Uhuru Kutokana na Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa—Jinsi Gani na Lini?
SAWA na Muumba wake, mwanadamu anaweza kupata shangwe katika kazi, ambayo hufafanuliwa ifaavyo kuwa “zawadi ya Mungu.” (Mhubiri 3:12, 13, New World Translation; Yohana 5:17) Kazi yenye kupendeza yaweza kutupa furaha na kutufanya tujihisi kuwa wenye mafaa na wanaohitajiwa. Hakuna yeyote atakaye kupoteza kazi, hata kama huenda haifurahii sana. Licha ya kutoa uhakikisho wa mshahara, kazi ya kuajiriwa ya kulipwa hutoa muundo, kusudi, na hisi ya utambulisho kwa maisha ya mtu. Haishangazi kwamba kwa kawaida “wasioajiriwa hutaka kazi zaidi ya kitu kinginecho chote.”
Kutafuta Kazi
Kama ambavyo tumekwisha kuona, hali katika kazi ya kuajiriwa ni tata sana. Likiwa tokeo, kuna njia nyingi zifaazo za kutafuta kazi. Wowote ambao wanastahili kupata misaada ya kifedha ya serikali kwa wasio na kazi ya kuajiriwa wanaweza kuitumia mahali inapopatikana; na mahali inapohusu, wanaweza kujiandikisha katika ofisi za wasio na kazi ya kuajiriwa na kutumia huduma zinazotolewa. Wengine hupata kazi kwa kujiajiri. Lakini mtu apaswa kutahadhari. Mara nyingi waliojiajiri wamelazimika kulipa gharama za juu sana za mwanzoni ambazo huenda zisiwe rahisi kurudisha. Ni muhimu pia kujua na kustahi sheria za ushuru na kodi—ambazo ni ngumu sana kutimiza katika nchi fulani!—Warumi 13:1-7; Waefeso 4:28.
Ili kupata kazi, wengine wamepata ugumu wa kutafuta kazi, wakijitoa kuitafuta kwa utaratibu na uvumilivu. Wengine wameandikia makampuni yanayotafuta wafanyakazi au wameweka matangazo katika magazeti ya habari ya kwao—baadhi yayo ambayo huchapisha matangazo ya kuomba kazi bila malipo. Mara nyingi Amkeni! limetoa shauri lenye mafaa na lenye kutumika juu ya habari hiyo—kwa vijana na watu wazima pia.a—Ona visanduku, ukurasa 11.
Ni lazima uwe mwenye kubadilikana—tayari kufanya aina zote za kazi, kutia ndani kazi ambazo huzipendi. Wataalamu husema kwamba miongoni mwa mambo ya kwanza yanayoulizwa kwenye mahoji ya kazi ni uzoefu wa kazi wa wakati uliopita na urefu wa wakati ulipokuwa nje ya kazi. Muda mrefu bila kazi si ishara nzuri kwa aelekeaye kuwa mwajiri.
Mtu aliyetumia kwa hekima wakati wake shuleni akipata stadi ana nafasi nzuri ya kupata kazi yake ya kwanza. “Ukosefu wa kazi ya kuajiriwa,” asema Alberto Majocchi, mwalimu wa masomo ya kifedha, “huathiri hasa wafanyikazi wasio na stadi zozote.”
Umaana wa Utegemezo wa Kihisia-Moyo
Jambo moja la maana ni mtazamo chanya. Huo waweza kufanyiza tofauti kati ya kupata kazi na kutopata. Wasioajiriwa huthamini sana utegemezo wa kihisia-moyo, ambao huwasaidia kuepuka kujitenga au kuingia katika hali ya kutojali. Huo pia hutumika kushinda upotezo wa kujistahi ambao unaweza kutokana na kujilinganisha na wengine ambao hawajapoteza kazi zao.
Kuweza kuishi kwa fedha chache huenda kusiwe rahisi. “Jinsi nilivyokuwa na wasiwasi, niliona ikiwa vigumu kutumia vizuri wakati niliokuwa nao,” asema Stefano. “Hiyo hali ilinifanya niwe na mkazo sana,” akumbuka Francesco, “hivi kwamba nilianza kutafuta makosa katika baadhi ya rafiki zangu wapendwa.” Hapa ndipo utegemezo wa familia unakuwa wa maana. Ukosefu wa mapato wahitaji kubadilikana kwa washiriki wote wa familia ili kupunguza kiwango cha maisha. Franco, aliyefutwa kazi akiwa na umri wa miaka 43 baada ya kufanya kazi kwa kampuni hiyohiyo kwa miaka 23, asema hivi: “Tangu wakati nilipofutwa kazi, mke wangu alikuwa na mwelekeo chanya na alikuwa chanzo cha kitia-moyo kingi.” Armando anamshukuru hasa mke wake kwa ajili ya “busara yake katika ununuzi wa vitu.”—Mithali 31:10-31; Mathayo 6:19-22; Yohana 6:12; 1 Timotheo 6:8-10.
Kanuni za Biblia zaweza kutusaidia kudumisha hali ya moyoni iliyo chanya na kutosahau mambo ya maana zaidi. Wale waliohojiwa na Amkeni!, waliotajwa juu, wamepata uhakikisho wenye kufariji kutoka kwenye Biblia. Hilo limewafanya wahisi kuwa karibu zaidi na Mungu. (Zaburi 34:10; 37:25; 55:22; Wafilipi 4:6, 7) Kuwa na uhusiano wa karibu pamoja na Yehova Mungu ndiko kwenye umaana zaidi, kwa kuwa yeye huahidi: “Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.”—Waebrania 13:5.
Iwe mtu ameajiriwa au sivyo, Neno la Mungu hutia kila mtu moyo kukuza sifa zenye mafaa kwa maisha ya kila siku. Haishangazi kwamba Mashahidi wa Yehova nyakati fulani hutafutwa na kuthaminiwa kuwa wafanyikazi wanaofuatia haki. Wao hufuata shauri la Biblia la kuwa wenye bidii na wenye kutegemeka, si wavivu.—Mithali 13:4; 22:29; 1 Wathesalonike 4:10-12; 2 Wathesalonike 3:10-12.
Uhuru Kutokana na Usumbufu wa Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa
Kuna kisababishi kikuu cha ukosefu wa kazi—choyo cha binadamu na pupa. Kama isemavyo Biblia, “mwanadamu ametawala mwanadamu kwa umizo lake.”—Mhubiri 8:9, NW.
Tatizo la ukosefu wa kazi ya kuajiriwa—na matatizo mengine pia—yatatatuliwa kwa kuondolewa kwa utawala wa binadamu, ulio sasa katika “siku [zao] za mwisho.” (2 Timotheo 3:1-3) Kuna uhitaji wa ulimwengu ambao ni mpya kwelikweli. Ndiyo, ulimwengu ambao katika huo jamii adilifu ya kibinadamu yaweza kuishi na kufanya kazi chini ya utawala wenye haki na usiopendelea, ambapo pupa haitakuwapo tena. (1 Wakorintho 6:9, 10; 2 Petro 3:13) Hiyo ndiyo sababu Yesu alifundisha watu waombe kwamba Ufalme wa Mungu uje na kwamba mapenzi Yake yatimizwe duniani.—Mathayo 6:9, 10.
Likifafanua kuondolewa kwa matatizo makuu ya wanadamu, Neno la Mungu huonyesha matokeo ya Ufalme huo: “Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine. . . . Wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi. Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu.” (Isaya 65:21-23) Usumbufu wa ukosefu wa kazi ya kuajiriwa karibuni utatoweka kabisa. Ikiwa unataka kujua zaidi kuhusu suluhisho la Mungu, tafadhali wasiliana na Mashahidi wa Yehova katika eneo lako.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Amkeni! la Oktoba 22, 1994, kurasa 16-18; Juni 8, 1992, kurasa 6-10; Aprili 1984, ukurasa 18-21; na Juni 8, 1982 (Kiingereza), kurasa 3-8.
[Sanduku katika ukurasa wa11]
Kubuni Kazi Nyumbani
• Kuwa yaya, utunzaji wa watoto
• Kuuza mboga au maua yaliyokuzwa nyumbani
• Kushona, kubadilisha, na kurekebisha mavazi
• Kuoka na utayarishaji wa chakula
• Kushona firashi, kusuka kwa nyuzi, kufuma; ufinyanzi; na ufundi mwingine
• Kutengeneza vitu vya kupambia nyumba
• Kazi ya utunzaji vitabu, kupiga taipu, huduma za kompyuta za nyumbani
• Huduma za kujibu simu
• Utengenezaji nywele
• Kuweka anwani na kujaza bahasha kwa ajili ya watangazaji wa bidhaa
• Kuosha magari na kuyapaka nta (mteja analeta gari nyumbani kwako)
• Utengenezaji kufuli na funguo (karakana ikiwa nyumbani)
[Sanduku katika ukurasa wa11]
Kubuni Kazi Nje ya Nyumbani
• Kukaa na nyumba za watu (wakati watu wamekwenda likizo na wataka makao yao yatunzwe)
• Kusafisha: maduka; ofisi; nyumba na vyumba baada ya ujenzi, baada ya visa vya moto, baada ya watu kuhama; kazi ya nyumbani (katika nyumba za wengine); madirisha (ya maofisi na nyumba)
• Urekebishaji: vitu vya kila aina (maktaba zina vitabu vilivyo rahisi kufuata juu ya urekebishaji)
• Kazi ndogo-ndogo za aina mbalimbali: kufanyiza mfanyizo wa nje wa nyumba; kutengeneza kabati, milango, sebule; kupaka rangi; kutengeneza ua; kutengeneza paa
• Kazi ya shamba: kupanda na kuvuna, kutunda matunda
• Kutengeneza mandhari za kiasili ndani ya majumba na kutunza mimea kwenye: ofisi, banki, majumba ya kununua vitu na kumbi na sebule
• Bima, kununua na kuuza mashamba
• Kuweka na kuosha zulia
• Kupeleka magazeti kwa ukawaida (watu wazima na watoto), huduma nyinginezo za kupeleka vitu: matangazo, bili za manispaa
• Kuhamisha, kuhifadhi vitu
• Kutengeneza mandhari za kiasili, kupogoa miti, kutunza bustani, kukata mbao
• Dereva wa basi la shule
• Upigaji picha (mandhari na matukio ya umma)
• Kutengeneza chambo kwa wavuvi
[Picha katika ukurasa wa 10]
“Wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.”—Isaya 65:22