Ni Nyangumi? Ama Ni Dolfini?—La, Ni Wolfini!
Na mleta habari za Amkeni! katika Hawaii
KUZALIWA kwa mnyama katika makao ya wanyama ni tukio la kusisimua nyakati zote. Lakini Mei 15, 1985, ilikuwa siku ya kipekee katika Hifadhi ya Viumbe vya Baharini ya Hawaii.
Mama aliyekuwa akitazamia kuzaa alikuwa dolfini wa Atlantiki ambaye jina lake la Kihawaii Punahele lamaanisha “Rafiki Mpendwa.” Punahele alikuwa amekuwa mkubwa kupita kiasi katika pindi za mwisho za mimba yake. Kwa hiyo tayari wafanyakazi wa hifadhi walikuwa wanahisi kwamba jambo fulani lisilo la kawaida lilikuwa likitendeka. Mashaka yao yakawa ya kweli wakati mtoto wa Punahele alipozaliwa. Aliitwa Kekaimalu. Kekaimalu alikuwa mweusi kidogo kuliko dolfini wengine na pua yake vilevile ilikuwa fupi kuliko kawaida.[1]
Kisha Kekaimalu akafungua kinywa chake.
Dolfini wa Atlantiki apaswa kuwa na meno 88. Lakini Kekaimalu alionyesha meno 66 pekee alipofungua mdomo—na yalikuwa makubwa sana. Ni kitu gani kilikuwa kimetendeka?
Mama ya mtoto huyo aliyezaliwa amekuwa akifanya wonyesho kila siku pamoja na dolfini wengine kadhaa katika wonyesho wa Whaler’s Cove katika Hifadhi ya Viumbe vya Baharini. Mmojapo wenzi wake wa wonyesho alikuwa nyangumi-muuaji wa bandia mwenye umri wa miaka 18, na uzito wa kilo 900.a[3] Baada siku kwisha, watumbuizaji hao wa maji walikuwa wakikubaliwa kuogelea huku na huku bila kuzuiwa katika tangi moja.
Naam, tokeo ambalo halikutazamiwa lilikuwa ni kuzaliwa kwa Kekaimalu—kiumbe ambacho kilikuwa nusu dolfini na nusu nyangumi.[5] Wafanyakazi wa hifadhi hiyo walimpatia kwa furaha mvyauso (kiumbe kilichozaliwa na wanyama wa jamii tofauti) huyo asiye wa kawaida jina “wolfini.” Meno yake 66 yalikuwa tofauti ya jumla ya meno 88 ya mama aliye dolfini na meno 44 ya baba aliye nyangumi. Ingawa rangi yake nyeusi-nyeusi na ukubwa wake ulionyesha urithi wake wa nyangumi, maofisa wa hifadhi hiyo wamfafanua kuwa “mchanganyiko wa kipekee wa wazazi wote wawili.” Mdomo wake wenye kuchongoka unafanana na wa dolfini ila tu unaonekana kuwa mfupi zaidi.[6]
Wolfini mwingine pekee ajulikanaye alizaliwa katika tangi kubwa katika Japani mwaka wa 1981. Kiumbe hicho cha mvyauso alikufa miezi kadhaa baadaye.[7] Je! Kekaimalu angeendelea vema zaidi?
Wolfini huyo aliye mtoto wa kilo 16 alionekana kuwa mwenye afya na kuanza kunyonya kama kawaida. Likiripoti maelezo ya ofisa mmoja wa hifadhi hiyo, gazeti Honolulu Star Bulletin and Advertiser lilisema hivi muda mfupi baada ya Kekaimalu kuzaliwa: “Hakuna tarajio zuri sana la mtoto huyo kuishi hadi ukomavu kama ilivyo na binamu zake wa wazazi wa jamii moja . . . Mara nyingi mivyauso huzaliwa wakiwa wamekufa ama wao husitawisha magonjwa na kufa wakiwa wangali wachanga. Kwa uzuri, . . . Punahele ni mama mwenye ujuzi na mwenye upendo ambaye amelea watoto wengine wawili wa dolfini hadi ukomavu [katika Hifadhi ya Viumbe vya Baharini].” Ofisa huyo alisema hivi: “Yeye ni mama mwenye kubadilikana sana na hali, yeye ni mama mzuri sana.”[8] Sifa ya Punahele kuwa mama mzuri ikathibitishwa kuwa kweli.
Kekaimalu sasa ameishi kwa zaidi ya miaka saba. Akiwa na uzito wa kilo 300, yeye ni mkubwa sana kushinda mama yake aliye dolfini. Na baada ya miaka michache akiwa mtumbuizaji katika Whaler’s Cove, wolfini huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitano, na aliyedhaniwa na watu wengi kuwa tasa, alifanya jambo la ajabu sana mnamo Juni 1990. Yeye mwenyewe akawa mama. “Kwa kawaida watu hudhani kwamba mivyauso ni tasa,” asema Marlee Breese, msimamizi wa jamii ya wanyama wa mamalia katika makao ya Makapuu. “Kumbe Kekaimalu hakuwa tasa.”[9] Kwa tukio baya, mzaliwa wake wa kwanza—robo moja nyangumi na robo tatu dolfini—aliishi kwa muda wa juma tu.
Inaonekana kwamba Kekaimalu hakujua jinsi ya kumnyonyesha mtoto wake. “Sifikiri kwamba hakuweza kumnyonyesha mtoto kwa sababu ya kuwa mvyauso,” asema Breese. Yeye anahisi kwamba inaelekea sana kwamba Kekaimalu hakumnyonyesha mtoto wake kwa sababu alikuwa mchanga na hakujua jinsi ya kumnyonyesha. “Kwa kawaida wanyama hao hufikia ukomavu wa kingono wakiwa na umri wa miaka kati ya 8 hadi 10,” asema Breese. Kekaimalu alikuwa na miaka mitano tu alipomzaa mtoto wake wa kwanza.[10]
Mnamo Novemba 8, 1991, Kekaimalu alimzaa mtoto wa pili. Lakini wakati huu wafanyakazi walikuwa tayari. Baada ya kutazamwa kwa muda wa saa 24 ili kuona kama mama huyo aliye wolfini angechukua hatua ya kumnyonyesha mtoto yeye mwenyewe, waliingilia kutatua mambo. Kekaimalu alinyanyuliwa juu ya maji kwa kamba, na maziwa yalikamuliwa kupitia pampu ya kukamua maziwa kwa mwanamke. ‘Ilikuwa muhimu hasa apate maziwa ya kwanza ya mama,’ asema Breese, ‘kwa sababu hayo huingiza viuaji-sumu katika mwili.’[10A] Kwa muda wa majuma, wafanya kazi hao walikuwa wakimkama mama huyo mara moja kwa siku bila kukosa, wakipata karibu lita moja ya maziwa kutoka kwake.[11]
Kisha maziwa ya wolfini huyo yalichanganywa na mchanganyiko wa maziwa uliotengenezwa na binadamu. Mchanganyiko huo ulifanyizwa katika Florida, U.S.A., katika jitihada za kuokoa dolfini mmoja aliyekuwa amekwama ufuoni. Kutokea saa kumi na mbili ya asubuhi hadi saa sita ya usiku, mtoto huyo wa wolfini alikuwa akilishwa kupitia mrija wa tumbo kila baada ya muda wa saa mbili na nusu. Alikuwa akiongeza uzito wa karibu nusu-kilo kila siku. Katika vipindi ambavyo halishwi, nyanya, mama, na mtoto walikuwa wakichezacheza pamoja katika tangi kubwa.
Kufikia wakati wa kuandika habari hii, kuna matazamio mazuri kwamba mjukuu wa pekee ajulikanaye wa mchanganyiko wa nyangumi na dolfini ataendelea kuishi.[12] Labda siku moja atafuata desturi ya familia yao ya kutumbuiza katika wonyesho wa Whaler’s Cove. Kwa wakati uo huo, ulimwengu umeona mara nyingine tena uwezo wa ajabu wa tofauti mbalimbali ambazo Mungu ameumba katika uumbaji wake.
[Maelezo ya Chini]
a Kulingana na kichapo cha Hifadhi ya Viumbe vya Baharini, “nyangumi-muuaji wa bandia wamepata jina lao kutokana na tafsiri ya neno kwa neno ya jina lao la kisayansi (Pseudo = bandia, Orca = aina ya nyangumi) na wana uhusiano wa karibu na wale nyangumi-wauaji wanaojulikana sana ambao huonyeshwa katika matangi mengi makubwa.”
[Picha katika ukurasa wa 15]
Wolfini akiwa na wenzake dolfini
[Hisani]
Monte Costa, Sea Life Park Hawaii