Safari Yangu Ndefu Kutoka Katika Uhai na Kifo Katika Kambodia
KAMA ILIVYOSIMULIWA NA WATHANA MEAS
ULIKUWA mwaka wa 1974, nilikuwa nikipigana na jeshi la Khmer Rouge katika Kambodia. Nilikuwa ofisa katika jeshi la Kambodia. Katika pigano moja tuliteka askari-jeshi mmoja wa Khmer Rouge. Jambo aliloniambia kuhusu mipango ya Pol Pot kwa ajili ya wakati ujao lilibadili maisha yangu na kunifanya nianze safari ndefu, kihalisi na kiroho pia.a
Acheni niwapeleke mwanzoni mwa safari yangu ndefu yenye matukio mengi. Nilizaliwa katika mwaka wa 1945, katika Phnom Penh, ambayo kwa lugha ya Khmer yajulikana kama Kampuchea (Kambodia). Hatimaye mama yangu alikuwa na wadhifa wa pekee katika kikosi cha polisi wa siri. Alikuwa mwakilishi wa pekee wa Mkuu Norodom Sihanouk, kiongozi wa nchi. Kwa kuwa alipewa haki ya kunitunza na ratiba yake ilikuwa yenye shughuli nyingi, aliwajibika kuniacha katika hekalu la Wabudha ili nielimishwe.
Malezi Yangu ya Kibudha
Nilikuwa na umri wa miaka minane nilipoenda kuishi na mtawa mkuu wa kiume wa dini ya Buddha. Kutoka mwaka huo mpaka mwaka wa 1969, niligawa matumizi ya wakati wangu kati ya hekaluni na nyumbani. Mtawa wa kiume niliyemtumikia alikuwa Chuon Nat, aliyekuwa na mamlaka kuu zaidi ya Kibudha katika Kambodia wakati huo. Kwa muda fulani, nilifanya kazi nikiwa mwandishi wake na kumsaidia katika kutafsiri kitabu kitakatifu cha Kibudha “The Three Baskets” (Tipitaka, au kwa Kisanskrit Tripitaka) kutoka katika lugha ya kale ya Kihindi hadi katika lugha ya Kambodia.
Niliitwa kuwa mtawa wa kiume katika mwaka wa 1964 na kuendelea hadi mwaka wa 1969. Katika kipindi hiki kulikuwa na maswali mengi ambayo yalinisumbua, kama vile, Kwa nini kuna kuteseka kwingi mno ulimwenguni, na kulianzaje? Niliona watu wakijaribu katika njia nyingi kupendeza miungu yao, lakini hawakujua jinsi ambavyo miungu yao ingetatua matatizo yao. Wala mimi wala watawa wengine wa kiume hatukuweza kupata jibu lenye kuridhisha katika maandishi ya Kibudha. Nilivunjika moyo sana hivi kwamba niliamua kuondoka katika hekalu hilo, nikaacha kutumikia nikiwa mtawa.
Mwishowe, katika mwaka wa 1971, nilijiunga na jeshi la Kambodia. Nilipelekwa Vietnam karibu mwaka wa 1971, na kwa sababu ya elimu yangu, nilipandishwa cheo kuwa luteni kanali nikapewa mgawo wa kutumikia katika jeshi la msituni. Tulikuwa tukipigana dhidi ya Wakomunisti wa Khmer Rouge na majeshi ya Vietcong.
Vita na Mabadiliko Katika Kambodia
Nikawa askari-jeshi mwenye uzoefu aliyeshupazwa moyo na vita. Nilizoea kuona kifo karibu kila siku. Mimi binafsi nilishiriki katika mapigano 157. Wakati mmoja, katikati ya msitu, tulizingirwa kwa zaidi ya mwezi mmoja na jeshi la Khmer Rouge. Zaidi ya wanaume 700 walikufa. Tulibaki na karibu waokokaji 15—nilikuwa mmoja wao, na nilijeruhiwa. Lakini niliokoka.
Katika pindi nyingine, katika mwaka wa 1974, tuliteka askari-jeshi wa Khmer Rouge. Nilipokuwa nikimhoji, aliniambia kwamba Pol Pot alipanga kuwaangamiza maofisa wote wa serikali wa hapo awali, kutia ndani wale waliokuwa katika jeshi. Aliniambia niache kila kitu na kutoroka. Alisema: “Endelea kubadili jina lako. Usiruhusu mtu yeyote ajue wewe ni nani. Tenda kama mtu asiye na ujuzi na asiyeelimika. Usimwambie mtu yeyote kuhusu maisha yako ya wakati uliopita.” Baada ya kumwachilia arudi nyumbani kwake, onyo hilo lilibaki akilini mwangu.
Sisi askari-jeshi tuliambiwa kwamba tulipigania nchi yetu, na bado, tuliwaua watu wa Kambodia. Kikundi kidogo cha Kikomunisti cha Khmer Rouge, kilichokuwa kikitafuta mamlaka, kilitoka miongoni mwa watu wetu. Kwa hakika, wengi wa wakazi milioni tisa wa Kambodia ni Wakhmer, ijapokuwa wengi wao si wa Khmer Rouge. Sikuelewa jambo hili. Tuliwaua wakulima wasio na hatia wasiokuwa na bunduki na ambao hawakuwa na upendezi wowote katika vita.
Sikuzote kurudi kutoka kwenye pigano kulikuwa jambo la kuhuzunisha sana. Wake na watoto wangekuwako, wakingojea kwa wasiwasi kuona ikiwa mume au baba angerudi. Nilihitaji kuwaambia wengi wao kwamba mshiriki wa familia yao alikuwa ameuawa. Katika mambo haya yote, uelewevu wangu wa Ubudha haukuniandalia faraja yoyote.
Sasa mimi hufikiri juu ya wakati uliopita kuhusu jinsi mambo yalivyobadilika katika Kambodia. Kabla ya mwaka wa 1970, kulikuwa na amani ya kiasi na usalama. Watu wengi hawakuwa na bunduki; ilikuwa kinyume cha sheria ikiwa hukuwa na leseni. Kulikuwa na uhalifu mdogo sana, au wizi. Lakini baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe kuanza, pamoja na uasi wa Pol Pot na jeshi lake, kila kitu kilibadilika. Bunduki zilikuwa kila mahali. Hata vijana wenye umri wa miaka 12 na 13 walikuwa wakizoezwa kwa ajili ya utumishi wa kijeshi, wakijifunza namna ya kupiga risasi na kuua. Watu wa Pol Pot hata walisadikisha watoto fulani wawaue wazazi wao. Askari-jeshi wangewaambia watoto, “Ikiwa unapenda nchi yako, lazima uwachukie adui zako. Ikiwa wazazi wako wanafanya kazi katika serikali, wao ni adui zako na lazima uwaue—au wewe uuawe.”
Pol Pot na Utakaso
Katika mwaka wa 1975, Pol Pot alishinda vita na Kambodia ikawa taifa la Kikomunisti. Pol Pot akaanza kuwaangamiza wanafunzi wote, walimu, maofisa wa serikali, na mtu yeyote aliyekuwa ameelimika. Ikiwa ulivalia miwani, ungeweza kuuawa kwa sababu ilidhaniwa kwamba ulikuwa umeelimika! Mfumo wa utawala wa Pol Pot uliwalazimisha watu wengi watoke majijini na mijini na kuwahamisha mashambani ili kufanya kazi wakiwa wakulima. Kila mtu alipaswa kuvalia kwa mtindo uleule. Tulihitaji kufanya kazi kwa muda wa saa 15 kwa siku, bila chakula cha kutosha, bila dawa, bila mavazi, na kulala kwa muda wa saa 2 au 3 tu. Niliamua kuondoka nchi yangu ya asili kabla haijawa kuchelewa mno.
Nilikumbuka shauri la yule askari-jeshi wa Khmer Rouge. Nilitupa picha zangu zote, hati, na kitu chochote ambacho kingeweza kunitia hatarini. Nilichimba shimo na kuficha baadhi ya hati zangu. Kisha nikasafiri upande wa magharibi kuelekea Thailand. Ilikuwa hatari. Nilihitaji kuepuka vizuizi vya barabarani na kuwa mwangalifu sana wakati wa saa za kafiu, kwa kuwa ni askari-jeshi wa Khmer Rouge pekee, waliokuwa na kibali cha kusafiri.
Nilienda kwenye eneo moja na kuishi na rafiki kwa muda fulani. Kisha askari-jeshi wa Khmer Rouge wakahamisha kila mtu kutoka katika sehemu hiyo hadi kwenye eneo jipya. Wakaanza kuwaua walimu na madaktari. Nilitoroka pamoja na marafiki watatu. Tulijificha msituni na kula tunda lolote tulilopata kwenye miti. Hatimaye, nilifika kwenye kijiji kidogo katika mkoa wa Battambang, ambapo rafiki yangu aliishi. Kwa mshangao, pale nilipata askari wa zamani aliyenishauri jinsi ya kutoroka! Kwa kuwa nilimwachilia huru hapo awali, alinificha ndani ya shimo kwa miezi mitatu. Alimwamuru mtoto fulani aniteremshie chakula lakini asiangalie ndani ya shimo.
Baada ya muda, niliweza kutoroka, na nilimpata mama yangu, shangazi yangu, na dada yangu, ambao pia walikuwa wakitoroka kuelekea mpaka wa Thai. Ulikuwa wakati wenye kunihuzunisha. Mama yangu alikuwa mgonjwa, na hatimaye alikufa katika kambi ya wakimbizi, kutokana na ugonjwa na ukosefu wa chakula. Hata hivyo, nilianza kupata tumaini maishani. Nilijuana na Sopheap Um, mwanamke aliyekuja kuwa mke wangu. Tulitoroka, pamoja na shangazi yangu na dada yangu, ng’ambo ya mpaka wa Thai na kuingia kwenye kambi ya wakimbizi ya Umoja wa Mataifa. Familia yetu iliteseka sana katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Kambodia. Tulipoteza washiriki wa familia 18, kutia ndani ndugu yangu na dada-mkwe wangu.
Maisha Mapya Marekani
Katika kambi ya wakimbizi tulihojiwa kuhusu maisha yetu ya wakati uliopita, na shirika la UM lilijaribu kutafuta mfadhili ili tuweze kwenda Marekani. Hatimaye, mfadhili alipatikana! Katika mwaka wa 1980, tuliwasili St. Paul, Minnesota. Nilijua kwamba ikiwa nitafanya maendeleo katika nchi yangu mpya nilihitaji kujifunza Kiingereza haraka iwezekanavyo. Mfadhili wangu alinipeleka shuleni kwa miezi michache tu, ijapokuwa nilipaswa kujifunza kwa muda mrefu zaidi. Badala ya hivyo, alinitafutia kazi ya bawabu katika hoteli. Lakini kwa sababu ya ufahamu wangu mdogo katika lugha ya Kiingereza, kazi hiyo ikawa tamthiliya ya kuchekesha yenye makosa. Mwenye hoteli angeniomba nimletee ngazi, na ningeleta takataka!
Ziara Yenye Kuogopesha
Katika mwaka wa 1984, nilifanya kazi katika zamu ya usiku na kulala wakati wa mchana. Tuliishi katika eneo ambalo lilikuwa na uvutano mwingi kati ya Waasia na weusi. Uhalifu na dawa za kulevya ulikuwa jambo la kawaida. Asubuhi moja, mke wangu aliniamsha saa nne asubuhi kuniambia kwamba palikuwa na mwanamume mweusi mlangoni. Aliogopa kwa sababu alifikiri mwanamume huyo alikuja kutuibia. Nilichungulia kupitia mlango, na kulikuwa na mwanamume mweusi aliyevalia vizuri akiwa na mkoba, na mwanamume mzungu alikuwa pamoja naye. Sikuona kasoro yoyote.
Nilimwuliza ni nini alichokuwa akiuza. Akanionyesha nakala za magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! Sikuelewa jambo lolote. Nilijaribu kuyakataa kwa sababu miezi kadhaa iliyotangulia, nilidanganywa kulipa dola 165 kwa seti ya vitabu vitano kutoka kwa mwuzaji Mprotestanti. Hata hivyo, yule mwanamume mweusi alinionyesha vielezi katika magazeti. Picha hizo zilipendeza na zilikuwa maridadi! Na mwanamume huyo alikuwa na tabasamu kubwa sana, ya kirafiki. Kwa hiyo nilichangia dola moja na kuyachukua.
Karibu majuma mawili baadaye, alirudi na kuniuliza ikiwa nilikuwa na Biblia ya lugha ya Kambodia. Kwa kweli, nilikuwa na moja ambayo niliipata kwenye kanisa la Nazarene, ingawa sikuielewa. Lakini nilivutiwa kuona watu wawili wa jamii tofauti wakija mlangoni pangu. Kisha aliniuliza, “Je, ungependa kujifunza Kiingereza?” Bila shaka nilipenda, lakini nilieleza kwamba sikuwa na pesa za kugharimia masomo. Aliniambia kwamba angenifundisha bila malipo, akitumia kichapo chenye msingi wa Biblia. Hata ingawa sikujua aliwakilisha dini gani, nilijiambia, ‘Angalau sihitaji kulipa, na nitajifunza kusoma na kuandika Kiingereza.’
Kujifunza Kiingereza na Biblia
Ilikuwa hatua ya polepole. Angenionyesha kitabu cha kwanza cha Biblia, Mwanzo, na kisha ningekitamka kwa lugha ya Kambodia, “Lo ca bat.” Angesema, “Biblia,” na ningesema, “Compee.” Nilianza kufanya maendeleo, na nilichochewa. Nilikuwa nikibeba kazini kamusi yangu ya Kiingereza na lugha ya Kambodia, gazeti la Mnara wa Mlinzi, Biblia ya Tafsiri ya Ulimwengu Mpya, na Biblia yangu ya lugha ya Kambodia. Wakati wangu wa mapumziko, nilichunguza na kujifunza Kiingereza, neno kwa neno, kwa kulinganisha vichapo hivyo. Hatua hii ya polepole, pamoja na masomo ya kila juma, ilichukua zaidi ya miaka mitatu. Lakini, mwishowe, ningeweza kusoma Kiingereza!
Bado mke wangu aliendelea kuhudhuria ibada katika hekalu la Wabudha, na angeweka chakula kando kwa ajili ya wazazi wa kale waliokufa. Bila shaka, wanufaikaji pekee wa chakula hiki walikuwa nzi! Nilikuwa na mazoea mabaya yaliyopenya sana ambayo niliyaanza wakati nilipokuwa jeshini na katika Ubudha. Nilipokuwa mtawa wa kiume, watu walizoea kuleta sadaka, kutia ndani sigareti. Waliamini kwamba ikiwa mtawa alivuta sigareti, ilikuwa kana kwamba wazazi wao waliokufa ndio waliovuta. Hivyo, nikawa mhasiriwa wa uraibu wa nikotini. Ndipo, pia, katika jeshi nilikunywa kupita kiasi na kuvuta kasumba ili kunipa ujasiri kwa ajili ya mapigano. Hivyo, nilipoanza kujifunza Biblia, nilihitaji kufanya mabadiliko mengi sana. Wakati huo ndipo nilipotambua kwamba sala ni msaada mkubwa. Kwa muda wa miezi michache, nilishinda mazoea yangu mabaya. Jinsi jambo hilo lilivyowafurahisha washiriki wengine wa familia yangu!
Nilibatizwa kuwa Shahidi katika mwaka wa 1989, katika Minnesota. Karibu wakati huo nilifahamu kwamba kulikuwa na kikundi cha Mashahidi kilichosema lugha ya Kambodia na pia idadi kubwa ya watu wa Kambodia katika Long Beach, California. Baada ya kuzungumzia jambo hili pamoja na mke wangu, tuliamua kuhamia Long Beach. Lilikuwa badiliko lenye maana sana! Dada yangu alibatizwa kwanza, kisha shangazi yangu (ambaye sasa ana umri wa miaka 85) na mke wangu. Watoto wangu watatu walifuata baadaye. Hatimaye, dada yangu aliolewa na Shahidi, ambaye sasa hutumikia akiwa mzee katika kutaniko.
Huku Marekani, tumepatwa na majaribu mengi. Tumepatwa na magumu makubwa sana ya kiuchumi na mengine ya afya, lakini kwa kushikamana na kanuni za Biblia, tumedumisha itibari yetu katika Yehova. Amebariki jitihada zangu katika shamba la kiroho. Katika mwaka wa 1992, nilipendekezwa kutumikia nikiwa mtumishi wa huduma katika kutaniko, na katika mwaka wa 1995, nikawa mzee hapa katika Long Beach.
Kwa sasa, safari ndefu iliyoanza nilipokuwa mtawa wa Buddha kisha nikiwa ofisa kwenye nyanja za mapigano za Kambodia iliyokumbwa na vita imemalizika kwa amani na furaha katika nyumba na nchi yetu mpya. Na tuna imani yetu tuliyopata karibuni katika Yehova Mungu na Kristo Yesu. Inanihuzunisha kujua kwamba bado watu wanauana katika Kambodia. Sababu iliyo kubwa hata zaidi kwa familia yangu nami kungojea na kutangaza ulimwengu mpya ulioahidiwa, ambapo vita vyote vitakwisha na watu wote watawapenda kikweli majirani wao kama wao wenyewe!—Isaya 2:2-4; Mathayo 22:37-39; Ufunuo 21:1-4.
[Maelezo ya Chini]
a Wakati huo Pol Pot ndiye aliyekuwa kiongozi wa Kikomunisti wa jeshi la Khmer Rouge, ambalo lilikuwa limeshinda vita na kuchukua mamlaka Kambodia.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 16]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
VIETNAM
LAOS
THAILAND
KAMBODIA
Battambang
Phnom Penh
Miaka nilipokuwa mtawa wa Buddha
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 18]
Nikiwa na familia yangu, kwenye Jumba la Ufalme