Kugema Mawingu
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AMERIKA KUSINI
WATAFITI wafanyao kazi katika Chile wamefanikiwa kutumia mbinu ya kale ya Kiarabu ambayo huvuta maji kutoka katika ukungu. “Mizeituni katika majangwa ya Oman,” chaeleza kijarida Health InterAmerica, “imekuzwa kwa karne nyingi na maji ya ukungu ambayo hujikusanya katika matawi na kutiririkia matangi madogo yaliyojengwa chini ya miti.” Badala ya mizeituni, watafiti hao huweka nyavu kubwa katika maeneo ya jangwa yenye milima ambayo kwa kawaida hufunikwa na ukungu uvumao kutoka baharini. Hizo nyavu, ambazo huonekana kama nyavu kubwa za voliboli, hunasa matone ya maji kutoka katika ukungu. Matone hayo hudondokea mchirizi ambao huyatia maji hayo katika mfereji, ambao nao huyasafirisha maji hayo hadi katika matangi ya kuhifadhia.
Chungungo, kijiji kidogo kilichoko katika jangwa la kaskazini la pwani ya Chile, kimethibitisha kwamba njia hii inafanya kazi kwa mafanikio. Miaka kumi na minne iliyopita, lasema IDRC Reports, gazeti lichapishwalo na Kituo cha Utafiti cha Maendeleo ya Kimataifa cha Kanada, wakazi wa Chungungo hawakuwa na chanzo cha kwao cha maji safi. Malori yalileta lita 5,000 za maji kwa siku, na kila familia ililazimika kupata kati ya lita 3-14 kwa siku. Hata hivyo, leo, kwa sababu ya nyavu hizo 75 zikusanyazo ukungu ambazo zimewekwa milimani juu ya kijiji hicho, kwa kushangaza, lita 11,000 za maji zinatiririka kuelekea Chungungo, zikiandalia kila mwanakijiji lita 30 za maji kwa siku. Mtafiti Dakt. Robert Schemenauer, mwanafizikia wa mawingu, asema kwamba mfumo wa ugemaji wa ukungu umeboresha afya za wanakijiji. “Kila mtu anakula mboga na matunda kutokana na bustani zao na mashamba yao ya matunda.”
Maji yatokanayo na ukungu hayachangii afya nzuri tu bali pia hayana gharama. Wastani wa uwekwaji wa nyavu hizo, asema Dakt. Schemenauer, hugharimu kiasi cha dola 75,000 (za Marekani) kwa kulinganisha na mamilioni ya dola yahitajiwayo kujenga bwawa. Watafiti wasema kwamba ingawa maeneo mengineyo mengi yenye ukame ulimwenguni kote yangeweza kufaidika na mpango huu, mashirika ya kimataifa yamezembea kutambua njia hii ya badala ya kupata maji.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Kushoto: Nyavu juu ya kilele cha mlima ambazo hukusanya matone ya maji kutoka katika ukungu
Chini: Picha ya karibu ya huo wavu
[Hisani]
Picha: IDRC