Spreso—Kahawa Bora
‘Laiti kahawa ingekuwa na ladha nzuri kama inavyonukia!’ Je, umepata kusema hivyo? Basi huenda ukataka kuonja “kahawa ya spreso.” Wataalamu wameiita kahawa “bora zaidi” na “kahawa tamu zaidi uwezayo kunywa.”
LABDA tayari umeonja spreso? Labda ulivutiwa sana na uzito wake na ladha yake nzito. Kwa upande mwingine, huenda ikawa uliamua: ‘Hii si kahawa nzuri. Kumbe ndiyo maana hutiliwa katika vikombe vidogo mno—nani awezaye kuvumilia kunywa zaidi ya mafunda machache tu ya kinywaji kikali na kichungu sana? Isitoshe, kwa hakika ina kafeini nyingi kiasi cha kudhuru afya!’
Hata hivyo, je, spreso iliyotayarishwa vizuri ni chungu? Na je, kikombe kidogo cha spreso kina kafeini nyingi zaidi kuliko kikombe cha kahawa ya kawaida? Huenda majibu yakakushangaza?
Ni Nini Huifanya Kuwa Spreso?
Kahawa ya spreso ilianzia Italia, ingawa nchi na tamaduni tofauti-tofauti zimekuza njia zake zenyewe za kuitayarisha. Ina ladha gani? Wapenzi wa spreso hueleza kuwa ni yenye kunukia, yenye ladha nzuri, nzito, ni tamu na chungu, kuwa ina ladha ya sukari iliyoungua, na ina manukato. Kikombe cha spreso kilichotayarishwa vizuri huwa na utando juu uitwao crema—povu la rangi ya dhahabu-kikahawia, ambalo kwa kawaida hupatikana kwa shida, huongeza utamu na kufanya harufu nzuri kubaki.
Kikombe kimoja ni sawa na mililita 30 hadi 40. Kwa ujumla huandaliwa pamoja na sukari katika kikombe kidogo mara baada ya kutayarishwa—ikiwa yenye kupendeza kwelikweli!
Inatayarishwaje? Utayarishaji wa spreso huanza kwa buni zilizotayarishwa kipekee, ambazo huchomwa kuwa rangi ya kahawia iliyokolea (lakini si nyeusi) na husagwa kuwa laini zaidi ya zile zitumiwazo katika kahawa ya kawaida. Lakini, jambo la msingi si juu ya kuchomwa au kusagwa kwa buni ambako hutokeza spreso—ni njia ya kipekee itumiwayo katika utayarishaji, ambayo hutumia msongo badala ya uzito. Kiasi cha kahawa itumiwayo katika kikombe kimoja ni karibu thuluthi mbili ya kiasi cha kahawa itumiwayo katika kutayarisha kahawa kwa njia ya mdondosho, lakini ikiwa na kiasi kidogo sana cha maji. Namna hii ya utayarishaji wa kahawa hutokeza ubora wa buni.
Waweza kuagiza kiasi cha kawaida au kiasi maradufu cha spreso katika mikahawa mingi. Lakini, tahadhari: Spreso iliyotayarishwa bila uangalifu ni chungu. Hivyo uandaliwapo spreso katika mkahawa, ichunguze. Ikiwa kikombe chako kimejaa pomoni au hakina crema juu ya kahawa, yaelekea sana utakuwa umepewa kahawa chungu, iliyotumia mvuke mwingi mno.
Vinavyohusika na spreso ni vinywaji vingine vingi. Ikiwa waona kwamba spreso ni chungu sana, kwa nini usijaribu kapuchino tamu au spreso ya maziwa moto iliyo na au isiyo na povu?
Vifaa vya Kutayarishia Spreso Nyumbani
Je, ungependa kutayarisha vinywaji vya spreso nyumbani? Uangalifu kwa maelezo yote ni muhimu, ili kuhakikisha unapata kinywaji kilicho kizito na kitamu.
Ni kifaa gani cha kutayarishia spreso unachopaswa kununua? Njia ya mdondosho haitokezi spreso halisi, bila kujali kama buni zimechomwa au ni laini kwa kadiri gani. Utahitaji kifaa kilichotengenezwa maalumu.
Kwa kawaida stove-top brewer ndiyo yenye bei nafuu zaidi. Watu wengi huridhika na utayarishaji wa spreso nyumbani kwa kutumia stove-top, ingawa kahawa itokezwayo ni nyepesi, na yaelekea haina crema. Waweza kupata spreso nzuri kwa kudhibiti kwa uangalifu kiasi cha maji yanayotiliwa katika birika au kwa kuacha sehemu ya juu wazi na kukiondoa chombo hicho motoni kabla ya kumaliza utaratibu wote wa kutayarisha.
Mashine za mvuke za kutumia umeme hutumia mvuke kulazimisha maji kupitia kahawa. Waweza kupataje matokeo yaliyo bora? Kwa kuzuia mtiririko wa kahawa katika kikombe baada ya mililita 30 hadi 60 za kwanza, ili kuzuia kukamuliwa kupita kiasi na kuokoa mvuke wa kutosha kutokezea maziwa yenye povu. Kwa hiyo, tafuta mashine ambayo ina swichi au kitu kingine kinachoweza kuzuia mtiririko wa kahawa. Mashine za mvuke hutayarisha kapuchino nzuri na spreso yenye maziwa moto, lakini kama ilivyo na stove-top brewer, hazina uwezo wa kutayarisha moja kwa moja spreso bora.
Mashine za pistoni kwa kawaida ni ghali zaidi na zina uwezo wa kutayarisha spreso zilizo bora kabisa. Katika kutumia mashine ya pistoni, waweka msongo kwa kufinya mpini, ambao hufinya pistoni yenye springi, ukilazimisha maji moto kupitia kahawa. Baadhi ya watu hupendelea mashine za pistoni kwa sababu zinaweza kuendeshwa kwa mkono na zapendeza kwa macho. Wengine huziona kuwa ngumu kutumiwa na zinafanya polepole sana katika kupasha maji moto.
Mashine za pampu pia hutokeza msongo wa kutosha kufanya spreso iliyo bora kabisa. Hizo ni rahisi zaidi kutumiwa nazo zinafanya kazi kwa haraka zaidi ya mashine za pistoni. Kwa hiyo, kwa wale watakao spreso iliyo bora kwa kawaida hupendelea mashine ya pampu. Zatofautiana, na baadhi ya mashine za pampu ni zenye kudumu zaidi ya nyingine. Kwa hiyo chunguza aina tofauti-tofauti kabla ya kununua. Maduka ambayo huonyesha matumizi ya mashine zao hukuweka katika hali nzuri ya kufanya uchaguzi wa kufaa.
Kahawa Ununuayo
Chagua spreso iliyochomwa karibuni. Mara nyingi kahawa ziuzwazo katika maduka makubwa si za karibuni, hivyo tafuta duka liuzalo kahawa tu—ni vizuri sana ikiwa uchomaji utafanywa katika duka la kahawa. Kahawa iliyosagwa huharibika upesi, ilhali buni nzima-nzima hudumisha hali zao kwa majuma kadhaa. Kwa hiyo, ikiwa inawezekana, nunua buni nzima-nzima na uzisage nyumbani, kulingana na unavyotaka. Usagaji mzuri ni ule ufanyao kahawa kuwa laini lakini si ungaunga. Ikiwa ni lazima ununue kahawa iliyosagwa, basi nunua kiasi kidogo na ukitumie mara moja.
Ili kahawa yako idumishe hali yake, uiweke katika kopo lisiloingia hewa na ambalo limefunikwa vizuri. Ikiwa utaitumia katika majuma machache, liweke kopo hilo la kahawa katika sehemu yenye baridi kidogo, na yenye giza. Ama sivyo, iweke katika friza.
Sanaa ya Utayarishaji
Hata kukiwa na vifaa bora kabisa na kahawa bora kabisa, ni lazima mtu ajifunze ustadi wa kutayarisha spreso, na hainunuliwi. Hatua za utayarishaji zitatofautiana kwa kutegemea mashine unayotumia, hivyo fuata miongozo inayoambatana kwa uangalifu. Tumia kahawa iliyosagwa yenye kutosha. Kiasi barabara karibu kitatosha kichujio kilichoko ndani, huku ikitoa nafasi kwa kahawa iliyosagwa kupanuka. Utahitaji uzoefu ili ufunge ifaavyo au uweke kahawa katika chungio vizuri, ili maji yatiririke kwa utaratibu na kwa usawaziko kufikia sehemu ya kahawa iliyosagwa, ikihakikisha ladha yote inatokeza.
Ni kosa gani lipaswalo kuepukwa? Kutayarisha kahawa iliyosagwa kwa kutumia maji mengi. Ukijaribu kutayarisha kiasi cha mililita 60 au 90 kutokana na kipimo kimoja, kiasi kilichotayarishwa kitakuwa chepesi na kichungu. Badala ya kupata spreso, utapata kinywaji kifananacho na kahawa aina ya mdondosho iliyo chungu—si kitu ulichotaka.
Kwa hiyo, jambo la maana ni kujua wakati wa kuacha kutayarisha. Wataalamu wapendekeza kwamba kiasi kinachofaa cha spreso chapaswa kitokane na mililita 30 hadi 40 ya umajimaji kwa sekunde 20 hadi 25. Kufikia hapa kahawa iliyosagwa inakuwa imekwisha kamuliwa kabisa na yapasa kutupwa.
Hata unapotayarisha kiasi maradufu cha spreso, “Kutayarisha kahawa kidogo ni bora zaidi.” Kadiri utayarishavyo kahawa kidogo zaidi, ndivyo kinywaji kiwavyo kitamu zaidi. Ufafanuzi wa spreso maradufu hutofautiana, lakini ni kama kuweka kiasi maradufu cha spreso katika kikombe kimoja, kwa kutumia kahawa iliyosagwa mara mbili zaidi.
Vipi Kuhusu Kafeini?
Kikombe kimoja cha spreso chaweza kuwa na kafeini kidogo kuliko kikombe cha kawaida cha kahawa. Je, hilo lakushangaza? Inawezekanaje, ukifikiria uzito wa spreso?
Sababu moja ni weusi wa buni zilizochomwa. Buni nyeusi zaidi huwa na kafeini kidogo. Pia, maduka mengi yauzayo kahawa tu hutumia buni aina ya arabica, ambayo mara nyingi huwa na kafeini kidogo kuliko buni aina ya robusta ambazo huwekwa katika makopo yapatikanayo katika maduka makubwa ya kuuza kahawa.
Lakini sababu kuu ni ujazo. Ingawa spreso hutia ndani kafeini nyingi zaidi kwa mililita moja kuliko kahawa ya kawaida, ina umajimaji kidogo sana katika kikombe. Hivyo, uchunguzi mbalimbali waonyesha kwamba kikombe chenye mililita 180 ya kahawa ya kawaida huweza kutia ndani miligramu 100 au zaidi za kafeini, huku kikombe kimoja cha spreso kikiweza kutia ndani kiasi kidogo hivi.
Hata hivyo, matokeo ya uchunguzi hutofautiana, na kiasi cha kafeini kitategemea buni zitumiwazo na pia kila hatua katika utayarishaji. Bila shaka, kiasi maradufu cha spreso kitakuwa na kafeini nyingi zaidi ya kiasi cha kawaida. Kiongozi bora zaidi cha kuamua kiasi cha kafeini bila shaka ni jinsi uhisivyo baada ya kunywa kinywaji hicho. Ikiwa wataka kupunguza kiasi cha kafeini unywayo na bado ufurahie spreso, waweza kutumia spreso isiyo na kafeini au waweza kuichanganya na buni za kawaida za spreso zilizochomwa, kulingana na kiasi cha kafeini utakayo.
Je, uko tayari kutayarisha spreso katika jiko lako? Matokeo mazuri huja na ustahimilivu, hivyo jaribu mwenyewe—jitayarishie kabla ya kuwapa marafiki wako. Utahitaji uzoefu ili kutokeza crema na maziwa yenye povu. Hata hivyo, udumifu wako utathawabishwa wakati marafiki wako watakapofurahia vinywaji vya spreso ambavyo ni vizuri kama vile viandaliwavyo katika mikahawa. Huenda hata ukaweza kukiri kwamba spreso ni kahawa bora zaidi.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Maagizo juu ya Kutokeza Maziwa Yenye Povu
Ili kutokeza povu na/au kuchemsha maziwa kwa ajili ya kapuchino na maziwa moto, utahitaji kuwa na jagi ya feleji, maziwa baridi, na kichemsha-maziwa. Ikiwa kitayarisha-spreso chako hakina kifimbo kwa ajili ya kuchemsha maziwa, waweza kununua chombo kilicho pekee kwa ajili ya kusudi hili.
1. Tia maziwa baridi katika jagi ya feleji kwa kiasi kisichozidi nusu ya jagi.
2. Weka kifimbo cha kuchemsha maziwa chini tu kidogo ya uso wa maziwa, kisha fungua vali ya mvuke.
3. Weka ncha ya kifimbo chini tu ya uso, ukiinamisha jagi na kuruhusu hewa zaidi ufanyapo povu.
4. Halijoto inayofaa kwa kawaida hufikiwa wakati jagi iwapo moto sana kiasi cha kushindwa kugusa.
5. Funga vali ya mvuke, na uondoe jagi chini yake. Kisha ufungue vali ya mvuke ili kuondosha maziwa yoyote yaliyobaki, na ukaushe kwa kutumia kitambaa chenye unyevu.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Buni hudumisha hali yake kwa muda mrefu zaidi kuliko kahawa iliyosagwa
Kitayarisha-spreso cha mvuke kimeonyeshwa