Kuutazama Ulimwengu
Matatizo ya Kudumisha Amani
“Mwongo mmoja uliopita, vikosi vya UM vya kudumisha amani vilisifiwa sana hivi kwamba vilipewa Tuzo la Amani la Nobeli,” gazeti la habari la Toronto la The Globe and Mail lataarifu. “Hivi sasa, washiriki wa vikosi vya kudumisha amani—raia, polisi na askari-jeshi—hudharauliwa na kupongezwa vilevile.” Kwa nini kuna badiliko hilo? “Tatizo la msingi ni hali ya mapambano ya kisasa. Vita vingi leo huwa baina ya vikundi vyenye kuzozana na majemadari wanaoajiri askari-jeshi vijana kwa ajili ya kupata faida, wala si baina ya majeshi yaliyopangwa vizuri, yenye miradi hususa na mafundisho. Vita hupiganwa kwa madhumuni ya kutawala taifa, wala si kati ya mataifa,” lasema gazeti Globe. Tokeo ni kwamba, laongezea gazeti hilo, “badala ya kusimamia kwa njia rasmi kukomeshwa kwa vita kati ya mataifa,” vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kudumisha amani “hujikuta vikisuluhisha mapambano baina ya vikundi vinavyozozana vyenye malengo—na nyakati nyingine hata mifumo ya uongozi—isiyo wazi na ambayo vilio vyake vya amani ni vyenye kutiliwa shaka.”
Kanuni Mpya Inatokeza Jeuri Katika Michezo
Kulingana na gazeti la Ufaransa L’Express, mashirika ya Ufaransa yanayosimamia soka yalishughulikia idadi kubwa sana ya visa 20,825 vya kukosa nidhamu katika msimu wa soka wa 1997/98, na visa vya jeuri viliongezeka sana katika michezo mingine pia. Kwa nini kuna jeuri nyingi hivyo? Kulingana na mtafiti Richard Pfister, sababu moja ni “uhitaji wa kushinda. Wakati watu wanapendelea fedha badala ya sifa njema, matokeo yanapokaziwa badala ya furaha ya kucheza, tokeo ni kwamba matendo ya aina yoyote yanakubaliwa.” Pfister asema kwamba mwenendo wa aina hiyo, unaozoewa na watu wanaoonwa kuwa violezo vya kuigwa wasiohofu kuadhibiwa, yaonekana unawatia moyo vijana wapende na kuiga jeuri.
Utumishi wa Hua Ungali Wenye Mafaa
Idara ya polisi katika jimbo la Orissa huko India ina mfumo wa mawasiliano ulio tata, lakini bado haitakomesha “utumishi wake wa hua,” ulio na hua wapatao 800, laripoti The Indian Express. Kulingana na Bw. B. B. Panda, mkurugenzi mkuu wa idara ya polisi ya Orissa, hua hawa wamekuwa muhimu kwa miaka 50 iliyopita katika kuokoa uhai wakati wa mafuriko na tufani na wangali wenye mafaa kunapokuwa na kasoro katika mawasiliano ya redio. Kwa mfano, mafuriko yalipokumba mji wa Banki mnamo 1982, hua hao ndio waliokuwa njia pekee ya mawasiliano kati ya mji na makao makuu ya wilaya ya Cuttack. Kikundi cha kwanza cha hua huko Orissa kilianzishwa mwaka wa 1946, kukiwa na hua wa jamii ya Ubelgiji walioitwa homer, wenye uwezo wa kupuruka hadi kimo cha kilometa 800 bila kutua kwa mwendo wa kilometa 80 hadi 90 kwa saa. Ndege hao wanaoweza kuishi kwa muda wa miaka 15 hadi 20, kwa sasa wanafugwa katika vituo vitatu vinavyotunzwa na makonstebo 34. Bw. Panda alitaarifu hivi: “Huenda hua hawa wakaonekana kuwa wa kale katika enzi ya simu za mkononi lakini wanaendelea kutolea nchi utumishi bora wa muda mrefu.”
Watoto Hawapati Elimu
Azimio la Haki za Kibinadamu kwa Wote, lililoidhinishwa na Kusanyiko Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo 1948, lilifasili haki ya msingi ya elimu. Ingawa jitihada nyingi zinazostahili pongezi zimefanywa, mradi huu ungali mbali sana kutimizwa. “Miaka hamsini baada ya kuidhinishwa kwa Azimio la Haki za Kibinadamu kwa Wote, bado kulikuwa na watoto zaidi ya milioni 130 wenye umri wa kwenda shule ambao hawakuwa wakienda shuleni,” laripoti gazeti la kila siku la Ujerumani Allgemeine Zeitung Mainz. “Hili lamaanisha kwamba asilimia 20 ya watoto wote ulimwenguni hawakupata elimu ya msingi.” Kulingana na Reinhard Schlagintweit, msimamizi wa Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa huko Ujerumani, itahitaji dola bilioni 7 za Marekani kupeleka watoto wote ulimwenguni katika shule ya msingi. Hiki ni kiasi kidogo kikilinganishwa na kiasi kinachotumiwa kununua aiskrimu kila mwaka huko Ulaya au kiasi kinachotumiwa kwa ajili ya vipodozi kila mwaka huko Marekani, na kiasi hicho ni kidogo sana kikilinganishwa na matumizi ya kijeshi ulimwenguni.
Asia Hukumbwa na Misiba Mingi
“Sita kati ya misiba mikubwa 10 iliyotukia ulimwenguni mwaka uliopita ilikuwa Asia, ikisababisha vifo vya watu 27,000 na hasara ya dola za Marekani bilioni 38,” lasema gazeti South China Morning Post. Hii yatia ndani mafuriko makubwa katika Bangladesh na China na mioto ya misitu huko Indonesia iliyoeneza moshi katika nchi jirani. “Asia hukumbwa na misiba mingi zaidi ya kiasili kuliko eneo jinginelo lote ulimwenguni,” yasema Tume ya Kiuchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa ya Asia na Pasifiki. “Katika Asia hasa, kupunguza hatari kutakuwa mojawapo ya matatizo makubwa sana ya karne ya 21.”
Sababu Huwezi Kujitekenya
“Kutekenya kwaweza kumfanya hata mtu mzima awe hoi kabisa. Lakini mtu mwenye hisi nyepesi angalau atafurahi kujua kwamba hawezi kujitekenya,” lataarifu gazeti The Economist. Kwa nini? Kulingana na utafiti wa karibuni, sababu inahusiana na ubongo-kati, ile sehemu ya ubongo ambayo inaelekeza utendaji wa misuli. Watafiti wanaamini kwamba ubongo-kati licha ya kuelekeza matendo pia huhusika na kufunua matokeo ya matendo hayo kwa ufahamu. Hivyo, watu wanapojaribu kujitekenya, ubongo-kati hutazamia hisia hiyo na huikandamiza. Unapotekenywa na mtu mwingine, kichocheo na kuitikia kwa ubongo-kati hakusadifiani, na hisia hiyo haikandamizwi. Gazeti la The New York Times, katika makala kama hiyo, lilitoa muhtasari hivi: “Ubongo unaweza kutambua wakati hisia za kutekenya zinasababishwa na mtu mwenyewe na hivyo kutoziitikia mara moja, ili uweze kuitikia mara moja hisia ambazo huenda ziwe muhimu zisababishwazo na vyanzo vingine.”
Njia ya Mawasiliano Inayochukua Mahali pa Ile ya Morse
Njia ya mawasiliano ya Morse, iliyobuniwa mnamo 1832, “imetimiza fungu muhimu katika ukuzi wa biashara na historia,” akiri Roger Cohn, wa shirika la Umoja wa Mataifa linalodhibiti safari za meli ulimwenguni. Imekuwa njia ya kimataifa inayotumiwa na meli zilizo katika hatari tangu mwaka wa 1912, mwaka ambao meli ya Titanic ilitoa wito wa msaada (SOS)—nukta tatu, dashi tatu, nukta tatu—lasema gazeti la The Toronto Star. Lakini kufikia Februari 1, 1999, mfumo mpya wa setilaiti, ulioanzishwa na Shirika la Kimataifa la Ubaharia, unaojiendesha wenyewe utapeleka data fulani kwa “vituo kadhaa vinavyosimamia shughuli za uokoaji ulimwenguni pote” wakati “swichi ya dharura” iliyoko katika kituo cha setilaiti melini inapobonyezwa. Mbali na nambari yenye tarakimu tisa ya kuitambulisha meli, habari zaidi zinazopelekwa “zaweza kutia ndani wakati, mahali ilipo meli na aina ya hatari—isiyotajwa, au mojawapo ya vikundi 12 vya hatari kuanzia moto hadi kuzama, kuegemea na shambulio la maharamia,” lasema gazeti la Star. Laongezea hivi kwa shauku: “Njia ya mawasiliano ya Morse ilitumiwa kutangazia ulimwengu baadhi ya habari bora zaidi katika historia: Ilitumiwa kutangaza kumalizika kwa Vita vya Ulimwengu viwili.”
Matatizo ya Kiafya Yahusishwa na Viatu
“Maoni ya wanatiba yanadokeza kwamba mtu mmoja kati ya sita ana matatizo mabaya ya miguu, ambayo mara nyingi yanaweza kuhusishwa na viatu,” laripoti gazeti la The Toronto Star. Magoti yanayouma, nyonga zinazouma, maumivu katika sehemu ya chini ya mgongo, na maumivu ya kichwa huenda yawe yanasababishwa na viatu unavyovaa. “Jambo muhimu la kukumbuka ni kuwa viatu haviwezi kubadilika vitoshee, miguu ndiyo inayoathiriwa,” lasema Star. “Usinunue viatu ukitarajia kuwa vitatoshea miguu yako. Iwapo havikutoshei dukani, usivinunue.” Nunua viatu wakati wa alasiri, kwa kuwa “kwa kawaida miguu hupanuka kidogo wakati wa mchana,” na “pima viatu hadi kwenye vidole, badala ya kujipima katika kisigino.” Takwimu zinaonyesha kwamba wanawake ndio walio na matatizo mengi ya miguu na ulemavu. Yaaminika kwamba hii ni kwa sababu asilimia 90 kati yao “wanavaa viatu vidogo sana na vyenye kubana sana miguu” na “kwa kawaida kuvaa viatu vyenye visigino virefu husababisha matatizo mabaya zaidi ya miguu.” Gazeti hilo laongezea: “Ni muhimu pia kukumbuka kwamba maumivu huibuka baada ya madhara kutukia.”
Uchapishaji wa Biblia Katika China
“Katika miongo miwili iliyopita China imechapisha nakala za Biblia Takatifu zaidi ya milioni 20 na Biblia [imekuwa] mojawapo ya vitabu vinavyopendwa sana nchini tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990,” lasema Shirika la Habari la Xinhua. Kulingana na Profesa Feng Jinyuan, wa Taasisi ya Dini za Ulimwengu katika Chuo cha China cha Mambo ya Kijamii, Wakristo katika China wana haki ya kununua nakala mbili. Zaidi ya chapa 20 tayari zimechapishwa, “kutia ndani chapa za Kiingereza zenye tafsiri za Kichina, chapa za Kichina zilizoandikwa katika herufi za kawaida na zilizo sahili, chapa katika lugha za kienyeji zinazozungumzwa na watu wachache na katika chapa za mfukoni na kubwa.” Kwa kuongezea, vitabu kadhaa vya hadithi za Biblia vimechapishwa na vinatarajiwa kupita idadi ya Biblia zinazouzwa. “Biblia inashikilia nafasi ya 32 katika orodha ya vitabu vinavyopendwa sana katika China kuanzia mapema miaka ya 1990,” yasema makala hiyo, lakini “kwa ujumla, Wachina hawapendezwi sana na dini kama watu wa Magharibi.”