Jina la Mungu Lapamba Usanifuujenzi wa Cheki
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Jamhuri ya Cheki
KATIKA sehemu nyingi za ulimwengu, jina Yehova huhusianishwa na Mashahidi wa Yehova bila kuhusisha wengine. Huenda utashangaa kujua kwamba katika Jamhuri ya Cheki, mapambo katika baadhi ya majumba ya kihistoria hutia ndani ile Tetragramatoni, zile herufi nne za Kiebrania (יהוה) ambazo zinafanyiza jina la kimungu, Yehova.
Labda kielelezo kinachojulikana zaidi cha Tetragramatoni ni kile kilicho juu ya daraja liitwalo Charles Bridge, lililojengwa katika mwaka wa 1357 kuvuka Mto Vltava ulio maridadi, karibu na mji uitwao Old Town wa Prague. Daraja hili limepambwa pande zote mbili kwa michongo, mchongo mmoja wavutia uangalifu wa karibu kila mtu anayepita. Ni sanamu ya Yesu Kristo akiwa juu ya msalaba, akiwa amezungukwa kwa herufi zenye kumetameta za Kiebrania—kutia ndani ile Tetragramatoni—ambayo inasomeka hivi “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Yehova wa majeshi.”
Msemo huu unaopatikana katika Biblia kwenye Isaya 6:3, ulikujaje kuwa katika sanamu hii? Mwandiko kwenye sehemu ya chini husema kuhusu Myahudi aliyepita hapo siku moja katika mwaka wa 1696, akadaiwa kuwa alisema kwa kukosa staha kuelekea msalaba huo. Kwa sababu ya hili, aliletwa mbele ya Mahakama ya Kukata Rufani ya Kifalme na akahukumiwa kulipa adhabu. Kwa kulipia, alitoa kitanga kilichopakwa dhahabu kwa ajili ya msalaba huo, kikiwa na nukuu lililo juu.
Karibu na hilo kuna Sinagogi liitwalo Old-New na makaburi ya Kiyahudi ya zamani zaidi katika Ulaya. Katika sinagogi hili jukwaa la kiongozi wa waimbaji lina Tetragramatoni katika fremu ya fedha. Lakini si katika majengo ya Kiyahudi tu ambapo Tetragramatoni yapatikana. Kusini-Mashariki mwa Prague, kwenye kilima chenye mawemawe chenye kuelekea Mto Sázava, kuna kasri ya enzi za kati ya Český Šternberk. Juu ya madhabahu ya kanisa la kasri hiyo kuna herufi nne za dhahabu—ile Tetragramatoni. Herufi hizo zaonekana kana kwamba zaelea hewani, kwa vile zimening’inizwa kwa waya. Nyuma yake nuru humulika—lakini si kutoka kwa taa! Nuru ya anga ambayo haiwezi kuonekana kutoka ndani, hutoa mwanga wa rangi ya waridi juu ya madhabahu hiyo nyeupe, ambayo juu yake ile Tetragramatoni huning’inia.
Tetragramatoni pia huonekana katika picha zilizochorwa ukutani chokaa ikiwa ingali mbichi katika majengo mengine ya Cheki. Hizo hutoa ushuhuda zaidi kwamba zamani wengi katika sehemu hii walijua jina la Mungu. Leo, katika Jamhuri ya Cheki na katika nchi nyingine zaidi ya 200, Mashahidi wa Yehova wanafurahia kujua jina hilo la kimungu na kuwafunza wengine kulihusu. (Isaya 43:10-12) Zaidi ya hilo, kitabu cha Biblia cha Isaya husema kuhusu wakati ambapo jina la Mungu—pamoja na sifa, kusudi, na matendo yake—‘yatajulikana katika dunia yote.’—Isaya 12:4, 5.