Je, Kaburi la Kristo Liko Japani?
KATIKA 1935, Koma Takeuchi, kuhani wa Shinto, alitangaza kwamba alikuwa amegundua kaburi la Yesu Kristo kwenye kilima fulani katika kijiji cha Shingo, kaskazini mwa Japani. Alidai kwamba hati zilizopatikana katika ghala ya familia moja zilionyesha kwamba Yesu alikuwa ameishi katika kijiji cha Shingo kwa muda fulani na kufa huko. Alipotafuta mahali ambapo Yesu alizikwa, alipata mwinuko fulani wa ardhi na kukata kauli ya kwamba mwinuko huo ulikuwa kaburi la Yesu.
Kisha, hati ya Kiebrania inayoripotiwa kuwa ilipatikana katika kihekalu cha familia ya Takeuchi, ilisisitiza kwamba Yesu alikuwa amezuru Japani mara mbili na hata alikuwa amesomea mafumbo pamoja na makuhani Wajapani. Simulizi hilo ladai kwamba baada ya kusalitiwa, Yesu alitoroka Yudea na kwenda katika nyika ya Siberia, kisha akasafiri kwenda Japani, akaoa msichana wa huko aliyeitwa Miyuko, akawa baba wa binti watatu, akafa akiwa na umri wa miaka 106. Kulingana na hadithi hiyo, mtu aliyeuawa Yerusalemu hakuwa Yesu bali alikuwa ndugu yake mdogo aliyeitwa Isukiri.
Ni nini huenda ikawa ndicho kichocheo cha simulizi kama hilo? Kulingana na gazeti la habari Mainichi Shimbun, uhusiano uliopo kati ya Yesu na Shingo “wadokeza uwezekano wa kupata faida za kiuchumi ambao wenye mamlaka wa huko wanajua vizuri sana.” Kwa hiyo, watu wanatiwa moyo kwenda kuona mahali hapo. Lakini haipendekezwi kuchunguza sana mambo hayo. “Tuseme kaburi hilo lingechimbuliwa na wapate kwamba hakuna kitu ila mifupa ya zamani ya ng’ombe,” akasema mchunguzi mmoja. “Ebu wazia jinsi ambavyo kila mtu angevunjika moyo.”
Kwa hiyo kila mwaka Mei 3, wageni hufanya wajibu wao wa kukusanyika mbele ya lile lisemwalo eti kuwa kaburi la Yesu ili kuadhimisha “Sherehe ya Kristo.” Kuhani wa Shinto husimamia sherehe hiyo na kufukuza roho waovu kabla ya mchezo wa dansi kuanza.
Je, kuna ukweli wowote katika hadithi hii? La. Biblia yatuambia kwamba Yesu alipofikia umri wa miaka 30, alikuwa amejulikana kuwa mwana wa seremala aliyekulia Nazareti wala hakujulikana kuwa msafiri wa ulimwengu. Zile Gospeli nne zina masimulizi ya watu waliojionea mahubiri ya Kristo katika Israeli tangu awe na umri wa miaka 30 hadi 33. Hayo yatia ndani mahali na tarehe na kuthibitisha kwamba ni Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyeuawa Yerusalemu. Kwa hiyo, Wakristo wa kweli hawakengeushwi na ripoti zilizotiliwa chumvi mno zinazotaka kupotoa kweli ya Biblia kwa ajili ya makusudi ya ubinafsi.