Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 5/22 kur. 18-20
  • Njia Tano za Kuendeleza Ubora wa Maisha Yako

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Njia Tano za Kuendeleza Ubora wa Maisha Yako
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Nambari 1: Panda Bustani
  • Nambari 2: Nunua kwa Wingi
  • Nambari 3: Jifunze Ufundi wa Kuhifadhi Chakula
  • Nambari 4: Jaribu Ufugaji wa Kiwango Kidogo
  • Nambari 5: Dumisha Usafi wa Kiafya Ufaao
  • Usafi—Kwa Nini Ni Muhimu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Chakula Kutoka Shamba Lako
    Amkeni!—2003
  • Unaweza Kusimamiaje Nyumba?
    Siri ya Furaha ya Familia
  • Fanya Ulaji Wako Uwe Salama
    Amkeni!—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 5/22 kur. 18-20

Njia Tano za Kuendeleza Ubora wa Maisha Yako

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

INFLESHENI, ugonjwa, utapiamlo, umaskini—matatizo haya yameenea pote katika nchi zinazoendelea. Na hakuna utatuzi wa mara moja unaopatikana, angalau kutokana na maoni ya binadamu. Ikiwa waishi katika nchi inayoendelea, je, kuna lolote uwezalo kufanya ili kuendeleza ubora wa maisha yako? Ndiyo, kunalo! Yafuatayo ni madokezo matano ambayo huenda ukayapata kuwa yenye msaada na yenye kutumika.

Nambari 1: Panda Bustani

“Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,” husema Biblia kwenye Mithali 28:19. Kwa kweli, yaweza kukushangaza kuona kiasi kinachoweza kutokezwa kwenye shamba dogo. Katika kitabu chake Le jardin potager sous les tropiques (Bustani ya Mboga Katika Nchi za Joto), mwandishi Henk Waayenberg adai kwamba shamba lenye ukubwa wa meta mraba 50 kwa 100 laweza kutokeza mboga za kutosha kulisha familia ya watu sita!

Kwa nini utumie mali zako kwa kununua vitu uwezavyo kukuza mwenyewe? Ikitegemea udongo na tabia ya nchi, yawezekana kupanda vitu kama vile mbinda, pilipili hoho, mchicha, kitimiri, lemongrass, kitunguu ya maji, mihogo, malenge, viazi vitamu, miwa, nyanya, bilimbi, na mahindi karibu tu na nyumba yako. Kwa kutaja machache, bustani kama hiyo yaweza kujaliza mlo wa familia yako, na huenda hata ukawa na mazao ya ziada ambayo waweza kuuza.

Ikiwa una shamba la kutosha, huenda pia ukafikiria kupanda aina mbalimbali za miti ya matunda. Katika visa fulani, mti mmoja wa matunda waweza kutokeza matunda mengi zaidi ya vile wewe na familia yako mwezavyo kula. Kujifunza kutengeneza mbolea—utaratibu wa kutengeneza samadi kutokana na mata ya viumbehai waliokufa—kutakusaidia uboreshe uzalishaji wako wa chakula. Miti yaweza kutokeza zaidi ya chakula na pato la ziada la familia yako. Miti iliyopangwa vizuri yaweza pia kutokeza kivuli, hewa safi, na kufanya mazingira yako yawe mazuri zaidi na yapendeze.

Ingawa hivyo, namna gani ikiwa wajua mambo machache kuhusu kilimo cha bustani? Je, una marafiki, majirani, au wajuani ambao wana uzoefu katika jambo hili? Basi kwa nini usiwaombe msaada au shauri? Huenda ikawezekana pia ununue au uazime vitabu vinavyohusu kilimo cha bustani.—Ona makala “Kwa Nini Usipande Bustani ya Mboga?” katika toleo la Amkeni! la Mei 22, 1974 (la Kiingereza).

Nambari 2: Nunua kwa Wingi

Je, wewe hununua vitu vya lazima kama unga, mchele, na mafuta kwa kiasi kidogo? Ikiwa ndivyo, waweza kuwa ukipoteza sehemu kubwa ya bajeti yako. Badala yake, ikiwa yawezekana kwa vyovyote, jaribu kununua vyakula hivyo kwa wingi, ukishiriki gharama na familia mbili, tatu, au zaidi. Kununua kwa wingi pia kwaweza kuokoa pesa zako wakati inapokuwa ni msimu wa matunda fulani au mboga. Katika visa fulani, waweza pia kununua vitu kwa ujumla.

Nambari 3: Jifunze Ufundi wa Kuhifadhi Chakula

Kununua kwa wingi huzusha swali la jinsi ya kuhifadhi vyakula vinavyoweza kuharibika. Kukausha chakula ni njia moja ipendwayo na yenye kutumika. Idadi kubwa ya wanawake Waafrika hupata riziki kwa kukausha matunda, mbinda, maharagwe, boga, mbegu za malenge, na viungo. Kukausha hakuhitaji kifaa chochote cha pekee. Chakula hicho chaweza kuwekwa mahali safi palipo juu au kuning’inizwa, labda kikifunikwa kwa kitambaa chembamba ili kuzuia nzi. Hewa na jua litafanya yanayobakia.—Ona makala “Je Waweza Kuishi kwa Kutegemea Mali Chache?” katika toleo la Amkeni! la Agosti 8, 1975, (la Kiingereza).

Nambari 4: Jaribu Ufugaji wa Kiwango Kidogo

Je, yawezekana ufuge kuku wako, mbuzi, hua, au wanyama wengine? Katika mahali pengi nyama imekuwa kitu cha anasa. Lakini kwa msaada kidogo kutoka kwa wengine, waweza kujifunza jinsi ya kufuga kundi dogo la wanyama. Je, wewe hufurahia kula samaki? Basi, waweza kujaribu kujifunza jinsi ya kutengeneza dimbwi dogo la samaki. Nyama, mayai, na samaki huwa na chuma, kalisi, vitamini, madini, na protini—vilivyo muhimu kwa afya ya familia yako.

Nambari 5: Dumisha Usafi wa Kiafya Ufaao

Usafi wa kiafya pia ni muhimu kwa afya ya familia yako. Hali zisizo safi huvutia panya, nzi, na mende—kisababishi cha kila namna ya magonjwa. Kudumisha usafi wa kiafya ufaao kutakugharimu wakati na jitihada. Lakini gharama ya usafi ni kidogo kuliko gharama ya dawa na gharama za daktari. Viwango vya usafi huenda vikatofautiana kwa kiasi fulani kutoka mtu mmoja hadi mwingine na kutoka nchi moja hadi nyingine. Hata hivyo, kuna kanuni chache za ujumla ambazo hutumika kila mahali.

Chukua kwa mfano, choo. Katika sehemu za mashambani mara nyingi watu huviacha vikiwa vichafu na vibovu na hivyo huwa chanzo kikuu cha ugonjwa na maradhi. Wafanyakazi wa afya wa mahali penu waweza kukuandalia maagizo juu ya jinsi ya kujenga msala usio na vijidudu vya maradhi au choo cha nje kwa gharama kidogo sana.

Namna gani nyumba yako yenyewe? Je, ni safi na imetunzwa vizuri? Je, hunukia vizuri? Namna gani jiko lako? Je, ni nadhifu na safi? Lazima chakula kiwe safi na kipikwe vizuri ili kuwa chenye afya. Vijidudu na vimelea huwa vingi ndani ya maji machafu. Kwa hiyo chuja au chemsha maji kabla ya kuyatumia. Suza vyombo vya kulia katika maji yaliyochemshwa, na nawa mikono yako kikamili kabla ya kushika chakula. Hifadhi maji ndani ya vyombo visafi, vilivyofunikwa.

Mbwa, paka, kuku, na mbuzi hawapasi kuruhusiwa kurandaranda jikoni—ikiwa wataka kudumisha hali safi za kiafya. Wala buku na panya hawapasi kuruhusiwa kukimbia juu ya sufuria na vikaango, hivyo wakichafua chakula chako. Mtego wa panya ulio sahili waweza kuondoa tatizo hilo.—Ona “Kutimiza Takwa la Usafi,” katika toleo la Amkeni! la Mei 8, 1989.

Hatimaye, ni Ufalme wa Mungu pekee utakaotatua kikamili matatizo yote ya wanadamu. (Mathayo 6:9, 10) Hata hivyo, katika wakati huohuo, madokezo haya sahili yaweza kukusaidia kuendeleza ubora wa maisha yako.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Panda bustani

[Picha katika ukurasa wa 19]

Nunua kwa wingi

[Picha katika ukurasa wa 19]

Jifunze ufundi wa kuhifadhi chakula

[Picha katika ukurasa wa 20]

Jaribu ufugaji wa kiwango kidogo

[Picha katika ukurasa wa 20]

Dumisha usafi wa kiafya ufaao

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki