Kucha Zako Je, Wewe Huzitunza?
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Sweden
MTU fulani akikuomba, “Hebu nione kucha zako?” ungeitikiaje? Je, ungemwonyesha kwa furaha kucha zako zilizotunzwa vizuri, au ungeweka mikono yako nyuma mara moja? Huenda ukawa na sababu nzuri za kuficha kucha zako. Labda hazionekani vizuri tu, au labda una tabia ya kuuma kucha zako. Kujua zaidi kuhusu anatomia ya kustaajabisha ya kucha zetu kutatusaidia kuzithamini zaidi na kwaweza kutuchochea tuzitunze vema.
Kucha zako hasa zimefanyizwa na seli zilizokufa ambazo zimekuwa ngumu zilizo na nyuzinyuzi za protini keratini. Kiwango ambacho kucha hukua hutofautiana kati ya kidole kimoja na kingine na kati ya mtu mmoja na mwingine. Kucha hukua kwa kiwango cha wastani cha milimeta tatu kwa mwezi. Kucha zilizoachwa bila kukatwa zaweza kufikia urefu wa kadiri kubwa. Kulingana na kitabu The Guinness Book of World Records 1998, mwanamume mmoja Mhindi aliacha kucha tano za mkono wake wa kushoto zikue kufikia jumla ya sentimeta 574. Ukucha wa kidole gumba ulikuwa na urefu wa sentimeta 132.
Muundo Ulio Tata
Kwa kuangalia mara moja waweza kufikiri kuwa ukucha ni kipande kimoja tu, bamba la ukucha. Huenda basi ukashangaa kujua kwamba kucha zaweza kufikiriwa kuwa na sehemu kuu kadhaa ziwezazo kuonekana vilevile sehemu fulani usizoweza kuziona. Hebu tuchunguze kwa ukaribu zaidi muundo wa ukucha.
1. Bamba la ukucha. Huu ni ule muundo mgumu ambao kwa kawaida sisi huuita ukucha. Bamba la ukucha lina tabaka mbili, ya juu na ya chini. Seli katika tabaka hizi mbili zimepangwa kwa njia tofauti na hukua kwa viwango tofauti. Uso wa juu ni laini, huku uso wake wa ndani ukiwa na ncha ambayo hulingana na mitiko iliyo kwenye msingi wa ukucha. Mitiko hii ni ya kipekee kwa kila mmoja na yaweza kutumika kama njia ya kujitambulisha.
2. Sehemu ya chini ya ukucha. Hii ni sehemu nyeupe iliyo na umbo kama la nusu mwezi iliyo katika msingi wa bamba la ukucha. Si vidole vyote vyenye sehemu ya chini ya ukucha yenye kuonekana. Ukucha hukua kutoka katika eneo dogo la tishu zilizo kwenye msingi wa sehemu ya chini ya ukucha, liitwalo matrix. Hii ndiyo sehemu muhimu zaidi katika kizio cha ukucha. Sehemu ya chini ya ukucha ni mwisho wa matrix ya ukucha, na hivyo, ndiyo sehemu ya ukucha iliyo hai ionekanayo. Sehemu iliyobakia ya bamba la ukucha hufanyizwa na seli zilizokufa.
3. Mikunjo ya ukucha, ya kati na ya pembeni. Hii hurejezea kwenye ngozi inayozunguka bamba la ukucha. Ngozi hii huitwa mkunjo wa ukucha kwa sababu haiishii kwenye bamba la ukucha lakini hujikunja chini na kufunika bamba la ukucha linalojitokeza. Mikunjo hii ya ngozi hulinda na kutegemeza sehemu zinazozunguka ukucha.
4. Eponychium. Huu ni mstari mdogo mno wa mkunjo wa ngozi ambao huonekana kwenye msingi wa bamba la ukucha. Nyakati nyingine, huu huitwa ukaya wa ukucha.
5. Ukaya wa ukucha. Ukaya wa ukucha wa kweli ni upanuzi mdogo mno ulio chini ya eponychium. Ni tabaka isiyo na rangi ya ngozi iliyochanwa ambayo hushikamana na uso wa mwisho wa bamba la ukucha.
6. Upeo wa ukucha. Sehemu ya bamba la ukucha ambayo hukua kupita ncha ya kidole.
7. Hyponychium. Hupatikana chini ya sehemu ya bamba la ukucha, tishu hii hutengeneza kifuniko kisichoingiza maji ambacho hukinga msingi wa ukucha usipate ambukizo.
Utumizi Wake
Kucha zetu ni zenye mafaa katika njia nyingi, kama vile kujikuna. Zinatumika wakati tunapomenya chungwa, kufungua tuta, au kuchukua vitu vidogo-vidogo. Zaidi ya hilo, kucha hutegemeza na kulinda ncha za vidole zilizo nyetivu na rahisi kuharibika.
Jambo ambalo halipasi kupuuzwa ni umaana mzuri wa kucha. Kucha zetu zaweza kudhihirisha tabia nzuri—au mbaya—za kujipamba kwetu. Hizo huwa na sehemu muhimu katika ishara za kawaida, na ikiwa zitatunzwa vizuri, zaweza kuremba mikono yetu. Bila hizo twaweza kuzuiwa katika maisha yetu ya kila siku, na mikono yetu ingeonekana kuwa isiyo kamili.
Utunzaji Mzuri Huzifanya Ziwe Zenye Nguvu
Zikiwa sehemu ya mwili wetu maridadi, kucha zetu zapasa kutunzwa vizuri. Ikiwa una tatizo kubwa na kucha zako, wapaswa kumwona daktari wako. Kwa hakika, kwenye ncha ya vidole vyako, waweza kuwa na dalili za tatizo la kimwili. Ndiyo, yadaiwa kuwa maradhi fulani ya kimwili yaweza kugunduliwa kwa kuangalia kucha zako.
Je, kula kalisi au vitamini nyingi zaidi kutafanya kucha ziwe ngumu zaidi? Katika kujibu swali hili, Profesa Bo Forslind, mtafiti katika habari ya kucha kwenye Taasisi ya Karolinska katika Stockholm, Sweden, aliambia Amkeni!: “Hakuna uthibitisho uliopo wa kuunga mkono maoni hayo. Mchanganuo wa kalisi iliyoko katika kucha zenye afya huonyesha idadi ndogo sana ya elementi hiyo.”
Hata hivyo, kile ambacho kwa hakika husaidia kucha zako zibaki zikiwa ngumu na zenye kunyumbulika, ni maji. Kama ilivyotajwa awali, kucha huwa na keratini. Nyuzi hizi za keratini huhitaji maji ili ziwe zenye kunyumbulika. Profesa Forslind atoa kielezi: “Hata ingawa kipande cha ukucha wako chaweza kuwa chenye kunyumbulika unapokikata mara ya kwanza, kipande hichohicho cha ukucha kitakuwa kigumu sana kinapokauka usiku kucha.” Unyevu utaziweka kucha zako zikiwa zenye kunyumbulika na zenye nguvu. Lakini unyevu huu hutoka wapi? Bamba la ukucha huonekana kuwa gumu, lakini maji yaweza kupenya. Unyevu kutoka kwenye ncha ya ukucha husonga juu kupitia bamba la ukucha hadi kwenye uso, ambapo huvukizwa. Ni nini kiwezacho kufanywa ili kuzuia kucha zako kukauka na kuziweka zikiwa na nguvu? Profesa Forslind asema: “Kuzipaka mafuta kila siku ni kwenye manufaa.”
Kutunza Ukuzi na Urembo Wake
Kwa kuwa ukucha hukua kutoka kwenye matrix, utunzaji mzuri kwa ajili ya sehemu hii ya ukucha ni muhimu. Kuchochea matrix kwa kuikanda kwa krimu au mafuta kwa ukawaida kwaweza kuwa kwenye faida kwa bamba la ukucha. Kwa kuongezea, kuweka tone la mafuta kwenye upeo wa ukucha kwaweza pia kusaidia, kwani hili hufanya ukucha usikauke.
Jinsi unavyochonga kucha zako au kuzikata kwaweza kuzifanya ziwe zenye nguvu au dhaifu. Inapendekezwa kwamba uchonge kucha zako kutoka upande ukielekea katikati. Kumbuka kwamba kuondoa miisho kwa kuchonga kutafanya ukucha uwe dhaifu. Hili litatokeza ukucha wenye ncha kali, ambao ndilo umbo dhaifu zaidi kwa kuwa halina utegemezo kwenye pande. Inapendekezwa kwamba ili kuwa na kucha fupi zenye nguvu, uache kucha zako zikue kufikia milimeta 1.5 kwenye pande na uchonge umbo la mviringo ambalo hufuata mstari wa ncha ya kidole.
Wanawake fulani huenda wakapenda kuwa na kucha ndefu kidogo. Lakini hapa kuna hadhari. Kucha zilizo ndefu kupita kiasi zaweza kuvutia uangalifu usiohitajiwa na pia kukuzuia kufanya kazi za kawaida. Kwa hiyo uwe na mtazamo uliosawazika wa urefu wa kucha zako. Ukifanya hivyo, kucha zako zitakuwa hazina na zitatokeza picha nzuri kwa wengine.
Kamwe usiwaruhusu wataalamu wachome kucha zako na chombo kikali. Hili laweza kusababisha madhara kwenye hyponychium, tishu iliyo chini ya upeo wa ukucha. Tishu hii hufanyiza kifuniko kigumu kinacholinda ukucha ulio chini. Ikiwa eneo hili litaharibiwa, ukucha waweza kujitenga na msingi wa ukucha na upate ambukizo. Kusafisha eneo lililo chini ya ukucha tumia burashi nyororo sana.
Kucha zenye nguvu na afya kwa njia fulani ni za kurithiwa. Hiyo ndiyo sababu watu fulani huwa na mabamba ya kucha yaliyo na nguvu na yenye kunyumbulika, huku wengine wakiwa na kucha zilizokauka na ngumu. Hata hali ya kucha zako iweje, waweza kuboresha jinsi zinavyoonekana kwa utunzaji wenye kiasi na wa kawaida. Ndiyo, kuelewa muundo wa ukucha, jinsi ufanyavyo kazi, na utunzaji unaofaa kwakupa ustadi zaidi. Kutumia habari kama hii vizuri kutatokeza matokeo mazuri.
Kwa kweli kucha ni sehemu ya kustaajabisha sana ya mwili wa mwanadamu. Muundo wazo na utumizi hutolea ushahidi wa akili yenye ubuni. Mfalme Daudi wa zamani kwa unyenyekevu alieleza kusifu kwa kustaajabia kuhusu Muumba wake, kama ilivyorekodiwa katika Zaburi 139:14: “Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, na nafsi yangu yajua sana.”
[Mchoro katika ukurasa wa 23]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
[Picha katika ukurasa wa 23]
1. Bamba la ukucha;
2. sehemu ya chini ya ukucha;
3. mikunjo ya ukucha, ya kati na ya pembeni;
4. eponychium;
5. ukaya wa ukucha;
6. upeo wa ukucha;
7. hyponychium;
8. matrix;
9. msingi wa ukucha