimko mwambatani—bado hakutoshelezi wacheza-kamari wengi. Huenda kichocheo cha kucheza kamari kikaimarika sana hata wakawa wacheza-kamari wa kushurutika. Katika uchunguzi ulioendeshwa na Dakt. Custer na wanachama wa Wacheza-Kamari Wasiotajwa Jina, asilimia 75 ya waliochunguzwa walisema walikuwa wakijigamba juu ya kushinda hata walipokuwa wakipata hasara![11] Ndiyo, kucheza kamari huenda kukawa uraibu mkali na mharibifu kama uraibu wa alkoholi au dawa nyingineyo ya kulevya. Ni wacheza-kamari wangapi wameteleza wakaangukia uraibu wa kucheza kamari wakiwaza wanajistarehesha tu? Ni wangapi wamefanya hivyo hata bila kujua hivyo?
Maoni ya Mungu
Biblia haizungumzii kucheza kamari kirefu. Hata hivyo, yaandaa kanuni zitusaidiazo kujua jinsi Mungu aonavyo kucheza kamari.
Yaliyoonwa yameonyesha kwamba kucheza kamari ni dalili ya pupa. Biblia hushutumu pupa vikali, ikionya kwamba ‘hakuna mtu mwenye pupa angekuwa na urithi wowote katika ufalme wa Mungu.’ (Waefeso 5:5, NW) Pupa huonwa hata wacheza-kamari wapatapo hasara. Kulingana na mjuzi mmoja, mcheza-kamari “hujaribu kushinda arudishe hasara aliyopata—akitafuta kushinda ‘donge nono.’ Akishinda kibunda, hushindania kikubwa zaidi, na hatimaye kupata hasara ya ‘donge nono’ lake.”[11a] Ndiyo, hakika pupa ni sehemu ya kucheza kamari.
Kucheza kamari hutumiwa na wengine kama njia ya kukuza majivuno yao. Uchunguzi mmoja ulioendeshwa pamoja na wacheza-kamari wa kushurutika ulionyesha kwamba asilimia 94 waliona kucheza kamari kuwa ni “utendaji wa kujiongezea hali ya kujiona,”[12] na asilimia 92 wakasema walihisi kwamba wao “si kidogo” walipocheza kamari.[13] Hata hivyo, Mungu asema: “Kiburi na majivuno . . . nakichukia.” Hivyo, Wakristo huhimizwa wasitawishe kiasi na unyenyekevu.—Mithali 8:13; 22:4; Mika 6:8.
Kucheza kamari huenda kukasababisha uvivu pia, maana huonekana kama njia rahisi ya kuchuma fedha bila ile jitihada ihusikayo kazini. Lakini Neno la Mungu lahimiza wazi Wakristo wafanye kazi ngumu, ya bidii nyendelevu.—Waefeso 4:28.
Tena, kile wakiitacho bahati ni cha maana sana kwa wacheza-kamari fulani hivi kwamba huwakolea sana, wakikifanya mungu wao. Ni kama ule usimulizi wa Biblia juu ya watu waliokuwa “wakiandika meza kwa ajili ya Bahati [“mungu wa Bahati Njema,” NW].” Kwa sababu ya tendo lao la ibada ya sanamu wangekufa “kwa upanga.”—Isaya 65:11, 12.
Namna gani mtu akitolewa bure tikiti ya bahati-nasibu au fedha za bure azitumie kucheza kamari? Kwa lolote la hayo, kukubali toleo hilo kungekuwa bado ni kuunga mkono shughuli ya kucheza kamari—shughuli isiyopatana na kanuni za kimungu.
Kucheza kamari hakuwafai Wakristo, hapana. Kama mhariri mmoja wa gazeti alivyoeleza, ‘si kwamba kucheza kamari ni kosa tu bali pia ni kishindanio kisichofaa.’[14]
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]
Valentin/The Cheaters, Giraudon/Art Resource