Kuutazama Ulimwengu
Uraibu wa Alkoholi Katika Mexico
Uchunguzi mbalimbali uliofanywa na Taasisi ya Usalama wa Jamii ya Mexico ulionyesha kwamba kulikuwa na zaidi ya waraibu wa alkoholi milioni nne katika Mexico katika mwaka wa 1991. Lakini kufikia mwaka wa 1997, huenda ikawa idadi hiyo imeongezeka maradufu, laripoti gazeti la habari la El Universal la Jiji la Mexico. Lanukuu Shirika la Kusaidia Waraibu wa Alkoholi likisema kwamba kati ya waraibu wa alkoholi milioni nane katika Mexico, milioni tatu wanapatikana katika Jiji la Mexico. Kulingana na El Universal, uhalifu mwingi katika Mexico unafanywa chini ya uvutano wa alkoholi. Matumizi mabaya ya alkoholi hutokeza kukosa kwenda kazini na kufanya vibaya shuleni. José Manuel Castrejón, ambaye ni mwakilishi wa Baraza la Taifa Dhidi ya Uraibu, asema kwamba “asilimia 50 ya ujeuri katika familia na aksidenti moja kati ya tano kazini zinahusika kwa ukaribu na matumizi ya alkoholi.”
Madokezo kwa Wasafiri wa Ndege
Usafiri wa mbali wa ndege hutokeza mkazo akilini na mwilini, na gazeti la habari la The Times la London latoa madokezo fulani ili kupata kitulizo. Haya yatia ndani “kuepuka kunywa alkoholi lakini kunywa soda nyingi, kula vyakula vyepesi tu na kujiona kwamba upo mahali pa kufurahisha.” Kukaa tuli kwa vipindi virefu kwaweza kusababisha kuvimba kwa miguu na kufanya nguo kubana. Kwa hiyo, laripoti The Times, “madaktari wadokeza kulegeza nguo, kuvua viatu na kuomba kukaa katika viti vilivyo kando ya njia ili uweze kutembea mara kadhaa kuelekea chooni.” Kunyoosha mikono na miguu yako wakati wa safari husaidia kuzuia matatizo ya mzunguko wa damu. Katika kupambana na uchovu wa kusafiri katika ndege, “wasafiri wazoefu mara nyingine hurekebisha utendaji wao wa kila siku kabla ya safari zao. Wale waelekeao mashariki huamka mapema kwa kipindi cha juma moja na wale waelekeao magharibi hulala wakiwa wamechelewa.”
Kunguru wa Tokyo Wanaosafiri
Kunguru katika Tokyo, Japani, wamekuwa na tabia ya kusafiri kati ya vitongoji na katika jiji kila siku, laripoti gazeti la The Daily Yomiuri. Wataalamu wa ndege wasema kwamba kusafiri huku kulianza wakati idadi ya kunguru katika bustani na viwanja vya mahekalu vya Tokyo ilipoongezeka sana kiasi cha kuwalazimisha kunguru kujenga viota vyao mahali pengine. Hapo ndipo walipogundua raha za maisha ya vitongojini. Hata hivyo, kitu walichokosa ni chakula kitamu cha mjini—takataka na mabaki ya chakula yaliyotupwa. Walitatua tatizo hili kwa kuanzisha “taratibu za kusafiri ambazo zafanana na za wafanyakazi wanaolipwa mshahara. Wao huruka kwenda maeneo ya mjini wakati wa asubuhi kutafuta chakula,” lasema The Daily Yomiuri, “kisha warudi vitongojini jioni.”
Mali ya Asili Yatishwa
◆ Eneo la kaskazini-mashariki mwa India, ambalo lina mimea mingi na wanyama wengi, sasa laorodhesha spishi 650 za mimea na spishi 70 za wanyama kuwa ziko hatarini mwa kutoweka. Mfumoikolojia ulio rahisi kuharibiwa katika jimbo la Meghalaya, mpakani na Bangladesh, umetambulishwa kuwa moja ya maeneo 18 yanayohitaji uangalifu wa haraka ambapo aina mbalimbali za mimea na wanyama zimo hatarini. Kama ilivyoripotiwa katika The Asian Age, mfumoikolojia umeshambuliwa na uharibifu mkubwa unaosababishwa na mwanadamu na uwindaji-haramu, miongoni mwa sababu nyingi. Aina mbalimbali za mimea na wanyama katika majimbo saba ya kaskazini-mashariki mwa India zinafikiriwa ni rahisi kuharibiwa na ni nyetivu kiikolojia zaidi ya sehemu nyingine za hiyo nchi.
◆ Katika Italia idadi ya spishi na spishi-ndogo za mimea ambazo ziko katika hatari inaongezeka. Katika mwaka wa 1992, 458 zilifikiriwa kuwa ziko hatarini mwa kutoweka, lakini kufikia mwaka wa 1997, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka kuwa 1,011. “Karibu sehemu moja kati ya saba ya mimea mbalimbali ya Italia iko hatarini mwa kutoweka kwa njia fulani, na karibu spishi 29 zimetoweka katika miaka michache iliyopita,” laeleza gazeti la Corriere della Sera. Zaidi ya spishi 120 ziko “katika hali ya hatari sana ya kutoweka katika wakati mfupi unaokuja,” na karibu 150 zaweza kuwa katika hatari ya kutoweka katika wakati mfupi ujao. Kulingana na maoni ya mwanabotania Franco Pedrotti, wa Chuo Kikuu cha Camerino, “tarakimu hizi zafunua hali ya hatari.” Mmea mmoja ulitoweka katika mazingira yake ya asili wakati eneo pekee ambalo lilikua lilipogeuzwa kuwa uwanja wa kandanda.
◆ Katika Argentina spishi 500 kati ya 2,500 za wanyama wa asili ziko hatarini, laripoti gazeti la habari la Buenos Aires Clarín. “Ingawa kuhifadhi namna za uhai ndio ufunguo wa kuhakikisha hali njema ya sasa na ya wakati ujao wa watu, wanyama wengi wapo katika hatari ya kutoweka,” kulingana na Claudio Bertonatti, mratibu wa idara ya hifadhi ya Wakfu wa Wanyama wa Pori. Miongoni mwa wanyama watishwao katika Argentina ni aina mbalimbali za armadilo, jagua, vicuña, nyangumi, na kobe wa nchi kavu. “Ingawa hairuhusiwi kuwauza,” yaona ripoti hiyo, katika jiji lenyewe la Buenos Aires “kiasi cha kobe wapatao 100,000 wanauzwa kila mwaka.” Bertonatti alisema hivi: “Mwanadamu, ambaye hasa alipaswa kuwa mtu mwenye kupendezwa kulinda utajiri huu, ndiye anayesababisha matisho mengi ambayo yanafanya spishi nyingi zikaribie kutoweka.”
Je, Maria Alikuwa Mtu wa Kwanza Kumwona Kristo Aliyefufuliwa?
Papa John Paul wa Pili amesisitiza kwamba “ni haki kufikiria kwamba Mama [ya Yesu, Maria] huenda ikawa alikuwa ndiye mtu wa kwanza kutokewa na Yesu aliyefufuliwa.” (L’Osservatore Romano) Hakuna yoyote kati ya masimulizi ya Gospeli nne izungumzayo kuhusu kuwapo kwa mama ya Yesu wakati kaburi lake lilipopatikana likiwa tupu. Hata hivyo, Papa alisema hivi pia: “Ingewezekanaje kwamba Bikira Mbarikiwa, akiwapo katika jumuiya ya kwanza ya wanafunzi (rejezea Matendo 1:14), hakuwapo miongoni mwa wale waliokutana na Mwana wake wa kimungu baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu?” Papa alitumia hoja mbalimbali kujaribu kueleza ni kwa nini hakuna rekodi katika Gospeli juu ya kukutana kokote kati ya Yesu na mama yake. Jambo la hakika ni kwamba roho takatifu haikuwapulizia waandikaji wa Gospeli kutaja tukio lolote kama hilo. Wala hata hatajwi katika barua za mitume.—2 Timotheo 3:16.
Hatari ya Kiangazi Katika Kizio cha Kusini
Katika Kizio cha Kusini, Januari ni mmoja kati ya miezi yenye joto zaidi. Wakati halihewa ni joto ni muhimu kujilinda dhidi ya ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto jingi, laeleza gazeti la FDA Consumer. Ingawa ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto jingi husababisha mamia ya vifo kila mwaka, waweza kuzuilika kabisa, asema mtaalamu wa matezi ya ndani Dakt. Elizabeth Koller. Ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto jingi waweza kutokezwa na kufanya kazi ngumu katika joto, lakini hushambulia pia wazee-wazee ambao hawana kiyoyozi na ambao wana matatizo ya msingi ya afya, kama vile kisukari au maradhi ya moyo. Wakati halijoto iongezekapo, lashauri gazeti la FDA Consumer, kunywa maji mengi—lita moja kwa saa ikiwa unafanya mazoezi. Ukiwa juani, vaa kizuia-jua, kofia yenye mviringo mpana, na nguo zisizobana. Ikiwa huna kiyoyozi na kuna hatari ya kuzirai kutokana na joto, “oga kwa maji baridi, jimwagilie maji kwa mara nyingi, na ukae mbele ya pepeo. Ikiwa wahisi kizunguzungu, waite wanatiba wa dharura.” Dakt. Koller aonya: “Ikiwa mtu fulani anapanda joto sana, una dakika chache tu za kufanya jambo fulani ili kumwokoa.”
“Mateso” Kazini
“Maumivu ya kichwa, uchovu, kupoteza kumbukumbu, matatizo ya kuona, kizunguzungu, matatizo ya kupumua, kutoweza kusikia kunakosababishwa na kuziba kwa pua, tinnitus, [na] magonjwa ya ngozi”—yote yaweza kutokezwa kwa sababu ya kufanya kazi ndani ya majengo, au SBS, asema Jack Rostron aliye mtafiti wa Chuo Kikuu cha John Moores. Ugonjwa wa SBS, uliotambuliwa rasmi na Shirika la Afya Ulimwenguni katika 1986, waweza kubadili “jambo la mwanadamu la kwenda kazini kuwa jambo la mateso,” adai. Majumba yenye mfumo wa kiyoyozi yaliyo na madirisha yaliyofungwa kabisa yaweza kukusanya vichafua-hewa, kama vile gesi zenye sumu na vipande vitolewavyo na mashine za fotokopi na mashine za kupiga chapa, laripoti gazeti la The Independent la London. Ili kuepuka SBS, mifumo ya kiyoyozi lazima isafishwe kwa mara nyingi na isafishwe kabisa. Rostron aona hivi: “Utendaji wa kazi huongezeka wakati vikundi vidogo vya watu washirikipo ofisi ndogondogo zenye madirisha ya kufunguka.”
Onyo la Majira ya Baridi Kali
Mtu yeyote atumiaye wakati nje ya nyumba wakati wa majira ya baridi kali na upepo yupo katika hali ya hatari ya kupoteza joto mwilini, lasema gazeti la habari la The Toronto Star. Jambo hili hutokea “wakati mwili upotezapo joto jingi zaidi ya lile uwezalo kulitokeza,” yaona ripoti hiyo, ikiongeza kwamba “halijoto haihitaji kuwa chini ya sufuri kwa mwili kupoteza joto.” Hali ya ujenzi na uvunjajivunjaji wa kemikali mwilini mwa wazee-wazee haiwezi mara nyingi kufidia upotevu wa joto. Wao, pamoja na watoto wapo katika hatari zaidi. Mtu anapokuwa “mwenye baridi, ameloa, amechoka, mwenye njaa, anatetemeka, mwenye kulalamika, [na] hafurahii kuwa nje ya nyumba,” aweza kuwa katika hatari ya kupoteza joto mwilini, chaeleza kitabu Wilderness First Aid Handbook. Mtu kama huyo apaswa kupewa makao, nguo ambazo zimekauka, chakula, na umajimaji lakini si alkoholi au kafeni. Ikiwa haonyeshi dalili za kupona, msaada wa kitiba wapaswa kutafutwa mara.