Sura 8
Dini ya Shinto—Jititada ya Japan ya Kutafuta Mungu
“Kwa sababu baba yangu alikuwa kuhani wa Dini ya Shinto, tuliambiwa tutoe sadaka bilauri moja ya maji na bakuli moja la mchele uliopikwa kwa mvuke kwenye kamidana [kihekalu cha nyumbani cha Dini ya Shinto] kila asubuhi baada ya kiamsha-kinywa. Baada ya tendo hilo la ibada, tulishusha bakuli hilo la wali na kula kutoka kwalo. Kwa kufanya hivyo, nilikuwa na uhakika kwamba miungu ingetulinda sisi.
“Tuliponunua nyumba, tulihakikisha kwa uangalifu ufaaji wa mahali pa nyumba hiyo mpya kuhusiana na ile ya zamani kwa kuuliza shamani, au mwasiliani-roho. Alitutahadharisha kuhusu malango matatu ya mashetani na kutuagiza tufuate utaratibu wa kutakasa ambao baba yangu alipendekeza. Kwa hiyo tulitakasa makao hayo kwa chumvi mara moja kila mwezi.”—Mayumi T.
1. (Tia ndani utangulizi.) Ni wapi hasa ambako Dini ya Shinto inazoewa, nayo inahusisha nini kwa baadhi ya waumini wayo?
DINI ya Shinto ni ya Kijapan hasa. Kulingana na Nihon Shukyo Jiten (Ensaiklopedia ya Dini za Kijapan), “Habari inayohusu Dini ya Shinto karibu inafanana kabisa na utamaduni wa kikabila wa Kijapan, nao ni utamaduni wa kidini ambao haukuzoewa kamwe isipokuwa kwa kuambatana pamoja na jamii hiyo ya kikabila.” Lakini sasa uvutano wa Kijapan wa biashara na wa kitamaduni umeenea sana hata kwamba yapasa itupendeze kujua ni mambo gani ya kidini yaliyoamua ilivyokuwa historia ya Japan na utu wa Kijapan.
2. Dini ya Shinto inaongoza kadiri gani maisha za Wajapan?
2 Ingawa Dini ya Shinto hudai ina washiriki zaidi ya 91,000,000 katika Japan, ambayo ni jumla ya karibu robo tatu za idadi yake ya watu, uchunguzi mmoja wafunua kwamba ni watu 2,000,000 pekee, au asilimia 3 ya watu wazima, wanaodai hasa kuamini Dini ya Shinto. Hata hiyo, Sugata Masaaki, mtafiti wa Dini ya Shinto, asema: “Dini ya Shinto imefumwa kwa njia iliyotatanika sana na misingi ya maisha ya kila siku ya Kijapan kadiri ya kwamba watu ni kama hawatambui sana kuwapo kwayo. Kwa Mjapan hiyo si dini hasa bali ni kama tu kawaida isiyoepukika katika mazingira, kama vile hewa wanayopumua.” Hata wale wanaodai ni wenye ubaridi kuelekea dini hununua hirizi za Dini ya Shinto za usalama wa barabarani, hufanya arusi zao kulingana na mapokeo ya Dini ya Shinto, na hutumia fedha zao katika misherehekeo ya kila mwaka ya Dini ya Shinto.
Ilianzaje?
3, 4. Dini ya Kijapan ilipataje kwanza kujulikana kuwa Dini ya Shinto?
3 Jina “Dini ya Shinto” lilitokea katika karne ya sita W.K. ili kutofautisha dini ya mahali hapo na Dini ya Buddha, iliyokuwa ikianzishwa katika Japan. “Bila shaka, ‘Dini ya Wajapan’ . . . ilikuwako kabla ya kuanzishwa kwa Dini ya Buddha,” aeleza Sachiya Hiro, mtafiti wa dini za Kijapan, “lakini ilikuwa dini isiyojitokeza wazi katika fahamu, ikijumlisha desturi na ‘maadili.’ Hata hivyo, Dini ya Buddha ilipoanzishwa watu wakatambua uhakika wa kwamba maadili hayo yalifanyiza dini ya Kijapan, iliyo tofauti na Dini ya Buddha, ambayo ilikuwa dini ya kigeni.” Dini hii ya Kijapan ilitokea-tokeaje?
4 Ni vigumu kutaja tarehe fulani ambayo Dini ya Shinto ya awali, au “Dini ya Kijapan,” ilipotokea. Ukulima wa mchele kwenye ardhi yenye maji ulipofika, “kilimo cha ardhi yenye maji kilitaka jumuiya zilizopangwa vizuri kitengenezo na zenye uimara,” chaeleza Kodansha Encyclopedia of Japan, “na sherehe za kilimo—ambazo baadaye zilitimiza fungu la maana sana katika Dini ya Shintō—zilisitawishwa.” Jamii za watu hao wa kale zilikuwa na mawazo ya vijimungu vingi vya asili nazo zilivipa kicho.
5. (a) Ni nini maoni ya Dini ya Shinto juu ya wafu? (b) Maoni ya Dini ya Shinto juu ya wafu yakoje yakilinganishwa na yale ya Biblia?
5 Kuongezea kicho hicho, hofu ya nafsi zilizoondoka iliongoza kwenye sherehe za kuvitambikia. Hatimaye hilo lilisitawi likawa ibada ya roho za wazazi wa kale waliokufa. Kulingana na imani ya Dini ya Shinto, nafsi “iliyoondoka” ingali ina utu wayo na hutiwa uchafu wa kifo mara tu baada ya kifo. Waliofiwa wanapofanya sherehe za ukumbusho, nafsi inatakaswa kufikia kiwango cha kuondoa kisirani yote, na kutwaa utu wa amani na wa ukarimu. Baada ya muda roho hiyo ya mzazi wa kale aliyekufa hupanda ngazi ya kuwa kiabudiwa, au mlinzi wa wazazi waliokufa. Kwa hiyo twaona kwamba imani ya nafsi isiyoweza kufa ni jambo la msingi kwa dini nyingine bado na huongoza mitazamo na vitendo vya waumini.—Zaburi 146:4; Mhubiri 9:5, 6, 10.
6, 7. (a) Wafuasi wa Dini ya Shinto walikuwa na maoni gani kuelekea vijimungu vyao? (b) Shintai ni nini, na kwa nini ni ya maana katika Dini ya Shinto? (Linganisha Kutoka 20:4, 5; Mambo ya Walawi 26:1; 1 Wakorintho 8:5, 6.)
6 Vijimungu vya asili na vijimungu vya wazazi wa kale waliokufa vilionwa kuwa roho “zenye kupaa” katika hewa na kuijaza. Nyakati za misherehekeo watu waliita vijimungu vishuke mahali fulani palipotakaswa kwa ajili ya pindi hizo. Ilisemekana vijimungu vilifanya makao ya muda katika shintai, vitu vya ibada kama vile miti, mawe, vioo, na panga. Washamani, au wawasiliani-roho, walisimamia desturi hizo za kuita vijimungu vishuke.
7 Hatua kwa hatua, “sehemu za kutua” za vijimungu hivyo, ambazo zilitakaswa kwa muda kwa ajili ya misherehekeo, zikawa za namna ya kudumu zaidi. Watu wakajenga vihekalu kwa ajili ya vijimungu vyenye kufadhili, vile viliyoelekea kuwabariki. Hapo kwanza hawakuchonga mifano ya vijimungu bali waliabudu shintai, ambazo ilisemekana roho za vijimungu zilifanya makao ndani yazo. Hata mlima mzima, kama vile Fuji, ungeweza kutumika kama shintai. Muda si muda kukaja kuwa vijimungu vingi mno hata kwamba Wajapan wakatokeza usemi yaoyorozu-no-kami, ambao kwa halisi humaanisha “vijimungu milioni nane” (“kami” maana yake ni “vijimungu”). Sasa usemi huo hutumiwa kuonyesha “vijimungu visivyo na hesabu,” kwa kuwa idadi ya viabudiwa katika Dini ya Shinto inaongezeka daima.
8. (a) Kulingana na ngano ya Dini ya Shinto, ni jinsi gani Amaterasu Omikami kilifanyizwa na kulazimishwa kitoe nuru? (b) Ni jinsi gani Amaterasu Omikami kikapata kuwa kijimungu cha kitaifa, na wamaliki walikuwa na uhusiano gani nacho?
8 Kwa kuwa ibada za sherehe za Dini ya Shinto zilitegemea vihekalu, kila mlango wa ukoo ulifanyia kihekalu kijimungu chao cha ulinzi. Hata hivyo, familia ya kifalme ilipounganisha taifa hilo katika karne ya saba W.K., ilikweza kijimungu-kike-jua chao, Amaterasu Omikami, kuwa kijimungu cha kitaifa na umbo kuu la vijimungu vya Dini ya Shinto. (Ona kisanduku, ukurasa 191.) Punde si punde ngano ikabuniwa kwamba maliki alikuwa mzao wa moja kwa moja wa kijimungu-kike-jua. Ili kuimarisha imani hiyo, maandishi mawili makuu ya Dini ya Shinto, Kojiki na Nihon shoki, yalifanyizwa katika karne ya nane W.K. Vikitumia ngano zilizokweza familia ya kifalme kuwa wazao wa vijimungu, vitabu hivyo vilisaidia kuimarisha ukuu wa wamaliki.
Dini ya Misherehekeo na Ibada za Sherehe
9. (a) Ni kwa nini Dini ya Shinto huitwa dini ya “haina” na somi mmoja? (b) Dini ya Shinto hushikilia kwa kadiri gani mafundisho yayo? (Linganisha Yohana 4:22-24.)
9 Hata hivyo, vitabu hivyo viwili vya imani ya kingano ya Dini ya Shinto havikuonwa kuwa maandiko yaliyopuliziwa na Mungu. Kwa kupendeza, Dini ya Shinto haina mwanzilishi anayejulikana au Biblia. “Dini ya Shinto ni dini ya mfululizo wa ‘haina,’” aeleza Shouichi Saeki, msomi wa Dini ya Shinto. “Haina mafundisho yaliyo waziwazi na haina theolojia iliyoelezwa kirefu. Ni kama haina maagizo yoyote ya kufuatwa. . . . Ingawa nililelewa katika familia ambayo imeshikilia kimapokeo Dini ya Shinto, sikumbuki nikipewa elimu ya kidini yenye uzito.” (Italiki ni zetu.) Kwa wafuasi wa Dini ya Shinto, mafundisho, maagizo, na, nyakati nyingine, hata kile wanachoabudu si cha maana. “Hata kwenye kihekalu kile kile,” asema mtafiti mfuasi wa Dini ya Shinto, “kijimungu kilichofanyiwa kihekalu hicho mara nyingi mahali pacho palichukuliwa na kingine, na nyakati nyingine watu walioabudu vijimungu hivyo na kutoa sala kwavyo hawakutambua badiliko hilo.”
10. Ni jambo gani la muhimu sana kwa wafuasi wa Dini ya Shinto?
10 Basi, ni nini lililo la maana kubwa kwa wafuasi wa Dini ya Shinto? “Hapo awali,” chasema kitabu kimoja juu ya utamaduni wa Kijapan, “Dini ya Shinto ilifikiria vitendo vilivyohimiza upatano na riziki ya jumuiya ndogo kuwa ‘vyema’ na vile vilivyozuia vitu hivyo kuwa ‘vibaya.’” Upatano na vijimungu, asili, na jumuiya ulionwa kuwa wenye thamani ya juu zaidi. Chochote kilichoharibu upatano wenye amani wa jumuiya kilikuwa kibaya hata kiwe na thamani gani ya kiadili.
11. Misherehekeo inatimiza fungu gani katika ibada ya Dini ya Shinto na maisha ya kila siku?
11 Kwa kuwa Dini ya Shinto haina fundisho lolote rasmi, njia yayo ya kuhimiza upatano wa jumuiya ni kupitia desturi na misherehekeo. “Kilicho cha maana zaidi katika Dini ya Shinto,” yaeleza ensaiklopedia Nihon Shukyo Jiten, “ni kama tunaadhimisha misherehekeo au la.” (Ona kisanduku, ukurasa 193.) Kula karamu pamoja kwenye misherehekeo kuzunguka vijimungu vya wazazi wa kale waliokufa kulichangia roho ya ushirikiano kati ya watu katika jumuiya yenye kukuza mchele. Misherehekeo mikubwa-mikubwa ilihusiana na ingali inahusiana na ukuzi wa mchele. Katika masika, watu wa kijiji huita “kijimungu cha mipunga” kishuke kwenye kijiji chao, nao husali kwa ajili ya zao zuri. Katika vuli, wanashukuru vijimungu vyao kwa ajili ya mavuno. Wakati wa misherehekeo, hubeba vijimungu vyao huku na huku juu ya mikoshi, au kihekalu kinachobebeka, na hunywa shirika divai ya mchele (sake) na kula chakula pamoja na vijimungu.
12. Ni sherehe za aina gani za kutakasa zinazofanywa katika Dini ya Shinto, na kwa kusudi gani?
12 Hata hivyo, ili kuwa na umoja na vijimungu, wafuasi wa Dini ya Shinto huamini kwamba ni lazima wasafishwe na kutakaswa uchafu wao wote wa kiadili na dhambi. Hapo ndipo desturi zinapoingia. Kuna njia mbili za kutakasa mtu au kitu. Moja ni oharai na ile nyingine ni misogi. Katika oharai, kuhani mfuasi wa Dini ya Shinto husuka-suka tawi la msakaki ambao daima ni wa kijani-kibichi likiwa limefungwa kwenye ncha ya karatasi au mmea ili kutakasa kitu au mtu, hali katika misogi, maji hutumiwa. Ibada hizo za sherehe za kutakasa ni za lazima sana kwa Dini ya Shinto hivi kwamba Mjapan mmoja mwenye ufahamu atoa taarifa hii: “Yaweza kusemwa kwa uhakika kwamba bila ya desturi hizo, Dini ya Shinto haiwezi kusimama [ikiwa dini].”
Kubadilikana kwa Dini ya Shinto
13, 14. Dini ya Shinto imejirekebishaje ilingane na dini nyinginezo?
13 Misherehekeo na ibada za sherehe zimeambatana na Dini ya Shinto yajapokuwa mabadiliko ambayo Dini ya Shinto imepitia kwa miaka mingi. Mabadiliko gani? Mtafiti mmoja mfuasi wa Dini ya Shinto afananisha mabadiliko katika Dini ya Shinto na yale ya mwana-sesere aliyevishwa na kupambwa vizuri. Dini ya Buddha ilipoanzishwa, Dini ya Shinto ilijivisha fundisho la Dini ya Buddha. Wakati watu walipohitaji viwango vya kiadili, ilivaa Dini ya Confucius. Dini ya Shinto imekuwa yenye kubadilikana kweli kweli.
14 Usinkreti, au uunganishaji wa visehemu vya dini moja na nyingine, ulitukia mapema sana katika historia ya Dini ya Shinto. Ingawa Dini ya Confucius na Dini ya Tao, zinazojulikana katika Japan kuwa “Njia ya yin na yang,” zilikuwa zimepenyeza katika Dini ya Shinto, Dini ya Buddha ilikuwa kisehemu kikubwa kilichochanganyikana na Dini ya Shinto.
15, 16. (a) Wafuasi wa Dini ya Shinto waliitikiaje Dini ya Buddha? (b) Kuunganishwa kwa Dini ya Shinto na Dini ya Buddha kulitukiaje?
15 Dini ya Buddha ilipoingia kupitia China na Korea, Wajapan walibandika mazoea yao ya kidini ya kimapokeo kuwa Dini ya Shinto, au “njia ya vijimungu.” Hata hivyo, dini mpya ilipowasili, Japan iligawanyika juu ya kama ikubali Dini ya Buddha au la. Kambi ya waunga-mkono Dini ya Buddha ilisisitiza, ‘Nchi zote jirani huabudu hivyo. Kwa nini Japan iwe tofauti?’ Kikundi cha wapinga-Dini ya Buddha kilikanusha, ‘Tukiabudu vijimungu jirani, tutakuwa tunachokoza hasira ya vijimungu vyetu wenyewe.’ Baada ya makumi mengi ya miaka ya mgawanyiko, waunga-mkono Dini ya Buddha walishinda. Kufikia mwisho wa karne ya sita W.K., wakati Mwana-Mfalme Shōtoku alipoichukua Dini ya Buddha, dini mpya hiyo ilikuwa imetia mzizi.
16 Dini ya Buddha iliposambaa kwenye jumuiya za mashambani, ilikutana na viabudiwa vya huko vya Dini ya Shinto ambavyo kuwapo kwavyo kulikuwa kumeimarishwa sana katika maisha ya kila siku ya watu hao. Dini hizo mbili zililazimika kuridhiana ili ziendelee kuwapo pamoja. Watawa wa Dini ya Buddha wenye kuzoea nidhamu ya kibinafsi katika milima walisaidia kuunganisha dini mbili hizo. Kwa kuwa milima ilionwa kuwa makao ya miungu ya Dini ya Shinto, mazoea ya kujinyima raha ya watawa hao katika milima yalitokeza wazo la kuchanganya Dini ya Buddha na Dini ya Shinto, ambalo pia liliongoza kwenye ujenzi wa jinguji, au “mahekalu-vikanisa.”a Hatua kwa hatua muungano wa dini hizo mbili ukatukia wakati Dini ya Buddha ilipochukua hatua ya kwanza katika kufanyiza nadharia za kidini.
17. (a) Ni nini maana ya kamikaze? (b) Kamikaze lilihusianaje na imani ya kwamba Japan ni taifa la kimungu?
17 Wakati uo huo, imani ya kwamba Japan ilikuwa taifa la kimungu ilikuwa inatia mzizi. Wakati Wamongoli waliposhambulia Japan katika karne ya 13, kulitokea imani katika kamikaze, kwa halisi “upepo wa kimungu.” Mara mbili Wamongoli walivamia kisiwa cha Kyushu wakiwa na misafara ya meli nyingi sana, na mara mbili walishindwa na dhoruba. Wajapan walivipa vijimungu vyao (kami) vya Dini ya Shinto sifa ya kuleta dhoruba hizi, au pepo (kaze), na hilo liliimarisha sana sifa ya vijimungu vyao.
18. Dini ya Shinto ilishindanaje na dini nyingine?
18 Uhakika katika viabudiwa vya Dini ya Shinto ulivyoongezeka, hivyo vilionwa kuwa ndivyo vijimungu vya awali, hali Mabuddha (“walionurishwa”) na wabodhisattva (waliotarajia kuwa Mabuddha ambao husaidia wengine kufikia mnurisho huo; ona kurasa 136-8, 145-6) walionwa kuwa midhihirisho ya kitambo tu kimahali ya uungu. Kwa sababu ya pambano hilo kati ya Dini ya Shinto na Dini ya Buddha, vikundi vyenye mawazo tofauti vya Dini ya Shinto vilisitawi. Vingine vilikazia Dini ya Buddha, vingine vilikuza jamii ya vijimungu vya Dini ya Shinto, na bado vingine vilitumia namna ya baadaye ya Dini ya Confucius kupamba mafundisho yavyo.
Ibada ya Maliki na Dini ya Shinto ya Serikali
19. (a) Lengo la wafuasi wa Dini ya Shinto ya Urejezo lilikuwa nini? (b) Mafundisho ya Norinaga Motoori yaliongoza kwenye kufikiri gani? (c) Mungu atualika tufanye nini?
19 Baada ya miaka mingi ya kuridhiana, wanatheolojia wafuasi wa Dini ya Shinto waliamua kwamba dini yao ilikuwa imenajisiwa na fikira ya kidini ya China. Kwa hiyo wakasisitiza kurudia njia ya kale ya Kijapan. Kikundi kipya chenye mawazo tofauti cha Dini ya Shinto, kilichojulikana kuwa Dini ya Shinto ya Urejezo, kilitokea, Norinaga Motoori, msomi wa karne ya 18, akiwa mmoja wa wanatheolojia wacho walio mashuhuri zaidi. Akiwa anatafuta chanzo cha utamaduni wa Kijapan, Motoori alijifunza vitabu bora sana, hasa maandishi ya Dini ya Shinto yanayoitwa Kojiki. Alifundisha kwamba kijimungu-kike-jua Amaterasu Omikami ndicho kikuu lakini kwa njia isiyo wazi akaachia vijimungu sababu ya matukio ya asili. Kuongezea hayo, kulingana na mafundisho yake, uongozi wa kimungu hautabiriki, na ni utovu wa heshima kwa binadamu kujaribu kuuelewa. Usiulize maswali yoyote na ujitiishe kwa uongozi wa kimungu lilikuwa ndilo wazo lake.—Isaya 1:18.
20, 21 (a) Mwanatheolojia mmoja mfuasi wa Dini ya Shinto alijaribuje kuiondolea mbali Dini ya Shinto uvutano wa “Kichina”? (b) Falsafa ya Hirata iliongoza kwenye kuanzishwa kwa chama gani?
20 Mmoja wa wafuasi wake, Atsutane Hirata, alifafanua wazo la Norinaga na kujaribu kutakasa Dini ya Shinto, aondolee mbali uvutano wote wa “Kichina.” Hirata alifanya nini? Aliunganisha Dini ya Shinto na theolojia ya “Ukristo” ulioasi imani! Alifananisha Amenominakanushi-no-kami, kijimungu fulani kinachotajwa katika Kojiki, na Mungu wa “Ukristo” na akaeleza juu ya kijimungu hicho chenye kusimamia ulimwengu wote mzima kuwa kina vijimungu viwili vya cheo cha chini, “Mfanyiza-Sana (Takami-musubi) na Mfanyiza-Uungu (Kami-musubi), ambao yaelekea huwakilisha kanuni za kiume na kike.” (Religions in Japan) Ndiyo, yeye alichukua fundisho la kijimungu cha utatu kutoka kwa Roma Katoliki, ingawa halikupata kamwe kuwa fundisho kuu la Dini ya Shinto. Hata hivyo, kuchanganya kwa Hirata uitwao Ukristo na Dini ya Shinto hatimaye kuliingiza namna ya imani ya kijimungu kimoja ya Jumuiya ya Ukristo katika akili ya mfuasi wa Dini ya Shinto.—Isaya 40:25, 26.
21 Theolojia ya Hirata ikaja kuwa msingi wa chama cha ‘Mche Maliki,’ kilichoongoza kwenye kupinduliwa kwa watawala wa kiimla wa kijeshi wenye kuzozana, mashoguni, na kurudishwa kwa utawala wa kifalme katika 1868. Serikali ya kifalme iliposimamishwa, wanafunzi wa Hirata waliteuliwa wawe wajumbe wa kiserikali wa ibada ya Dini ya Shinto, nao waliunda chama cha kufanya Dini ya Shinto kuwa dini ya Serikali. Chini ya katiba hiyo mpya ya wakati huo, maliki, aliyeonwa kuwa mzao wa moja kwa moja wa kijimungu-kike-jua Amaterasu Omikami, alichukuliwa kuwa “mtakatifu na aliye safi.” Hivyo akawa kijimungu kikuu cha Serikali ya Dini ya Shinto.—Zaburi 146:3-5.
“Maandiko Matakatifu” ya Dini ya Shinto
22, 23. (a) Ni amri gani mbili zilizotolewa na maliki? (b) Ni kwa nini amri hizo zilionwa kuwa takatifu?
22 Ingawa Dini ya Shinto ilikuwa na kumbukumbu za kale, desturi, na sala katika Kojiki, maandishi ya Nihongi, na Yengishiki, Dini ya Shinto ya Serikali ilihitaji kitabu kitakatifu. Katika 1882 Maliki Meiji alitoa Amri Nyingine ya Kifalme kwa Askari-Jeshi na Mabaharia. Kwa kuwa ilitoka kwa maliki, ilionwa na Wajapan kuwa maandishi matakatifu, na ikawa msingi wa kutafakari kwa kila siku kwa wanaume katika majeshi yenye silaha. Ilikazia kwamba wajibu wa mtu kulipa madeni na madaraka yake kwa kijimungu-maliki ulikuwa wa maana zaidi ya wowote ule ambao huenda mtu akawa nao kwa mwingineye yote.
23 Nyongeza nyingine ya maandishi matakatifu ya Dini ya Shinto ilitukia wakati maliki alipotoa Amri ya Kifalme juu ya Elimu mnamo Oktoba 30, 1890. “Si kwamba tu ilionyesha misingi kwa ajili ya elimu ya shule bali kwa ujumla ikawa maandiko matakatifu ya Dini ya Shinto ya Serikali,” aeleza Shigeyoshi Murakami, mtafiti wa Dini ya Shinto wa Serikali. Amri mpya hiyo ilidhihirisha kwamba uhusiano “wa kihistoria” kati ya wale wazazi wa kale wa kifalme waliokufa wa kingano na raia zao ulikuwa ndio msingi wa elimu hiyo. Wajapan walikuwa na maoni gani kuelekea maagizo hayo?
24. (a) Toa kielelezo cha jinsi amri nyingine za kifalme zilionwa na watu. (b) Dini ya Shinto ya Serikali iliongozaje kwenye kuabudu maliki?
24 “Nilipokuwa msichana, kaimu wa mkuu [wa shule] alikuwa akiinua kisanduku cha mbao kwenye kiwango cha jicho na kukileta jukwaani kwa kicho,” akumbuka Asano Koshino. “Mkuu angekipokea kisanduku hicho na kuchukua hati-kunjo ambayo juu yayo Amri ya Kifalme juu ya Elimu ilikuwa imeandikwa. Amri hiyo ilipokuwa ikisomwa, tulipaswa kuinamisha vichwa vyetu mpaka tusikie maneno ya kumalizia, ‘Jina la Mfalme Mheshimiwa na Muhuri Wake.’ Tuliisikia mara nyingi sana hivi kwamba tukakariri maneno yayo.” Kufikia 1945, na kupitia mfumo wa kielimu wa ngano, taifa lote lilizoezwa lijiweke wakfu kwa maliki. Shinto ya Serikali ilionwa kuwa dini kubwa zaidi, na yale madhehebu mengine 13 ya Shinto yenye kufunza mafundisho tofauti-tofauti yakashushwa cheo hata kurejezewa kuwa Dhehebu la Kishinto.
Utume wa Kidini wa Japan—Kuushinda Ulimwengu
25. Maliki Mjapan alionwaje na watu?
25 Dini ya Shinto ya Serikali ilikuwa na sanamu yayo pia. “Kila asubuhi, nilipiga makofi kuelekea jua, alama ya kijimungu-kike Amaterasu Omikami, halafu nilitazama mashariki kuelekea Ikulu ya Kifalme na kuabudu maliki,” akumbuka Masato, mwanamume mzee-mzee Mjapan. Maliki aliabudiwa kuwa kijimungu na raia zake. Alionwa kuwa aliye juu zaidi kisiasa na kidini kwa sababu ni mzao wa kijimungu-kike-jua. Profesa mmoja Mjapan alitoa taarifa hii: “Maliki ni kijimungu kilichofunuliwa kwa wanadamu. Yeye ni Mwabudiwa aliyedhihirishwa.”
26. Ni fundisho gani lililotokana na kuheshimu mno maliki?
26 Kama tokeo, fundisho lilisitawishwa kwamba “kitovu cha ulimwengu huu wa ajabu ni bara la Mikado [Maliki]. Kutoka kwenye kitovu hiki ni lazima tupanue Roho Kubwa hii ulimwenguni pote. . . . Upanuzi wa Japan Kubwa ulimwenguni pote na ulimwengu wote kukwezwa uwe bara la Vijimungu ndiyo shughuli ya haraka zaidi ya wakati huu na, kwa mara nyingine, ndilo lengo letu la milele na lisilobadilika.” (The Political Philosophy of Modern Shinto, cha D. C. Holtom) Katika hilo hapakuwepo mtengano kati ya Kanisa na Serikali!
27. Ibada ya maliki Mjapan ilitumiwaje na watu wa kivita?
27 Katika kitabu chake Man’s Religions, John B. Noss aeleza hivi: “Jeshi la Wajapan halikukawia kufuata maoni hayo. Walifanya ikawa sehemu ya maongezi yao ya vita kwamba ushindi ndio uliokuwa utume mtakatifu wa Japan. Hakika katika maneno hayo twaweza kuona matokeo ya kiakili ya utukuzo wa taifa yaliyotiwa pamoja na kanuni zote za kidini.” Jinsi msiba ulivyopandwa kwa Wajapan na kwa jamii nyingine za watu, kwa kutegemea hasa ngano ya Dini ya Shinto ya uungu wa maliki na kuchanganywa kwa dini na utukuzo wa taifa!
28. Dini ya Shinto ilitimiza fungu gani katika harakati ya Kijapan ya vita?
28 Wajapan kwa ujumla hawakuwa na jingine ila kuabudu maliki chini ya Dini ya Shinto ya Serikali na mfumo wayo wa kifalme. Fundisho la Norinaga Motoori la ‘Usiulize chochote, bali jitiishe kwa uongozi wa kimungu’ lilitawala na kuongoza kufikiri kwa Kijapan. Kufikia 1941 taifa lote lilielekezwa kwenye harakati ya Vita ya Ulimwengu 2 chini ya beramu ya Dini ya Shinto ya Serikali na kwa kujiweka wakfu kwa “kijimungu-binadamu aliye hai.” ‘Japan ni taifa la kimungu,’ watu walidhani, ‘na kamikaze, upepo wa kimungu, utavuma kukiwa na hatari.’ Askari-jeshi na familia zao waliomba dua kwa vijimungu vyao vyenye kulinda ili wafanikiwe katika vita hiyo.
29. Ni nini kilichoongoza kwenye wengi kupoteza imani baada ya Vita ya Ulimwengu 2?
29 Taifa hilo la “kimungu” liliposhindwa katika 1945, chini ya dharuba maradufu za angamizo la kiatomi la Hiroshima na sehemu kubwa ya Nagasaki, Dini ya Shinto ilikabili hatari kubwa. Usiku kucha, Hirohito mtawala wa kimungu aliyedhaniwa kuwa kijimungu kisichoshindika akawa tu maliki wa kibinadamu aliyeshindwa. Imani ya Kijapan ilipondwa-pondwa. Kamikaze ulishindwa kusaidia taifa. Yasema ensaiklopedia Nihon Shukyo Jiten: “Moja ya sababu ilikuwa kukata tamaa kwa taifa kwa sababu ya kusalitiwa. . . . Lililo baya zaidi, ulimwengu wa Dini ya Shinto haukutoa maelezo ya hali ya juu ya kidini wala yanayofaa juu ya shaka zilizotokana na [kushindwa]. Kwa hiyo, itikio la kidini la haraka ya kuwa ‘Hakuna mungu wala Buddha’ likawa ndio mtindo wa ujumla.”
Njia Inayoongoza Kwenye Upatano wa Kweli
30. (a) Ni somo gani tunaloweza kujifunza kutokana na yaliyopata Dini ya Shinto katika Vita ya Ulimwengu 2? (b) Kwa nini ni jambo muhimu kutumia nguvu zetu za kufikiri kuhusiana na ibada yetu?
30 Mwendo ambao Dini ya Shinto ya Serikali ilifuata wakazia uhitaji kwa kila mtu mmoja mmoja kuchunguza imani za kimapokeo anazoshikilia. Huenda wafuasi wa Dini ya Shinto wakawa walitafuta njia ya upatano pamoja na majirani wao Wajapan walipounga mkono hatua za kijeshi. Bila shaka, hilo halikuchangia upatano wa ulimwenguni pote, na wachuma riziki na vijana wao wakiwa wamekwisha kuuawa katika pigano, wala halikuleta upatano nchini mwao. Kabla hatujaweka wakfu maisha zetu kwa yeyote, ni lazima tuhakikishe ni kwa nani na ni kwa kusudi gani tunajitoa wenyewe. “Mimi nawasihi nyinyi,” akasema mwalimu Mkristo kwa Waroma ambao hapo mbele walikuwa wamejitoa wakiwa na bidii kwa ibada ya maliki, “mtoe miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, yenye kukubalika kwa Mungu, utumishi mtakatifu pamoja na nguvu zenu za kufikiri.” Sawa na ambavyo Wakristo Waroma walipaswa kutumia nguvu yao ya kufikiri ili kuchagua watajiweka wakfu kwa nani, ni muhimu kwetu kutumia nguvu yetu ya kufikiri katika kuamua ni nani tunapaswa kuabudu.—Warumi 12:1, 2, New World Translation.
31. (a) Ni nini kimeridhisha waumini walio wengi wa Dini ya Shinto? (b) Ni swali gani linalohitaji kujibiwa?
31 Kwa wafuasi wa Dini ya Shinto kwa ujumla, jambo la maana katika dini yao halikuwa kutambua waziwazi kijimungu kimoja. “Kwa makabwela,” asema Hidenori Tsuji, mfunzi wa historia ya kidini ya Kijapan, “vijimungu au Mabuddha vilikuwa ni mamoja tu. Viwe ni vijimungu au Mabuddha, maadamu vilisikia miito ya kusihi ili kupata zao zuri, kuondolewa maradhi, na kupata usalama wa familia, hayo yaliridhisha watu.” Lakini je! hilo liliwaongoza kwa Mungu wa kweli na baraka yake? Jibu la historia liko wazi.
32. Sura yetu ifuatayo itazungumza juu ya nini?
32 Katika jitihada ya kutafuta mungu fulani, kwa kuweka imani zao juu ya msingi wa ngano, wafuasi wa Dini ya Shinto waligeuza binadamu hoi, maliki wao, kuwa kijimungu, kilichoitwa ati mzao wa kijimungu-kike-jua Amaterasu Omikami. Na hali, maelfu ya miaka kabla ya Dini ya Shinto kuanza, Mungu wa kweli alikuwa amejifunua mwenyewe kwa mwanamume wa imani wa mlango wa Shemu katika Mesopotamia. Sura yetu ifuatayo itazungumza juu ya tukio hilo la maana sana na matokeo yalo.
[Maelezo ya Chini]
a Katika Japan majengo ya kidini ya wafuasi wa Dini ya Shinto huonwa kuwa vihekalu na yale ya wafuasi wa Dini ya Buddha, kuwa mahekalu.
[Sanduku katika ukurasa wa 191]
Kijimungu-Kike-Jua Katika Ngano ya Dini ya Shinto
Ngano ya Dini ya Shinto husema kwamba zamani za kale, kijimungu Izanagi “kiliosha jicho lacho la kushoto, na kwa hiyo kikazaa kijimungu-kike kikuu Amaterasu, kijimungu-kike cha Jua.” Baadaye, Susanoo, kijimungu cha nyanda za bahari, kilikiogopesha sana Amaterasu hivi kwamba “kikajificha katika pango la Mbingu lenye miamba, na kuziba mwingilio kwa jiwe kubwa. Ulimwengu ulitumbukizwa ndani ya giza.” Kwa hiyo vijimungu vikabuni mpango wa kukiondoa Amaterasu nje ya pango hilo. Vilikusanya jogoo wenye kuwika wanaoshangilia mapambazuko na vikafanyiza kioo kikubwa. Kwenye misakaki, vilining’iniza johari na vibendera vya kitambaa. Halafu kijimungu-kike Ama no Uzume kilianza kucheza dansi na kudunda-dunda kiogeo kwa nyayo zacho. Katika kucheza dansi iliyokiondosha fikira zote, kikavua nguo zacho, na vijimiungu vikaangua kicheko. Utendaji wote huo uliamsha udadisi wa Amaterasu, kilichotazama nje na kujiona kwenye kioo. Sura yacho katika kioo ilikivuta kitoke nje ya pango hilo, ndipo kijimungu cha Kani kikakishika mkono na kukitoa nje. “Kwa mara nyingine tena ulimwengu ukanurishwa na miale ya kijimungu-kike-Jua.”—New Larousse Encyclopedia of Mythology.—Linganisha Mwanzo 1:3-5, 14-19; Zaburi 74:16, 17; 104:19-23.
[Sanduku katika ukurasa wa 193]
Dini ya Shinto—Dini ya Misherehekeo
Mwaka wa Kijapan umejaa misherehekeo ya kidini, au matsuri. Ifuatayo ni baadhi ya ile mikubwa-mikubwa:
◼ Sho-gatsu, au Msherehekeo wa Mwaka Mpya, Januari 1-3.
◼ Setsubun, kutupa maharage ndani na nje ya nyumba, huku kelele ikipigwa, “Maibilisi nje, bahati njema ndani”; Februari 3.
◼ Hina Matsuri, au Msherehekeo wa Wanasesere kwa ajili ya wasichana, hufanywa Machi 3. Jukwaa la wanasesere, likiwakilisha nyumba ya kifalme ya kale, huonyeshwa.
◼ Msherehekeo wa Wavulana, mnamo Mei 5; Koinobori (vibendera mfano wa samaki vikifananisha nguvu) hupeperushwa kwenye milingoti.
◼ Tsukimi, kustaajabia mwezi mpevu wa vuli ya kati, na wakati ule ule kutoa sadaka vitumbua na malimbuko ya mazao.
◼ Kanname-sai, au maliki kutoa sadaka malimbuko mapya ya mchele, katika Oktoba.
◼ Niiname-sai huadhimishwa na familia ya kifalme katika Novemba, wakati malimbuko ya mchele yanapoonjwa na maliki, ambaye husimamia akiwa kuhani mkuu wa Dini ya Shinto ya Kifalme.
◼ Shichi-go-san, maana yake “saba-tano-tatu,” huadhimishwa na familia za Dini ya Shinto mnamo Novemba 15. Saba, tano, na tatu huonwa kuwa miaka ya maana ya badiliko; watoto waliovaa kimono (majoho) yenye rangi nyingi huzuru kihekalu cha familia.
◼ Misherehekeo mingi ya Dini ya Buddha huadhimishwa pia, kutia ndani siku ya kuzaliwa ya Buddha, mnamo Aprili 8, na Msherehekeo wa Obon, Julai 15, ambao humalizika kwa taa zikielea kwenye bahari au kijito “ili kuongoza roho za wazazi wa kale waliokufa zirejee kwenye ulimwengu ule mwingine.”
[Picha katika ukurasa wa 188]
Mjitoaji kwa Dini ya Shinto akiviomba vijimungu hisani
[Picha katika ukurasa wa 189]
Dini ya Shinto, ‘Njia ya Vijimungu’
[Picha katika ukurasa wa 190]
Mlima wote, kama vile Fuji, nyakati nyingine huonwa kuwa shintai, au kitu cha kuabudiwa
[Picha katika ukurasa wa 195]
Wafuasi wa Dini ya Shinto wamebeba mikoshi, au kihekalu kinachochukulika, na juu, wamevaa majani ya mholihoki (aoi) wakati wa Msherehekeo wa Aoi katika Kyoto
[Picha katika ukurasa wa 196]
Kuzungushwa kwa karatasi au katani iliyofungwa kwenye tawi la mti unaokuwa kijani-kibichi daima hufikiriwa hutakasa binadamu na vitu, na kuwahakikishia usalama
[Picha katika ukurasa wa 197]
Mjapan hana hisi inayopingana kuabudu mbele ya vyote viwili kihekalu cha Dini ya Shinto, kushoto, na pia madhabahu ya Dini ya Buddha
[Picha katika ukurasa wa 198]
Maliki Hirohito (jukwaani) aliabudiwa kuwa mzao wa kijimungu-kike-jua
[Picha katika ukurasa wa 203]
Mwanamke kijana abandika kwenye kihekalu ema, au bamba la mbao la sala alilolinunua