“Pengo Linalopanuka Kati ya Makasisi na Watu wa Kawaida”
“KATIKA makanisa ya kievanjeli ya Marekani kuna pengo linalopanuka kati ya makasisi na watu wa kawaida,” aonelea Robert K. Johnston, profesa wa theolojia na utamaduni. Katika Ministerial Formation, gazeti la Baraza la Makanisa ya Ulimwengu, ataja baadhi ya hali zinazosababisha mtengano huu: Huku misongo ya familia ikiongezeka, mapasta wanataka ratiba za kazi zinazofanana na zile za “madaktari kufanya kwa zamu katika mwisho-juma.” Ikiwa pasta afanya kazi kwa saa za ziada, hutarajia kulipwa kwa ajili ya hiyo jitihada. Kwa kuongezea, asema huyo profesa, “kadiri misongo ya elimu-maadili na ya kisheria inavyoongezeka,” seminari za theolojia hutahadharisha wahitimu wake kuzuia matatizo kwa kuwa na “marafiki wa karibu miongoni tu mwa ‘klabu’ yao ya makasisi wengine” na kuwaona wakazi wa parokia zao kuwa “wateja.” Haishangazi kwamba wakazi wengi wa parokia, nao, huwaona mapasta wao kuwa wa jamii bora isiyofahamu mahitaji na matatizo ya mtu wa kawaida aendaye kanisani.
Ni pasta wa aina gani angeweza kuziba pengo hilo? Uchunguzi mmoja ambao ulichanganua kwa nini mapasta hukosa kufaulu katika huduma yao ulipata kwamba wakazi wa parokia hawaoni ujuzi wa usomi na stadi za kitaaluma za pasta kuwa za maana. Washiriki wa kanisa hawatazamii mtu aliyesoma sana, msemaji mwenye ufasaha, au msimamizi stadi. Zaidi ya yote, wanataka pasta wao awe “mtu wa Mungu” ambaye hutenda yale anayohubiri. Ikiwa sifa hiyo yakosekana, asema Profesa Johnston, “hakuna kiasi chochote cha habari iwasilishwayo au ustadi uonyeshwao” utakaoziba hilo pengo.
Biblia husemaje kuhusu matakwa kwa ajili ya mzee katika kutaniko? “Kwa hiyo mwangalizi apaswa kuwa asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi katika mazoea, timamu katika akili, mwenye utaratibu, mkaribishaji-wageni, mwenye sifa ya kustahili kufundisha, si mwenye fujo ya ulevi, si mpiga-watu, bali mwenye kukubali sababu, si mtaka-vita, si mpenda-fedha, mtu anayesimamia watu wa nyumbani mwake mwenyewe kwa njia bora, akiwa na watoto walio katika ujitiisho pamoja na uchukuaji-mambo kwa uzito wote . . . Zaidi ya hayo, yeye apaswa pia kuwa na ushuhuda bora kutoka kwa watu walio nje, ili asipate kuanguka ndani ya shutumu na mtego wa Ibilisi.”—1 Timotheo 3:2-4, 7.