Tabia ya Nchi Ijayo
UCHAFUZI wa angahewa letu ni moja tu ya matatizo ya kimazingira ambayo wanadamu wametokeza. Mengine yanatia ndani ukataji-misitu wa kiwango kikubwa, kuharibiwa kwa spishi za wanyama, na uchafuzi wa mito, maziwa, na bahari. Kila moja ya matatizo haya limechanganuliwa kwa uangalifu, na mapendekezo yamefanywa ili kuyarekebisha. Kwa kuwa matatizo haya ni ya tufeni pote, yanahitaji utatuzi wa tufeni pote. Kuna makubaliano ya kiasi kikubwa juu ya matatizo na liwezalo kufanywa ili kuyarekebisha. Mwaka baada ya mwaka, twasikia miito inayodai hatua zichukuliwe. Mwaka baada ya mwaka, ni machache sana hufanywa. Pia mara nyingi wachanganuaji wa sera huombolezea matatizo na kukubali kwamba lazima jambo fulani lifanywe lakini wanaongezea, kwa kweli, “si na sisi, si hivi sasa.”
Katika mwaka wa 1970 kwenye chanzo cha Siku ya Dunia, waandamanaji katika New York City walibeba ishara kubwa. Ishara hiyo ilikuwa na picha ya sayari Dunia ikipiga yowe “Saidia!!” Je, kuna mtu yeyote atakayeitikia ombi hilo? Neno la Mungu huandaa jibu: “Msiwatumainie wakuu, wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake. Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake, siku hiyo mawazo yake yapotea.” (Zaburi 146:3, 4) Kisha mtunga-zaburi aelekeza kwa Muumba, kwa kuwa Yeye peke yake ndiye aliye na nguvu, hekima, na atatatua matatizo yote yaliyo tata yanayokabili jamii ya kibinadamu. Twasoma: “Heri ambaye . . . tumaini lake ni kwa BWANA, Mungu wake, aliyezifanya mbingu na nchi, bahari na vitu vyote vilivyomo.”—Zaburi 146:5, 6.
Ahadi Yenye Upendo ya Muumba
Dunia ni zawadi kutoka kwa Mungu. Aliibuni na kuiumba, pamoja na utaratibu wote ulio tata na wenye kustaajabisha ambao hufanya tabia ya nchi ya dunia ipendeze. (Zaburi 115:15, 16) Biblia hutaarifu: “[Mungu] ameiumba dunia kwa uweza wake, ameuthibitisha ulimwengu kwa hekima yake, na kwa ufahamu wake amezitandika mbingu. Atoapo sauti yake, pana mshindo wa maji mbinguni, naye hupandisha mawingu toka ncha za nchi; huifanyia mvua umeme, huutoa upepo katika hazina zake.”—Yeremia 10:12, 13.
Upendo wa Muumba kwa ajili ya jamii ya kibinadamu ulifafanuliwa na mtume Paulo kwa watu wa Listra la kale. Alisema: “[Mungu] hakujiacha mwenyewe bila ushahidi kwa kuwa alitenda mema, akiwapa nyinyi mvua kutoka mbinguni na majira yenye kuzaa matunda, akijaza mioyo yenu kikamili kwa chakula na uchangamfu.”—Matendo 14:17.
Wakati ujao wa sayari hautegemei jitihada na mikataba ya wanadamu. Kuhusiana na tabia ya nchi, Yule aliye na nguvu za kuidhibiti aliwaahidi watu wake wa kale: “Ndipo nitazinyesha mvua zenu kwa nyakati zake, na nchi itazaa maongeo yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake.” (Mambo ya Walawi 26:4) Karibuni watu watafurahia hali za namna hiyo duniani pote. Kamwe wanadamu watiifu hawataogopa dhoruba ziletazo uharibifu, vibobo, mafuriko, majangwa, au msiba asilia mwingine wowote.
Mawimbi, upepo, na halihewa yote yatapendeza. Watu bado waweza kuzungumza kuhusu halihewa, lakini hawatafanya lolote kuihusu. Katika wakati ujao ambao Mungu ataleta, maisha yatakuwa yenye kupendeza sana hivi kwamba hakutakuwa na uhitaji wa kufanya lolote ili kurekebisha halihewa.