Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 9/22 kur. 6-8
  • Wacheza-Kamari Wenye Ushurutisho—Hupoteza Sikuzote

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wacheza-Kamari Wenye Ushurutisho—Hupoteza Sikuzote
  • Amkeni!—1995
  • Habari Zinazolingana
  • Wazoezwaji Wapya wa Uchezaji Kamari—Vijana!
    Amkeni!—1995
  • Je! Kucheza Kamari Kwafaa Wakristo?
    Amkeni!—1994
  • Kuna Ubaya Gani Kucheza Kamari?
    Amkeni!—2002
  • Nimenaswa! Naweza Kuachaje Kucheza Kamari?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 9/22 kur. 6-8

Wacheza-Kamari Wenye Ushurutisho—Hupoteza Sikuzote

“UCHEZAJI kamari wenye kushurutisha ni ugonjwa kama vile uraibu wa alkoholi na dawa za kulevya ulivyo ugonjwa,” akatangaza Profesa Jean Ades, kutoka Ufaransa. “Ni uraibu usioletwa na dawa za kulevya,” yeye akasema, na “watu wengi zaidi wanagundua kwamba wameraibika.” Hata baada ya wachezaji kamari wenye ushurutisho kupoteza kiasi kikubwa mno cha pesa, mara nyingi wao huchochewa na uhitaji wa kulipia mapotezo yao kwa kucheza kamari hata zaidi. “Wapotezaji wengi hushinda kwa haraka hali yao ya kupoteza. Lakini kwa wengine, shurutisho la kucheza kamari ni gumu mno kudhibitiwa hivi kwamba laweza kuzorotesha maisha zao,” akaandika mwandishi mmoja wa habari katika Ufaransa. “Wao huendelea kujiahidi kwamba watakuja kuacha hilo zoea, lakini hilo huwadhibiti sikuzote. Wao ni waraibu wa uchezaji kamari.”

Mchezaji kamari mmoja wa Afrika Kusini aliungama hivi: “Ikiwa wewe ni mraibu wa uchezaji kamari, na waketi kwenye kizungushi duara na meza ya kuchezea karata, hujali kitu kinginecho chote. Wasisimka sana, na utacheza kamari kila ndururu uliyo nayo kwa mzunguko mmoja tu wa duara, au duru moja tu ya mchezo. . . . Kwa sababu ya msisimko wangu, nilikuwa nikikesha kwa siku kadhaa mchana na usiku bila kupumzika, nikiangalia kadi na nambari, na kungojea malipo hayo makubwa ambayo sikuzote hayapatikani kwa urahisi.” Kisha yeye akamalizia hivi: “Kuna wengi walio kama mimi ambao hawawezi kuacha mchezo [baada ya kupoteza] mamia machache au hata maelfu machache ya rand. Tutaendelea kucheza kamari hadi tumalize pesa zote tulizo nazo, na mahusiano yetu ya kifamilia huharibika yasiweze kurekebika.”

Henry R. Lesieur, profesa wa mambo ya jamii kwenye Chuo Kikuu cha St. John’s, New York, aliandika kwamba tamaa ya kucheza kamari, bila kujali kushinda au kushindwa, ni yenye nguvu mno “hivi kwamba wacheza-kamari wengi watapitisha siku kadhaa bila usingizi, bila kula, na hata bila kwenda msalani. Kukaza fikira zote kwenye uchezaji kamari huondoa mahangaiko mengine yote. Katika kipindi cha matarajio, pia kuna ‘msisimko’ fulani, ambao kwa kawaida huonyeshwa na viganja vyenye jasho-jasho, mpigo wa haraka wa moyo, na kuhisi kutapika.”

Mmoja aliyekuwa mraibu wa uchezaji kamari akiri kwamba si kushinda kulikosukuma zoea lake lenye kuendelea, bali ulikuwa ule “msisimko,” raha ya kucheza kamari yenyewe. “Kucheza kamari huleta hisia zenye nguvu isivyo kawaida,” yeye akasema. “Kizungushi duara kigeukapo, unapongojea Bahati yako, kuna wakati ambapo akili huzunguka vuruvuru na mtu huhisi kuzirai.” Mcheza-kamari Mfaransa André akubali hivi: “Uchezapo kamari Franca 10,000 za Ufaransa kwa farasi na meta 100 zinabaki ili mbio ziishe, mtu aweza kukuambia mke wako au mama yako amekufa na hutajali hata kidogo.”

André afafanua jinsi alivyoweza kuendelea kucheza kamari hata baada ya kupoteza kiasi kikubwa cha pesa. Yeye alikopa kutoka banki, marafiki, na wakopeshaji wenye kutoza riba za juu mno. Yeye aliiba hundi na kudanganya kwa vitabu vya akaunti ya akiba ya posta. Alishawishi wanawake wapweke alipozuru majumba ya kamari na kutokomea na kadi zao za mkopo. “Kufikia wakati huo,” akaandika mwandishi wa habari Mfaransa, “André hata hakujali tena ikiwa angeweza kupanga vizuri fedha zake. Mizururo yake ilichochewa hasa na shurutisho lake.” Aligeukia uhalifu na kupelekwa jela. Ndoa yake ikavunjika.

Katika visa vingi wacheza-kamari wenye ushurutisho, kama vile waraibu wa dawa za kulevya na waraibu wa alkoholi, huendelea kucheza kamari, ingawa hilo hufanya wapoteze kazi zao, biashara zao, afya yao, na, hatimaye, familia zao.

Majiji mengi katika Ufaransa hivi majuzi yamekubali uchezaji kamari. Mahali ambapo biashara nyingine zimeshindwa, maduka ya rehani yanafanya biashara zenye kusitawi mno. Wenye maduka hayo wanasema kwamba wacheza-kamari mara kwa mara hupoteza pesa zote walizo nazo na huuza pete, saa za mkononi, mavazi, na vitu vingine vyenye thamani ili kupata pesa za petroli ya kurudia nyumbani. Katika miji mingine ya pwani katika Marekani, maduka mapya ya rehani yamefunguliwa; katika visa fulani matatu au manne au zaidi yaweza kupatikana kwa mfuatano.

Wengine hata wamegeukia maisha ya uhalifu ili kutegemeza zoea lao la kucheza kamari. Chunguzi zilizofanywa hadi wakati huu, kulingana na Profesa Lesieur, “zilifunua namna mbalimbali za tabia zisizo halali miongoni mwa wacheza-kamari . . . kudanganya kwa hundi, wivi wa fedha zilizowekwa amana, wivi, unyang’anyi kwa silaha, ubahatishaji, kupata pesa kwa hila, udanganyifu, na kuuza vitu vilivyoibwa.” Juu ya hayo kuna uhalifu wa hali ya juu ambapo wacheza-kamari huiba kutoka kwa waajiri wao. Kulingana na Gerry T. Fulcher, mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu na Utibabu wa Wacheza-Kamari Wenye Ushurutisho, asilimia 85 ya maelfu ya wacheza-kamari wenye ushurutisho wanaojulikana walikubali kuwa waliwaibia waajiri wao. “Kwa hakika, kifedha, shurutisho la kucheza kamari laweza kuwa baya zaidi ya uraibu wa alkoholi pamoja na matumizi ya dawa za kulevya yakichanganywa,” akasema.

Chunguzi zaidi zimeonyesha kwamba ni kadiri ya thuluthi mbili ya wacheza-kamari wenye ushurutisho ambao hawakufungwa na asilimia 97 ya wale waliofungwa wanakubali kwamba walijiingiza katika mwenendo usio halali ili kulipia uchezaji kamari au kulipia madeni yaliyotokezwa na uchezaji kamari. Katika mwaka wa 1993 katika miji iliyoko Ghuba ya Pwani ya Marekani, mahali ambapo uchezaji kamari uliohalalishwa ni mwingi mno, kulikuwa na visa 16 vya wivi wa mabavu katika banki, ongezeko la mara nne kuliko mwaka uliotangulia. Mtu mmoja aliiba kimabavu jumla ya banki nane kiasi cha dola 89,000 ili kuendeleza zoea lake la kucheza kamari. Banki nyingine zimeibwa kimabavu kwa bunduki na wacheza-kamari waliolazimishwa kulipa deni la kiasi kikubwa mno cha fedha kwa wenye kuwadai.

“Wacheza-kamari wenye ushurutisho wanapojaribu kuacha hilo zoea, wanapata ugonjwa wa kuacha zoea hilo, kama vile wavutaji sigareti au waraibu wa dawa za kulevya,” lasema The New York Times. Hata hivyo, wacheza-kamari wanakiri kwamba kushinda zoea la kucheza kamari kwaweza kuwa kugumu kuliko kushinda mazoea mengine. “Baadhi yetu tumepata kuwa waraibu wa alkoholi na matumizi mabaya ya dawa za kulevya pia,” akasema mmoja, “na sote twakubali kwamba uchezaji kamari wenye ushurutisho ni mbaya zaidi sana kuliko uraibu mwengineo wote.” Dakt. Howard Shaffer, wa Kitovu cha Uchunguzi wa Uraibu kwenye Chuo Kikuu cha Harvard, alisema kwamba angalau asilimia 30 ya wacheza-kamari wenye ushurutisho ambao hujaribu kuacha “huonyesha ugonjwa wa kuchokozeka, au kupata mkazo wa tumbo, matatizo ya usingizi, msongo wa damu na mpigo wa moyo wa juu isivyo kawaida.”

Hata wakiendelea kubahatisha, akasema Dakt. Valerie Lorenz, mkurugenzi wa Kitovu cha Kitaifa cha Uchezaji Kamari Usio wa Kawaida katika Baltimore, Maryland, Marekani, “wacheza-kamari wenye ushurutisho hupata magonjwa ya kitiba: kuumwa na kichwa kusikokoma, maumivu ya kichwa yanayoandamana na kisunzi na kutapika, magumu ya kupumua, maumivu ya kusongwa pumzi, kubadilika kwa mwendo wa mpigo wa moyo na kufa ganzi katika mikono au miguu.”

Halafu kuna ujiuaji. Nini kiwezacho kuwa kibaya kuliko kile kijulikanacho kwa kawaida kuwa “uraibu usio hatari” usababishao kifo? Kwa kielelezo, katika wilaya moja ya Marekani, ambapo majumba ya kuchezea kamari yamefunguliwa majuzi, “kiwango cha ujiuaji kimerudufika isivyoelezeka,” likaripoti The New York Times Magazine, “ingawa hakuna ofisa wa afya aliyekuwa tayari kuhusianisha hilo ongezeko na uchezaji kamari.” Katika Afrika Kusini, wacheza-kamari watatu walijiua katika juma moja. Idadi halisi ya ujiuaji kwa sababu ya uchezaji kamari na madeni uliotokea kupitia njia hii, kihalali au isivyo halali, haijulikani.

Ujiuaji ni njia yenye msiba ya kumaliza mshiko mkali wa uchezaji kamari. Katika makala ifuatayo, fikiria jinsi wengine wamepata njia ya kujiweka huru.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Maduka ya rehani yanasitawi —ndivyo na uhalifu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki