Wewe Hupendelea Watu wa Aina Gani?
“BIBI-ARUSI ATAKIKANA. Apaswa awe mweupe-mweupe na mwembamba, mhitimu wa chuo au yafaa zaidi akiwa ni mhitimu anayeendelea na masomo ya juu zaidi. Ni lazima atoke kwa familia tajiri yenye mali. Yafaa zaidi akiwa wa tabaka sawa.”
NDIVYO lisemavyo tangazo la ndoa la kawaida ambalo huenda ukaona katika gazeti la habari katika India. Yaelekea, waweza kuona jambo lilo hilo katika sehemu nyinginezo nyingi za ulimwengu. Katika India kwa kawaida taarifa hiyo hutolewa na wazazi wa yule atakayekuwa bwana-arusi. Huenda majibu yakatia ndani picha ya msichana mwenye sari nyekundu-nyangavu na aliyejivika vito vingi vya dhahabu. Familia ya mvulana ikikubali, mashauri kwa kusudi la ndoa yangeanza.
Viwango vya Kawaida vya Thamani
Katika India maombi ya kupata bibi-arusi mweupe-mweupe ni ya kawaida sana. Hiyo ni kwa sababu ya ile imani yenye kusitawi sana ya kwamba yale yaitwayo eti matabaka ya chini zaidi ya jamii ya Kihindu ni yenye watu weusi-weusi. Hivi karibuni, kipindi kimoja katika televisheni ya India kilisimulia hadithi ya wasichana wawili, mmoja alikuwa mweupe-mweupe na yule mwingine alikuwa mweusi-mweusi. Yule msichana mweupe-mweupe alikuwa mkatili na mwenye tabia mbaya; yule msichana mweusi-mweusi alikuwa mwenye fadhili na mwanana. Badiliko la kimuzungu likatukia, na yule msichana mweupe-mweupe akaadhibiwa akawa mweusi-mweusi, hali yule msichana mweusi-mweusi akathawabishwa akawa mweupe-mweupe. Kwa wazi somo la kiadili la hadithi hiyo lilikuwa kwamba ingawa wema hushinda hatimaye, rangi nyeupe-nyeupe ni thawabu inayotamaniwa.
Hisia hizo za ubaguzi-rangi ni zenye kusitawi zaidi ya vile ambavyo huenda mtu akatambua. Kwa kielelezo, huenda mtu kutoka Esia akazuru nchi ya Magharibi na kulalamika kwamba alitendwa vibaya kwa sababu ya rangi ya ngozi yake au macho yake yenye kwenda upande. Matendo hayo humsumbua, naye ahisi amebaguliwa. Lakini anaporudi kwao, huenda yeye akawatenda wengine wa kabila tofauti kwa njia iyo hiyo. Hata leo rangi ya ngozi na malezi ya kikabila yanaathiri sana kadirio la watu wengi la kufaa kwa mtu mwingine.
“Fedha huleta jawabu la mambo yote,” akaandika Mfalme Sulemani wa nyakati za kale. (Mhubiri 10:19) Hiyo ni kweli kama nini! Utajiri huathiri pia jinsi watu wanavyoonwa. Chanzo cha utajiri huo hakitiliwi shaka mara nyingi. Je! mtu amekuwa tajiri kwa sababu ya kujitahidi au usimamizi wenye uangalifu au kutofuatia haki? Hiyo haidhuru hata kidogo. Mali, iwe zimepatikana kwa haramu au sivyo, huongoza watu wengi wajaribu kupata upendeleo wa mwenye mali hizo.
Elimu ya juu zaidi huthaminiwa sana pia katika ulimwengu huu wenye ushindani. Mara mtoto azaliwapo, wazazi huhimizwa waanze kuweka pesa nyingi akibani kwa ajili ya elimu. Wakati anapofika miaka miwili au mitatu, wanahangaika juu ya kumwingiza katika shule ya vitoto ifaayo hiyo ikiwa hatua ya kwanza kwenye mwendo mrefu kuelekea digrii ya chuo kikuu. Yaonekana watu fulani hufikiri kwamba diploma yenye fahari huwaletea upendeleo na staha kutoka kwa wengine.
Naam, rangi ya ngozi, elimu, pesa, malezi ya kikabila—hayo yamekuja kuwa viwango ambavyo kwavyo watu wengi humkadiri mtu mwingine au, kumchukia mwingine bila sababu. Hayo ndiyo mambo yanayoamua ni nani watakaoonyesha na ni nani watakaomnyima upendeleo. Namna gani wewe? Wewe humpendelea nani? Je! wewe humwona mtu mwenye pesa, mwenye ngozi nyeupe-nyeupe, au mwenye elimu ya juu zaidi kuwa mwenye kustahili zaidi upendeleo na staha? Ikiwa ndivyo, unahitaji kufikiria kwa uzito msingi wa hisia zako.
Je! Hivyo Ni Viwango Vifaavyo?
Kitabu Hindu World huonelea hivi: “Mtu yeyote wa matabaka ya chini zaidi ambaye angemwua brāhmin angeweza kuteswa hadi kifo na kunyang’anywa mali zake, na nafsi yake ilaaniwe kwa umilele. Brāhmin aliyemwua mtu yeyote angeweza kutozwa faini tu na hangeadhibiwa kufa kamwe.” Ingawa kitabu hicho kinasema juu ya nyakati za kale, namna gani leo? Ubaguzi-rangi na uvutano wa kijumuiya umesababisha damu nyingi kumwagwa hata katika karne ya 20. Hiyo haijatukia katika India peke yake. Chuki na jeuri inayosababishwa na ubaguzi-rangi katika Afrika Kusini, ubaguzi-rangi katika United States, ubaguzi wa kitaifa katika nchi za Baltiki—orodha hiyo yazidi kuendelea—yote husababishwa na hisia za ubwana mkubwa wa kiasili. Kwa hakika, kupendelea huko mtu mmoja juu ya mwingine kwa sababu ya rangi au utaifa hakujatokeza matunda mazuri, ya amani.
Namna gani utajiri? Bila shaka, wengi huwa matajiri kupitia kazi ya kufuatia haki, yenye bidii. Hata hivyo, utajiri mwingi mno umekusanywa na wahalifu wa kisiri, wafanya magendo, wauzaji dawa za kulevya, wafanyi biashara ya silaha haramu, na wengineo. Ni kweli, baadhi yao hutoa msaada kwa mipango ya ufadhili au kutegemeza mipango ya kuwasaidia maskini. Hata hivyo, matendo yao ya uhalifu yamewaletea wenye kupatwa nayo kuteseka na huzuni isiyoweza kusimuliwa. Hata wenye kutenda uhalifu kwa kadiri ndogo, kama vile wale wanaokula rushwa au kushiriki katika mazoea ya biashara yenye udanganyifu, wamesababisha fadhaiko, madhara, na kifo wakati mazao au utumishi wao mbalimbali unapokosa kufaulu na kufanya kazi ifaavyo. Kwa kweli, kuwa na utajiri kwenyewe si msingi wa kadirio lenye upendeleo.
Basi, namna gani elimu? Je! orodha ndefu ya digrii na majina ya vyeo baada ya jina la mtu ni uthibitisho wa kwamba yeye ni mwenye kufuatia haki na ni mnyoofu? Je! inamaanisha kwamba anapaswa aonwe kwa upendeleo? Ni kweli, elimu yaweza kupanua maarifa ya mtu, na wengi ambao wametumia elimu yao ili kuwanufaisha wengine wanastahili heshima na staha. Lakini historia imejaa vielelezo vya utumizi wa ubinafsi na uonevu wa matungamano ya watu uliosababishwa na lile tabaka la wenye elimu. Na ebu fikiria yale yanayotukia kwenye eneo la chuo kikuu leo. Vyuo vikuu vimekumbwa na matatizo ya utumizi mbaya wa dawa za kulevya na magonjwa ya kuambukiza kingono, na wanafunzi wengi hujiandikisha kwa kusudi tu la kufuatia pesa, uweza, na umaarufu. Elimu ya mtu peke yayo si ishara yenye kutegemeka ya sifa yake ya kweli.
La, rangi ya ngozi, elimu, pesa, malezi ya kikabila, au mambo mengine kama hayo si msingi ufaao wa kukadiria kufaa kwa mtu mwingine. Wakristo hawapaswi kujishughulisha sana na mambo hayo wakijaribu kupata upendeleo kutoka kwa wengine. Kwa hiyo, mtu apaswa ahangaikie nini? Mtu apaswa afuate viwango gani?