Kufutwa Kazi— Hofu ya Mwajiriwa
“Kulinilemea sana sana. Nilishtuka sana.”—Meneja wa mawasiliano, umri wa miaka 44
“Ni pigo baya sana kwa hali ya kujitumainia. Unajihisi kuwa bure kabisa.”—Msimamizi wa mambo ya kifedha, umri wa miaka 38
“Ni aina gani ya uchumi tumetokeza ambao huachisha watu kazi wakiwa katika upeo wao?”—Msimamizi wa kiwanda cha mavazi umri wa miaka 47.
WATU hao walishiriki maono gani? Kila mmoja wao alipatwa na ono lenye kuumiza sana kihisia-moyo la kufutwa kazi.
Angalia tena umri wa wafanya kazi hao. Hawakuwa watu wapya kazini, hivyo walihisi kwamba walikuwa na usalama mkubwa wa kikazi. Na walikuwa katika kile ambacho wengi wangefikiria kuwa kilele cha miaka ya chumo lao. Lakini mwisho wa kuajiriwa kwao ulikuja upesi na bila kutazamiwa. “Waliniambia niondoe kila kitu juu ya dawati yangu na kufunga mizigo yangu,” akasema meneja wa mawasiliano aliyetajwa juu. “Nikawa nimeenda, hivyo tu. Kwisha.”
Kulitukia Nini?
Shida za kiuchumi si jambo jipya. Katika nchi nyingi, sikuzote kumekuwa vipindi vya usitawi wa kadiri vikifuatwa na kupungua kwa utendaji wa kiuchumi. Na mshuko wa uchumi wa hivi karibuni katika ulimwengu wote, hata kabla ya vita katika Ghuba ya Uajemi, ulionyesha jinsi uchumi ungeweza kuvunjika hata baada ya miaka mingi ya usitawi. Watu wengi, baadhi yao kwa mara ya kwanza, walitambua kwamba haiwapasi kudhania tu kwamba kazi zao na mapato yao ni salama sikuzote.
Athari za kupungua kwa uchumi juu ya wafanya kazi zilikuwa kubwa sana. Makampuni yalilazimishwa kupunguza sana matumizi yao, mara nyingi ikitokeza kuachishwa kazi watu wengi sana. Katika mataifa yenye utajiri kiviwanda yaliyo washiriki wa Economic Cooperation and Development (Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Usitawi), jumla ya watu milioni 25 walikuwa hawana kazi wakati mmoja.
“Karibu kila siku napokea simu kutoka kwa marafiki ambao wameachishwa kazi katika makampuni makubwa,” akasema mpambaji wa ndani ya nyumba. “Makampuni mengi ninayofanya kazi nayo, yameshuka kufikia nusu ya biashara waliyokuwa nayo mwaka mmoja uliopita.”
Kufutwa kazi sikuzote kumekuwa sehemu ya maisha ya wafanyakazi wa viwandani. Katika mshuko wa hivi karibuni, hesabu yenye kuongezeka ya wafanyakazi wa ofisini pia walipoteza kazi zao. “Hizi ndizo kazi zenye kuwakilisha uchumi,” akasema Dan Lacey, mhariri wa gazeti la Workplace Trends, “kazi zilizotupatia uwezo wa kununua nyumba katika ujirani mwema na kuwa na magari mawili.”
Nyingi za kazi hizo zilipotezwa katika miaka michache iliyopita. Na wafanyakazi waliofutwa kazi “wamelemewa sana na daraka la kulipa rehani za nyumba, familia zilizo changa, madeni makubwa, na kukosa uhakika juu ya wakati ujao.”
Ni Nini Zilizo Athari?
Kuna aina mbili za pigo kwa hayo: Wafanya kazi waliofutwa wanapata pigo la kiuchumi na kihisia moyo. Mkazo wa kiuchumi ni wazi. Akiwa na mapato machache, ni lazima mmoja ajirekebishe kulingana na hali yake ya maisha. Na kutoajiriwa kuna athari ya kihisia-moyo pia.
Kwa mfano, maoni ya vijana kuelekea usalama wa kazi yanabadilika. Kutokea huku na huko kwa kuajiriwa kunakuwa maisha ya kawaida, aina ya maisha yenye kukubaliwa. Gazeti The Wall Street Journal liliandika kwamba mara kufutwa mara kuajiriwa kumegeuza wengi wa vijana wa Uingereza kuwa “wabalehe wa kudumu.”
Kuna matatizo mengi ya hisia-moyo za ndani kwa wale wenye kufutwa baada ya miaka ya kuajiriwa imara. “Wakati kuna kufutwa,” akasema mwanasaikolojia Neil P. Lewis, “si kupoteza tu mshahara, bali ni kama kujipoteza mwenyewe.”
Kwa kweli, wanasaikolojia wametambua kwamba uchungu wa kufutwa kazi ni sawa na uchungu ulio kama wa kufiwa na mpenzi au wa talaka. Shtuko la kwanza huleta hasira, ambayo huongoza kwenye huzuni halafu kukubali hali. “Watu wengine huchukua muda wa siku mbili tu kuhuzunika,” akasema Lewis. “Wengine huchukua majuma na miezi.”
Pigo la kihisia-moyo linaonekana pia kwa njia ya kwamba wale wenye kufutwa huwa wanazoea kileo na dawa za kulevya. Mvunjiko wa moyo pia waweza kuongoza kwenye jeuri na mvunjiko wa familia. “Hisia hizo zapaswa kwenda mahali pengine,” akasema Stephen Pilster-Pearson, mkurugenzi wa usaidizi wa waajiriwa katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, U.S.A., “na mmojapo ya mahali hapo, bila shaka, ni nyumbani.”
Katika hali mbaya sana, mhitimu mmoja wa chuo kikuu katika Hong Kong alichagua kujiua baada ya miaka mitano ya kutoajiriwa. Alisimama katika reli ya gari moshi iliyokuwa ikija.
Kwa hivyo wakati kazi zinapotezwa, si mkoba wa pesa peke yake unaopata athari. Hivyo, ni lazima kuona zaidi ya tatizo la kiuchumi. Hisia zenye uchungu sana zatiwa ndani, na familia lazima zijitahidi pamoja na kufanyia kazi suluhisho kwa umoja.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Je! Ni Mwisho wa Mpanuko wa Uchumi?
Katika mwaka uliopita, woga wa ghasia za kiuchumi umeripotiwa ulimwenguni pote. Fikiria mifano kadha:
Ufaransa: “Ulimwengu unafikia mwisho wa kipindi kirefu cha mpanuko wa uchumi ambao haujapata kujua. . . . Ikiwa nchi za Ulaya hazina mengi ya kuogopa katika muda mfupi, ni kwa ajili ya muungano wa Ujerumani, hawawezi kutazamia kuepuka kabisa kabisa. . . . Soko zimeona kuja kwa hatari.”—Le Monde, Paris.
Brazili: Kushuka kwa hali ya kiuchumi katika United States kungekuwa na “kuathiri kusikoepukika na kuhisiwa na nchi nyingine zenye viwanda na, hatimaye, kungetokeza vizuizi vikubwa kwa ukuzi wa kuuza bidhaa nje kutoka kwa nchi ambazo hazijasitawi sana.”—Fôlha de S. Paulo, São Paulo.
Uingereza: “Uchumi wa Uingereza, pamoja na infuleshoni yake kubwa sana, viwango vya juu vya faida, na ukuzi wa polepole, pia hauleti tumaini lolote.”—Financial Times, London.
Kanada: “Waajiri wachache zaidi wanatafuta wafanyakazi wachache zaidi.”—The Toronto Star.
Ujerumani:“Mlingano wa bei ya mafuta ya 1973 iliyoshtua tayari unaonekana. . . . Kama vile ishara [za] kushuka kwa hali ya kiuchumi.”—Neues Deutschland, Berlin.
Japan: “Thamani za ardhi sasa ni kama kombora lililo kwenye uchumi wa ulimwengu. Ikiwa kombora lingeruhusiwa kulipua bei za ardhi zishuke, benki za Japan zingekuwa hazina thamani. Hili, nalo pia, lingetokeza kushuka kwa hali ya kiuchumi ulimwenguni pote.”—Australian Financial Review, Sydney.
Hata hivyo, mwisho wa vita ya Ghuba mapema katika 1991 ulileta matumaini mapya ya utendaji wa kiuchumi katika ulimwengu wote. Bado, kuna ushuhuda kwamba uchumi wa kitaifa kwa kweli ni wa muda mfupi, hasa ikifikiriwa kuhusu mzigo wa deni ambao umetwika nchi nyingi.