Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 10/8 kur. 24-25
  • Siri za Usingizi wa Wanyama

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Siri za Usingizi wa Wanyama
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mabingwa wa Usingizi
  • Kulala Usingizi ‘Wakiwa Angani’?
  • Usingizi Chini ya Maji
  • Kuacha Jicho Moja Likiwa Wazi
  • Sababu ya Mwili Wako Kuhitaji Usingizi
    Amkeni!—1995
  • Nifanye Nini Ili Nipate Usingizi wa Kutosha?
    Vijana Huuliza
  • Usingizi Ni Starehe Tu au Ni Muhimu?
    Amkeni!—2003
  • Usingizi—Kwa Nini Ni Muhimu Sana?
    Amkeni!—2011
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 10/8 kur. 24-25

Siri za Usingizi wa Wanyama

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA

USINGIZI—sisi hutumia thuluthi moja hivi ya maisha zetu katika hali hiyo ya mapumziko. Mbali na kupoteza wakati, yaonekana usingizi hutimiza mahitaji kadhaa ya maana ya kifiziolojia na kisaikolojia. Kwa hiyo usingizi waweza kuonwa kama zawadi yenye thamani kutoka kwa Mungu.—Linganisha Zaburi 127:2.

Haishangazi kuwa usingizi unatimiza pia fungu la maana katika ulimwengu wa wanyama. Kwa kweli, spishi nyingi huweza kulala katika njia zenye kuvutia sana, wakati mwingine za kuchekesha, na mara nyingi kwa njia zisizo za kawaida. Acheni tutazame vielelezo vichache.

Mabingwa wa Usingizi

Yeyote ambaye amemwona simba akiwa amelala chali na miguu ikiwa imeelekea juu katika jua kali la adhuhuri la Afrika aweza kufikiri kwamba mnyama huyu mkali ni mpole kama paka wa nyumbani. Hata hivyo, mwonekano hudanganya. Mwandikaji wa karne ya 17 Thomas Campion aliandika hivi: “Ni nani awezaye kuthubutu kumchokoza simba anayelala usingizi?” Ndiyo, hata simba mwenye uweza ahitaji usingizi—karibu muda wa saa 20 kwa siku—ili kumwezesha kuendelea na mtindo-maisha wake wa kuwinda.

Fikiria pia, tuatara, mnyama mwenye kusinzia-sinzia anayefanana na mjusi apatikanaye huko New Zealand. Yeye hutumia nusu ya mwaka akiwa katika hali ya kutotenda sana. Kwani, tuatara ni mvivu sana hivi kwamba yeye hulala usingizi hata anapotafuna chakula! Lakini usingizi huo wote bila shaka ni wenye manufaa, kwani wanasayansi wakadiria kuwa tuatara wengine waweza kuishi kufikia miaka 100!

Kama vile Rip Van Winkle katika hadithi za kubuniwa, viumbe wengine pia hulala usingizi kwa vipindi virefu. Hii ndiyo njia ambayo wengi wa wanyama hao huendelea kuishi katika majira baridi ya kipupwe. Kwa kujitayarisha, mnyama huyo huweka akiba ya tabaka kubwa za mafuta ambayo yatakuwa kama lishe kwa kipindi chake kirefu cha usingizi. Ingawa hivyo, ni nini kinachomzuia mnyama huyo anayelala usingizi asigande na kufa? Kama vile kitabu Inside the Animal World kinavyoeleza, ubongo hutendesha badiliko katika kemikali zilizo katika damu ya mnyama, ikitokeza kitu cha kiasili cha kuzuia kuganda. Kadiri hali joto ya mnyama inavyopungua kufikia karibu tu kuganda, mpigo wake wa moyo hupunguka kuwa sehemu ndogo tu ya mpigo wa kawaida; kupumua kwake pia hupungua. Kisha usingizi mzito huanza, na aweza kulala usingizi kwa majuma mengi.

Kulala Usingizi ‘Wakiwa Angani’?

Wanyama wengine hulala usingizi katika njia zisizo za kawaida sana. Fikiria ndege wa baharini aitwaye membe-masizi. Wakati membe-masizi mchanga akiachapo kiota, huelekea kwenye bahari na huendelea kuruka kwa miaka michache itakayofuata bila kutua! Kwa kuwa hana manyoya yawezayo kukinza maji wala utando wa ngozi kati ya vidole vyake kama vile vya membe wengine wanaoweza kutua majini, membe-masizi huepuka kuzamishwa baharini. Yeye huwinda kwa kuchukua haraka samaki wadogo walio kwenye uso wa maji.

Lakini yeye hulala wakati gani? Kitabu Water, Prey, and Game Birds of North America chasema: “Haielekei kuwa wanalala usingizi baharini kwani mabawa yao yatalowa maji. Wanasayansi fulani hudokeza kwamba ndege hawa waweza kulala usingizi wakiwa angani.”

Usingizi Chini ya Maji

Je, samaki hulala usingizi? Kulingana na The World Book Encyclopedia, kati ya wanyama wenye uti wa mgongo “ni wanyama-watambaazi, ndege, na mamalia tu wanaolala usingizi halisi, kukiwa na mabadiliko katika vigezo vya wimbi katika ubongo.” Hata hivyo, samaki hufurahia vipindi vya mapumziko vinavyofanana na usingizi—ingawa wengi hawawezi kufumba macho yao.

Samaki wengine hulala kwa upande; wengine, vichwa vikiwa chini na mikia juu, au wakiwa wima. Samaki wengine walio bapa kama vile kibingirike, hukaa chini kwenye sakafu ya bahari wakati wako macho. Wanapokuwa wamelala, wao huwa katika hali ya kuelea sentimeta kadhaa kutoka kwenye sakafu ya bahari.

Yule parrot fish mwenye rangi yenye kupendeza ana kawaida ya kipekee ya saa ya kulala: Yeye huvaa “gauni ya usiku.” Kadiri kipindi chake cha kupumzika kinavyokaribia, yeye hutoa ute wenye utelezi, ambao hufunika kabisa mwili wake. Kusudi likiwa nini? “Yaonekana ili kuzuia wawindaji wasimtambue,” asema mwandikaji wa mambo ya asili Doug Stewart. Yeye hutoka kwenye nguo hiyo yenye utelezi anapoamka.

Sili vilevile wana kawaida ya ajabu ya saa ya kulala. Wao hufurisha koo zao kama baluni, wakifanyiza namna ya jaketi ya asili ya kuokoa uhai. Wakielea hivi, wanaweza kulala wakielea wima katika maji pua zao zikiwa nje ili wapumue.

Kuacha Jicho Moja Likiwa Wazi

Bila shaka, kulala usingizi porini hufanya mnyama kuwa rahisi kushambuliwa na wanyama wawindaji. Hivyo, ni kana kwamba viumbe wengi hulala usingizi jicho moja likiwa wazi. Ubongo wao huwa chonjo kiasi fulani wanapolala usingizi, hilo likiwaruhusu kuitikia kwa sauti zozote zinazoashiria hatari. Na bado wanyama wengine husalimika kwa kufanya uchunguzi wa usalama wa mara kwa mara. Kwa kielelezo, ndege wanaolala katika vikundi, mara kwa mara watafungua jicho moja na kuchungulia, wakiangalia ikiwa kuna hatari.

Makundi ya aina fulani ya paa na punda-milia katika Afrika vilevile huchunga wenzao katika vipindi vya mapumziko. Wakati mwingine kundi nzima hujilaza chini vichwa vikiwa juu wakiwa wametahadhari. Pindi kwa pindi, mnyama mmoja atapinduka na kulala kwa upande na kupata usingizi mzito. Baada ya dakika chache, mshiriki mwingine wa hilo kundi anachukua zamu yake.

Tembo vilevile hulala usingizi wakiwa kundi. Hata hivyo, tembo wazima huendelea kusimama na hawalali usingizi mzito, wakifumbua macho yao mara kwa mara, wakiinua na kusambaza masikio yao makubwa kusikiliza sauti zozote za hatari. Wakiwa chini ya kivuli cha walinzi hawa wakubwa, ndama wadogo zaidi wana uhuru wa kulala kwa upande na kupata usingizi mzito. Katika kitabu chake Elephant Memories, mwandikaji Cynthia Moss akumbuka akiona kundi zima la tembo likilala usingizi: “Kwanza ndama wachanga, kisha wale wakubwa, na mwishowe tembo wazima wa kike wote walilala chini na kupata usingizi. Katika mwangaza wa mbalamwezi walionekana kama majabali ya kijivu, lakini kukoroma kwao kutoka ndani kwa hali yenye amani kulitofautiana na mwono huo.”

Tungali tuna mengi ya kujifunza kuhusu tabia za usingizi za wanyama. Lakini unapofikiria yale machache tunayojua, je, hausukumwi kufikiria kuhusu hekima yenye kutisha ya Yule ambaye ‘aliviumba vitu vyote’?—Ufunuo 4:11.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki