Tulitoroka Mabomu—Miaka 50 Baadaye!
“Mabomu yatakuwa yakilipuka hapa karibuni. Kila mtu aende mahali pa kujisetiri!”
KWA maneno hayo mume wangu nami tulionywa na polisi tuondoke nyumbani na kwenda kwenye kimbilio katika handaki lililojengwa kwa saruji lililokuwa karibu. Tangazo hilo lilitushtua sana. Kwa vyovyote, hatukuwa katika eneo fulani la ulimwengu lililo na vita; tulikuwa tukiwazuru marafiki katika moja ya visiwa vya matumbawe vilivyo vizuri nje ya Visiwa vya Marshall, katika Mikronesia.
Tulikuwa tumekuja kutumia juma moja pamoja na rafiki na mume wake kwenye kisiwa kidogo cha Tõrwã. Mke ndiye aliyekuwa Shahidi wa Yehova pekee katika kisiwa hicho, na tulitaka kumsaidia kuwahubiria watu walioishi huko.
Kwa asili watu wa Marshall ni wenye urafiki na wana hamu ya kuongea juu ya Biblia. Kwa vile kitabu Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani kilikuwa kimetolewa hivi karibuni katika lugha ya wenyeji, tulikuwa na fursa nzuri ya kuwaangushia watu nakala kadhaa. Wote ambao walitaka kitabu hicho walituhakikishia kwamba wangekisoma na kutokitumia kama ken karawan, au “hirizi ya bahati njema,” ili kufukuzia mbali roho waovu. Desturi inayopendwa sana huko ni ile ya kuweka ukurasa wa Biblia uliokunjwa ndani ya chupa na kuining’iniza kutoka kwenye boriti au kwenye mti ulio karibu, kwa kuwa hilo hufikiriwa kuwa hufukuzia mbali roho waovu.
Kwa siku kadhaa tulikuwa tukifurahia ziara yetu, lakini Jumamosi ilipofika, upesi tulitambua kwamba mambo yangebadilika. Tulianza siku kwa kujifurahisha kuogelea asubuhi mapema ndani ya maji ya wangwa yaliyo maangavu na yenye joto. Tulipokuwa tukirudi kutoka ufuoni, tuliona meli ya rangi ya kijivujivu yenye kuogofya ikikaribia. Upesi, tuligundua ilicholeta. Polisi alieleza kwamba kikundi cha wanaume saba wa jeshi la Marekani kilikuwa kimewasili ili kulipua mabomu ya zamani katika kisiwa hicho. Ili kuhakikisha usalama wa umma, makao yangehamwa na wakazi wa kisiwani wangetumia siku hiyo ndani ya mahandaki yaliyojengwa na Wajapani wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili.
Mahandaki hayo, ambayo wageni wanaotembelea Tõrwã huyaona karibu mara tu wanapowasili, ni ushuhuda wa wakati uliopita wenye kuogofya. Kwa umbali kisiwa hicho hufanana kabisa na paradiso ya tropiki, lakini kwa kukikaribia inadhihirika kuwa uzuri wa Tõrwã umeharibiwa na makovu ya vita iliyoisha miaka 50 hivi iliyopita. Wakati mmoja kisiwa hicho kilikuwa kituo kikuu cha ndege za jeshi la Wajapani, sasa kimejaa takataka ya mabaki ya Vita ya Ulimwengu ya Pili. Kila mahali pana masalio ya vita yaliyo na kutu—ndege za kivita, bunduki za kufanyia mashambulio, na topido— zilizofunikwa na mimea ya aina mbalimbali ya tropiki.
Hata hivyo, ni mabomu yaliyosalia, ambayo yanashtua kwa hofu. Wakati wa vita, majeshi ya Marekani yaliangusha zaidi ya tani 3,600 za mabomu, napamu, na roketi huko Tõrwã, na majeshi ya Wajapani yalikuwa na ghala lao la mabomu na silaha ardhini. Ingawa haielekei kwamba bomu la miaka 50 lingelipuka, sikuzote yanakuwa na uwezekano wa kutokeza hatari, jambo linaloonyesha sababu kwa nini vikundi vya kutegua mabomu vimezuru kisiwa hicho angalau mara tano tangu 1945, mwaka ambao vita iliisha.
Tulishangaa ikiwa onyo hilo lilikuwa la kweli, kwa hiyo tulitembea hadi eneo ambalo kikundi cha kutegua mabomu kilikuwa kimeshuka pwani na kusema nacho. Walisema, onyo hilo halikuwa la kweli tu, bali milipuko ya mabomu ingeanza katika muda wa saa moja! Tuliambiwa, ikiwa hatukujificha kwenye handaki, tungelazimika kutoka kwenye kisiwa hicho saa hiyohiyo.
Rafiki yetu aliamua kubaki Tõrwã na kupata kinga ndani ya handaki kubwa ambapo bombomu ziliwekwa wakati wa vita pamoja na familia kadhaa. Baadaye alituambia kwamba madirisha pekee yaliyokuwa ndani ya handaki hilo zee lililojengwa kwa saruji yalikuwa mashimo kwenye kuta ambapo bunduki zingefyatuliwa na kwamba, ndani, kulikuwa hakustareheshi kwa sababu ya joto na msongamano. Kutumia siku ndani ya handaki hilo kulileta tena kumbukumbu za miaka ya vita, na aliungama kwamba ingawa mabomu yaliyolipuka yalimvutia sana akiwa mtoto, sasa yalionekana yakitia woga mwingi.
Mume wake alikuwa amekubali kutusafirisha hadi Kisiwa cha Wollet, kilicho umbali wa kilometa mbili na nusu, ndani ya mashua iliyo na mota ya nje. Tulikuwa tumesafiri kwa dakika chache tu tuliposikia mngurumo mkubwa. Tulipotazama nyuma yetu kuelekea Tõrwã, tuliona wingu la moshi likipaa juu karibu na eneo la makazi ya kisiwa hicho. Upesi, kulikuwa na mlipuko mwingine na kisha wa tatu, mpasuko mkubwa zaidi.
Tulitumia siku hiyo tukihubiri huko Wollet, na ilikuwa siku yenye milipuko ya mbali ya mabomu ya mara kwa mara. Mabomu ya zamani yalikuwa yamepatikana na mipaka ikawekwa miezi kadhaa iliyotangulia. Mizinga ilipatikana kila mahali—katika pwani, katika bara kandokando ya barabara ya ndege, na hata kwenye nyua za nje za nyumba za watu! Ili kupunguza idadi ya milipuko, vikundi vya kutegua mabomu vilikusanya idadi ya mabomu madogo kisha kuyalipua yote pamoja.
Ilikuwa karibu kuchwa tuliporudi Tõrwã. Tulipokaribia kisiwa hicho, tuliona kwamba moshi wa kawaida unaotokana na moto wa kupikia ulikosekana. Tulijua jambo fulani lilikuwa baya. Kwa ghafula, mashua ndogo ilikuja kwa kasi kutuelekea, ikituonya tusiende karibu zaidi. Bomu moja kubwa lililokuwa limezama bado lilibaki kulipuliwa karibu na mwamba. Hivyo, tulipokuwa tunapeperuka karibu na bara wakati wa utusitusi, tuliona kitu ambacho watu wengi walio hai leo hawajapata kuona kamwe—mlipuko wa chini ya maji wa bomu la Vita ya Ulimwengu ya Pili, ambao ulirusha maji mengi na moshi mamia ya meta hewani!
Kwa kufurahisha, hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa katika Tõrwã siku hiyo. Je, kikundi cha kutegua mabomu hatimaye kilikuwa kimeondolea mbali mabomu yaliyosalia katika kisiwa hicho? Yamkini la. Kiongozi wa kikundi alisema kwamba alitarajia wakazi wa kisiwani wajikwae kwa mizinga ya zamani zaidi katika wakati ujao. Bila shaka, tukio hilo lilitupatia jambo la kusema na watu tulipomaliza kazi yetu ya kuhubiri katika Tõrwã. Lilikuwa pendeleo kubwa kuambia watu hawa wa kisiwani kuhusu wakati ambao Ufalme wa Yehova ‘utakomesha vita hata mwisho wa dunia.’—Zaburi 46:9.
Kama ilivyosimuliwa na Nancy Vander Velde
[Picha katika ukurasa wa 27]
Bomu ambalo bado kulipuliwa