Msaada kwa Nyayo Zinazouma
“NYAYO zangu zaniua!” Bila shaka, msemo huo umetiliwa chumvi mno. Hata hivyo, tatizo la nyayo zinazouma ni kubwa sana katika Marekani hivi kwamba maelfu ya wataalamu wa nyayo hawakosi kazi.
Baada ya kupitia upasuaji wa nyayo zaidi ya 2,000 aliofanya katika kipindi cha miaka 14, Dakt. Michael Coughlin, daktari-mpasuaji wa kasoro na magonjwa ya mifupa, alifanya ugunduzi wenye kushtusha. “Kwa kushangaza,” yeye asema, “nilipata kuwa karibu upasuaji wote huu ulifanywa kwa wanawake.” Kwa nini wanawake ndio hasa wana mwelekeo wa kupatwa na matatizo ya nyayo?
Jinsi Vinavyotosha, Mtindo, na Nyayo
Uchunguzi wa wanawake 356 ulipata kwamba karibu wanawake 9 kati ya 10 walivaa viatu ambavyo, kwa wastani, vilikuwa vyembamba zaidi kwa nyayo zao kwa saizi nzima! Sehemu ya tatizo ni njia ambayo viatu vya wanawake vimetengenezwa. “Watengeneza-viatu hawatumii tena vibao vya kutengenezea viatu vyenye muundo wa kisigino chembamba na mguu-mbele mpana,” aeleza daktari-mpasuaji wa kasoro na magonjwa ya mifupa, Francesca Thompson.
Hivyo, wanapojaribu viatu, wanawake wengi hupata ya kwamba ikiwa mbele chatosha vizuri, kisigino ni kikubwa; lakini wakati kisigino chatosha vizuri, mbele chabana. Wengine huchagua kisigino kinachotosha vizuri na mbele kubanwa, kwani chaguo jingine lingefanya kiatu kitoke katika kila hatua.
Kufinya sehemu ya mbele ya wayo katika sehemu nyembamba ya mbele ya kiatu hakuonekani kama kunastarehesha. Lakini tatizo lazidi wakati wabuni wa viatu warefushapo kisigino cha kiatu kwa sentimeta kadhaa. Ingawa huonekana kuwa ya mtindo, kisigino kirefu huweka mkazo wote katika kidole kikubwa cha mguu, nacho husukuma wayo kwenye sehemu ya mbele ya kiatu ambayo huenda tayari ni nyembamba mno. “Hakuna kitu kama kiatu chenye kisigino kirefu cha kiafya,” adai Dakt. David Garrett, mtaalamu wa nyayo za kibinadamu. Wengine husema kuwa visigino virefu hatimaye vyaweza kuharibu nyayo, vifundo, shavu la mguu, magoti, na mgongo. Vyaweza pia kufupiza misuli ya miguu na kano, ambalo laweza kufanya iwe rahisi hasa kwa wakimbiaji kupata majeraha.
Wayo wa mwanamke haufanyi vizuri ukitendwa vibaya hivyo. Kwa kweli, kadiri miaka inavyopita sehemu ya mbele ya wayo huelekea tu kupanuka—hata baada ya mtu kufikia utu mzima. Lakini sivyo na kisigino. “Kisigino kina mfupa mmoja tu,” asema Dakt. Thompson, “nao hubaki ukiwa mwembamba katika umri wa miaka 84 kama tu ulivyokuwa katika umri wa miaka 14.” Hili lafanya iwe vigumu hata zaidi kwa mwanamke kupata kiatu kinachomtosha vizuri kutoka kisigino hadi kidole cha mguu.
Madokezo ya Ununuzi
Kutoshea na mtindo wa viatu vyao vikiwaweka katika hali ngumu, wanawake wanawezaje kuzuia nyayo zinazouma? Jibu laanzia katika duka la viatu. Wataalamu fulani wapendekeza yafuatayo:
● Nunua viatu kuelekea mwisho wa siku, wakati ambapo nyayo zako zimepanuka kidogo.
● Jaribu viatu vyote viwili—si kimoja tu.
● Hakikisha kuwa kisigino chatoshea vizuri na kwamba urefu, upana, na kimo cha sehemu ya mbele ya kiatu chatosha.
● Fikiria pia kuwa hilo duka laweza kuwa na zulia nene, likifanya hata viatu vyenye kubana viwe vyenye ustarehe kwa muda.
● Epuka viatu vyenye ngozi ngumu yenye kumetameta au vyenye maunzi ya sanisia. Tofauti na ngozi nyepesi au suede, maunzi kama hayo hayapanuki unapotembea.
● Ukinunua viatu vyenye visigino virefu, jaribu kuweka ngozi ndani ili kuongezea wororo wa ndani. Fikiria kuvaa viatu vyenye visigino virefu kwa muda tu, ukibadili mara kwa mara kuvaa viatu vyenye visigino vifupi pindi kwa pindi katika siku.
Kwa kuongezea yaliyo juu, kumbuka sikuzote kwamba viatu vyapaswa kuwa vyenye ustarehe wakati wa kuvinunua. Tofauti na itikadi ya wengi, hakuna kipindi cha kupanuka na kuvizoea. “Kamwe, kamwe usimwache mwenye duka akusadikishe kuwa kiatu kinachofinya kitakuwa sawa baada ya kupanuka na kukizoea,” aonya Dakt. Coughlin. “Kile tu kitakachoumia ni wayo wako.”
Lakini namna gani ikiwa chaguo ulilonalo tu ni ama kiatu kinachobana kwa mbele na kisigino chenye ustarehe ama kiatu chenye ustarehe mbele na kisigino kikubwa? Dakt. Annu Goel, mtaalamu wa nyayo za miguu, asema kuwa wahitaji kuamua ni jipi lililo rahisi kurekebisha. “Kuna njia mbili za kufanya hivi,” yeye asema. “Kwanza, waweza kununua viatu vilivyo vipana vyakutosha mbele na kuweka kitu chororo ndani ili kufanya kisigino kitoshee vizuri zaidi. . . . Njia ya pili ni kununua kiatu chenye kisigino kinachokutoshea vizuri kisha sehemu ya mbele ya kiatu inyooshwe. Lakini hili laweza kufaulu tu ikiwa viatu vimetengenezwa kwa ngozi.”
Kwa kuwa wanawake wengi hutembea kilometa 15 hivi kwa siku, wangefanya vema kuchunguza viatu vyao. Kama vile gazeti la American Health lisemavyo, “kwa kutendea nyayo kwa uangalifu zaidi—hasa kwa kuvaa viatu vinavyokutoshea—waweza kuzuia kutokea kwa matatizo mengi ya wayo.”
[Sanduku katika ukurasa wa 26]
Matatizo Manne ya Kawaida ya Wayo
Vivimbe. Hiki ni kivimbe cha kidole gumba cha mguu. Vikiwa si vya kuridhiwa, vivimbe hivi vyaweza kusababishwa na viatu vyenye kubana au vyenye visigino virefu. Kuviwekea kitu chenye joto au barafu kwaweza kuandaa kitulizo cha maumivu cha muda, lakini upasuaji wahitajika ili kuondoa kivimbe kabisa.
Hammertoes. Vidole vya miguu vilivyokunjika kuelekea chini vyaweza kusababishwa na viatu vinavyoweka msongo mwingi sana kwenye sehemu ya mbele ya wayo. Upasuaji huenda ukahitajiwa ili kurekebisha kuharibika umbo huko.
Sagamba. Vivimbe vinavyofanana na pia kwenye vidole vya miguu, vinavyosababishwa na msuguano na msongo, mara nyingine hutokea kwa sababu ya kuvaa viatu vyembamba sana. Vitulizo vya nyumbani vyaweza kutoa kitulizo cha muda, lakini upasuaji huhitajika kwa kawaida ili kurekebisha vidole vilivyoharibika umbo vinavyosababisha msuguano.
Sugu. Tabaka za ngozi nene ambayo imekufa za kukinga wayo kutokana na kusuguana kwa kurudia-rudia. Kuweka nyayo ndani ya maji yenye joto na haluli ya chumvi kwaweza kuzilainisha. Lakini usijaribu kuzikata kwa kuwa kufanya hivyo kwaweza kusababisha ambukizo.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck