Funga Mkanda wa Usalama
◼ Katika Marekani, aksidenti za magari ndizo kisababishi kikuu cha vifo miongoni mwa vijana kutoka umri wa miaka 5 hadi 24.
◼ Katika Japani, aksidenti za barabarani husababisha vifo mara mbili zaidi ya kansa ya matiti na kuua mara nne zaidi ya kansa ya tezi-shahawa.
◼ Katika Ulaya, aksidenti za magari husababisha vifo vya watu mara nne zaidi ya uuaji wa kimakusudi.
TAKWIMU hizi zenye kushtua zakazia mojawapo ya hatari za kiasili za kusafiri kwa gari—mwendo wa kasi waweza kuua. Na mwendo wa kasi pamoja na alkoholi huua kimakusudi. Kwa uzuri, hatari za aksidenti na kujeruhiwa zaweza kupunguzwa. Hilo lawezekanaje?
Kukuza mazoea salama ya kuendesha ni mwanzo mzuri. Wataalamu fulani wa usalama wanadai kwamba aksidenti 9 kati ya 10 zingeweza kuzuiwa au kuepukwa. Kuzidi kikomo cha mwendo kilichoangikwa barabarani, kupindapinda katikati ya magari, kukaribia sana gari lililoko mbele, kuendesha ukiwa umetumia madawa ya kulevya au alkoholi, na kuendesha gari lisilotunzwa vizuri ni baadhi tu ya vielelezo vichache vya mazoea ya uendeshaji yasiyo salama. Staha kwa ajili ya uhai na upendo kwa binadamu mwenzetu wapaswa kutusukuma kujitwalia mtazamo wenye hadhari na kuwa wenye jukumu kuelekea kuendesha gari.—Mathayo 7:12.
Mikanda ya usalama ni hatua nyingine sahili ya usalama, lakini ambayo hukosa kutiliwa maanani mara nyingi. Kulingana na Tim Hurd, msemaji wa Wizara ya Uchukuzi ya Marekani, “mkanda wa usalama ndiyo njia yenye matokeo zaidi ya kuokoa maisha yako katika aksidenti. Inarudufisha uwezekano wa kuokoka.” Kwa abiria wenye umri mdogo zaidi, kiwango cha kuokoka kinakuwa karibu mara tatu zaidi wakitumia viti vya usalama vya mtoto.a
Licha ya hayo, uchunguzi unaonyesha kwamba karibu thuluthi moja ya wenye kusafiri katika magari ya abiria katika Marekani hawatumii mikanda ya usalama ya viti. Ukiwa mzazi, je, wahakikisha kwamba watoto wako wamefungwa kwa usalama ndani ya viti vyao kabla hujaanza kuendesha gari lako? Ule wakati ambao unatumika katika kujifunga mikanda bila shaka unastahili.
[Maelezo ya Chini]
a Shirika la Usimamizi wa Kitaifa wa Usalama Barabarani lapendekeza: “Watoto wanaoketi katika viti vya watoto vinavyoangalia nyuma hawapaswi kuketishwa katika viti vya mbele vya magari yaliyoandaliwa mifuko ya hewa katika upande wa abiria. Lile pigo la mfuko wa hewa wenye kuenea unaopiga kiti cha mtoto kinachoangalia nyuma lingeweza kutokeza majeraha kwa mtoto.”