Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 3/8 kur. 2-5
  • Pigo la Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Pigo la Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuendelea kwa Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa
  • Gharama Kubwa ya Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa
  • ‘Wafungwa wa Mfumo Mpotovu’
  • Matabiri na Mitamauko
  • Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa?—Kwa Nini Upo?
    Amkeni!—1996
  • Uhuru Kutokana na Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa—Jinsi Gani na Lini?
    Amkeni!—1996
  • “Kazi ya Kudumu” Imepatwa na Nini?
    Amkeni!—2000
  • “Tunakuachisha Kazi”
    Amkeni!—2010
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 3/8 kur. 2-5

Pigo la Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA

Huo ni tatizo kubwa katika nchi kadhaa zilizositawi—lakini pia huhangaisha mataifa yanayositawi. Huo umekumba mahali ambapo wakati mmoja ulionekana kama haukuwapo. Huathiri mamia ya mamilioni ya watu—wengi wao ambao ni akina mama na baba. Kwa thuluthi mbili ya Waitalia, huo ni “tisho kubwa zaidi.” Hutokeza matatizo mapya ya kijamii. Kwa kiwango fulani, ndio msingi wa matatizo ya vijana wengi ambao wanajiingiza katika dawa za kulevya. Husumbua usingizi wa mamilioni, na kwa mamilioni mengine, huo unawaotea . . .

“YAELEKEA ukosefu wa kazi ya kuajiriwa ndio tukio la wakati wetu linalohofiwa na watu wengi mno,” lasisitiza Shirika la Ushirikiano na Usitawi wa Kiuchumi (OECD). “Mweneo na matokeo ya tukio hili yajulikana,” yaandika Tume ya Jumuiya ya Ulaya, lakini “ni vigumu kushughulika nalo.” Hilo ni “mzuka,” asema mtaalamu mmoja, ambao “unarudi kutokea-tokea kwenye barabara za Ulaya.” Katika Muungano wa Ulaya (EU), wasioajiriwa sasa wafikia idadi ya karibu milioni 20, na katika Oktoba 1994, katika Italia pekee walifikia kirasmi idadi ya 2,726,000. Kulingana na maoni ya Padraig Flynn, kamishna wa Muungano wa Ulaya, “kupambana na ukosefu wa kazi ya kuajiriwa ndilo tatizo kuu zaidi la kijamii na kiuchumi tunalokabili.” Ikiwa hujaajiriwa au umo hatarini mwa kupoteza kazi yako, unajua hofu inayosababishwa na jambo hilo.

Lakini ukosefu wa kazi ya kuajiriwa si tatizo la Ulaya tu. Huo hupata nchi zote za Amerika. Huo hauachi kando Afrika, Asia, au visiwa. Mataifa ya mashariki mwa Ulaya yamelazimika kukabili tatizo hilo katika miaka ya majuzi. Ni kweli, haupigi kwa kadiri ile ile kila mahali. Lakini kulingana na wataalamu fulani wa uchumi, viwango vya ukosefu wa kazi ya kuajiriwa katika Ulaya na Amerika Kaskazini vitabaki kwa muda mrefu vikiwa juu zaidi kuliko miongo iliyotangulia.a Na hiyo hali “inafanywa kuwa mbaya zaidi na ongezeko la kutoajiriwa kufanya kazi kwa wakati wote na kuzorota kwa ujumla kwa ubora wa kazi zinazopatikana,” ataja mtaalamu wa uchumi Renato Brunetta.

Kuendelea kwa Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa

Ukosefu wa kazi ya kuajiriwa umeathiri sekta zote za uchumi moja baada ya nyingine: kwanza sekta ya kilimo, ikiwa na utumiaji wayo ulioongezeka wa mashine, ambao unaondoa watu kazini; kisha sekta ya viwanda, ambayo imeathiriwa na tatizo la nishati tangu 1970 na kuendelea; na sasa, sekta ya huduma—biashara, elimu—sekta ambayo mbeleni ilionwa kuwa isiyoweza kushambuliwa. Miaka 20 iliyopita kiwango cha ukosefu wa kazi ya kuajiriwa cha kupita asilimia 2 au 3 kingesababisha wasiwasi mwingi. Leo taifa lenye viwanda vingi hujiona kuwa na mafanikio ikiwa ukosefu wa kazi ya kuajiriwa unadumishwa chini ya asilimia 5 au 6, na mataifa mengi yaliyositawi yana viwango vya juu zaidi.

Kulingana na Shirika la Kimataifa la Wafanyikazi (ILO), mtu asiyeajiriwa ni yule ambaye hana kazi, yuko tayari kufanya kazi, na anatafuta kazi kwa bidii. Lakini namna gani mtu ambaye hana kazi ya kudumu ya muda wote au yule ambaye huweza kufanya kazi muda wa saa chache tu kwa juma? Kazi isiyo ya muda wote huonwa kwa njia tofauti kutoka nchi moja hadi nyingine. Katika mataifa fulani wale ambao kwa uhalisi ni wasioajiriwa wanahesabiwa kirasmi kama walioajiriwa. Hali zisizofafanuliwa vizuri kati ya kuajiriwa na kutoajiriwa hufanya iwe vigumu kupambanua ni nani hasa asiyeajiriwa, na kwa sababu hii takwimu hufafanua sehemu tu ya uhalisi. “Hata idadi rasmi ya wasioajiriwa 35 milioni [katika nchi za OECD] haionyeshi mweneo kamili wa ukosefu wa kazi,” yasema ripoti moja iliyochapishwa ya uchunguzi ya Ulaya.

Gharama Kubwa ya Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa

Lakini hizo idadi hazielezi hali yote. “Gharama za kiuchumi na za kijamii za ukosefu wa kazi ya kuajiriwa ni kubwa mno,” yasema Tume ya Jumuiya za Ulaya, nazo hutokea “si tu katika gharama ya moja kwa moja za malipo ya misaada ya kifedha kwa wasioajiriwa bali pia kutokana na hasara ya ushuru ambao wasioajiriwa wangelipa ikiwa wangekuwa wameajiriwa.” Na misaada ya kifedha kwa wasioajiriwa inaendelea kuwa mzigo si kwa serikali bali tu pia kwa walioajiriwa, wanaotozwa kodi zilizoongezeka.

Ukosefu wa kazi ya kuajiriwa si tu jambo la mambo ya hakika na tarakimu. Matokeo ni hali za kibinafsi zenye kusumbua, kwa kuwa pigo hilo hupata watu—wanaume, wanawake, na vijana wa kila tabaka la kijamii. Ukiunganishwa na matatizo mengine yote ya hizi “siku za mwisho,” ukosefu wa kazi ya kuajiriwa waweza kuwa mzigo mkubwa mno. (2 Timotheo 3:1-5; Ufunuo 6:5, 6) Hasa akipatwa na “ukosefu wa kazi ya kuajiriwa kwa muda mrefu,” bila mambo mengine kuathiri hiyo hali, mtu ambaye hajakuwa na kazi kwa muda mrefu ataona ikiwa vigumu hata zaidi kupata kazi. Kwa kuhuzunisha, huenda wengine hata wasipate kuajiriwa tena kamwe.b

Wanasaikolojia wanapata kwamba miongoni mwa wasioajiriwa leo, matatizo ya kiakili na kisaikolojia yanaongezeka, na vilevile ukosefu wa uthabiti kihisia-moyo, kukata tamaa, kutojali kwenye kuendelea, na kuacha kujistahi. Mtu mwenye watoto wa kutunza anapopoteza kazi, ni msiba wa kibinafsi mbaya sana. Ulimwengu umewaporomokea. Usalama umetoweka. Leo, hata wataalamu fulani huona kuzuka kwa “hangaiko la kutarajia” linalohusiana na uwezekano wa kupoteza kazi. Hangaiko hilo laweza kuathiri vibaya sana mahusiano ya familia na laweza hata kuwa na matokeo mabaya mno, kama ujiuaji-kimakusudi wa hivi majuzi wa watu wasioajiriwa unavyoonyesha. Isitoshe, ugumu wa kupata kazi kwa mara ya kwanza umo miongoni mwa mambo yawezayo kusababisha jeuri na kujitenga kijamii kwa vijana.

‘Wafungwa wa Mfumo Mpotovu’

Amkeni! limehoji watu kadhaa ambao wamepoteza kazi zao. Armando mwenye umri wa miaka 50 alisema kwamba kwake ilimaanisha “kuona jitihada za kazi ya miaka 30 zikiharibiwa, akilazimika kuanza upya,” akihisi “kama mfungwa wa mfumo mpotovu.” Francesco ‘aliona ulimwengu ukiporomoka juu yake.’ Stefano “aliudhika sana na mfumo wa sasa wa maisha.”

Kwa upande ule mwingine, Luciano, aliyefutwa kazi baada ya kufanya katika usimamizi wa kiufundi katika kiwanda kimoja cha magari cha Italia kwa karibu miaka 30, “alipatwa na hasira na fadhaiko alipoona kwamba jitihada zake, mwenendo wake wa kufuatia adili nzuri na hali ya kutumainiwa wakati wa miaka mingi sana ya kazi yalionwa kuwa bure.”

Matabiri na Mitamauko

Wataalamu fulani wa uchumi walikuwa wametazamia mandhari tofauti sana. Katika 1930 mtaalamu wa uchumi John Maynard Keynes kwa kutazamia mazuri alitabiri “kazi kwa kila mtu” katika kipindi cha miaka 50, na kwa miongo mingi kuajiriwa kikamili kumeonwa kuwa mradi uwezao kufikiwa. Katika 1945 Mkataba wa Umoja wa Mataifa ulikuwa na lengo la mfikio wa haraka wa uajiri kamili. Hadi hivi majuzi sana iliaminika kwamba maendeleo yangemaanisha kazi na muda wa saa chache kazini kwa wote. Lakini mambo hayajakuwa hivyo. Upungufu mkubwa wa kiuchumi wa mwongo uliopita umesababisha “tatizo baya zaidi la duniani kote la kazi ya kuajiriwa tangu ule Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi wa miaka ya 1930,” lasema ILO. Katika Afrika Kusini angalau watu milioni 3.6 hawana kazi, kutia ndani Waafrika weusi wapatao milioni 3. Hata Japani—ikiwa na watu zaidi ya milioni mbili ambao hawakuwa na kazi mwaka jana—inapitia tatizo hilo.

Kwa nini ukosefu wa kazi ya kuajiriwa ni pigo lililoenea sana hivyo? Kuna masuluhisho gani ambayo yametolewa ili kuushughulikia?

[Maelezo ya Chini]

a Kiwango cha ukosefu wa kazi ya kuajiriwa ni asilimia ya jumla ya wafanyikazi ambao hawajaajiriwa.

b Wale “wasioajiriwa kwa muda mrefu” ni wale ambao wamekuwa bila kazi kwa zaidi ya miezi 12. Katika Muungano wa Ulaya karibu nusu ya wasioajiriwa wamo katika kikundi hiki.

[Picha katika kurasa za 2 and 3]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kanada—Asilimia 9.6

Marekani—Asilimia 5.7

Kolombia—Asilimia 9

Ireland—Asilimia 15.9

Hispania—Asilimia 23.9

Finland—Asilimia 18.9

Albania—Asilimia 32.5

Afrika Kusini—Asilimia 43

Japani—Asilimia 3.2

Filipino—Asilimia 9.8

Australia—Asilimia 8.9

[Hisani]

Mountain High Maps™ copyright © 1993 Digital Wisdom, Inc.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki