Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 8/8 kur. 25-27
  • Vita ya Plataea—“Dubu” Ashindwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Vita ya Plataea—“Dubu” Ashindwa
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Dalili za Mapigano Hayo
  • Je, Mardonius Alikuwa Mpiganaji Asiyependa Vita?
  • Vita ya Mwisho
  • “Dubu” Aliyejeruhiwa
  • Ushinde Wenye Kuhuzunisha wa Shasta
    Amkeni!—1999
  • Lile Pigano la Marathoni—Mtwezo wa Serikali Kubwa ya Ulimwengu
    Amkeni!—1995
  • Umedi-Uajemi—Ile Serikali Kubwa ya Nne ya Ulimwengu Katika Historia ya Biblia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Ni Nani Atakayeutawala Ulimwengu?
    Sikiliza Unabii wa Danieli!
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 8/8 kur. 25-27

Vita ya Plataea—“Dubu” Ashindwa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UGIRIKI

MAGOFU machache matulivu ya hekalu. Mawe yaliyochongwa na vijia vya changarawe vilivyoachwa. Uwanda tambarare uliopo kati ya vilima kwenye kingo za Mto Asopós, umbali wa kilometa 50 kaskazini-magharibi ya Athens, Ugiriki.

Hakuna dalili yoyote kwamba tumesimama mahali hususa ambapo mojawapo ya vita ya mwisho baina ya Uajemi na Ugiriki ilipiganwa miaka ipatayo 2,500 iliyopita. Hapa ndipo palikuwa na vita kubwa zaidi ya nchi kavu kati ya vile Vita vya Uajemi—Vita ya Plataea.

Dalili za Mapigano Hayo

Kama hati iliyoandikwa vizuri, unabii wa Biblia ulitabiri karne nyingi awali juu ya kuinuka na kuanguka kwa serikali za ulimwengu. Kama ilivyotabiriwa serikali ya ulimwengu ya Umedi na Uajemi, ikifananishwa na dubu na kondoo mume, ilitwaa maeneo katika jitihada zake za kupanua eneo lake upande wa magharibi. (Danieli 7:5; 8:4) Lakini, majeshi ya Uajemi yaliyokuwa yakiongozwa na Mfalme Dario wa Kwanza yalishindwa vibaya na Ugiriki kule Marathoni mwaka wa 490 K.W.K. Dario akafa miaka minne baadaye.

Unabii wa Danieli ulitaja pia ‘kusimama kwa wafalme watatu katika Uajemi’ kisha mfalme wa nne wa Uajemi, ambaye “atawachochea wote juu ya ufalme wa Uyunani.” Yaonekana kwamba mfalme huyo ni Shasta mwana wa Dario. (Danieli 11:2) Ili kulipiza kisasi kushindwa kwa Uajemi kule Marathoni, Shasta alitumia majeshi mengi sana kushambulia sehemu za bara za Ugiriki mwaka wa 480 K.W.K. Lakini baada ya kupata ushindi ambao ulimgharimu sana kule Thermopylae hatimaye majeshi yake yalipigwa vibaya Salamis.a

Je, Mardonius Alikuwa Mpiganaji Asiyependa Vita?

Kwa aibu kubwa, Shasta aliharakisha kwenda Lidia, akiacha wanajeshi 300,000 chini ya amri ya Mardonius aliyekuwa shujaa mwenye ujuzi ambaye alikuwa amepewa jukumu la kusimamia maeneo ya Ugiriki yaliyokuwa yametekwa. Akiwa katika kambi yake wakati wa majira ya baridi kali katika Thessaly, Mardonius alituma balozi aende Athene akiwa na pendekezo ambalo lingefanya Athene lisishambuliwe kamwe, na kuruhusu kujengwa upya kwa mahekalu yaliyochomwa, na kurudishiwa maeneo yao, na kupewa madaraka ya kuwa jiji huru linalojitawala. Lakini Waathene walikataa kwa madharau pendekezo hilo wakaomba Wasparta wawasaidie vitani.

Mardonius alishauriwa na Wagiriki waliopinga mamlaka ya kwao na ambao walimpendelea kwamba anaweza kuwashinda Wagiriki hao wakaidi kwa kuwahonga viongozi wao. Lakini alikataa kwa madharau kutumia hongo. Bado alikuwa akijaribu kuepuka pambano la moja kwa moja na Wagiriki, na tena akapendekeza kwamba Waathene wasalimu amri nao watapata faida nyingi. Lakini Waathene walikataa katakata.

Vita ya Mwisho

Basi, vita ya mwisho baina ya Uajemi na Ugiriki ilipiganwa kule Plataea mnamo Agosti 479 K.W.K. Huko, wanajeshi wapatao 40,000 wa miguu wa Ugiriki—waliotia ndani Waathene, Wasparta, na majeshi ya majiji mengine ya Ugiriki—wakiongozwa na jemadari wa Sparta Pausanias walikabili majeshi hodari 100,000 ya Mardonius.

Kwa majuma matatu vikosi vikuu vya majeshi ya pande zote mbili, vyote vikiogopa vita ya ana kwa ana, vilikuwa vikitwangana hapa na pale ng’ambo ya Mto Asopós. Hekaya zasema kwamba eti wapiga-ramli wa pande zote mbili waliwaahidi ushindi iwapo wangetumia mbinu ya kutoshambulia kwanza vitani. Hata hivyo, wanajeshi wa farasi wa Uajemi walikuwa wakiwanyanyasa Wagiriki daima, wakiteka vifaa muhimu na kutia sumu visima vya maji ambavyo Wagiriki walitegemea.

Kwa maoni ya Mardonius, vita hiyo ni kama ilikuwa imekwisha. Lakini kamanda huyo wa Uajemi hakujua uwezo wa upiganaji wa adui zake. Jenerali huyo alidanganywa na tumaini la kupata ushindi wa haraka na wenye kutokeza sana. Basi, akaharakisha majeshi yake yavuke mto na kushambulia.

Waajemi waliweka ukuta wa ngao za fito nao walinyeshea maadui wao mishale kutoka nyuma ya ukuta huo. Wagiriki wapinzani waliokuwa wakiunga mkono Waajemi walishambulia Waathene 8,000, huku kikosi kikuu cha majeshi ya Mardonius kikishambulia Wasparta 11,500. Ili Wasparta wajikinge dhidi ya mishale mingi iliyokuwa ikiwanyeshea, wao walichuchumaa chini ya ngao zao. Lakini kwa kufuata utaratibu wakainuka pamoja na kushambulia. Wakiwa na mikuki mirefu zaidi na wakiwa wamevalia kinga za mwili ambazo ni nzito zaidi, waliwakaribia upesi Waajemi.

Wakipigwa butaa, Waajemi wakarudi nyuma. Wakati uo huo, tayari Waathene walikuwa wamewaponda wale Wagiriki waasi. Majeshi ya Mardonius yakarudi nyuma mbiombio kuvuka mto huku wakilindwa na wanajeshi wao wa farasi. Mardonius alipigwa kutoka mahali alipokuwa na kuuawa. Majeshi ya Uajemi yalipoona hayana kiongozi, yalisambaratika na kutifua vumbi.

Wakati uleule, ng’ambo ya bahari kwenye pwani ya Mycale katika Ionia, majeshi ya baharini ya Ugiriki yalishinda vibaya majeshi ya baharini ya Uajemi, ambayo karibu yaangamizwe katika ile vita ya Salamis mwaka mmoja awali. Majeshi yote ya Uajemi yenye nguvu yalikuwa yamepigwa vibaya sana.

“Dubu” Aliyejeruhiwa

Majeshi ya Uajemi hayakuweza tena kupigana katika Ulaya. Majeshi ya Uajemi yaliharibiwa kabisa. Baadaye, kwa mujibu wa kitabu A Soaring Spirit, “Shasta akatulia kwenye majiji yake makubwa na kufuatilia anasa za wake zake. Pindi kwa pindi angetekeleza maagizo ya babake na kufanya ujenzi, akizidi kujenga majumba ya fahari kwenye makao makuu ya serikali ya Uajemi, Persepolis. Lakini hakuna mambo mengine makubwa aliyotimiza.”

Akiwa na ulinzi kwenye makao ya kifalme, mfalme huyo aliyependa makuu zamani sasa akawa anafuatilia tu hila ndogondogo za kisiasa na kusikiliza porojo za makao ya kifalme. Na hata alivunjika moyo hapo. Mnamo mwaka wa 465 K.W.K., alifanyiwa njama na kikundi fulani akauawa kwenye kitanda chake.

Kitabu A Soaring Spirit chasema: “Kati ya wafalme wa Uajemi waliofuata—kwa maoni ya waandikaji Wagiriki ambao ndio wanatoa habari nyingi kuhusu milki hiyo katika wakati huo—hakuna hata mmoja wao aliyekuwa na uwezo na akili nyingi kama Koreshi au Dario. Chini ya utawala wa mwana wa Shasta aliyeitwa Artashasta wa Kwanza, jambo kuu la sera ya serikali ya Uajemi likawa pesa wala si majeshi. Alitumia sarafu ya milki hiyo kuingilia masuala ya Ugiriki, akihonga [jiji moja lenye kujitawala] la Ugiriki na kisha jiji jingine ili kuchochea ghasia . . . Sarafu hizo za dhahabu za daric zilikuwa na mchoro wa Dario akiwa na uta na podo; kwa madharau Wagiriki waliziita ‘wapiga-mishale wa Uajemi.’”

Hila na mauaji yaliendelea kuchafua makao ya kifalme ya Uajemi hadi milki hiyo ilipotokomea hatimaye. Milki hiyo iliporomoka polepole, na watawala wa Uajemi wakaanza kupoteza mamlaka yao na uwezo wao wa kutawala.

Japo jitihada za mwisho-mwisho za kuimarisha milki hiyo, watawala walikuwa tayari kuporomoka kufikia wakati Aleksanda Mkuu—ambaye miradi yake na tamaa yake ya upanuzi zilifanana na zile za Koreshi—alipoanza kushambulia milki hiyo katika karne ya nne K.W.K. Kwa pindi nyingine tena unabii wa Biblia ukatimizwa kwa usahihi kabisa.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa maelezo zaidi, ona makala ya “Lile Pigano la Marathoni—Mtwezo wa Serikali Kubwa ya Ulimwengu,” katika toleo la Amkeni! la Mei 8, 1995, na makala ya “Ushinde Wenye Kuhuzunisha wa Shasta,” katika toleo la Amkeni! la Aprili 8, 1999.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

Umedi na Uajemi Dhidi ya Ugiriki-Karne Mbili za Mapigano

539 K.W.K. Umedi na Uajemi zapata kuwa serikali ya nne ya ulimwengu. Zatwaa maeneo katika sehemu tatu kuu: kaskazini (Ashuru), magharibi (Ionia), na kusini (Misri) (Danieli 7:5; 8:1-4, 20)

500 K.W.K. Wagiriki wa Ionia (Asia Ndogo) waasi dhidi ya watawala wa Uajemi

490 K.W.K. Waathene wakomesha Waajemi kule Marathoni

482 K.W.K. Shasta ‘awachochea wote juu ya ufalme wa Uyunani’ (Danieli 11:2)

480 K.W.K. Ushindi wa Waajemi uliowagharimu sana kule Thermopylae; Waajemi washindwa vibaya Salamis

479 K.W.K. Waathene na Wasparta wawashinda Waajemi kule Plataea

336 K.W.K. Aleksanda awa mfalme wa Makedonia

331 K.W.K. Majeshi ya Uajemi yapondwa vibaya na Aleksanda Mkuu kule Gaugamela; Ugiriki yapata kuwa serikali ya tano ya ulimwengu (Danieli 8:3-8, 20-22)

[Picha]

Mpiga-mshale wa Uajemi

Msafara wa wanajeshi wa farasi wa Ugiriki

[Hisani]

Musée du Louvre, Paris

Photograph taken by courtesy of the British Museum

[Sanduku katika ukurasa wa 26]

Matokeo ya Mwisho ya Jitihada Zote za Kibinadamu za Kutawala

“Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.”—Danieli 2:44.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mahali pa vita ya Plataea ambapo majeshi ya Uajemi yalisambaratishwa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki