Wakristo na Mfumo wa Tabaka
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA
NI NINI huja akilini mwako unaposikia maneno “mfumo wa tabaka”? Labda unafikiri juu ya India na mamilioni ambao hawana tabaka. Ijapokuwa mfumo wa tabaka ni sehemu ya dini ya Kihindu, Wahindu wenye kutaka mabadiliko wamejaribu kuondoa madhara yaliyosababishwa na mfumo huu kwa wale walio wa matabaka ya chini na wale wasiokuwa na tabaka. Kutokana na haya, ungesemaje ikiwa ungesikia kwamba hata makanisa yanayodai kuwa ya Kikristo yanafuata mfumo wa tabaka?
Kile Kiwezekanacho Kuwa Chanzo cha Mfumo wa Tabaka Katika India
Mgawanyo wa watu katika matabaka ya kijamii ambayo katika hayo wengine huhisi kuwa bora zaidi si jambo geni katika India. Kontinenti zote zimejionea ubaguzi wa aina moja au nyingine. Jambo ambalo limefanya mfumo wa tabaka wa India uwe tofauti ni uhakika wa kwamba kwa zaidi ya miaka 3,000 iliyopita, hatua ya kutumikisha jamii iliingizwa ndani ya dini.
Ijapokuwa chanzo cha mfumo wa tabaka hakijulikani kwa hakika, wenye mamlaka fulani husema mfumo huo ulianza katika ustaarabu wa kale wa Bonde la Indus katika Pakistan ya kisasa. Akiolojia huelekea kuonyesha kwamba wakazi wa mapema zaidi baadaye walishindwa na makabila yaliyotoka kaskazini-magharibi, ambayo yalikuwa katika kile kinachoitwa kwa ukawaida “kuhama kwa Waarya.” Katika kitabu chake The Discovery of India, Jawaharlal Nehru huita kuhama huku “muungano na mchanganyiko mkubwa wa kwanza wa kitamaduni,” ambao ulitokeza “jamii za Kihindi na utamaduni wa msingi wa Kihindi.” Hata hivyo, mchanganyiko huu haukutokeza usawa wa kijamii.
Kitabu The New Encyclopædia Britannica kinataarifu hivi: “Wahindu ndio waliotokeza matabaka (jātis, kihalisi ‘uzawa’) kwa kugawanya vile vikundi vinne, kwa sababu ya ndoa ya mseto (ambayo imekatazwa na vitabu vya Kihindu kwenye sheria takatifu). Hata hivyo, wananadharia wa kisasa, hudhania kwamba matabaka yaliibuka kutokana na tofauti katika desturi za mazoea ya kifamilia, tofauti za kijamii, na kutokana na upambanuzi wa kazi maalumu. Wasomi wengi wa kisasa hushuku kama mfumo wa matabaka ulio sahili ulikuwa tu wazo la kinadharia la kijamii na kidini na wasomi hao wamesisitiza kwamba mgawanyo ulio tata wa jamii ya Kihindu wenye matabaka na matabaka madogo yanayokaribia 3,000 labda ulikuwako hata katika nyakati za kale.”
Kwa muda fulani ndoa za mseto zilifanywa kati ya jamii, na ubaguzi wa hapo awali uliotokana na rangi ya ngozi ukawa si dhahiri sana. Sheria kali zilizoongoza tabaka zilikuwa ubuni wa kidini wa baadaye, zilizotajwa katika maandiko ya Vedi na Mfumo (au Kanuni) za Manu, Mhindu mwenye hekima. Wabrahman walifundisha kwamba matabaka ya juu yalikuwa yamezaliwa yakiwa na utakato uliowatofautisha na matabaka ya chini. Walikazia kikiki katika Wasudra, au tabaka la chini zaidi, itikadi ya kwamba kazi yao ya hali ya chini ilikuwa adhabu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya matendo mabaya waliyoyafanya wakati wa maisha yaliyopita na kwamba majaribio yoyote ya kuvunja mipaka ya tabaka yangewafanya kuwa wasiokuwa na tabaka. Ndoa ya mseto, kula pamoja, kutumia maji yaleyale, au kuingia hekalu lilelile kama Msudra kungeweza kumfanya mtu aliye wa tabaka la juu apoteze tabaka.
Tabaka Katika Hali za Kisasa
Baada ya kujinyakulia uhuru katika mwaka wa 1947, serikali ya India isiyo ya kidini ilibuni katiba ambayo ilifanya ubaguzi wa tabaka kuwa uhalifu. Ikitambua kwamba Wahindu wa tabaka la chini walikuwa wameonewa kwa karne nyingi, serikali hata ilitunga sheria ya kuwekwa kwa nyadhifa za serikali vilevile nafasi katika vyuo vya elimu, kwa ajili ya scheduled caste na makabila.a Neno linalotumiwa kwa vikundi hivi vya Kihindu ni “Dalit,” linalomaanisha “aliyepondeka au aliyedharauliwa.” Lakini hivi majuzi kichwa kimoja cha habari cha gazeti la habari kilitaarifu: “Wakristo wa Dalit Wanadai Haki [watengewe kazi na nafasi za kuingia vyuo vikuu].” Jambo hili limetokeaje?
Misaada mingi ambayo serikali imewapa Wahindu wa matabaka ya chini hutegemea uhakika wa kwamba wameonewa kwa sababu ya mfumo wa tabaka. Kwa hiyo ilionwa kwamba dini ambazo hazikufuata mfumo wa tabaka haziwezi kutarajia misaada hiyo. Hata hivyo, kwa sababu walikuwa wa tabaka la chini, au wasioguswa, wageuzwa-imani, wasema Wakristo wa Dalit, wao pia wanabaguliwa, si na Wahindu tu bali pia na ‘Wakristo wenzao.’ Je, hiyo ni kweli?
Wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo na Mfumo wa Tabaka
Wahindu wengi waligeuzwa imani na wamishonari Wareno, Wafaransa, na Waingereza, ambao walikuwa Wakatoliki na Waprotestanti, wakati wa ukoloni. Watu kutoka matabaka yote wakawa Wakristo kwa jina tu, wahubiri fulani wakiwavutia Wabrahman, wengine wakiwavutia Wasioguswa. Mafundisho na mwenendo wa wamishonari yaliathirije itikadi katika mfumo wa tabaka iliyokuwa imepenya kwa kina kirefu?
Kuhusu Waingereza walio India, mwandishi Nirad Chaudhuri asema kwamba makanisani “kutaniko la Wahindi halingeketi pamoja na Wazungu. Utambuzi wa ubora wa kijamii ambao ulitegemeza utawala wa Uingereza juu ya India haukufichwa na Ukristo.” Akionyesha mtazamo kama huo, katika 1894 mmishonari mmoja aliripoti kwenye Kamati ya Misheni za Kigeni ya Marekani kwamba kugeuza imani watu wa tabaka la chini kulikuwa ni “kukusanya takataka Kanisani.”
Kwa wazi, ile hisia ya ubora wa kijamii kwa upande wa wamishonari wa mapema na mchanganyiko wa mafundisho ya Kibrahman na mafundisho ya kanisa yamechangia sana mfumo wa tabaka ambao unaungwa mkono waziwazi na wengi wanaojiita eti Wakristo katika India.
Tabaka Katika Makanisa Leo
Askofu Mkuu Mkatoliki George Zur, alipokuwa akihutubia Mkutano wa Maaskofu Wakatoliki wa India katika 1991, alisema: “Wageuzwa-imani wa Scheduled caste hawaonwi kuwa wa tabaka la chini na Wahindu wa tabaka la juu peke yao bali pia na Wakristo wa tabaka la juu. . . . Mahali palipotengwa huwekwa kando kwa ajili yao katika makanisa ya parokia na katika makaburi. Ndoa za mseto kati ya tabaka huchukiwa . . . Itikadi ya tabaka imeenea sana miongoni mwa makasisi.”
Askofu M. Azariah, wa Kanisa la Church of South India, ambalo ni la United Protestant Church, alisema katika kitabu chake The Un-Christian Side of the Indian Church: “Kwa hiyo Wakristo wa Scheduled Caste (Dalit) hubaguliwa na kuonewa na Wakristo wenzao walio katika makanisa yao kadhaa na si kutokana na kosa lao bali kwa sababu ya kuzaliwa katika matabaka ya chini, hata wanapokuwa ni Wakristo wa kizazi cha 2, 3 au 4. Wakristo wa tabaka la juu ambao ni wachache Makanisani huendeleza ubaguzi wao wa tabaka hata baada ya vizazi kadhaa, bila kuathiriwa na imani na mazoea ya Kikristo.”
Uchunguzi wa serikali juu ya matatizo ya jamii za hali ya chini katika India, unaojulikana kuwa Tume ya Mandal, ulipata kwamba wanaojidai kuwa Wakristo katika Kerala waligawanyika katika “vikundi mbalimbali vya kikabila kwa kutegemea matabaka yao. . . . Hata baada ya kugeuzwa, wageuzwa-imani wa tabaka la chini walizidi kuonwa kuwa Harijanb . . . Wasiria na Wapulaya ambao ni washiriki wa Kanisa lilelile walifanya desturi za kidini wakiwa wamejitenga katika majengo mbalimbali.”
Ripoti ya habari katika Indian Express katika Agosti 1996 ilisema hivi kuhusu Wakristo wa Dalit: “Katika Tamil Nadu, maeneo yao ya makazi hutengwa na matabaka ya juu. Katika Kerala, wao ni vibarua wasio na mashamba, na wao hufanyia kazi Wakristo wa Siria na wengine wa matabaka ya juu walio na mashamba. Hakuna kula pamoja au ndoa za mseto kamwe kati ya Dalit na Wakristo wa Siria. Katika visa vingi, Dalit huabudu katika makanisa yao, yanayoitwa ‘kanisa la Pulaya’ au ‘kanisa la Paraya.’” Haya ni majina ya matabaka madogo-madogo.
Maitikio ya Kutoridhika
Vikundi vya watu wa kawaida wenye kuteta, kama vile FACE (Baraza Linalopinga Kutumiwa Vibaya kwa Wakristo), vinataka serikali iwasaidie Wakristo wa Dalit. Hangaiko kubwa ni msaada wa kiuchumi kwa Wakristo wageuzwa-imani. Hata hivyo, wengine wanahangaikia jinsi mambo yanavyotendeka kanisani. Katika barua waliyoandikia Papa John Paul wa Pili, karibu waweka-sahihi 120 walitaarifu kwamba walikuwa “wameukubali Ukristo ili wakombolewe kutoka kwenye mfumo wa tabaka” lakini sasa hawaruhusiwi kuingia katika kanisa la kijijini au kushiriki ibada. Walilazimishwa kujenga nyumba kandokando ya mtaa mmoja ambao hakuna Mkristo yeyote wa tabaka la juu—wala kasisi wa parokia—ambaye aliwahi kwenda! Vivyo hivyo mwanamke mmoja Mkatoliki mwenye kutaabishwa alisema: “Bila shaka ni jambo la maana kwangu kwa mwana wangu kusoma katika chuo cha elimu kilicho bora. Lakini ni jambo la maana hata zaidi aonwe kuwa sawa na waumini wenzake [Wakatoliki].”
Ingawa wengine wanajaribu kuboresha hali ya Wakristo wa Dalit, wengi wanakosa subira. Mashirika kama vile Vishwa Hindu Parishad (Shirika la Wahindu Ulimwenguni) vinajaribu kuwarudisha tena wageuzwa-imani Wakristo ndani ya kundi la Wahindu. Sherehe iliyohudhuriwa na watu 10,000, iliripotiwa na gazeti Indian Express, ambayo zaidi ya familia 600 za aina hiyo za “Kikristo” zilikubali tena Dini ya Hindu.
Njia ya Kweli ya Kikristo
Ikiwa wamishonari wa mashirika ya makanisa wangefundisha mafundisho ya Kristo yenye kutegemea upendo, hakungekuwa na “Wakristo wa Brahma,” wala “Wakristo wa Dalit,” wala “Wakristo wa Paraya.” (Mathayo 22:37-40) Hakungekuwa na makanisa yaliyotengwa kwa ajili ya Dalit na hakungekuwa na kubaguliwa wakati wa milo. Ni jipi fundisho la Biblia ambalo hushinda tofauti za kitabaka?
“Kwa maana BWANA, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu . . . . asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa.”—Kumbukumbu la Torati 10:17.
“Sasa nawahimiza nyinyi kwa bidii, akina ndugu, kupitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kwamba nyote mseme kwa upatano, na kwamba kusiwe na migawanyiko miongoni mwenu, bali kwamba mpate kuunganishwa kwa kufaa katika akili ileile na katika mstari uleule wa fikira.”—1 Wakorintho 1:10.
“Kwa hilo wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwenu wenyewe.”—Yohana 13:35.
Biblia hufundisha kwamba Mungu alifanya wanadamu wote kutoka kwa mtu mmoja. Pia husema kwamba wazao wote wa mtu huyo mmoja wanapaswa ‘wamtafute Mungu na wampate, ijapokuwa, kweli, yeye hayuko mbali sana na kila mmoja wetu.’—Matendo 17:26, 27.
Wakati tofauti za kitabaka zilipoanza kuingia katika kutaniko la Kikristo la mapema, mwandikaji Yakobo, chini ya upulizio, alizishutumu waziwazi. Alisema: “Nyinyi mna tofauti za kitabaka miongoni mwenu wenyewe nanyi mmekuwa mahakimu mkitoa maamuzi maovu, je, sivyo ilivyo?” (Yakobo 2:1-4) Mafundisho ya kweli ya Kikristo hayaruhusu kuwe na mfumo wa tabaka wa aina yoyote.
Uhitaji wa Kufikiria Ulimwengu Mpya
Mamilioni ya Mashahidi wa Yehova wamekuwa tayari kubadilisha itikadi na mienendo yao ya zamani waliyojifunza kutoka kwa dini nyingi tofauti. Mafundisho ya Biblia yametoa mioyoni na akilini mwao hisia za ubora au uduni, ziwe zililetwa na utawala wa ukoloni, jamii, sera ya ubaguzi wa rangi, au mfumo wa tabaka. (Waroma 12:1, 2) Wana uelewevu ulio wazi wa kile ambacho Biblia huita “dunia mpya,” ambamo “uadilifu utakaa.” Ni tazamio tukufu namna gani kwa wengi wanaoteseka ulimwenguni!—2 Petro 3:13.
[Maelezo ya Chini]
a Miongoni mwa Wahindu “scheduled caste” ni maneno rasmi ya matabaka ya chini, au wasiokuwa na tabaka, Wasioguswa, ambao walipatwa na uhitaji wa kijamii na kiuchumi.
b Neno lililotungwa na M. K. Gandhi kwa ajili ya matabaka ya chini. Linamaanisha “Watu wa Hari,” moja ya jina la mungu Vishnu.
[Blabu katika ukurasa wa 25]
“Mungu si mwenye ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye humhofu na kutenda uadilifu akubalika kwake.” Matendo 10:34, 35
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]
Mtu Huhisi Namna Gani?
Ndiyo, mtu huhisi namna gani anapotendewa kama wa tabaka la chini na watu wanaodai kuwa Wakristo? Mkristo mmoja, ambaye wazazi wake waliokufa walikuwa wamegeuzwa imani kutoka kwa tabaka la Dini ya Hindu inayojulikana kuwa Cheramar au Pulaya asimulia kisa kilichotukia katika jimbo la nyumbani kwao la Kerala miaka kadhaa iliyopita:
Nilialikwa kwenye arusi ambapo idadi kubwa ya wageni walikuwa washiriki wa kanisa. Waliponiona kwenye sehemu ya makaribisho, vurugu fulani ilitokea, na wale waliokuwa wa Kanisa la Othodoksi la Siria walisema kwamba hawangebaki katika sehemu hiyo ya makaribisho ila tu nikiondoka, kwa kuwa hawangekula pamoja na mtu wa tabaka la pulaya. Wakati baba ya bibi-arusi alipokataa sharti lao, waligomea mlo huo kwa pamoja. Walipoondoka, mlo uliandaliwa. Lakini wale waliokuwa wakihudumu walikataa kuondoa jani la mgomba nililotumia kama sahani na kusafisha meza yangu.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Kanisa la kawaida katika India Kusini, ambapo watu wa tabaka la chini pekee hukutania