Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Msitu wa Mvua wa Amazon Nilivutiwa sana na mfululizo wa makala “Msitu wa Mvua wa Amazon—Hekaya na Uhalisi.” (Machi 22, 1997) Nikiwa mwanaekolojia wa mimea wa U.S. Forest Service, ni lazima nisome fasihi nyingi sana juu ya mazingira. Na bado, nafikiria makala yenu kuwa bora zaidi ambayo nimepata kusoma wakati wowote juu ya habari hii. Ilifanyiwa utafiti vizuri sana, ilikuwa yenye kufundisha, na ya kisasa, na ilikuwa yenye kupendeza kusoma. Ilinitia moyo kuona dhana kama vile namna-namna za uhai, uziduaji, utenganishaji wa spishi za mimea na wanyama katika visehemu vidogo vya msitu, na mfumikiolojia zikitokea katika jarida lenye ugawanyaji mwingi mno wa kimataifa. Hii itaboresha tu mambo.
D. S., Marekani
Nina umri wa miaka 12, na nataka kuwashukuru sana kwa ajili ya hizo makala. Nililazimika tu kuzisoma jioni ileile tuliyopokea hilo gazeti! Kwa kuwa twashughulika na habari hii katika somo la jiografia shuleni, nilimpa mwalimu wangu wa jiografia nakala moja siku iliyofuata. Bila shaka, hilo liliamsha udadisi wa wengine katika darasa, na ninatumaini kuwaangushia magazeti mengine zaidi.
T. E., Ujerumani
Kwa kweli hizo makala zilikuwa zenye kuvutia sana. Spishi za wadudu waliotajwa ni nyingi sana, kila moja ikiwa na kazi ya kufanya chini ya majani kwenye ardhi ya msitu. Yehova huhakikisha kwamba chakula hugawiwa wale wote wanaoishi pale. Naweza kuelewa kwa nini “ataleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia.”—Ufunuo 11:18.
D. K. H., Marekani
Kudhulumu—Kuna Ubaya Gani? Asanteni kwa makala “Vijana Huuliza . . . Kudhulumu—Kuna Ubaya Gani?” (Machi 22, 1997) Shuleni kila mtu humwaibisha aliye mnyonge zaidi, na mimi vilevile nilishawishwa kufanya jambo hilohilo. Lakini shauri lililotolewa katika makala hii la kujitia wenyewe katika hali ya mtu mwingine lilinisaidia sana kujizuia nisidhulumu. Asanteni kwa mara nyingine tena.
M. N., Ufaransa
Nina umri wa miaka 17, na ninawashukuru sana kwa ajili ya hiyo makala. Ni jibu kwa sala yangu, na kwa kweli ilinitia moyo. Kujua kwamba Yehova huchukia udhalimu kumenisaidia sana kufanya mabadiliko yanayotakikana katika mwenendo wangu. Ile Kanuni Bora na kielelezo cha Yesu pia kilinivutia, na zinanisaidia kutenda ifaavyo.
V. T., Italia
Hivi karibuni, katika chumba cha kusubiri, nilipata Amkeni! na kugundua makala hii iliyoandikwa vizuri. Bila shaka naelewa madhara ya kudumu yanayoweza kusababishwa na udhalimu. Ndugu yangu alikuwa akinidhulumu [mimi, dada yake] kwa maneno, kihisia-moyo, na kimwili. Ikiwa angeulizwa, angepuuza tu jambo hilo, acheke, na kudai ulikuwa ni mzaha tu. Angeniambia kwamba tatizo lilikuwa langu kwa sababu nilikosa ucheshi! Wakati nilipokuwa na miaka 13 na yeye miaka 15, alianza kunitisha kunisumbua kingono. Niliishi katika hali ya kumhofu daima kwa sababu alikuwa mwenye umri mkubwa zaidi, mwili mkubwa zaidi, na mwenye nguvu nyingi zaidi! Wazazi wangu hawakunilinda kamwe. Shukrani kwa Amkeni!, kwa ajili ya kushughulikia masuala mazito ya maisha. Najua inahitaji moyo mkuu. Nahisi mmechochea mioyo mingi na makala hii.
B. S. M., Marekani
Chungu Watunza-Bustani Baada ya kusoma ile makala “Mtunza-Bustani Stadi” (Machi 22, 1997), niliweza kuzuru maonyesho na kushuhudia utendaji uleule mliofafanua. Ilionekana kana kwamba majani yalikuwa yakisonga kwenye kamba ambayo ilining’inia kutoka kwenye dari. Kwa hakika, chungu walikuwa wamebeba hayo majani, na hapo karibu walikuwa wenye shughuli nyingi wakilima bustani ya kuvu. Kuona yale ambayo mlitaja kwa kweli ulikuwa ni mwono wenye kustaajabisha na ulituleta mimi na wasichana wangu wadogo wawili karibu zaidi na Baba yetu wa kimbingu mwenye upendo, Yehova.
P. F., Scotland