Dolfini Katika Eneo Letu
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA
YEYE hupenda maji ya tropiki yenye ujoto, yasiyo na kina, yenye chumvi au yasiyo na chumvi, yaliyo meusi-meusi au yaliyo maangavu. Yeye hupatikana katika eneo linaloanzia Ghuba ya Bengal ya India kupitia Jamii-Visiwa ya Malay hadi kaskazini mwa Australia.
Lakini, ni watu wachache—hasa Waaustralia, ambao pwani yao ya kaskazini huenda ikawa na idadi kubwa zaidi ya wanyama hao ulimwenguni pote—wamepata kuona au hata kusikia juu ya dolfini wa Irrawaddy. Je, ni jambo la kushangaza? Ndiyo na la.
Katika karne ya 19, mtaalamu wa wanyama John Anderson aliona idadi kubwa ya dolfini wenye rangi ya buluu na kijivu, wenye vichwa mviringo, wasio na mdomo wenye kuchomoza, katika Mto Irrawaddy kule Myanmar (wakati huo iliitwa Burma). Akayaita dolfini wa Irrawaddy.
Sababu Inayofanya Awe Nadra Kuonekana
Dolfini wa Irrawaddy husitawi katika milango ya mito iliyo katika mwambao wenye joto na unyevu, na maeneo ya mito. Mara nyingi makao yao huwa maji yenye matope-matope, mikoko, msitu, mbu wengi na, katika sehemu nyinginezo, hata miongoni mwa mamba—si mazingira yenye kuvutia wanadamu.
Kwa kawaida maji katika maeneo haya pia huwa meusi-meusi, kwa hiyo wakati tu unaweza kumwona dolfini ni aibukapo kifupi juu ya maji ili kupumua. Hata wakati huo, mwili wake hauonekani sana. Sehemu kidogo ya mgongo wake huonekana, na pezi lake la mgongoni ni dogo kwa kulinganisha na mapezi ya dolfini wengine.
Lakini katika sehemu nyinginezo, dolfini wa Irrawaddy huonekana mara nyingi. Wavuvi na wenye kuendesha mashua za mto katika Mto Irrawaddy katika Myanmar, na mito mingine ya Asia iliyo katika eneo la dolfini hao, mara nyingi huwaona wanyama hao wakiwinda na kurukaruka katika sehemu za mto mbali sana na pwani, hata wakichiriza maji kama bubujiko kutoka kwenye midomo yao au kama kisanamu katika bustani yenye maji.
Katika maji ya Australia, dolfini wa Irrawaddy hupatikana kandokando ya pwani ya magharibi, kuzunguka juu ya kontinenti hiyo, na kuelekea chini kwenye pwani ya mashariki. Mara nyingi wao huonekana katika vikundi vyenye dolfini wapunguao 6 lakini mara kwa mara wao waweza kufikia 15. Tofauti na wenzao wa Asia, dolfini wa Australia hawajapata kujulikana kwa kuigiza bubujiko la maji.
Je, Yeye Ni Dolfini?
Dolfini wa Irrawaddy huishi karibu na bara nao huogelea polepole wakilinganishwa na wenzao waishio katika maji yasiyo na matope-matope. Lakini, wanasayansi wamepata ugumu wa kuwachunguza. Makao yao yasiyopendeza ndiyo sababu kuu. Hata hivyo, dolfini wa Irrawaddy wamechunguzwa katika Tangi la Viumbe vya Bahari la Jaya Ancol, katika Djakarta, Indonesia.
Kwa sababu mengi hayajulikani kuhusu dolfini wa Irrawaddy, mpaka hivi karibuni wanabiolojia hawakuwa na uhakika wa mahali pa kuwaainisha katika familia ya nyangumi na dolfini. Kwa wazi, wana mambo mengi yafananayo na dolfini. Lakini, kwa umbo, wala si rangi (wao huwa na rangi ya kijivu hadi nyeusi yenye buluu na kijivu), wao karibu wafanane kabisa na nyangumi wa Aktiki au nyangumi mweupe. Hata shingo yao yenye kupindika isivyo kawaida inafanana sana na ile ya nyangumi mweupe. Kwa hiyo, wao ni nini—je, ni mwenzi aishiye ikweta wa nyangumi mweupe au ni dolfini halisi?
Njia moja ya kujua jambo hilo ni kuchunguza viungo vya mwili wake na jeni zake, na kuona ni upande gani unaoungwa mkono zaidi. Inatukia kwamba uthibitisho unaonyesha dolfini.
Yale Machache Tunayojua
Wanapozaliwa, watoto wa dolfini wa Irrawaddy huwa na urefu upunguao tu meta moja na kuwa na uzani wa kilogramu 12. Wa kiume hukua kufikia meta 2.75, na wa kike, hupungua kidogo tu kufikia kiwango hicho. Wao waweza kuishi kwa miaka 28.
Vitu vilivyopatikana katika tumbo la Irrawaddy waliokufa vyafunua kwamba dolfini hula ngisi, uduvi, kamba, na samaki—hasa wale waishio kwenye sakafu ya bahari au mito. Wanasayansi fulani wafikiria kwamba zoea lisilo la kawaida la dolfini wa Asia kuchiriza maji kutoka kwenye midomo yao huenda ikawa linawasaidia kushika samaki katika maji meusi-meusi.
Kama ilivyo na dolfini wengine, hao dolfini wa Irrawaddy hutoa vidoko vyenye kusikika. Dakt. Peter Arnold, wa Jumba la Makumbusho la Tropical Queensland aliambia Amkeni! kwamba “kulingana na utafiti uliofanywa katika Tangi la Viumbe vya Bahari la Jaya Ancol, dolfini wa Irrawaddy huenda anatumia kidoko ili kupata windo kama ilivyo na dolfini wengine.”
Je, Ana Wakati Ujao?
Wanasayansi hawajui kuna dolfini wangapi wa Irrawaddy katika ulimwengu. Lakini kuna hangaiko lenye kuzidi kwamba wamo hatarini mwa kutoweka. Katika sehemu fulani za Asia ya Kusini-Mashariki, wanapungua, na katika sehemu nyinginezo, hawapatikani tena kamwe.
Mara nyingi hii ni kwa sababu ya ukataji wa miti na uchafuzi ambao hutokana na huo na kujaa matope kwa mito. Katika Australia, eneo kubwa la dolfini wa Irrawaddy halijakaliwa sana na wanadamu. Lakini katika maeneo yenye kuvutia zaidi ya pwani ya mashariki, kujengwa kwa miji na utalii umewaathiri. Dolfini wengine wa Irrawaddy hufa maji katika nyavu, na wengine, hufa katika nyavu za kushikia papa ambazo zimewekwa karibu na ufuo ili kuwakinga waogeleaji. Kuvua kupita kiasi chakula cha dolfini wa Irrawaddy pia kunaathiri idadi yao.
Hata hivyo, tisho kubwa zaidi laweza kuwa ongezeko la vichafuzi ambavyo huingia mitoni na milango-bahari ya mito. Miongoni mwa vichafuzi vibaya zaidi ni kemikali ambazo huelekea kudumu katika mazingira. Hizo ni kemikali ambazo hutumiwa kutengenezea vitu vya elektroni, rangi, mafuta ya kulainisha, rangi za mbao na vyuma, na bidhaa nyingine.
Kwa upande mzuri, katika hati The Action Plan for Australian Cetaceans, ya Shirika la Hifadhi ya Asili ya Australia lasema hivi: “Eneo kubwa la [dolfini wa Irrawaddy] katika Queensland liko katika Hifadhi ya Viumbe vya Bahari ya Great Barrier Reef; kwa hiyo uwezekano wa kusimamiwa kwa dolfini wa Irrawaddy katika maji ya Queensland ni mzuri.”
Katika hatua nyingine ya usimamizi bora, shirika hilo lapendekeza kwamba pamoja na nyangumi mkubwa, nyangumi wenye vichwa vikubwa, na dolfini wenye midomo yenye kuchomoza, dolfini wa Irrawaddy waweza kuwa spishi ya msingi ya kuelekezewa uangalifu katika programu za kujulisha umma kuwahusu. Hiyo itawafaa dolfini wa Irrawaddy—na kutufaa sisi.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Picha: Kwa hisani ya Dakt. Tony Preen