Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Je, Tunabadili Halihewa Yetu? Nina umri wa miaka 17 na ninajitayarisha kupata diploma. Mtihani unatia ndani somo la jiografia, na mfululizo wa makala “Je, Tunabadili Halihewa Yetu?” (Mei 22, 1998) ulinisaidia sana kujitayarisha. Baada ya mtihani, wanadarasa wenzangu waliniuliza nilikotoa habari hizo juu ya halihewa, na nusu kati yao wakaomba nakala.
A. G., Uswisi
Nilipendezwa sana na uchanganuzi juu ya ongezeko la joto katika toleo hilo la Amkeni! Mimi ni mtetezi wa ikolojia na pia Mkristo. Mara nyingi Mashahidi wa Yehova hushutumiwa na vyombo vya habari. Lakini yaliyomo katika gazeti lenu yanastahili ufikirio. Ikolojia na imani vimepuuzwa kabisa. Mwishowe, kunao watu wa kidini wanaopendezwa na uumbaji wa Mungu!
M. C., Ufaransa
Nina umri wa miaka 14 nami nawashukuru sana kwa ajili ya makala hizo. Sikujishughulisha sana na mambo ya halihewa, lakini sasa kwa mara ya kwanza nimefikiria kwa uzito yale ambayo huenda tunaifanyia sayari yetu. Hizo makala zapasa kuwafanya watu wengi wawe macho, kwani ni nani atakaye kuyaharibu mazingira yetu? Hatupaswi kuitupilia mbali tu zawadi ya Mungu.
S. Q., Ujerumani
Nilichangamka sana kusoma jambo fulani juu ya tabia ya nchi, katika gazeti ambalo watu huliona kuwa la kidini. Hiyo yaonyesha jinsi ambavyo Amkeni! huwajali watu—si kwa mambo ya kidini tu bali pia ya kimwili. Ijapokuwa tunaipuuza, halihewa huathiri maisha yetu kwelikweli.
M. F. M., Ujerumani
Kutunza Kucha Ni jambo la kushangaza kwamba kwa karibu miaka 52, isipokuwa kwa vipindi viwili tu vifupi, nimeziuma kucha zangu. Baada ya kusoma makala “Kucha Zako—Je, Wewe Huzitunza?,” katika Amkeni! la Mei 22, 1998, nimeacha kuziuma. Kwa nini? Kwa sababu Yehova Mungu ndiye Mbuni wa kucha naye hutaka, kama ilivyo na vitu vingine vyote, tuzitunze. Asanteni kwa vikumbusha vyenu vizuri.
D. H., Uingereza
Kwa kuwa ninatunza nyumba na shamba na pia mama-mkwe wangu aliyelemaa, unaweza kuona kwamba nina mengi ya kufanya kuliko tu kutunza mikono yangu. Kucha zangu zimenitatiza kwa muda fulani, kwa kuwa zimevunjika na kupasuka. Hivyo makala hiyo ilikuja tu wakati ufaao.
W. B., Ujerumani
Tangu utoto wangu, nimeziuma kucha zangu na kuaibikia sura yake mbaya. Uthamini wangu wa kwamba kucha ni sehemu ya ajabu ya mwili wa binadamu uliongezeka nilipokuwa nikiisoma hiyo makala. Ilinitia moyo kufanya kazi ya kurekebisha tabia yangu.
K. Y., Japani
Kiolezo cha Kuigwa Niliposoma makala katika Amkeni! la Mei 22, 1998, yenye kichwa “Vijana Huuliza . . . Ni Nani Apaswaye Kuwa Kiolezo Changu cha Kuigwa?,” nilitafakari jinsi ambavyo makala kama hiyo zimeyaboresha maisha yangu. Baada ya familia yetu kuvunjika, kwa asili nilivutiwa kwanza na marafiki wa rika langu. Lakini ndipo nikaanza kutafakari kwa uzito juu ya watu ambao walikuwa wamenijenga zaidi katika maisha yangu—dada Wakristo wakomavu. Hivi sasa mimi hutafuta urafiki kama ule wa Paulo na Timotheo au Ruthu na Naomi. Rafiki yangu mkubwa zaidi ni dada mwenye umri wa karibu miaka 50 ambaye amenifundisha kuhusu shangwe, upendo, huruma, fadhili, na ukarimu. Tunafanya kazi kwa muungano—tunaishi katika chumba kimoja nasi tumeanza huduma ya wakati wote. Asanteni kwa mwongozo na mwelekezo wenu mzuri.
C. F., Marekani