Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa?—Kwa Nini Upo?
KATIKA nchi kadhaa watu wengi wanalazimika kujiruzuku kwa kufanya kazi ngumu ya kimwili ya muda wa saa nyingi mno kwa mwendo wenye kuchosha, labda hata wakifanya kazi hatari kwa malipo kidogo. Hadi hivi majuzi wengi katika nchi nyinginezo walikuwa na uhakika kwamba baada ya kuajiriwa na kampuni kubwa au na idara ya serikali, wangekuwa na kazi iliyo salama hadi wakati wa kustaafu. Lakini leo hakuonekani tena kuwa na makampuni au mashirika ambayo yanaweza kutoa kazi ya kuajiriwa inayotamanika na usalama katika cheo chochote kile. Kwa nini?
Sababu za Hilo Tatizo
Maelfu ya vijana hawawezi hata kupata kazi yao ya kwanza—iwe wana digrii ya chuo au hawana. Kwa kielelezo, katika Italia zaidi ya thuluthi ya wasioajiriwa ni watu wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24. Umri wa wastani wa wale ambao tayari wanafanya kazi na kujaribu kudumisha kazi zao unaongezeka, na kwa hiyo ni vigumu zaidi kwa vijana kuingia kazini. Hata miongoni mwa wanawake—ambao wanaongezeka sana katika kazi ya kuajiriwa—kuna kiwango cha juu cha ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. Hivyo, idadi isiyo ya kawaida ya wafanyikazi wapya inajikakamua kupata kazi ya kuajiriwa.
Tangu wakati wa mashine za kwanza za viwanda, uvumbuzi wa kiufundi umepunguza uhitaji wa wafanyikazi. Kwa kuwa ilikuwa lazima watu wengi wafanye kazi ngumu ya kupokezana zamu, wafanyakazi walitumaini kwamba mashine zingepunguza kazi au hata kuimaliza. Mashine zimeongeza utokezaji na kuondosha hatari nyingi, lakini pia zimepunguza kazi. Wale wanaofutwa kazi wamo hatarini mwa ukosefu wa muda mrefu wa kazi ya kuajiriwa isipokuwa wajifunze stadi mpya.
Wengine wahisi kwamba tayari tumefikia vilele vya ukuzi. Kwa kuongezea, kukiwa na walioajiriwa wachache, kuna wanunuzi wachache. Hivyo ulimwengu wa biashara hutokeza bidhaa nyingi kuliko ziwezavyo kutumiwa. Majengo yaliyojengwa ili kushughulikia maongezeko katika utokezaji ambayo hayafai tena kiuchumi yanafungwa au kubadilishwa ili kufaa kazi nyingine. Mielekeo kama hii inavuna majeruhi—wale ambao wanapoteza kazi ya kuajiriwa. Katika upungufu wa kiuchumi, uhitaji wa wafanyikazi hupungua, na kazi zilizopotezwa wakati wa upungufu wa kiuchumi hazifanyizwi tena wakati wa ukuzi wa kibiashara. Kwa wazi, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa una zaidi ya kisababishi kimoja.
Pigo la Kijamii
Kwa kuwa unaweza kupata mtu yeyote, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa ni pigo la kijamii. Nchi fulani huandaa njia za kulinda wale ambao bado wanafanya kazi—kwa kielelezo, kufanya kazi saa chache kwa juma kwa malipo yaliyopunguzwa. Hata hivyo, hili laweza kuharibu mataraja ya wengine wanaotafuta kazi.
Wote walioajiriwa na wasioajiriwa hupinga zaidi na zaidi kuhusu matatizo yanayohusiana na kazi. Lakini ingawa wasioajiriwa hudai wapewe kazi, wale walio na kazi hujaribu kutunza usalama wao wenyewe—makusudi mawili ambayo sikuzote hayapatani. “Wale walio na kazi mara nyingi huombwa kufanya kazi kwa saa za ziada. Wale wasio na kazi hubaki bila kazi. Kuna hatari kwamba jamii yaweza kugawanyika mara mbili . . . kwa upande mmoja, wale wenye kufanya kazi kwa saa za ziada na kwa upande ule mwingine, wale wasioajiriwa waliokataliwa, ambao yaelekea wanategemea kabisa hisani ya wale wengine,” lasema gazeti la Italia Panorama. Wataalamu wasema kwamba katika Ulaya, matokeo ya ustawi wa kiuchumi yamefurahiwa kwa sehemu kubwa na wale wanaofanya kazi tayari, badala ya wale wasio na kazi.
Na zaidi, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa unahusianishwa na hali ya uchumi ya mahali, hivi kwamba katika mataifa fulani, kama vile Ujerumani, Italia, na Hispania, tofauti kubwa zipo kati ya mahitaji ya eneo moja na yale ya eneo jingine. Je, wafanyikazi wako tayari kujifunza stadi mpya au hata kuhamia eneo jingine au nchi nyingine? Kutafuta kazi ya kuajiriwa kwaweza kuwa jambo litakaloamua.
Je, Kuna Masuluhisho Yoyote Karibuni?
Kwa sehemu kubwa, matumaini yanawekwa kwenye kuboreka kwa hali ya uchumi. Lakini watu fulani wana shaka na kufikiri kwamba kuboreka huko hakutatukia hadi karibu na mwaka 2000. Kwa maoni ya wengine, kurudi kwa uchumi katika hali nzuri tayari kumeanza, lakini kuna matokeo ya polepole, kama ilivyo wazi kutokana na kupungua kwa hivi majuzi kwa kazi ya kuajiriwa katika Italia. Kurudia hali njema kiuchumi si lazima kumaanishe kupungua kwa ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. Wakati ukuzi ni wa kiasi, makampuni hupendelea kutumia wafanyikazi bora zaidi yaliyo nao tayari badala ya kuajiri watu wengine—yaani, kuna “ukuzi wa kiuchumi bila fursa za kupata kazi.” Zaidi, idadi ya wasioajiriwa mara nyingi huongezeka haraka kuliko idadi ya kazi mpya zinazofanyizwa.
Leo uchumi wa kitaifa unaenezwa duniani kote. Wataalamu fulani wa uchumi wanafikiri kwamba kufanyizwa kwa maeneo mapya makubwa ya mataifa mengi, kama yale ya Mkataba wa Biashara Huru wa Amerika Kaskazini (NAFTA) na Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia-Pasifiki (APEC), huenda pia ukatoa kichocheo kwa uchumi wa ulimwengu. Hata hivyo, mwelekeo huu huchochea mashirika makubwa yajistawishe mahali ambapo wafanyikazi hawalipwi mishahara mikubwa, kukiwa na matokeo kwamba mataifa yaliyo na viwanda vingi hupoteza kazi. Kwa wakati huohuo, wafanyikazi ambao hawachumi fedha nyingi huona mishahara yao midogo ikiendelea kupungua. Haishangazi kwamba katika nchi kadhaa, wengi wameandamana, hata kwa fujo, dhidi ya mikataba hii ya biashara.
Wataalamu wanadokeza njia nyingi za kupambana na ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. Njia nyingine hata zinapingana, ikitegemea kama zinadokezwa na wataalamu wa uchumi, wanasiasa, au wafanyikazi wenyewe. Kuna wale wanaodokeza kutolea makampuni vichochezi vya kuongeza wafanyikazi kwa kupunguza mzigo wa kodi. Wengine hushauri mwingilio mkubwa wa serikali. Wengine wanadokeza kugawanya kazi kwa njia tofauti na kupunguza muda wa kufanya kazi. Hili tayari limefanywa katika makampuni makubwa, hata ingawa katika karne iliyopita, muda wa saa za kazi kwa juma umepunguzwa mno katika mataifa yote yaliyositawi kiviwanda lakini hili halijapunguza ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. “Hatimaye,” asisitiza mtaalamu wa uchumi Renato Brunetta, “kila sera yakosa kufanikiwa, kukiwa na gharama zinazopita manufaa.”
“Hatupaswi kujidanganya,” lamalizia gazeti L’Espresso, “hilo tatizo ni gumu.” Je, ni gumu mno lisiweze kutatuliwa? Je, kuna suluhisho kwa tatizo la ukosefu wa kazi ya kuajiriwa?
[Sanduku katika ukurasa wa8]
Tatizo la Kale
Ukosefu wa kazi ya kuajiriwa ni tatizo la kale. Kwa karne nyingi mara kwa mara watu bila ya kupenda kwao wamejipata wakiwa bila kazi. Mara kazi ilipomalizika, makumi ya maelfu ya wafanyikazi waliotumika katika miradi mikubwa ya ujenzi wakawa wasioajiriwa wenyewe—angalau hadi walipoajiriwa mahali penginepo. Kwa wakati huo bila kusema sana, waliishi maisha yasiyo salama.
Wakati wa Enzi za Kati, “hata ingawa tatizo la ukosefu wa kazi ya kuajiriwa katika maana ya kisasa halikuwapo,” wasioajiriwa walikuwapo. (La disoccupazione nella storia [Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa Katika Historia] Hata hivyo, katika siku hizo, wowote ambao hawakuwa na kazi walionwa hasa kuwa, wasiofaa kitu au wazururaji. Mwishoni-mwishoni kufikia karne ya 19, wachanganuzi wengi Waingereza “walihusianisha wasioajiriwa hasa na watu wenye ghasia na watu wasio na makao ambao walilala nje au kutembea barabarani usiku,” aeleza Profesa John Burnett.—Idle Hands.
“Ugunduzi kwamba ukosefu wa kazi ya kuajiriwa ni tatizo” ulitokea karibu na mwisho wa karne ya 19 au mwanzoni mwa karne ya 20. Tume za kipekee za serikali zilianzishwa ili kuchunguza na kutatua hilo tatizo, kama vile Halmashauri Teule ya Bunge la Watu wa Kawaida la Uingereza kuhusu “Taabu Kutokana na Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa,” katika 1895. Ukosefu wa kazi ulikuwa umekuwa pigo la kijamii.
Utambuzi huu mpya ulikua kwa kutazamisha, hasa baada ya vita ya ulimwengu ya kwanza. Vita hiyo, ikiwa na utokezaji wayo usio na mpango wa silaha, kihalisi ilikuwa imemaliza ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. Lakini kuanzia miaka ya 1920 ulimwengu wa Magharibi ulikabili mfululizo wa upungufu wa kiuchumi ukifikia upeo kwenye Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi ambao ulianza katika 1929 na kukumba uchumi wote wa kiviwanda ulimwenguni. Baada ya vita ya ulimwengu ya pili, nchi nyingi zilipata ukuzi wa kiuchumi, na ukosefu wa kazi ya kuajiriwa ukashuka. Lakini “mianzo ya tatizo la ukosefu wa kazi ya kuajiriwa leo yaweza kufuatiwa nyuma hadi katikati ya miaka ya 1960,” lasema Shirika la Ushirikiano na Ukuzi wa Kiuchumi. Kazi ya kuajiriwa ilipatwa na pigo jipya lililosababishwa na matatizo ya mafuta ya 1970 na utumizi ulioenea wa kompyuta ukitokeza kufuta watu kazi. Ukosefu wa kazi ya kuajiriwa umeanza mpando wenye azimio, ukipenya hata katika zile sekta za wanaofanya kazi za ofisi na za usimamizi zilizofikiriwa wakati mmoja kuwa salama.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kudai kazi zaidi hakutasuluhisha tatizo la ukosefu wa kazi ya kuajiriwa
[Hisani]
Reuters/Bettmann