Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 11/8 kur. 24-27
  • Waetruria—Fumbo Linalodumu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Waetruria—Fumbo Linalodumu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Asili Yenye Fumbo
  • Jinsi Walivyoishi na Kusitawi
  • Kufurahia Maisha kwa Waetruria
  • Itikadi za Kidini za Ajabu
  • Kufyonzwa na Kutoweka Kabisa
  • Urithi Wenye Kudumu
  • Asili ya Helo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Michongo ya Alabasta Usanii wa Zamani wa Volterra
    Amkeni!—2002
  • Carthage—Jiji Lililokaribia Kuangusha Roma
    Amkeni!—2001
  • Jinsi ya Kutafuta Maandiko Katika Biblia Yako
    Habari Zaidi
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 11/8 kur. 24-27

Waetruria—Fumbo Linalodumu

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UFARANSA

“Etruria ilikuwa na nguvu sana hivi kwamba ilikuwa mashuhuri katika mabara na bahari.”—Livy, Mwanahistoria wa Karne ya Kwanza.

LINAPOKUJA suala la Waetruria, waweza kuhisi kwamba hujui hata mambo ya msingi ya suala hilo. Hata hivyo, ikiwa lugha unayozungumza hutumia alfabeti ya Kilatini, bila kujua umefaidika kutokana na Waetruria. Kama si Waetruria, alfabeti ya Kilatini ingeanza na a, b, g (kama Kigiriki alpha, beta, gamma au Kiebrania aleph, beth, gimel). Hata hivyo, ingawa wataalamu wa lugha wajua kwamba alfabeti ya Kietruria ilianza na a, b, c, bado ni vigumu kuelewa lugha ya Waetruria. Na hii ni mojawapo tu ya fumbo la Waetruria.

Katika karne zilizopita wanahistoria wamekisia juu ya asili ya huu ustaarabu wenye kutokeza sana. Wakati wa upeo wao wa usitawi katika karne ya tano K.W.K., Waetruria waliunda shirikisho la majiji 12 ya mfumo wa biashara uliotapakaa Ulaya na Afrika Kaskazini. Hata hivyo, karne nne tu baadaye, walimalizwa kabisa na mamlaka ya Roma iliyokuwa ikiibuka. Lakini tunafahamu nini kuhusu Waetruria, na kwa nini hili fumbo linadumu?

Asili Yenye Fumbo

Wanahistoria, waakiolojia, na wataalamu wa lugha kwa muda mrefu wamekuwa wakijiuliza juu ya asili ya Waetruria. Je, walihama kutoka Lidia, mkoa katika Asia Ndogo, kama alivyodokeza Herodotus, au walikuwa watu wa asili ya Kiitalia, kama alivyodai Dionysius wa Halicarnassus katika karne ya kwanza K.W.K.? Je, ingeweza kuwa kwamba walikuwa na asili tofauti-tofauti? Hata jibu liwe nini, tofauti za kijamii na za kitamaduni kati yao na majirani wao zilikuwa kubwa sana kiasi cha kwamba sasa hatuwezi kuwa na hakika juu ya chanzo chao.

Hata hivyo, twajua kwamba kuanzia karibu karne ya nane K.W.K., Waetruria walisitawi kotekote Italia ya kati. Waroma waliwaita Tusci, au Etrusci, na eneo walilokaa, kati Mto Arno katika kaskazini na Mto Tiber katika kusini, lilikuja kujulikana kuwa Tuscany. Wakati fulani ustaarabu wa Waetruria ulitawala zaidi ya makundi yapatayo 50 ya watu wa Kiitalia.

Ingawa kimsingi lugha ya Kietruria hutumia aina ya zamani ya alfabeti ya Kigiriki, ikifanya iwe rahisi kujulikana, kwa hakika ni tofauti kabisa na lugha nyingine ijulikanayo. Sehemu kubwa ya msamiati wa Waetruria hufanya kazi ya utafsiri iwe ngumu. Hata hivyo, fasihi zao zilikuwa nyingi, kwani vitabu vilikuwa sehemu kuu ya utamaduni wao, hasa kuhusu mambo ya kidini. Ingawa maelfu ya vielelezo vya miandiko ya Waetruria bado yako leo—kwenye mawe ya kaburi, vyombo vya kuwekea maua, na majeneza ya alabasta—huwa na kiasi kidogo cha maandishi, kwa hiyo huandaa msaada kidogo katika kueleza asili na maana ya maneno ya Waetruria.

Jinsi Walivyoishi na Kusitawi

Waetruria walijipanga katika majiji yenye kujitawala yenyewe, ambayo mwanzoni yalitawaliwa na wafalme na baadaye na mahakimu. Majiji haya yaliunganishwa kuwa shirikisho la Waetruria, ambalo lilikuwa ushirika usio thabiti wa kidini, kiuchumi, na kisiasa. Baadhi ya nyumba za Waetruria zilikuwa na maji ya mfereji na zilikuwa kwenye barabara za mawe, zenye mifumo ya mifereji ya kuondolea maji machafu. Mifumo ya kuondoa maji yalitumiwa sana. Wafalme Waetruria walilibadilisha Roma lenyewe kutoka kuwa kikundi cha vijiji hadi jiji lenye fahari, na lenye ukuta ambalo lilikuwa na mifumo ya mifereji ya kuondolea maji machafu, ikitia ndani Cloaca Maxima, ambao bado unaweza kuonekana leo.

Waetruria walisitawi kutokana na madini mengi yaliyokuwa katika maeneo yaliyokuwa chini ya utawala wao, kama vile machimbo ya chuma katika kisiwa cha Elba kilichokuwa karibu. Ili kuridhisha tamaa yao ya metali, Waetruria walitengeneza chuma, fedha, na shaba—hata wakiagiza bati kutoka Visiwa Vidogo vya Uingereza. Mbali na utajiri huu, maeneo waliyokaa yaliandaa ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo na ufugaji, ikitokeza nafaka, zeituni, na zabibu na vilevile mbao. Mali hizo za asili na vilevile biashara kubwa ya ndani ya nchi na ya kigeni iliwapa Waetruria uchumi wenye kusitawi.

Waetruria walikuwa mabaharia hodari. Katika mwaka wa 540 K.W.K., Muungano wa meli za Waetruria na Wakathage ulishinda Wagiriki, na hivyo Waetruria wakajihakikishia biashara ya ng’ambo. Wakiwa wamebuni meli za kivita zenye kugonga meli za adui, walikuwa tayari kwa vita. Bidhaa kama vile bucchero iliyo maarufu (vyungu vyeusi) zilisafirishwa kupitia baharini hadi mbali kama Hispania na Misri. Kwa kutumia njia za biashara za bara, Waetruria walisafirisha divai hadi Gaul (Ufaransa) na Germania (Ujerumani), hivyo wakisambaza umaarufu wao.

Kufurahia Maisha kwa Waetruria

Kati ya vyanzo vya habari vyenye kudumu na vyenye kufunua sana habari za Waetruria ni sanaa zao. Watu wenye kupenda anasa, Waetruria walitengeneza mapambo ya dhahabu ya kifahari, kutia ndani vipuli, bizimu, vidani, bangili, na mikufu. Hata leo jinsi walivyounda hazina zenye kuvutia sana kwa madoido na mapambo, wakitumia vipande vidogo vya dhahabu, bado ni fumbo. Mbali na bilauri, sahani, vikombe, na seti za vyombo vya chakula vya fedha na metali nyingine za thamani, Waetruria walichonga na kutia nakshi vitu vingine vyenye thamani, kama vile pembe za ndovu.

Michongo mingi, sanaa, na michoro ya ukuta ambavyo vimegunduliwa vimefunua jinsi Waetruria walivyofurahia maisha. Walifurahia kutazama mashindano ya farasi, mashindano ya masumbwi, michuano ya mieleka, na riadha. Mfalme angetazama michezo hii, labda akiwa ameketi katika kiti chake cha pembe za ndovu, akiwa amezungukwa na watumwa waliotekwa katika vita. Vazi lake la rangi ya zambarau, likiwa ishara ya cheo chake, baadaye liliigwa na Waroma. Nyumbani, angeegama kando ya mke wake wakati wa chakula na kusikiliza filimbi au zumari ikipigwa huku akimtazama mtu akicheza muziki huo, wakati huo akihudumiwa na watumwa wake.

Wakitofautiana kabisa na Wagiriki au Waroma, wanawake katika jamii ya Etruria walifurahia hali ya usawa katika jamii. Wangeweza kumiliki mali, na walifurahia matukio ya kijamii. Wanawake Waetruria walikuwa na majina ya kibinafsi na ya familia, jambo linalothibitisha kwamba walikuwa na haki za kisheria.

Itikadi za Kidini za Ajabu

Mwanahistoria mmoja wa karne ya kwanza aliwaita Waetruria “watu waliojitoa kwa desturi za kidini zaidi ya watu wengine wowote.” Waetruria waliabudu miungu mingi sana, wakipendelea sana miungu ya utatu, ambayo kwa heshima yao walijenga mahekalu yenye sehemu tatu, au yenye vyumba vitatu. Kila chumba kilikuwa na sanamu. Ustaarabu wa Waetruria ulitegemea hasa mawazo ya kifumbo ya Kibabiloni. Wazo kuu miongoni mwa hayo lilikuwa ni lile la kuendelea kuishi baada ya kifo na kuzimu. Maiti ama zilizikwa ama zilichomwa kwa moto. Ikiwa zilichomwa kwa moto, majivu yaliwekwa katika vyombo vya aina na muundo mbalimbali. Kuwekwa kwa chombo hicho katika kaburi, pamoja na kila kitu kilichofikiriwa kuwa ni muhimu katika kuzimu, kuliambatana na desturi mbalimbali, matoleo, na matoleo ya vinjwaji. Makaburi ya watu matajiri yalichorwa picha nyingi zenye rangi zikionyesha mandhari mbalimbali, mara nyingine zikionyesha roho waovu au wonyesho wa viumbe vyenye kutisha. Kama chanzo kimoja kisemavyo, “sikuzote Waetruria walipenda mnyama atishaye.”

Zoea la Waetruria la kuchunguza ini, likiwa njia ya uaguzi, laweza kufuatiliwa hadi Babiloni. (Linganisha Ezekieli 21:21.) Mambo yote katika maisha na maamuzi yao yalitegemea miungu. Watu wangeangalia duniani au angani wakitafuta ishara. Uaguzi ulikuwa wa kawaida sana hivi kwamba mazoea hayo yakaja kujulikana kuwa disciplina Etrusca, sayansi ya Waetruria.

Kufyonzwa na Kutoweka Kabisa

Katika mwaka wa 509 K.W.K., nasaba ya karne moja ya wafalme Waetruria waliokuwa wakitawala Roma ilikwisha. Hili lilikuwa ishara ya mambo yajayo. Kaskazini Waetruria walitishwa na Waselti, ambao mashambulio yao yalivunja nguvu za Waetruria katika eneo hilo. Kuelekea kusini, mapigano ya mpakani yenye kuendelea na watu wa Kiitalia yalidhoofisha misingi ya nguvu zao, ikikuza mavutano ya kijamii ya kindani.

Kufikia karne ya tatu K.W.K., eneo la Waetruria lilikuwa limekuja chini ya utawala wa Waroma. Hivyo kikaanza kipindi cha kuingizwa kwa tamaduni za Kiroma, au kufanya kila kitu kama Waroma. Hatimaye, katika mwaka 90 K.W.K., watu wote wa Kiitalia walipopewa uraia wa Roma, alama ya mwisho itambulishayo Waetruria ilikwisha. Waetruria walipaswa kuongea Kilatini na walifyonzwa katika ulimwengu wa Kiroma. Kwa wazi, si wasomi wengi wa Kiroma waliofanya jitihada ya kutafsiri au hata kuhifadhi maandishi za Waetruria. Hivyo basi, ustaarabu wa Waetruria ulipotea, ukiacha fumbo. Lakini pia uliacha urithi.

Urithi Wenye Kudumu

Urithi wa Waetruria unaonekana hadi leo katika Roma. Waroma walipata kutoka kwa Waetruria hekalu lao la Capitoline, lililowekwa wakfu kwa miungu ya utatu ya Jupiter, Juno, na Minerva; mahekalu yao yenye sehemu tatu; kuta zao za kwanza za jiji; na mfereji wa kuondolea maji machafu ambao uliondoa maji kwenye lile Baraza. Hata mbwa-mwitu wa Capitoline (Lupa Capitolina), iliyo ishara ya Roma, ina asili ya Waetruria. Kwa kuongezea, Waroma walichukua desturi kadhaa za Waetruria, kama vile michezo ihusishayo kupigana hadi kifo na kupigana na wanyama. (Linganisha 1 Wakorintho 15:32.) Aina ya mwandamano wenye shangwe ya ushindi ambao bila shaka Paulo alikuwa nao akilini katika kimojawapo cha vielezi vyake ina asili ya Waetruria.—2 Wakorintho 2:14.

Alama za Waetruria zimetumika pia kwa njia nyingi. Fimbo ya kuhani wa Etruria, ifananayo na fimbo ya uchungaji, imetambuliwa kuwa inahusiana na fimbo ya maaskofu wa Jumuiya ya Wakristo. Fimbo ya Waetruria (fito zilizofungwa pamoja kuzunguka shoka) ilitumiwa na Waroma ikiwa alama ya mamlaka, ikiwa ufananisho wakati wa Mapinduzi ya Ufaransa, na chama cha Kifashisti cha Italia katika karne ya 20.

Japo jitihada za pamoja za waakiolojia za kugundua yaliyopita, asili ya Waetruria na mambo mengi ya maisha zao yabaki yakiwa fumbo.

[Ramani katika ukurasa wa 24]

ETRURIA

ITALIA

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

1. Mbwa-mwitu jike wa Capitoline, ishara ya jiji la Roma, nakala ya shaba ya Waetruria ya karne ya tano K.W.K.

2. Ikiandikwa katika Kietruria (kulia) na Kifoinike (kushoto), mabamba haya ya dhahabu yamebeba wakfu kwa Uni (Astarte)

3. Jeneza la jiwe la wenzi la Waetruria

4. Tao la Waetruria kutoka karne ya nne K.W.K. Waroma walijifunza kujenga tao kutoka kwa Waetruria

5. Jagi la Waetruria na kitegemezi kutoka karne ya saba K.W.K., lililotumiwa kuchanganyia divai

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Mabamba ya dhahabu: Museo Nazionale di Villa Giulia, Roma; jeneza la mawe na jagi la kuchanganyia divai: Musée du Louvre, Paris

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki