Paradiso isiyo na taabu—Je, ni Ndoto Tu?
“KUNA utulivu sana!” Mandhari iliyoonekana kutoka kwenye msitu wa misunobari juu ya Ziwa Redfish katika jimbo la Idaho, Marekani, hakika ilikuwa shwari. “Inafanana tu na jinsi ninavyowazia paradiso kuwa,” huyo msafiri akasema.
Jua liliangaza pwani ya kusini mwa kisiwa cha Mediterania cha Saiprasi. Mawimbi yalitua kwa uanana ufuoni. Akiwa ameketi katika mkahawa mmoja ulio juu ya genge kuelekea mandhari hiyo ya mbali, huyo mgeni akapaaza sauti akisema: “Hii ni paradiso!”
Wengi wetu huthamini sana kumbukumbu za mandhari kama hizi. Lakini wakazi hutambua kwamba mazingira ya kiparadiso mara nyingi hufunika uhalisi mgumu wa maisha ya kila siku: mioto ya misitu kwenye miteremko ya Milima ya Rocky, uchafuzi wa bahari unaoathiri samaki na hatimaye wanadamu—kwa kuongezea mapambano yenye kutisha uhai ya kimataifa na ya kijumuiya.
Paradiso—Hiyo Ni Nini?
Wewe waionaje paradiso? Kamusi The New Shorter Oxford English Dictionary yasema hivi katika ufafanuzi wake wa kwanza: “Bustani ya Edeni ambayo imefafanuliwa katika Mwa[nzo] 2, 3.” Huo warejezea ufafanuzi ulio katika kitabu cha kwanza cha Biblia kuhusu eneo ambalo Mungu alimweka mwanadamu wa kwanza, Adamu. Katika Paradiso hiyo ya awali, miti ‘inayotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa’ ilisitawi sana.—Mwanzo 2:9.
Ufafanuzi wa pili wa kamusi hiyo huhusisha “paradiso” na “Mbingu, katika theolojia ya Kikristo na ya Kiislamu” lakini kisha inaongezea: “Sasa hasa ni ya [ki]shairi.” Hata hivyo, kwa msafiri wetu na mgeni anayezuru, paradiso ilikuwa “eneo la uzuri au upendezi usio na kifani,” ambao ni ufafanuzi wa tatu wa ile kamusi.
Mkuu wa serikali ya Uingereza wa karne ya 16, Sir Thomas More, aliandika kitabu chenye kichwa Utopia ambamo ndani yake alifafanua nchi ya kuwaziwa ambamo sheria, serikali, na hali za kijamii zilikuwa kamilifu. Ufafanuzi wake haukuwa halisi hivi kwamba leo kamusi Webster’s New Collegiate Dictionary hutoa ufafanuzi mmoja kwa neno “Utopia” kuwa “mpango usioweza kutumika wa kufanya maendeleo ya kijamii.”
Kwa wafuasi wa kiongozi wa madhehebu ya People’s Temple aliyeitwa Jim Jones, Utopia ilikuwa mahali fulani palipo wazi katika msitu wa Guyana. Kwa kusikitisha, katika 1978 paradiso hiyo iliyotumainiwa ikawa mahali pa vifo vya zaidi ya watu 900 kati yao—ogofyo kwelikweli! Tokeo likawa kwamba nyakati nyingine watu huhusisha wazo la paradiso na madhehebu ya ajabu-ajabu yenye mazoea ya kushtusha na kusumbua.
Katika ulimwengu ambamo uhalifu na ujeuri hutisha, ambamo maradhi hutisha watu wazima kwa watoto, na ambamo tofauti za kidini hugawanya jumuiya, mazingira maridadi mara nyingi hufunika uhalisi wa hali. Si ajabu kwamba watu hufikiri paradiso kuwa ndoto tu! Lakini jambo hili halijakomesha wengine wasijaribu kutafuta au hata kujifanyizia paradiso yao wenyewe. Wao wamefanikiwa kadiri gani?