Njia Sita za Kulinda Afya Yako
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NIGERIA
KULINGANA na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), karibu asilimia 25 ya watu wanaoishi katika nchi ambazo hazijasitawi sana hawawezi kupata maji yaliyo salama. Zaidi ya asilimia 66—angalau watu bilioni 2.5—wanakosa njia zifaazo za kuondolea takataka na maji machafu. Kwa wengi matokeo yanakuwa ugonjwa na kifo.
Katika hali kama hizo, kudumisha hali nzuri ya usafi wa kiafya ni vigumu. Na bado, ukifanya usafi wa afya yako binafsi uwe njia yako ya maisha, utajikinga dhidi ya maradhi mengi. Hapa pana hatua sita uwezazo kuchukua ili kujilinda wewe na familia yako dhidi ya vijidudu viwezavyo kuingia mwilini na kusababisha afya mbaya.
1. Nawa mikono kwa sabuni na maji baada ya kugusa kinyesi na kabla ya kugusa chakula.
Njia moja muhimu ya kuzuia ugonjwa ni kuhakikisha kwamba sabuni na maji zapatikana kila wakati ili kila mmoja katika familia yako aweze kunawa mikono. Sabuni na maji huondoa vijidudu kwenye mikono—vijidudu ambavyo huenda vikaingia katika chakula au mdomoni. Kwa kuwa watoto wachanga mara nyingi huweka vidole vyao midomoni, ni jambo muhimu kuosha mikono yao mara kwa mara, hasa kabla ya kuwapa chakula.
Ni jambo muhimu hasa kunawa mikono kwa sabuni baada ya kutoka msalani, kabla ya kugusa chakula, na baada ya kumpangusa mtoto mchanga au mtoto aliyeenda choo.
2. Tumia Msala.
Ili kuzuia kuenea kwa vijidudu, ni jambo la muhimu kuondosha kinyesi kwa njia inayofaa. Magonjwa mengi, hasa kuhara, hutokana na vijidudu katika kinyesi cha binadamu. Vijidudu hivi vyaweza kuingia katika maji ya kunywa au chakula, kwenye mikono, au kwenye vyombo na mahali patumiwapo kutayarishia au kuandalia chakula. Hilo linapotukia, watu waweza kumeza vijidudu na kuwa wagonjwa.
Ili kuzuia hili, tumia msala. Kinyesi cha wanyama chapasa kuwekwa mbali na nyumba na vyanzo vya maji. Huenda ukashangaa kujua kuwa kinyesi cha watoto wachanga na watoto wadogo ni hatari zaidi kuliko cha watu wazima. Kwa hiyo hata wachanga wapaswa kufundishwa kutumia msala. Watoto wanapoenda choo mahali pengine, kinyesi chao chapasa kuondolewa mara moja na kutupwa msalani au kufukiwa.
Msala wapasa kuwekwa ukiwa safi na kufunikwa.
3. Tumia maji safi.
Familia zilizo na ugavi mwingi wa maji safi, ya mfereji huwa wagonjwa mara chache zaidi ya wasio nayo. Wale wasio na maji ya mfereji wanaweza kuilinda afya yao kwa kufunika visima na kuweka maji machafu mbali na maji ya kunywa, kuoga, au kusafishia. Ni jambo muhimu pia kuwaweka wanyama nje ya nyumba na mbali na maji ya kunywa.
Njia nyingine ya kujilinda kutokana na maradhi ni kuweka ndoo, kamba, na mitungi ya kutekea na kuhifadhia maji zikiwa safi iwezekanavyo. Kwa kielelezo, ni afadhali, kuangika ndoo badala ya kuiacha kwenye ardhi.
Maji ya kunywa yanayowekwa nyumbani yapasa kuwekwa katika chombo safi, kilichofunikwa. Ili kuondoa maji kwenye chombo hicho wapaswa kutumia kata au kikombe safi. Usiwaruhusu watu kuweka mikono ndani ya maji ya kunywa au kunywa moja kwa moja kutokana na chombo cha kuhifadhia maji.
4. Chemsha maji ya kunywa isipokuwa yawe yanatoka katika mfereji ulio salama.
Maji ya kunywa yaliyo salama zaidi kwa kawaida hutoka katika mfereji. Ni rahisi kwa maji kutoka vyanzo vingine kuwa na vijidudu, hata ingawa yaweza kuonekana kuwa safi.
Kuchemsha maji huua vijidudu. Kwa hiyo unapoteka maji kutoka katika vidimbwi, vijito, au matangi, ni jambo la hekima kuyachemsha na kisha kuyaacha yapoe kabla ya kuyanywa. Maji ya kunywa yasiyo na vijidudu ni muhimu hasa kwa watoto wachanga na watoto wadogo, kwa sababu kinga yao dhidi ya vijidudu ni ndogo kuliko ya watu wazima.
Ikiwa haiwezekani kuchemsha maji ya kunywa, yaweke katika chombo kilichofunikwa kilichotengenezwa kwa plastiki nyangavu ama kioo. Kisha kiache chombo kikae kwenye jua kwa siku mbili kabla ya kuyatumia maji hayo.
5. Weka chakula chako kikiwa safi.
Chakula cha kuliwa kikiwa kibichi chapaswa kusafishwa vizuri. Vyakula vingine hasa nyama na kuku, vyapasa kupikwa kikamili.
Ni vizuri kula chakula mara tu kinapopikwa; kwa njia hiyo hakitakuwa na wakati wa kuharibika. Ikiwa ni lazima uweke chakula kilichopikwa kwa zaidi ya muda wa saa tano, lazima ukiweke kikiwa moto ama katika friji. Kabla ya kukila wapaswa kukipasha moto kikamili.
Nyama mbichi kwa kawaida huwa na vijidudu, kwa hiyo hupaswi kuiruhusu iguse chakula kilichopikwa. Baada ya kutayarisha nyama mbichi, safisha vyombo na uso wowote wa jikoni ambao huenda imeugusa.
Uso wa kutayarishia chakula wapaswa kuwa safi kila wakati. Chakula chapasa kufunikwa na kuwekwa mbali na nzi, panya, na wanyama wengine.
6. Choma au funika takataka za nyumbani.
Nzi, ambao hueneza vijidudu, hupenda kuzaana mahali palipo na takataka za chakula. Kwa hiyo takataka za nyumbani hazipasi kutupwa kwenye sakafu. Kila siku, zapasa kufunikwa, kuchomwa, au kutupwa katika njia nyingine.
Kwa kufuata miongozo hii, waweza kujilinda wewe na familia yako dhidi ya kuhara, kipindupindu, homa ya matumbo, maambukizo ya minyoo, usumishaji wa chakula, na magonjwa mengine mengi.
[Hisani]
Chanzo: Facts for Life, kimechapishwa kwa ushirikiano wa United Nations Children’s Fund, United Nations Educational, Scientific, and Cultural Organization, na WHO.