Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 12/8 kur. 20-23
  • Mbilikimo—Watu wa Katikati ya Msitu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mbilikimo—Watu wa Katikati ya Msitu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Habari ya Kufanyiwa Utafiti
  • Ziara ya Kwanza
  • Maisha ya Kila Siku, Ndoa, na Familia
  • Dini
  • Watu Wenye Akili
  • Kuwahubiria Mbilikimo Kweli za Biblia
    Amkeni!—2004
  • Mambo Tuliyojifunza Kutoka kwa Mbilikimo
    Amkeni!—2003
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2004
  • Magumu ya Vita Yalinitayarisha kwa Ajili ya Maisha
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 12/8 kur. 20-23

Mbilikimo—Watu wa Katikati ya Msitu

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

NJOO ukutane na BaBinga, ambao ni Mbilikimo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, nyumbani kwetu. Yaelekea umesikia na kusoma habari fulani kuhusu Mbilikimo, lakini huenda hujakutana kamwe na mmoja wao. Utembeleapo Bangui, jiji kuu, safari inayopungua muda wa saa mbili itakufikisha moja kwa moja hadi kwenye eneo lao.

Mashahidi wa Yehova wana ujumbe wa maana kwa mataifa, makabila, jamii na vikundi vyote vya watu. Katika utendaji wetu wa Kikristo, tunahubiria aina zote za watu. Hawa hutia ndani Mbilikimo.—Ufunuo 14:6.

Kwa hiyo tafadhali jiunge nasi uone jinsi wanavyoishi na namna wanavyoitikia habari njema ya Ufalme wa Mungu, ambao utaleta Paradiso kwenye dunia. Itakuwa siku yenye kupendeza na yenye kukuvutia sana.

Habari ya Kufanyiwa Utafiti

Kabla ya kwenda, inafaa tufanye utafiti fulani juu ya watu ambao tutawatembelea. Kuna vitabu ambavyo vimeandikwa na watu ambao waliishi kwa miezi kadhaa miongoni mwa hao Mbilikimo, wakijifunza utamaduni, dini, na mazoea yao.

Kusoma juu ya watu hawa wenye amani na urafiki na kisha kuwatembelea kutajibu maswali fulani, kama vile: Mbilikimo walitoka wapi? Twaweza kujifunza nini kutokana nao? Wanaishi wapi? Ni nini kinachowafanya wawe tofauti na vikundi vingine vya Kiafrika? Wanapatanaje na watu wengine wote?

Kamusi Webster’s Third New International Dictionary inataarifu kwamba Mbilikimo ni “watu wadogo wa ikweta ya Afrika wenye kimo kinachopungua futi tano [meta 1.5], . . . wakitumia lugha za majirani wao.” Mbilikimo wa Afrika wanadhaniwa kuwa hawana asili moja na Wanegrito (limaanishalo “Wanegro Wadogo”) wa visiwa vya Bahari ya Pasifiki na sehemu ya kusini-mashariki mwa Asia.”

Neno “pygmy” (mbilikimo) linatokana na neno la Kigiriki linalomaanisha “umbali wa kutoka kiwiko hadi konzi.” Mbilikimo wanajulikana kuwa wawindaji na wakusanya-vitu. Idadi ya jumla ya Mbilikimo ulimwenguni pote inakadiriwa kuwa inayozidi kidogo 200,000.

Serge Bahuchet na Guy Philippart de Foy wanatupatia habari zaidi zenye kupendeza katika kitabu chao Pygmées—peuple de la forêt (Mbilikimo—Watu wa Msitu). Wao wasema, Mbilikimo wanakaa katikati ya misitu ya Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Gabon, Kamerun, na Jamhuri ya Afrika ya Kati na wanaweza kupatikana hata mashariki ya mbali huko Rwanda na Burundi.

Hakuna mtu yeyote ajuaye sawasawa walikotoka Mbilikimo au ni lini walipowasili. Hawatumii neno “mbilikimo” kamwe kujitambulisha. Katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwa ujumla wanaitwa BaBinga, lakini katika nchi nyinginezo, wanajulikana kama BaKola, BaBongo, BaAka, BaMbènzèlè, BaTwa, na BaMbuti.

Ziara ya Kwanza

Twaondoka Bangui katika gari aina ya Land Cruiser asubuhi mapema, saa moja hivi, kuelekea kusini hadi M’Baiki Mongoumba. Barabara imetiwa lami kwa kilometa 100 za kwanza. Ni vyema kuwa na gari lenye kuendeshwa kwa magurudumu manne, kwa kuwa barabara ni yenye utelezi kufuatia mvua ya usiku wa jana.

Twaendesha kupitia mashambani yenye kusitawi yaliyo ya kijani kibichi yenye misitu mikubwa na kupitia vijiji vidogo ambapo watu huuza ndizi, ndizi mbichi, mananasi, mihogo, mahindi, maboga, na njugu kando za barabara kwenye meza ndogo. Njaa kuu haijulikani hapa. Udongo mzuri na tabia ya nchi yenye unyevunyevu hutokeza vyakula aina mbalimbali kwa wingi. Ndipo, kwa ghafula, twafikia “kijiji” cha kwanza, ama tuseme kambi ya BaBinga.

Wanaishi ndani ya vibanda vidogo vya kushangaza vyenye umbo la kuba vilivyo na mwingilio mmoja uruhusuo tu kutambaa ndani. Wanawake hujenga vibanda hivyo wakitumia vijiti na majani kutoka kwenye msitu ulio karibu. Karibu vibanda 10 hadi 15 hupangwa katika mviringo. Hivi hutumika kama makao ya kulala pekee ama kujilinda kutokana na mvua nzito. Maisha ya kila siku huwa ni nje.

Tunatoka kwenye gari kusalimu wanawake fulani, kila mmoja akiwa amebeba mtoto kwenye nyonga yake. Wakiwa wamesikia gari letu, baadhi ya wanaume waja mbio kuona sisi ni nani na tunalotaka. Wako na mbwa kadhaa, kila mmoja akiwa amefungiwa kengele ndogo kuzunguka shingo yake.

Kutokana na utafiti wetu twakumbuka kwamba wanyama wa kufugwa pekee ambao Mbilikimo wanao ni mbwa. Hao ni waandamani wao katika kuwinda. Na wanyama wawezao kuwindwa waweza kupatikana kila mahali, kutoka ardhini hadi juu ya miti. Kama vile kitabu Pygmées—peuple de la forêt kinavyoeleza, wao watia ndani ndege, tumbili, tembo, nyati, panya, paa, nguruwe-mwitu, kindi, na wengineo wengi. Mbwa mwaminifu ni wa lazima kwa kila mwindaji.

Katika kuongea na watu hawa, tunatumia Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia na broshua Furahia Milele Maisha Duniani!a Hivi huonyesha kwa vielezi kwamba karibuni dunia itakuwa paradiso iliyo na misitu maridadi, ambapo hakutakuwa na ugonjwa au kifo. (Ufunuo 21:4, 5) Vichapo vyote viwili huchapwa katika Sango, lugha inayosemwa na zaidi ya asilimia 90 ya idadi ya watu, kutia ndani Mbilikimo. Watu hawa wenye amani, mahali popote wanapoishi, hutumia lugha ya majirani wao wa Kiafrika. Hii ni lazima kwa sababu wao ni wafanya-biashara wenye kubadilishana vitu na majirani wao.

Punde si punde, wanaume na wanawake kadhaa wamesimama kutuzunguka, wakitazama kwa msisimuko picha moja baada ya nyingine huku wakisikiliza maelezo yanayotolewa. Kutokana na ziara za hapo zamani kwa miaka iliyopita, wanatujua kama Mashahidi wa Yehova. Wanafurahi kupokea nakala za vichapo hivyo. Hata hivyo, tatizo ni kwamba hawawezi kusoma. Kwa miaka ambayo imepita, jitihada zimefanywa na serikali pamoja na taasisi mbalimbali za kuwafundisha kusoma na kuandika, lakini imekuwa kazi bure. Shule ilipangwa kwa ajili ya watoto wao. Shule zilitenda kwa muda, lakini watoto wengi waliacha baada ya muda fulani. Mwalimu ambaye amefanya kazi na Mbilikimo alitaarifu kwamba wanapokuwa darasani wanaonyesha uwezo wa ajabu wa kujifunza, lakini baada ya miezi kadhaa ya kuhudhuria shule, wanatoweka tu. Hata hivyo, jitihada za kuandaa mafunzo rasmi zaendelezwa na wenye mamlaka wa mahali hapo na wengineo.

Mashahidi wa Yehova wanajulikana kwa kutembelea tena watu wanaoonyesha upendezi katika Neno la Mungu. Lakini hatutazamii kukutana na BaBinga walewale wakati ujao tunapokuja huku, kwa kuwa daima wao huhama mwaka wote. Wao hutoweka na kwenda kwenye makao yao yaliyo katikati ya msitu. Jitihada za kuwafanya wazoee makazi ya kudumu zimekosa mafanikio. Kwa kweli, wao ni watu wa katikati ya msitu. Kuhama kila mahali na kuwinda ndiyo njia yao ya maisha, na hakuna kitu kinachoweza kuwabadili.

Maisha ya Kila Siku, Ndoa, na Familia

Kwa msingi, wanaume huwinda na wanawake hukusanya, wakikusanya karibu kila kitu kinachotokezwa na msitu: uyoga, mizizi, matunda madogo, majani, njugu, wadudu, mchwa, asali ya mwitu, na, bila kusahau, viwavi ambavyo wanavipenda sana. Vitu vyote hivi vyahitajiwa kwa ajili ya chakula na kwa biashara. Majirani wa Kiafrika wa Mbilikimo hawa, ambao mara nyingi huitwa les grands noirs (weusi warefu), huwategemea sana kwa vitu hivi. Katika kubadilishana, wao huandalia Mbilikimo nyungu, sufuria, panga, vyombo kama mashoka na visu, chumvi, mawese, mihogo, ndizi mbichi, na pia kwa kusikitisha, tumbako, kileo cha kienyeji, na bangi. Vitu hivyo vitatu vya mwisho ni tatizo kubwa sana kwa watu hawa wanyenyekevu. Mara nyingi wanaingia katika deni ili kuvipata, na pole kwa pole maisha zao huharibika.

Wanaume kwa kawaida huoa mke mmoja. Hata hivyo, wao ni wepesi wa kutaliki au kutengana ili kuishi na mwenzi mwingine. Baba au aliye mzee kuliko wote katika kambi hustahiwa zaidi. Yeye hatoi amri, lakini shauri lake hufuatwa kwa ukawaida. Utaona ya kwamba Mbilikimo hupenda watoto wao. Mara nyingi mama na baba hubeba mtoto wao. Wadogo hawa daima huwa na wazazi wote wawili kila mahali wanapokwenda na chochote wanachofanya, iwe ni kufanya kazi, kuwinda, au kucheza dansi.

Usiku mtoto mchanga hulala katikati ya wazazi. Wakati wa mchana, wazazi, ndugu, dada, wajomba, na wazakuu hulinda walio wachanga, na licha ya hayo, wana uangalifu wa kambi nzima. Ziara miongoni mwa wazazi na jamaa hufanywa mara nyingi. Yote haya huimarisha vifungo vya familia. Katika ustaarabu wa Magharibi vifungo vya familia mara nyingi hulegea au kuvunjika, lakini hapa hali ni tofauti sana.

Ingawa Mbilikimo huishi mbali na majirani wenzao wa Kiafrika, wana uhusiano wa kiuchumi nao. Mbali na kuwa na uhusiano wa kawaida kupitia biashara, mara nyingi wanaombwa kufanya kazi kama vibarua katika mashamba ya kahawa na kakao. Wanaweza kufanya kazi kwa majuma machache, walipwe, kisha warudi katikati ya msitu kwa muda mrefu. Nani ajuaye? Ile kahawa uliyofurahia asubuhi ya leo yaweza kuwa ilipitia mikononi mwa Mbilikimo wa Afrika ya Kati.

Dini

BaBinga ni watu wa kidini, lakini ushirikina na mapokeo hutawala maisha yao ya kidini. Wanazoea desturi zao zikiandamana na muziki, kuimba (kwa madoido), na kucheza dansi. Kile Kitabu Ethnies—droits de l’homme et peuples autochtones (Makabila—Haki za Kibinadamu na Wenyeji) chatoa maelezo haya: “Kwa watu wa katikati ya msitu, Mungu aliumba ulimwengu, ikimaanisha msitu. Baada ya kuumba wenzi wa kwanza wa kibinadamu . . . alistaafu mbinguni na kupoteza upendezi katika mambo ya kibinadamu. Sasa roho mkuu kuliko wote, yule mungu wa msitu, anatenda kwa ajili yake.” Bila shaka, hili latofautiana sana na maelezo juu ya Mungu na kusudi lake kama yapatikanavyo katika Biblia—Mwanzo, sura ya 1, 2; Zaburi 37:10, 11, 29.

Watu Wenye Akili

Ni kawaida kwa watu fulani kudhihaki au hata kuwadharau Mbilikimo, wakiwafikiria kuwa wa hali ya chini na wasio na akili sana. Lakini Patrick Meredith, profesa wa fizikia ya akili kwenye Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza, alisema: “Ukiwaona Mbilikimo katika mazingira yao ya asili wakitengeneza daraja kutoka kwa nyuzi za mimea na kuishi maisha yenye mafanikio huenda ukajiuliza ni nini linalomaanishwa na kuwa mwenye akili.”

Twajua ya kwamba wanadamu wote ni wazao wa wanadamu wawili wa kwanza Adamu na Hawa. Matendo 17:26 husema: “[Mungu] alifanya kutoka kwa mtu mmoja [Adamu] kila taifa la watu, ili wakae juu ya uso mzima wa dunia.” Na Matendo 10:34, 35 hutaarifu kwamba “Mungu si mwenye ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye humhofu na kutenda uadilifu akubalika kwake.” Kwa hiyo, tunataka kupeleka kweli za Biblia kwa watu hawa ili wao pia waweze kuwa na tumaini la kuishi wakati ambao karibuni dunia yote itageuzwa iwe paradiso nzuri yenye misitu minene mingi.

[Maelezo ya Chini]

a Vilivyochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 23]

1. Kushiriki ujumbe wa Biblia na Mbilikimo; 2. Mbilikimo mchonga-vinyago; 3. kao halisi la Mbilikimo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki