Mshipi Unaookoa Uhai
“UTUMIAJI mshipi-kingaji ni mojapo ya njia yenye matokeo ya kupunguza idadi na uzito wa majeraha katika migongano ya magari,” lasema Morbidity and Mortality Weekly Report (MMWR). Kulingana na uchunguzi mmoja, hatari ya kufa katika gari inapunguzwa kwa asilimia 43 abiria wanapotumia ifaavyo mishipi ya kujikinga. Hatari ya majeraha mazito inapunguzwa kwa karibu asilimia 50.
Uhalalishaji wa utumizi wa mshipi-kingaji kwanza uliidhinishwa na Serikali ya Australia katika 1970. Sasa nchi zipatazo 35 zashurutisha utumizi wa mshipi-kingaji. Wakiukaji mara nyingi hutozwa faini na katika visa vingine hata wanahatarisha kazi yao ya uendeshaji kwani wanaweza kufutwa kazi. Serikali nyingine zimeidhinisha sheria zihitajizo abiria katika maeneo yote ya ukaaji (viti vya mbele na vya nyuma) kuvaa mishipi ya kujikinga.
MMWR laripoti kwamba “watu wakadiriwao kuwa 300,000 hufa na watu milioni 10-15 hujeruhiwa kila mwaka katika migongano ya magari ulimwenguni pote.” Idadi hiyo ingepunguzwa mno ikiwa watu wote hao wangekuwa wamevaa mishipi ya kitini.