Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 2/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ugunduzi wa Mapema wa Kansa ya Matiti
  • Waraibu wa Dawa Zinazouzwa Kihalali Bila Agizo la Daktari
  • Uwezo wa Wasichana wa Shule
  • Mtu Mzee Zaidi Ulimwenguni Afa
  • Watoto Wasemao Lugha Mbili
  • Hangaiko la Wachina Kuhusu Kulea Watoto
  • Adui Mbaya Zaidi wa Papa?
  • Kuwakusanya Kutoka Angani
  • Wakanada Wenye Shughuli Nyingi
  • Mkazo wa Kukosa Kazi ya Kuajiriwa
  • Papa-mweupe Mkubwa Ashambuliwa
    Amkeni!—2000
  • Papa Wanaangamizwa
    Amkeni!—2007
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2003
  • Pigo la Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 2/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Ugunduzi wa Mapema wa Kansa ya Matiti

Kansa ya matiti ndiyo yenye kuleta madhara zaidi kati ya wanawake wa Brazili, ikiathiri kwa kukadiria mwanamke 1 kati ya kila 12, laripoti jarida la Brazili Medicina Conselho Federal. Jarida hilo latia moyo kujichunguza matiti kwa ukawaida kwa wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 25. Medicina pia lapendekeza kuwa wanawake wapate picha ya matiti ya eksirei ya kwanza kati ya umri wa miaka 35 na 40, picha ya matiti ya eksirei kila miaka miwili kati ya miaka 40 na 50, na picha za matiti za eksirei za kila mwaka baada ya hapo. Ijapokuwa wanawake wanaokula milo iliyo na wingi wa mafuta kifu na wale walio na historia ya ugonjwa huo katika familia zao wako katika hatari kubwa zaidi, asilimia 70 ya wagonjwa wa kansa ya matiti hawakuwa na sababu yoyote ya hatari kubwa iliyojulikana. Jambo hili, laeleza Medicina, “laonyesha waziwazi umuhimu wa sera ya ugunduzi wa mapema.”—Ona Amkeni! la Aprili 8, 1994.

Waraibu wa Dawa Zinazouzwa Kihalali Bila Agizo la Daktari

Uraibu kwa dawa zinazouzwa kihalali bila agizo la daktari waongezeka katika Kaskazini mwa Ireland, laripoti The Irish Times. Katika Kaskazini mwa Ireland kama vile katika nchi nyingine nyingi, bidhaa kama vile dawa za kutuliza maumivu na dawa za kukohoa zilizo na kodeini au dawa nyingine zilizo na uwezekano wa kuraibisha zaweza kupatikana bila agizo la daktari. Watu fulani wanaokuwa waraibu bila kutaka hupigana kudumisha zoea lao, kwani kuiacha kwaweza kuwa kwenye maumivu makali na kutia ndani kichefuchefu na kushuka moyo. Mraibu mmoja alitumia urithi wake, akauza nyumba yake, akapata deni la pauni 18,000 (dola 29,000) ili kulipia chupa 70 za dawa kila juma. Frank McGoldrick, wa Kikundi cha Utafiti Kuhusu Utegemeo wa Madawa, asema kuwa wengi wa watu wanaotumia vibaya madawa yanayouzwa kihalali bila agizo la daktari hawataki kufanya lolote ili kukubali utegemeo na wanaonyesha hangaiko kidogo kwa kupuuza wazo la kwamba wanajiletea madhara. “Hawavunji sheria,” aeleza McGoldrick. “Wengi hata hawatambui kuwa wanatumia vibaya dawa hizo.”

Uwezo wa Wasichana wa Shule

Wasichana wa shule za upili ndio wateja-waanzisha-mitindo katika Japani, yasema ripoti iliyochapishwa katika The Daily Yomiuri. Mitindo huenea upesi kupitia uwasiliano na marika zao, ambao waweza kuzidi wajuani 1,000. Uvutano wao pia huenea kufikia marika wengine kupitia wazazi na ndugu zao. “Wasichana hao wamebarikiwa kwa sifa za wateja: pesa, udadisi kuhusu mapya na wakati wa kujiingiza katika hayo.” Karibu asilimia 68 ya matineja wa Japani hupata ruzuku ifikayo dola 220 kwa mwezi, na wengi pia hupokea pesa kutoka kwa wazakuu wanaowaendekeza na kutoka kwa kazi za muda. Wanasoshiolojia wanahangaika kuhusu genzai shiko ya wasichana hao, au mtazamo wa kuishi kwa ajili ya leo, na kuhusu ukosefu wao wa jumla wa miradi ya kibinafsi yenye maana zaidi. Uchunguzi wa karibuni waonyesha kwamba wasichana wa shule za upili wa leo “wanateseka kutokana na kuchoshwa na kupata chochote wanachotaka bila kukifanyia kazi kwa bidii.”

Mtu Mzee Zaidi Ulimwenguni Afa

Jeanne Louise Calment, mtu mzee zaidi ulimwenguni kulingana na Guinness Book of World Records, alikufa Agosti 4, 1997, akiwa na umri wa miaka 122, laripoti gazeti la habari la Ufaransa Le Figaro. Jeanne alizaliwa Februari 21, 1875, katika Arles, kusini-mashariki ya Ufaransa—kabla ya kuanzishwa kwa balbu ya taa, kinanda cha gramafoni, na gari. Aliolewa katika mwaka wa 1896, akazaa binti mmoja ambaye aliishi miaka 63 kuliko binti huyo, na akawa na mjukuu mmoja wa kiume aliyekufa katika mwaka wa 1963. Alikumbuka kukutana na mpaka-rangi Vincent van Gogh katika mwaka wa 1888, alipokuwa tineja, na alikuwa rafiki ya mshairi Frédéric Mistral, aliyeshinda tuzo la Nobeli katika mwaka wa 1904. Jeanne alitoa maoni mengi ya kuchekesha kuhusu siri za kuishi sana, akitaja mambo kama vile kicheko, utendaji, na “tumbo kama la mbuni.”

Watoto Wasemao Lugha Mbili

Kadiri mtoto ajifunzavyo lugha yake ya asili, mwingi wa uwezo wake wa kutekeleza usemi umewekwa thabiti katika sehemu ya ubongo ijulikanayo kuwa eneo la Broca. Majuzi watafiti katika Memorial Sloan-Kettering Cancer Center katika New York walitumia mfumo wa kutokeza mfano wa vitu kwa kutumia picha za eksirei kuhakikisha ni sehemu gani ya ubongo inayokuwa tendaji wakati watu wanaozungumza lugha mbili wanapotumia mojawapo ya hizo lugha. Waligundua kwamba wakati mtu anapojifunza lugha mbili wakati uleule akiwa mtoto mchanga, lugha zote mbili huwekwa katika sehemu moja katika eneo la Broca. Hata hivyo, mtu ajifunzapo lugha ya pili wakati wa ubalehe au baadaye, huonekana kuwa imewekwa kandokando ya ile ya kwanza, badala ya kuwa imechanganyika nayo. Gazeti la habari la London The Times laeleza: “Ni kana kwamba kujifunza lugha ya kwanza kumeweka mizunguko katika eneo la Broca, na kwa hiyo lugha ya pili lazima iwekwe mahali pengine.” Watafiti hao wahisi kwamba hili laweza kueleza sababu kwa nini ni vigumu zaidi kujifunza lugha ya pili katika maisha ya baadaye.

Hangaiko la Wachina Kuhusu Kulea Watoto

Uchunguzi mkubwa kuhusu uhusiano kati ya mzazi na mtoto ulifanywa majuzi chini ya uelekezi wa Chuo cha Sayansi-Jamii katika China, laripoti China Today. Uchunguzi huo ulitokeza hangaiko kwa upande wa wazazi wengi kuhusu kuwalea watoto wa siku hizi. Kulingana na China Today, “wengine huhisi kutokuwa na uhakika kabisa kuhusu kile ambacho watoto wao wapasa kufunzwa—maadili ya kitamaduni ya Kichina kama vile ufuatiaji wa haki, kiasi, uvumilivu wenye subira na kujali, au maadili ya jamii ya kisasa ya mashindano?” Karibu asilimia 60 ya wazazi walihofu kuhusu matokeo yasiyofaa ya televisheni kwa watoto. Mtafiti wa habari Bu Wei ashauri wazazi kudhibiti programu ambazo mtoto anatazama kulingana na umri na utu wake, kutazama na kuzungumzia programu pamoja na mtoto, na kutoruhusu televisheni kuchukua wakati mwingi mno wa mtoto.

Adui Mbaya Zaidi wa Papa?

Kwa kawaida papa huamsha hofu katika wanadamu. Lakini kwaelekea kuna sababu kubwa zaidi kwa papa kuhofu mwanadamu. “Wanadamu wanaopungua mia moja” hufa kila mwaka likiwa tokeo la mashambulizi ya papa, huku papa 100,000,000 wanakadiriwa kuwa huuawa kila mwaka na wavuvi, laripoti gazeti la habari la Ufaransa Le Monde. Jambo hili huwatia wasiwasi wanabiolojia wa majini, ambao huhofu kwamba usawaziko wa kiasili wa bahari waweza kuvurugwa ikiwa uharibifu huo waendelea. Papa huwa na sehemu kubwa katika kudhibiti idadi za wanyama wa baharini. Kwa kuwa papa ni wa polepole kufikia ukomavu wa kingono na hupata watoto wachache tu baada ya kuchukua mimba kwa muda mrefu, kuvua kupita kiasi kwahatarisha kumaliza spishi fulani za papa. Zoea moja ambalo wataalamu wa majini walaumu hasa ni “finning”—kukata mapezi kwa ajili ya chakula na kumtupa tena papa majini ili afe.

Kuwakusanya Kutoka Angani

Ndege ndogo zenye kwenda polepole ziitwazo ultralight sasa zinatumika na wafugaji fulani katika Australia ili kusaka vituo vyao vikubwa vya ng’ombe na kondoo, laripoti gazeti la habari la The Sunday Mail la Brisbane, Australia. Mfugaji mmoja kutoka Queensland asema kuwa ultralight yake ilimwokoa mshahara wa majuma mawili wa wanaume kadhaa kila wakati alipowakusanya kondoo zake. “Pikipiki ilichukua mahali pa farasi, na sasa ultralight inachukua mahali pa pikipiki,” yeye alisema. Ndege hizi nyepesi zimewekwa tepe zenye nguvu ambazo hutangaza mirekodio ya mbwa wakibweka. Wanaposikia sauti hizi, “ng’ombe na kondoo walioshtushwa huanza kukimbia na wanaelekea kwenye malisho yaliyo karibu,” jarida hilo lataja.

Wakanada Wenye Shughuli Nyingi

Wakanada wanafanya kazi kwa muda wa saa nyingi zaidi, na wengi wanateseka kutokana na athari za kufanya hivyo, lasema gazeti la habari The Globe and Mail. Hofu za kiuchumi zimewaweka wanaume na wanawake, kutia ndani wazazi wa watoto wachanga, chini ya mkazo wa kufanya kazi kwa bidii zaidi na kwa muda mrefu zaidi. Karibu Wakanada 2,000,000 hufanya wastani wa muda wa saa tisa za ziada kwa juma, na 700,000 wana kazi za ziada, wakifanya angalau kazi moja zaidi. Watafiti fulani wasema kuwa viwango vya hangaiko vimeongezeka sana hasa miongoni mwa wale wanaofanya kazi za ofisini. Wataalamu wanahangaikia matokeo ya mwendo huu kwa watoto, ambao hawawaoni wazazi wao sana. Dakt. Kerry Daly wa idara ya uchunguzi wa familia katika Chuo Kikuu cha Guelph, Ontario, aonelea: “Watu wanahisi kuwa hawawezi kuyasimamia maisha yao. Hawana uhakika wa jinsi ya kutoka katika mtindo-maisha huu wenye shughuli nyingi.”

Mkazo wa Kukosa Kazi ya Kuajiriwa

Mikazo ya kihisia-moyo na ya kijamii ya kukosa kazi ya kuajiriwa yaweza kuathiri afya ya mtu, kulingana na uchunguzi uliotajwa katika gazeti la habari la Ujerumani Süddeutsche Zeitung. Inasemekana kuwa mfumo wa kinga wa mwili hudhoofishwa na mkazo wa jinsi hiyo. Watu wasio na kazi ya kuajiriwa pia wana uwezekano wa kupatwa na msongo mkubwa wa damu na mishiko ya moyo kuliko wale ambao wana kazi ya kuajiriwa. “Mkazo ambao mtu asiyekuwa na kazi ya kuajiriwa alazimika kukabiliana nao ni mbaya sana na matokeo yaliyojaa wasiwasi kuliko ya wale walio na kazi ya kuajiriwa,” ataarifu Profesa Thomas Kieselbach wa Chuo Kikuu cha Hannover, Ujerumani. “Karibu wote wa wale wasio na kazi za kuajiriwa huteseka kwa namna moja au nyingine ya matatizo ya kushuka moyo.” Idadi ya wasio na kazi za kuajiriwa katika Muungamano wa Ulaya yasemekana kuwa karibu yatoshana na idadi za watu wa Denmark, Finland, na Sweden zikijumlishwa pamoja.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki