Halihewa Yenye Mchafuko
KATIKA njia za namna nyingi, wengi wetu hutegemea fueli zenye kaboni. Sisi huendesha magari yanayoendeshwa na fueli ya petroli au dizeli. Sisi hutumia stima inayotokezwa na stesheni za umeme ambazo hutumia makaa ya mawe, gesi asili, au mafuta. Sisi huwasha kuni, makaa, gesi asili, na makaa ya mawe ili kupikia au kujipasha joto. Utendaji huu wote huongeza kaboni dioksidi kwenye angahewa. Gesi hii hunasa joto kutoka kwa jua.
Pia sisi huongeza gesi nyingine za kuongeza joto kwa angahewa. Oksidi nitrasi huongezwa kutoka kwenye mbolea za naitrojeni zitumiwazo katika kilimo. Methani hutokezwa na shamba la mpunga na mashamba ya kulisha mifugo ya kuuzwa. Klorofluorokaboni (CFC) hutokana na utengenezaji wa povu ya plastiki na kutokana na utengenezaji mwingine wa kiviwanda. CFC hazinasi tu joto lakini pia huharibu eneo la anga ya juu la dunia na tabaka ya ozoni.
Isipokuwa CFC, ambazo sasa zinadhibitiwa, gesi hizi zenye kunasa joto hutokezwa kwenye angahewa kwa viwango vinavyozidi kuongezeka daima. Hii ni kwa sababu, kwa sehemu, idadi ya watu duniani inakua, pamoja na ukuzi wa matumizi ya nishati, utendaji wa kiviwanda, na kilimo. Kulingana na Shirika la Ulinzi wa Kimazingira lililoko Washington, kwa sasa wanadamu hutokeza tani bilioni sita za kaboni dioksidi na gesi nyinginezo za kuongeza joto kwenye angahewa kila mwaka. Gesi hizi za kuongeza joto hazitoweki tu; zaweza kuendelea kukaa katika angahewa kwa miongo kadhaa.
Kwa ujumla wanasayansi wana uhakika kuhusu mambo mawili. Kwanza, katika miongo na karne za karibuni, kiasi cha kaboni dioksidi na gesi nyingine za kuongeza joto katika angahewa kimeongezeka. Pili, kwa miaka mia moja iliyopita, wastani wa halijoto ya uso wa dunia umeongezeka kati ya digrii 0.3 na 0.6 Selsiasi.
Swali lazuka, Je, kuna uhusiano kati ya ongezeko la joto la tufeni pote na ongezeko la polepole lililoanzishwa na binadamu la gesi za kuongeza joto? Wanasayansi fulani husema labda sivyo, wakionyesha kwamba ongezeko katika halijoto huwa ndani ya eneo la badiliko asili na kwamba huenda jua likahusika. Hata hivyo, wataalamu wengi wa tabia ya nchi hukubaliana na maneno ya ripoti ya Shirika baina ya Serikali kuhusu Badiliko la Tabia ya Nchi. Shirika hili lilitaarifu kwamba ongezeko katika halijoto “halielekei kuwa ni chanzo cha kiasili kabisa” na kwamba “kwa kufikiria uthibitisho wote, yaelekea kwamba kuna uvutano wa kibinadamu uonekanao juu ya tabia ya nchi ya tufeni pote.” Na bado, ukosefu wa uhakika wabaki kuhusu kama shughuli za kibinadamu zinaongeza joto kwenye sayari—hasa kuhusu jinsi ulimwengu unavyoweza kuwa na joto kwa wepesi katika karne ya 21 na yawezayo kuwa matokeo kamili.
Ukosefu wa Uhakika Husababisha Mjadala
Wakati wataalamu wa tabia ya nchi watabiripo tokeo la wakati ujao la ongezeko la joto la tufeni pote, wao hutegemea climate model programu iendeshwayo na kompyuta zilizo na mwendo wa haraka zaidi na zenye nguvu zaidi ulimwenguni. Hata hivyo, tabia ya nchi ya dunia huamuliwa na utendeano ulio tata zaidi wa mzingo wa dunia, angahewa, bahari, barafu, sura za nchi, na jua. Kukiwa na mambo mengi jinsi hiyo yanayoathiri tabia ya nchi ya dunia kwa kiwango kikubwa hivyo, haiwezekani kwa kompyuta yoyote kutabiri kwa uhakika kile kitakachotukia miaka 50 au 100 kuanzia sasa. Hivi karibuni gazeti Science lilitaarifu hivi: “Wataalamu wengi wa tabia ya nchi wanatahadharisha kwamba bado haijawa dhahiri kwamba shughuli za kibinadamu zimeanza kuongeza joto kwenye sayari—au jinsi ongezeko la joto litakavyokuwa mbaya litokeapo.”
Ukosefu wa uhakika hufanya iwe rahisi kukana kwamba kuna tisho lolote. Wanasayansi ambao hutilia shaka ongezeko la joto la tufeni pote, pamoja na viwanda vyenye nguvu ambavyo vina upendezi wa kiuchumi katika kudumisha hali kama ilivyo, wanatoa hoja kwamba ujuzi wa kisasa hauthibitishi uhalali wa iwezayo kuwa hatua ya marekebisho iliyo ghali. Hata hivyo, wanasema kwamba, huenda wakati ujao usiwe mbaya kama watu wengine wafikirivyo.
Wanamazingira wanapinga kwa kusema kwamba ukosefu wa uhakika wa kisayansi haupaswi kuliwaza wachanganuaji wa sera waridhike kupita kiasi na kukosa kuona hatari. Ingawa ni kweli kwamba tabia ya nchi ijayo huenda isiwe mbaya kama wengine wahofuvyo, yawezekana pia kwamba hali ingeweza kuwa mbaya hata zaidi! Isitoshe, wao husababu kwamba kutojua kwa uhakika kitakachotukia wakati ujao hakumaanishi kwamba jambo lolote halipasi kufanywa ili kupunguza hatari. Kwa kielelezo, watu wanaoacha kuvuta sigareti, hawadai kwanza kupewa ithibati ya kisayansi kwamba ikiwa wataendelea kuvuta sigareti, bila shaka watapatwa na kansa ya mapafu miaka 30 au 40 baadaye. Wao huacha kwa sababu wanatambua hatari na wanataka kuipunguza au kuiondoa.
Ni Nini Linalofanywa?
Kwa kuwa kuna mjadala mwingi kuhusu mweneo wa tatizo la ongezeko la joto la tufeni pote—na hata kama tatizo lenyewe liko kwa kweli—haishangazi kwamba kuna maoni tofauti kuhusu jambo la kufanya. Kwa miaka kadhaa vikundi vya kimazingira vimeendeleza matumizi yaliyoenea pote ya vyanzo vya nishati visivyo na uchafuzi. Nguvu za umeme zaweza kutengenezwa kutoka kwa jua, upepo, mito, na mabwawa ya mvuke na maji moto yaliyo chini ya ardhi.
Wanamazingira pia wamehimiza serikali zipitishe sheria za kupunguza utokezaji wa gesi zenye kunasa joto. Serikali zimeitikia kwa kutia sahihi mikataba. Mathalani, katika mwaka wa 1992, kwenye Mkutano wa Dunia katika Rio de Janeiro, Brazili, wawakilishi wa karibu nchi 150 walitia sahihi mkataba wakithibitisha uwajibikaji wao wa kupunguza utokezaji wa gesi za kuongeza joto, hasa kaboni dioksidi. Mradi ulikuwa kwamba kufikia mwaka wa 2000, utokezwaji wa gesi za kuongeza joto kutoka kwa nchi zilizositawi ungepunguzwa kufikia viwango vya mwaka wa 1990. Ingawa nchi chache zimefanya maendeleo katika upande huu, nchi nyingi zilizo tajiri hata hazijakaribia kutimiza kiapo chao kidogo. Badala ya kupunguza, mataifa mengi yanatokeza gesi nyingi zaidi za kuongeza joto kuliko wakati wowote! Kwa kielelezo, katika Marekani, inafikiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2000, utokezwaji wa kaboni dioksidi waelekea kuongezeka kwa asilimia 11 zaidi ya ulivyokuwa katika mwaka wa 1990.
Hivi karibuni zaidi, kumekuwako hatua za “kutekelezwa kwa nguvu” kwa miafaka ya kimataifa. Badala ya kufanya upunguzaji kuwa jambo la hiari kama lilivyokuwa katika makubaliano ya mwaka wa 1992, miito inatolewa kuweka miradi ya lazima inayohusu kutokezwa kwa gesi za kuongeza joto.
Gharama ya Badiliko
Viongozi wa kisiasa hutamani sana kuonwa kuwa marafiki wa dunia. Hata hivyo, wao pia wanaangalia kwa makini matokeo ambayo badiliko laweza kuleta kwa uchumi. Kwa kuwa, kulingana na gazeti The Economist, asilimia 90 ya ulimwengu hutegemea fueli zenye kaboni kwa ajili ya nishati, kuacha kuzitumia kungeleta mabadiliko makubwa; na gharama ya badiliko hilo inajadiliwa kwa ukali.
Ingegharimu kiasi gani kupunguza kutokezwa kwa gesi za kuongeza joto kufikia mwaka wa 2010 kwa kiwango cha asilimia 10 chini ya ilivyokuwa katika mwaka wa 1990? Jibu la swali hilo lategemea utakayemwuliza. Fikiria maoni katika Marekani, nchi ambayo hutokeza gesi za kuongeza joto zaidi katika angahewa kuliko nchi nyingine yoyote. Washauri mabingwa wa viwanda wanaonya kwamba upunguzaji huo ungegharimu uchumi wa Marekani mabilioni ya dola kila mwaka na kusababisha watu 600,000 wakose kazi za kuajiriwa. Kwa kutofautisha, wanamazingira wanasema kwamba kufikia mradi huohuo kungeweza kufanya uchumi kuokoa mabilioni ya dola kila mwaka na kutokeza nafasi mpya za kazi za kuajiriwa 773,000.
Licha ya miito kutoka kwa vikundi vya wanamazingira vinavyotaka hatua ya haraka ichukuliwe, kuna viwanda vyenye nguvu—watengenezaji wa magari, kampuni za mafuta, na watengenezaji makaa ya mawe, tukitaja chache—ambavyo hutumia kiasi kikubwa cha fedha zao na kushawishi kupuuzwa kwa tisho la ongezeko la joto la tufeni pote na kutilia chumvi tokeo la kiuchumi la kuacha matumizi ya fueli za kisukuku.
Mjadala waendelea. Hata hivyo, ikiwa wanadamu wanabadili tabia ya nchi na kutofanya jambo lolote ila kuongea tu, msemo wa kwamba kila mtu huongea juu ya halihewa lakini hakuna mtu afanyaye jambo lolote utakuwa na maana mpya yenye kuogofya.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Itifaki ya Kyoto
Katika Desemba 1997 zaidi ya wajumbe 2,200 kutoka nchi 161 walikutana Kyoto, Japani, ili kujadili mwafaka au itifaki, kufanya jambo fulani kuhusu tisho la ongezeko la joto la tufeni pote. Baada ya zaidi ya juma moja la mazungumzo, wajumbe waliazimia kwamba nchi zilizoendelea zapasa zipunguze utokezaji wa gesi zenye joto kwa wastani wa asilimia 5.2 chini ya viwango vya 1990 kufikia mwaka wa 2012. Adhabu kwa wavunjaji-sheria wa mwafaka huo ingeamuliwa baadaye. Tukidhania kwamba mataifa yote yatashikamana na mkataba huo, upungufu wa asilimia 5.2 utafanyiza tofauti gani? Kwa wazi, kidogo sana. Gazeti Time liliripoti: “Ingechukua upunguzaji wa asilimia 60 ili kupunguza kwa kiwango kinachofaa gesi zenye joto ambazo zimekuwa zikiongezeka katika angahewa tangu mwanzo wa mvuvumko wa kiviwanda.”
[Sanduku/Mchoro katika ukurasa wa 7]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Tokeo la Ongezeko la Joto Latolewa Kielezi
Tokeo la Ongezeko la Joto: Angahewa la dunia kama vioo vya glasi katika kibanda cha kukuzia mimea, hunasa joto la jua. Nuru ya jua hupasha joto dunia, lakini joto litokezwalo—linalobebwa na mnururisho wa miale isiyoonekana—haliwezi kuponyoka angahewa kwa urahisi. Badala ya hivyo, gesi za kuongeza joto huziba mnururisho huo na kurudisha baadhi yake kuelekea dunia, hivyo ikiongeza joto kwa uso wa dunia.
1. Jua
2. Kunaswa kwa mnururisho wa miale isiyoonekana
3. Gesi za kuongeza joto
4. Mnururisho unaotoweka
[Sanduku/Mchoro katika ukurasa wa 8, 9]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Kani Zinazodhibiti Tabia ya Nchi
Ikiwa tutaelewa mjadala wa kisasa kuhusu ongezeko la joto la tufeni pote, twahitaji kuelewa baadhi ya kani zenye kutia kicho ambazo hufanya tabia ya nchi yetu iwe kama ilivyo. Hebu tufikirie mambo fulani ya msingi.
1. Jua—Chanzo cha Joto na Nuru
Uhai katika dunia hutegemea tanuri kubwa sana ya nyukilia tunayoiita jua. Likiwa na ukubwa uzidio dunia milioni moja, jua huandaa ugavi wenye kutegemeka daima wa joto na nuru. Kupungua kwa nishati ya jua kungefunika sayari yetu ndani ya barafu; ongezeko lingeifanya dunia kuwa kikaango chata. Kwa kuwa dunia huzunguka ikiwa katika umbali wa kilometa milioni 150 kutoka kwa jua, hupokea nusu ya sehemu moja ya bilioni ya nishati itokayo kwa jua. Hata hivyo, hiki ni kiasi kifaacho kabisa ili kutokeza tabia ya nchi ambayo inaweza kuruhusu kusitawi kwa uhai.
2. Angahewa—Blanketi Lenye Joto la Dunia
Si jua pekee liamualo halijoto ya dunia; angahewa letu huchangia sehemu ya maana pia. Dunia na mwezi ziko katika umbali sawa kutoka kwa jua, kwa hiyo zote mbili hupokea kiasi cha joto kinachotoshana kutoka kwa jua. Hata hivyo, ingawa halijoto ya wastani ya dunia ni digrii 15 Selsiasi, mwezi una wastani wa mzizimo wa digrii -18 Selsiasi. Kwa nini tofauti hiyo? Dunia ina angahewa; mwezi hauna.
Angahewa letu—nguo ya kufungia ya dunia ya oksijeni, nitrojeni na gesi nyinginezo—huzuia kiasi fulani cha joto la jua na kuachilia kiasi kingine. Mara nyingi utaratibu huu hulinganishwa na kibanda cha kukuzia mimea. Labda kama ujuavyo, kibanda cha kukuzia mimea, ni kibanda kilicho na kuta na paa zilizotengenezwa kwa glasi au plastiki. Nuru ya jua hupenya kwa urahisi na kupasha joto sehemu ya ndani. Wakati huohuo, paa na kuta hufanya joto lisipungue kwa haraka.
Vivyo hivyo, angahewa letu huruhusu nuru ya jua ipenye ndani yake ili kupasha joto uso wa dunia. Kisha dunia, hurudisha nishati hiyo katika angahewa ikiwa mnururisho wa miale isiyoonekana. Mwingi wa mnururisho huu hauendi moja kwa moja kwenye anga kwa sababu gesi fulani katika angahewa hufyonza na kuuelekeza tena kwenye dunia, ikiongeza joto kwa dunia. Utaratibu huu wa kupasha joto huitwa tokeo la ongezeko la joto. Ikiwa angahewa letu halikunasa joto la jua kwa njia hii, dunia ingekuwa bila uhai kama mwezi.
3. Mvuke wa Maji—Gesi ya Kuongeza Joto Iliyo Muhimu Zaidi
Asilimia 99 ya angahewa letu imefanyizwa na gesi mbili; nitrojeni na oksijeni. Ingawa gesi hizi huchangia sehemu ya maana katika mibembeo iliyo tata ambayo hutegemeza uhai duniani, karibu hazichangii moja kwa moja kudhibiti tabia ya nchi. Kazi ya kudhibiti tabia ya nchi hufanywa na asilimia 1 inayobakia ya angahewa letu, gesi hizi za kuongeza na kunasa joto, hutia ndani mvuke wa mvua, kaboni dioksidi, oksidi nitrasi, methani, kloroflourokaboni (CFC), na ozoni.
Gesi ya kuongeza joto iliyo ya maana zaidi—mvuke wa maji—kwa kawaida haifikiriwi kuwa gesi hata kidogo, kwa kuwa tumezoea kufikiria maji yakiwa katika umbo lake la kioevu. Na bado, kila molekuli ya mvuke wa maji katika angahewa imejazwa nishati. Kwa kielelezo, wakati mvuke katika mawingu unapopoa na kugeuka kuwa maji, joto hutokezwa, likisababisha mikondo ya mvuke yenye nguvu. Utaratibu wenye nguvu wa mvuke wa maji katika angahewa letu huchangia sehemu muhimu na iliyo tata katika kuamua halihewa na tabia ya nchi.
4. Kaboni Dioksidi—Muhimu kwa Maisha
Gesi ambayo hutajwa mara nyingi zaidi katika mazungumzo kuhusu ongezeko la joto la tufeni pote ni kaboni dioksidi. Inapotosha kuilaumu kaboni dioksidi kuwa ni kichafuzi tu. Kaboni dioksidi ni kiambato muhimu katika usanidimwanga, utaratibu ambao mimea ya kijani kibichi hujitengenezea chakula. Wanadamu na wanyama huvuta pumzi ya oksijeni na kutoa pumzi ya kaboni dioksidi. Mimea huvuta pumzi ya kaboni dioksidi na kutoa pumzi ya oksijeni. Kwa kweli, ni mojawapo maandalizi ya Muumba ambayo hufanya uhai uwezekane kwenye dunia.a Hata hivyo, kuwa na kaboni dioksidi nyingi kupita kiasi katika angahewa kungekuwa sawa na kuongeza blanketi la ziada juu ya kitanda. Ingeongeza joto.
Kani Nyingi Zilizo Tata
Si jua na angahewa tu zinazoamua tabia ya nchi. Zinazotiwa ndani pia ni bahari na vilele barafu, madini yaliyo ardhini na uoto, mifumikolojia ya dunia, utaratibu mwingi wa biogeochemical, na mbinu za mzingo wa dunia. Uchunguzi wa tabia ya nchi huhusisha karibu sayansi yote ya dunia.
Jua
Angahewa
Mvuke wa maji (H20)
Kaboni dioksidi (CO2)
[Maelezo ya Chini]
a Karibu uhai wote ulio duniani hupata nishati kutokana na vyanzo vya kikaboni, hivyo ukitegemea nuru ya jua moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Hata hivyo, kuna viumbehai wanaositawi ndani ya giza kwenye sakafu ya bahari kwa kupata nishati kutokana na kemikali zisizo na uhai. Badala ya usanidimwanga, viumbehai hawa hutumia utaratibu uitwao chemosynthesis.